My Blog List

Wednesday, December 12, 2007

UHURU NA AKILI MGANDO ZA BAADHI YA WATAWALA

Taifa letu lilitimiza miaka arobaini na sita (46) tangu lizaliwe; jumapili iliyopita ilikuwa ni kumbukumbu ya siku ya uhuru kwa maana nyingine. Kama mtanzania, na mzalendo sina budi kuchukua kalamu na kutafakari kwa kina miongo kadhaa kama Taifa ni changamoto gani tumezikabili na zipi inatubidi tupandishe soksi (pull up socks) ili kuendeleza nchi yetu. Binafsi, naamini kama tutafanyia kazi changamoto ya “Utawala Bora” basi uhuru wetu utakuwa na maana sana. Mada yangu itaegemea sana hapa tu.

Kabla ya kujadili, nitoe pongezi kwa watanzania wote tangu raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na kwa ujumla watu wa kada zote hapa nchini kwa kuadhimisha siku hii.

Bila ubishi kabisa, nchi yetu imefanikiwa sana katika nyanja mbalimbali tangu uhuru hasa ukilinganisha na nchi nyingine za dunia ya tatu. Hapa ieleweke hata kama tungekuwa tumefanikiwa kiuchumi kama vile Wachina ama Wajapan bado kungekuwa tu na matatizo. Hivyo si vyema kubeza kuwa labda kila kitu ni mrama; yapo mafanikio kama vile umoja wa kitaifa ambao ni mfano dunia nzima. Binafsi nimekutana wa watu kadhaa kutoka pande mbalimbali za dunia wanaposikia umetoka Tanzania watasifia Umoja wetu. Hii yote ni heshima za mwasisi wa Taifa, hayati Mwalimu Nyerere.

Kuendana na mfumo wa kiutawala duniani, yapo mapungufu mengi ambayo nadhani ni vigumu kujikwamua nayo hasa ukizingatia mfumo mzima wa biashara ulimwenguni ni wa upendeleo na ukandamizaji kwa sera za mashirika makubwa ya kiuchumi na kibiashara ulimwenguni. Hapa nazungumzia sera za Mfuko wa Kimataifa wa Fedha (IMF), Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Biashara Ulimwenguni (WTO) mwanzoni likijulikana kama GATT.

Ndio maana kama mtu anafuatilia hata yale majadiliano kibiashara ya kule DOHA yamekwama kabisa na ni wazi watawala wa dunia hawataki kabisa kukubali baadhi ya hoja ambazo zitalikwamua bara la Afrika kutoka umasikini usiokwisha. Hata hivi majuzi, Taifa letu limesaini makubaliano mapya ya mashirikiano ya kiuchumi na Jumuiya ya Ulaya (EU) yajulikanayo kama (EPA) kwa kutumia mgongo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ni wazi yameshinikizwa na hayatailetea nchi yetu tija sana kinyume na inavyodhaniwa na wale waliosaini. Inajulikana wazi tumelazimishwa kwa kuharakisha kusaini kabla ya ule mkataba wa Cotonou kumalizika hapo December 31 mwaka huu. Nisijadili hili zaidi labda siku nyingine.

Ni katika mchakato huu wa changamoto hizi za mabepari basi hata kama watawala wetu wanao utashi inakuwa vigumu kuweza kusimamia maslahi yenye tija kwa nchi zetu. Kwani mara nyingine watawala wetu wanapokuwa na utashi wa dhati basi mambo kama yanayomkuta Robert Mugabe hayazuiliki kwani wanaishia kufanya maamuzi kwa pupa, bila kufikiri kwa mpangilio na kwa logiki ambayo yanagharimu maisha na uchumi wa nchi zao. Ndio changamoto za “Uhuru” ambazo kwangu ni jinamizi tu; kwani, tunaposherehekea siku hii lazima tuelewe inawezekana kabisa siku ile ilikuwa ni mwanzo wa kipindi cha giza. Ningependa nielezwe hivi Mwalimu Nyerere alipokwenda kule Lancaster alikwenda kusaini mambo gani? Manake inatia shaka huenda ndio ulikuwa wakati wa kujitia kitanzi badala ya kuwa huru. Kwani nina mashaka sana kama kweli tuko huru.

