My Blog List

Tuesday, December 09, 2008

TAMASHA LA MARIALE CUP LAMALIZIKA MOSHI


Timu ya Kaloleni United ya Kata ya Kaloleni katika Manispaa ya Moshi ambayo iliibuka kidedea jana na kushinda kikombe na ng'ombe katika uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi bao 1-0 dhidi ya Langasani ya Moshi Vijijini.
Nahodha wa Kilimanjaro Queen akipokea kikombe kwa kushinda netiboli katika tamasha la Chifu Mariale
Afisa Tawala wa Wilaya ya Moshi Manispaa akimkabidhi Kikombe Nahodha wa Kaloleni baada ya kushinda bao 1-0 timu ya Langasani kutoka Moshi Vijijini.

Monday, December 08, 2008

MIAKA 47 YA UHURU TANZANIA

Huku tukiwa tumetimiza miaka arobaini na saba ya uhuru, Tanzania ni nchi ambayo inaweza kujivunia mafanikio mengi sana ikilinganishwa na nchi nyingine za kiafrika. Ziko nchi nyingi ambazo zilipata uhuru wake miaka arobaini na saba iliyopita kama Tanzania ambazo kwa sasa ziko hoi kabisa katika nyanja nyingi na pia ziko zingine zimetuacha kabisa. Leo ninaitizama Tanzania ikisherehekea uhuru wake kwa mashaka makubwa sana.
Kama Taifa, naamini tumefanikiwa sana katika kudumisha na kujenga jamii ambayo ni ya amani tangu enzi za awamu ya kwanza, shukrani za pekee zimwendee Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Ila tuna tatizo kubwa ambalo kama litafanyiwa kazi basi uhuru wetu utakuwa na maana kubwa kwa wananchi wengi kwa ujumla kuliko ilivyo sasa. Nasema hivi kwasababu nasikitika sana kuwa jamii ya kitanzania kwa kiasi kikubwa imepotea njia.

Tuna tatizo kuu la “Utawala Bora” ambapo tumeshindwa kabisa kuweza kuiongoza nchi yetu kwa misingi ya kuzingatia uwajibikaji, uwazi, uadilifu na weledi. Hasahasa bado hatujaweza kujenga utamaduni wa Serikali kufanya kazi kwa kuheshimu taasisi (Institutions) zake zifanye kazi bila kuingiliwa na bwana mkubwa. Tatizo hili utaliona kila sekta ya utawala katika nchi yetu na ndio kitu cha pekee ambacho naamini kabisa kama tungaliweza kukishinda basi Tanzania tunayoisherehekea leo hii ya miaka arobaini na saba ingekuwa na mandhari na mielekeo mingine na mizuri kuliko hii tunayodhani ndio mafanikio leo hii.

Kiini kikuu cha kushindwa huku kwa “Utawala Bora” ni mfumo wetu wa elimu naamini una matatizo. Kwa maana nyingine utekelezaji wa sera ya elimu nadhani una mapungufu kiutendaji. Nchi yetu kwa miaka hii arobaini na saba ya uhuru inajivunia idadi kubwa tu ya wasomi kuanzia diploma, shahada, uzamili hadi maprofesa. Ila tatizo ni kwamba wasomi hawa ni wav yeti kuliko matendo. Ukitizama kuongezeka kwa kashfa nyingi za ubadhirifu na za kifisadi zinahusisha watu mbalimbali ambao ni wasomi sana tu.

Mfumo wetu wa elimu kwa kiasi kikubwa unatoa aina ya wataalamu wasio na haiba ya kuzingatia weledi (professionalism) katika utendaji wao wa kazi. Matokeo yake wasomi wengi wanaona ni afadhali wawe wanasiasa kuliko kufanya kazi ambazo wamezisomea. Ndio maana leo hii bunge letu limejaa wasomi lukuki lakini ukitizama na kusikiliza wanapojenga hoja mbalimbali bungeni unagundua kabisa kuwa kuna tatizo la ukosefu wa haiba ya kuhoji (critical) miongoni mwa wabunge wengi. Kwa ujumla, elimu yetu imetuzalishia viongozi na watendaji ambao ni watumwa wa fedha, tumbo na anasa za kila aina. Wao nchi haina nafasi kubwa sana bali maslahi binafsi ndio jambo la msingi.

