My Blog List

Saturday, December 01, 2007

TANZANIA BILA UKIMWI INAWEZEKANA?

Siku ya Ukimwi duniani; ni wakati wa kila mtu hasa mwafrika kutafakari juu ya balaa hili ambalo limeshachukua roho za watu lukuki. Wakati naandika makala hii mara nasikia redioni kuwa huko Mbagala Kizuiani kuna jamaa mmoja kaamua kujiua baada ya kuthibitishiwa kuwa ana virusi mwilini mwakeMwingine kaamua kumuua mkewe huko Mbeya baada ya kusikia mkewe kapima bila ruhusa yake

.Ni habari za kusikitisha lakini ni lazima tujiulize hivi kweli hizi kampeni za upimaji ndio jibu la dhahama hili? Na pia tujiulize kwanini tunahofu juu ya kuambiwa tumeathirika?Je hatupo tayari kuwajibika na matokeo ya tabia zetu za ngono zembe?

Napenda niseme kuwa hizi kampeni za upimaji ukimwi zinanitia wasiwasi kama kweli ndio muarobaini wa gonjwa hili. Nasema hivi kwani ni zaidi ya miaka ishirini sasa tangu nimeanza kusikia habari za ugonjwa huu. Na kwa muda wote huo kampeni mbalimbali za kuhamasisha na kuelimisha kuhusu ugonjwa huu zimekuwepo. Ndio maana leo hii katika kampeni hizi za rais Jakaya Kikwete, hakuna jipya linalosemwa. Nimesikiliza, kutizama na hata kuhudhuria semina juu ya gonjwa hili kwa kweli sijaona kipya chochote juu ya elimu ya gonjwa hili.

Nikirejea kwenye mafunzo yatolewayo shuleni: msingi, sekondari na hata katika vyuo kupitia mitaala mbalimbali, nadhani watanzania kama jamii tuna tatizo. Ni jamii isiyojishughulisha kabisa kusoma na kujielimisha binafsi. Habari juu ya gonjwa hili zimesambaa kila kona kwa miaka ishirini iliyopita: vitabuni, majarida, vibwagizo, kwenye mitandao ya intaneti na magazetini, lakini watanzania hatujishughulishi kupata mafunzo lakini tunataka semina, makongamano na hata vipindi vya redio na televisheni visivyo na jipya juu ya gonjwa hili kila kukicha. Kuna haja ya watanzania kuamka katika kujali umuhimu wa kujua mambo yanayohusu maisha yao. Bila hivyo sidhani kama tutafika popote katika vita ya gonjwa hili.

Hivi kweli inaingia akilini kuwa hadi leo hii watanzania watu wazima kwa vijana hatuna uelewa wa gonjwa hili?Miaka yote tumeishi na gonjwa hili yaani hatulifahamu? Nisingetegemea tuwe na kampeni kubwa kama ya sasa na ambayo hatima yake bado ni kutokupungua kwa maambukizi kwani kuna kila dalili watu wengi wameziba masikio.

Nashangazwa na upimaji kwa siri: mosi, hivi kama napima kama nina virusi alafu nasema ni siri yangu, na sitaki watu wajue kama nimeathirika, si kuwa ninataka kuendelea kujichanganya visivyo na watu wengine ili niwaambukize? Kwanini tusiwe na utaratibu wa kistaarabu wa waathirika kuhimizwa kwa ushauri nasaha ili wajiweka wazi na hata kujiunga kwa uwazi na taasisi za waathirika kwani kwa sasa wengi wao ni kwa siri sana. Hapa siongelei unyanyapaa, ila ni vyema watu wawe huru kutambuliwa kwani kama usiri utaendelea kutiliwa maanani zaidi, basi hii kampeni haitatusaidia sana kwani kuna kila shaka ya kuendeleza uambukizi zaidi.

Uwazi huu pia ungeoneshwa hata kwa wanajamii vinara: wabunge, mawaziri, na viongozi mbalimbali wa jamii. Kwa mfano, kama tungejulishwa angalau taarifa za upimaji kule bungeni, je wangapi walipima, wangapi walionekana kuathirika ama kutoathirika. Lakini kupambana na ukimwi kwa usiri hakutakomesha ukimwi kamwe.

Pia nashangazwa na hizi juhudi za upimaji hazijaonekana sana katika taasisi za elimu hasa elimu ya juu. Huku kuna vijana lukuki na ingekuwa vyema hapa watu wapimwe manake ndio viongozi wa kesho tunaowatarajia na tukiwaacha ngono mbele kwa mbele basi tujue kuna mahali ambapo paangaliwe manake kwa muono wa karibu ni sehemu ambapo maambukizi yanawezekana kuwa kwa kasi sana.

Linalonishangaza sana ni kuwa Ukimwi umekuwa ni mradi mkubwa kwa baadhi ya watu flani na vitaasisi vyao vyenye utegemezi wa wafadhili. Ni wazi kuna watu wanafurahi sana ongezeko la wagonjwa wa ukimwi na hata yatima. Bila gonjwa hili watu wengi hawataajiriwa na wengine wangekuwa masikini kabisa. Najua siku hizi imani za kidini ni kiini macho kwa wengi kutokana na matendo yao. Ni kwa misingi hii vita ya gonjwa la Ukimwi inaonesha kama vile hakuna Mungu.

Ukimwi bado ni kiini macho kupambana nao kwani hadi leo bado watu wanaugua gonjwa hili lakini utasikia eti wamekufa kwa vigonjwa vingine ama wamelogwa na mambo mengine ambayo mtu mwenye akili inashangaza sana. Kuna haja mtu anaugua gonjwa hili awe tayari kusema nilikuwa naugua gonjwa hili bila aibu. Tunazika watu wengi hata wasomi kabisa ambao wakati wa kuugua anaonekana anaugua Ukimwi ila siku ya kufa utasikia eti anaumwa sijui kansa, presha na kadhalika. Ni usiri wa kijinga tunauendekeza na ambao hatima yake ni kiini macho cha vita ya ukimwi. Umefika wakati tuache usiri bila hivyo ni vifo bila mabadiliko.

Mwisho, nadhani kwa mwenendo wa sasa, “Tanzania bila Ukimwi” haitawezekana kama raisi wetu anavyotusihi. Usiri huu kwa kisingizio cha kuzuia unyanyapaa ni chanzo cha janga hili kuendelea. Siamini nchi yetu inaweza kuendelea, ni wazi gonjwa hili litaendelea kudumaza na kuwamaliza wasomi wa nchi yetu. Ni mwaka wa ishirini na saba tangu gonjwa hili livamie nchi yetu na bado watanzania wengi hawajaamua kuacha ngono zembe, ni mwanzo wa kiama Tanzania.

1 comment:

Anonymous said...

Asante kwa makala yako Tanzania bila ukimwi inawezekana, lakini muheshimiwa nadhani umepitiwa au haujazisoma haki za binadamu inavyotakiwa. CONFIDENTIALITY au usiri ni miongoni mwa nguzo za haki za binadamu.Haiwezekani kusema kusiwepo na usiri eti tu ndio sababu ya kupunguza UKIMWI utakuwa unakosea. Mi naamini tukifikia watu wa TANZANIA tukaelimishana juu ya umuhimu wa kuheshimu haki za binadamu kwa kufahamu kuwa nimuambukizapo mtu ukimwi kwa maksudi ni takuwa navunja haki za binadamu.Hili litaifanya TANZANIA BILA UKIMWI KUWEZEKANA.

Naomba tembelea blog hii utaona jinsi tunavopambana na UKIMWI kwa kuheshimu haki za binadamu.
http://kisili-ibrahim.blogspot.com