Na ndio maana bado tuna changamoto nyingi sana za kutafakari na kujiuliza tufanye nini? Kwa mtizamo wa serikali ya awamu ya nne, ni wazi changamoto kuu ambayo lazima ifanyiwe kazi ni hii ya “utawala bora”. Hii imebaki kuwa ngonjera na kama hatubadiliki kwa hili basi kamwe hatutapiga hatua yeyote. Nasema hivi kwani naamini pamoja na changamoto za jinamizi la uhuru linaloongozwa na sera dhalimu za kimataifa bado tuna mengi ya kufanya kwa hapa nyumbani ambayo yatatuwezesha tuwe bora tu mbali na mashinikizo dhalimu ya mabepari.

JE TUFANYE NINI?

Tunahitaji kufikiri zaidi ya kuongea sana; hii itatuwezesha kuwekeza katika kuwajibika kwa bidii (hardworking) badala ya kupiga siasa kwa muda mrefu zaidi. Ni wazi hadi leo hii, bado utendaji wetu umetawaliwa na mashiko ya kisiasa zaidi kuliko nidhamu ya kazi katika nyanja mbalimbali. Hasa katika chombo kama Bunge, ni lazima tubadilike; miaka arobaini na sita itufanye tuamue sasa ni mwisho wa siasa za upande mmoja usiozingatia maslahi ya umma. Njozi za chama kushika hatamu zisipoachwa basi hatufiki popote kama Taifa la miongo hii minne na ushehe.

Kwa watawala wetu, lazima kung’amua kuwa kama mhimili wa utawala (executive) unakuwa na nguvu kubwa dhidi ya mihimili mingine basi hatufiki. Pamoja na nguvu ya kikatiba ya taasisi ya uraisi, Uhuru unakuwa na maana kama kiongozi mkuu wa nchi atang’amua hili na kuruhusu utendaji unaoruhusu majadiliano ya vyama vyote vya mitizamo tofauti ndani ya bunge badala ya kuzingatia tu upitishaji wa maamuzi yenye kuegemea uchama na si umma.

Ingawa demokrasia inasema ‘wengi wape’, lakini nadhani pia tuangalie mfumo wetu wa upigaji kura na maamuzi ya upitishaji sheria ama maamuzi bungeni ukoje? Je unaruhusu upigaji kura wa wabunge wa chama tawala unaozingatia uhuru wa mawazo ya mbunge au ni kushurutisha kwa kuegemea maslahi ya chama yaliyofichwa ili kulinda maslahi ya vigogo wa chama tawala bila kutoa sababu za msingi kuhusu jambo fulani ili kulinda maslahi ya nchi.Uhuru unaweza usiwe na maana sana kama mfumo wa maamuzi ndani ya chombo kama Bunge unambana mbunge mwenye mawazo tofauti.

Hata ndani ya vyama vya siasa, ni changamoto pia kujiuliza hivi kuna uhuru wa mawazo wa mbunge katika kujadili mambo na hata kuhoji ndani ya chama? Yaani kwa miaka yote hii arobaini na sita, bado ni kosa la jinai ndani ya chama tawala kwa mtu kujadili hisia zake kwa uwazi inavyoonekana na hata kupinga ama kupiga kura ni udikteta tu (intra-party disagreement, debate and even voting is still a crime). Hapa lazima watawala wakumbuke hili ndilo linalokwamisha maendeleo yetu na hapana budi tuweke mizani ya usawa (strike a balance) katika utendaji wa serikali dhidi ya mihimili mingine miwili hasa ule wa Bunge tukianzia ndani ya vyama vya siasa.