Uhuru wa miaka arobaini na saba umeshindwa kutupatia mafanikio yanayoendana na muda huo kwa viongozi na wananchi kwa ujumla kushindwa kuwa na haiba ama hulka ya “kuwajibika”. Watu hawataki kukosolewa kabisa, hasa viongozi watendaji mbalimbali wa serikali na wanasiasa wao ndio mwisho wa kila kitu. Kwao mtu akijaribu kuwakosoa basi ni ‘mpinzani’ na anatishwa kuwa atapelekwa mahakamani kwa kumchafulia bwana mkubwa jina. Na ndio maana naweza kusema kuwa kwa kweli uhuru huu wa miaka arobaini na saba kama tusipokuwa makini naufananisha na hali ya kurudi nyuma (retrogressive) tangu tupate uhuru badala ya kwenda mbele(progressive).

Wakati tunasherehekea uhuru ni wakati wa wananchi kwa ujumla wao kuja na mtizamo mpya juu ya maendeleo kama kweli tunataka maendeleo ya nchi na wala si ya mtu binafsi. Lazima nikiri kuwa elimu yetu si bora kwani kwa kiasi Fulani imeshindwa kumfanya anayeipata kuweza kumudu maisha kwa njia za kawaida. Ni dhahiri mafisadi wengi ni watu wenye elimu bora tu lakini wengi wao wameamua kutumia njia za mkato kupata utajiri wa haraka kwa mvuto wa ubinafsi.

Kwa mfano hii hali ya kuongezeka kwa migomo na maandamano hapa nchini siku za karibuni ni kielelezo tosha kuwa kizazi cha viongozi wa sasa bado wameshindwa kuitizama Tanzania katika mtizamo wa kileo na pia kupambana na changamoto za kiutawala za kileo ama kisasa. Matokeo yake bado wanakuwa wagumu sana kukubali mfumo wa demokrasia ufanye kazi inavyotakiwa. Wanahakikisha wanadhibiti vyombo vya habari kwa kila hali ili visiandike baadhi ya habari ambazo wanatumia kisingizi cha usalama wa Taifa. Baadhi ya watawala bado hawajui ama wameamua kutokujali kuwa mfumo wetu wa kisiasa ni wa vyama vingi. Kwao “Chama kushika hatamu bado ndio mawazo na fikra zao”.

Pamoja na udhaifu mkubwa wa mfumo mzima wa kisiasa ambao bado ni mzigo mkubwa wan chi yetu hasa kwa kukosa utashi wa dhati kutekeleza maneno ambayo tunaimbiwa lakini lazima pia tuwaatizame wafanyakazi ama watumishi wa umma. Kwa miaka arobaini na saba ya uhuru, ni dhahiri wafanyakazi wa serikali ni mzigo sana. Nathubutu kusema kuwa serikali ni jamvi la uoza wote wa wafanyakazi wengi ambao hawana kazi za kufanya bali wanapokea fedha tu za bure. Serikali imejaza wafanyakazi wenye elimu haba katika kada mbalimbali ambao kwao hata umuhimu wa kufuata taratibu haupo kabisa. Ndio maana hata mara nyingi tunapopiga kelele kuwa wanasiasa ni mafisadi huwa ninapiga picha wafanyakazi wa umma napatwa na kichaa.

Umefika wakati serikali kama kweli inataka tuingie karne ya sayansi na teknolojia kwa uhakika basi hakuna sababu kuwa na wafanyakazi wasiohitajika katika shughuli zake katika maofisi mbalimbali. Umefika wakati wafanyakazi wahakikiwe uwezo wao kielimu yaani vyeti vyao vya taaluma mbalimbali. Nasema hivi kwani ukienda ofisi mbalimbali utakutana na wafanyakazi wasiojali kazi, wasio na uelewa wa umuhimu wa huduma kwa wateja, wasiokuwa na weledi katika utendaji wao na pia wasiojali kutunza muda. Napendekeza kwa miaka hii arobaini na saba ya uhuru basi serikali iwaondoe watu wa aina hii.

Mwisho kabisa, nampongeza Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na serikali nzima katika kuadhimisha siku hii muhimu kwa Taifa letu. Naamini nchi yetu iko katika wakati mgumu hasa katika vita dhidi ya ufisadi. Bado siamini sana kama kweli kuna utashi wa kisiasa katika mashtaka machache ambayo yameanza kushughulikiwa ila niseme tu ni wakati wa kuamua kikwelikweli kwa Raisi Jakaya Kikwete kutowahurumia baadhi ya maswahiba wake kama kweli anataka kusafisha nchi hii. Ni kwa mantiki hiyo tu ndio atakapoweza kunitoa mashaka pamoja na wengine ambao ni kama mimi.

Mungu Ibariki Tanzania.