Kwa mfano, kama tutazingatia utawala bora, basi lazima tubadili mitizamo yetu (mentality): yaani serikali iwe kwa ajili ya umma na si kama jamvi la kuficha mafisadi kama ilivyokwishajidhihirisha kwa watuhumiwa wa ufisadi kutajwa hadharani na wao kuamua kukaa kimya bila kujisafisha. Hata mamlaka yenye uwezo wa kuwawajibisha nayo haikuchukua hatua zozote. Ndio hapa bado inaonesha tunawaza zaidi katika kulinda maslahi ya kisiasa kuliko ya umma. Yote hii inashawishi mtu mwenye akili timamu kuwaza na kuamini labda ni kwa sababu ya utawala mbovu. Mfumo wa “Check and Balance” uko likizo ili tu kulinda maslahi ya kisiasa ya chama kinachotawala. Huu ni ugonjwa mkubwa barani Afrika na kama hatubadili mtizamo “Uhuru” unakuwa hauna maana.

Ninaamini kama watanzania, tuna bahati ya kuwa na raisi wa nchi ambaye ana karama ya kuongoza kwa kujali demokrasia; kwani anajitahidi kujumuisha pande na hisia mbalimbali za kisiasa katika utendaji wake. Mashaka yangu bado nadhani waliomzunguka raisi wetu mitizamo yao imepitwa na wakati na si endelevu. Ni mitizamo ya kusisitiza zaidi ‘umilele-chama’ (party-omnipresence) kuwa na woga labda chama kitaangushwa madarakani kwa kile wasichokijua. Na hii ndio chanzo cha madhila kadhaa zinazoisumbua serikali ya awamu hii.

Ni changamoto nzuri za kumfanya raisi na wasaidizi wake kuliona hili na kuamua kubadilika. La sivyo tuna hatari ya kubakiwa na “Kiongozi mwenye karama asiye na mwelekeo” (a charismatic leader without a cause). Mwelekeo wa sasa kwa nchi huru unatia shaka kwani uwezo wa kufikiri wa vigogo wengi ni mdogo sana na ni wazi unasababishwa na tamaa ya fedha na ulafi wa kila aina. Kitu woga kwa viongozi wetu ndio chanzo cha udhaifu wa viongozi wetu kuanzia juu.

Siku ya leo tujiulize ni kwa jinsi gani utawala wa shaghala baghala ulivyogharimu taifa letu kwa kipindi chote cha uhuru. Tunaweza tukalaumu sana na kusingizia mfumo wa kidunia (world order) ambao nimeuelezea awali, lakini kama tuna akili timamu ni wazi kwa nafasi yetu kwa mambo ya hapa nyumbani tuna mapungufu pia ambayo lazima tuamue kwa dhati kuyafanyia kazi. Ndio maana hata Raisi wetu majuzi alisikika akisema na kukiri hata hii mikataba ya madini ni sisi wenyewe wa kujilaumu mbele ya Waziri Mkuu wa Canada mheshimiwa Stephen Harper.

Kama Taifa, miaka arobaini na sita ya Uhuru haina maana sana kwani tumeshindwa kukabili changamoto za ndani kabisa. Inakuwa vigumu kukabili zile za nje manake watawala wa dunia wanatumia udhaifu wetu huu kutulaghai kwa kila hali. Kama hatubadiliki kwa kuruhusu kukosoana ndani ya vyama vyetu, bunge letu na kila mahali ili kulinda maslahi ya umma basi kamwe sioni maana sana ya uhuru. Ninachokiona ni sana sana ni juhudi kubwa tena hasi (highest retrogressive endeavour) za watawala na wanasiasa katika kuirudisha nyuma nchi yetu kwa kasi.

Uhuru bila ‘utawala bora’ ni kwa wachache na si kwa umma wa watanzania. Kama siku ya Jumapili, leo nitamwomba Mungu aizindue akili ya watawala na wanasiasa kwa ujumla wao kubadili mitizamo. Tuachane na akili mgando ndio uhuru utakuwa na maana. Miaka arobaini na sita ya Uhuru ije na mtimzamo (mentality) mpya kuhusu utawala wa Taifa hili. Hii ndio tafakuri yangu ya siku hii ya uhuru kwa leo.

No comments: