My Blog List

Friday, August 22, 2008

VITA YA UKIMWI UGANDA YASHINDIKANA

Uganda ile nchi iliyokuwa inasifiwa vizuri kuwa ndio bingwa wa kudhibiti Ukimwi nayo imeshindwa vita hii.

Thursday, August 21, 2008

KIKWETE AHUTUBIA BUNGE

Hatimaye Kikwete kahutubia Bunge na kama ilivyotarajiwa na wengi wanaomfahamu, hakuna la maana aliloteta sana ukiacha machache.

Tuesday, August 19, 2008

MWANAWASA HATUNAYE DUNIANI

Rais wa Zambia, Levy Mwanawasa amefariki dunia.
Kifo hiki nilikitarajia tangu jana usiku.

Sunday, August 10, 2008

CHACHA WANGWE LABDA HAKUFAA KUWA MWANASIASA

CHACHA WANGWE HAKUFAA KUWA MWANASIASA

Mara baada ya mazishi ya mbunge wa Tarime kufanyika, nimejiuliza mambo mengi sana kuhusu jamii ya kitanzania. Yaliyotokea Tarime kwa hali ya kawaida yamenifanya nishindwe kujua hivi kweli mtu anaweza kufa alafu wafiwa waamue kuwa mazishi yasifanyike dakika za mwisho? Sina hakika kama hali imewahi kutokea Tanzania hasa kwa watu waheshimiwa kama mbunge. Ila nadhani umefika wakati tuutizame kwa kina mfumo mzima wa uendeshaji wa siasa zetu.

Nimesema hivyo kwani naamini kabisa hisia za mbunge Chacha Wangwe kuuawa zilijitokeza kwa sababu kuna mazingira yanayoonesha kwa sasa jamii ya kitanzania haina imani na mfumo mzima wa uendeshaji siasa. Hii inaweza kujidhihirisha kama ifuatavyo:
Kwanza, kupitia vyombo vya habari vyote viliiripoti habari ya kuwa Chacha aliuawa kwa kushabikia hasa. Hali hii inaonesha ni jinsi gani Tanzania ya leo baadhi ya viongozi wanapokufa basi moja kwa moja kuna kuwa na hisia za kifo cha kupangwa. Tumshukuru rais Kikwete kwa ulegezaji wa sheria za kubana uhuru wa magazeti na vyombo vya habari kwa ujumla, hii inatupa wasaa mzuri kupima na kujua nini hisia za watanzania juu ya matukio mbalimbali nchini Tanzania.

Pili, wanatarime na hasa wanafamilia ya Chacha Wangwe waliamua kwa dhati kabisa kutia shaka kifo kile. Sijui walitaka Chacha afe vipi ama labda walikuwa wanajua kuwa Chacha atakufa je, ila napata mashaka sana kama watanzania tumeamua kuishi kwa kuamini kila jambo lina mchezo mchafu. Kwa maana nyingine nchi yetu imegeuzwa jamvi la wapiga ramli ama watu wasioaminiana kwa jambo lolote. Hila ndio umebaki mchezo pekee katika masuala ya kisiasa.

Tatu, tujiulize alipokufa Amina Chifupa (RIP) yalisemwa mengi na hata baadhi ya wakubwa fulani walihusishwa na kifo kile. Mwisho wa siku mtu alikufa na mpaka leo kifo kile kimebaki na maswali mengi kwa watu wenye akili timamu. Matukio kama haya ya vifo vya viongozi wa kijamii katika utata yanalidhalilisha bunge letu sana na hata jamii nzima ya Tanzania. Inapofikia mahali jamii kwa kiasi kikubwa inapoteza imani na serikali na hata chombo chake kama bunge basi ujue kuna kila dalili za mpasuko.

Kwa upande mwingine, kifo cha Mbunge Chacha kimenifanya nijiulize hivi inakuwaje Mbunge anasafiri safari ya usiku tena na rafiki yake na wala si dereva. Na hata kama itathibitika yule Bwana aliyesafiri naye alikuwa dereva, inakuwaje mbunge aendeshwe na dereva asiyekuwa na sifa kama vile leseni ya udereva. Hii inanipa taabu sana ya umakini wa viongozi wetu. Hebu nikumbushe kuwa Mh. Mudhihir Mudhihir alipata ajali wala hakuwa na dereva; Mh. Kapuya alipata ajali akiwa na dereva, lakini mazingira ya ajali dhahiri yanaonesha ilikuwa kwasababu ya mwendo kasi wa dereva na labda dereva kutozingatia uendeshaji salama wa gari katika barabara ambayo nina hakika hakuwa ameizoea. Ni katika mazingira haya mtu mwenye akili timamu najiuliza : hivi kweli hizi ajira za kuendesha viongozi wetu zinafuata weledi wa dereva ama ni haya masuala ya kuendeshwa na marafiki ama ndugu tu kama alivyokuwa marehemu Wangwe?

Jambo lingine ambalo nadhani kifo cha Wangwe kimetuachia kulidurusu ni juu ya muundo wa vyama vya siasa Tanzania. Inasemwa kuwa aliwahi kutuhumu kuwa Chadema ni chama cha wachaga. Nimeshuhudia mheshimiwa Zitto Kabwe akijitutumua na kuwalaumu wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari kwa kuripoti vibaya juu ya vitisho alivyofanyiwa mwenyekiti wa Chadema kule Tarime. Anafananisha uandishi ule kama ule wa Rwanda ambao ulichangia kwa mauaji ya kimbari kwa kusema kuwa wachaga kule Mara sasa wanatishwa.

Kuna kitu ningependa Mheshimiwa Zitto na wapenda demokrasia wajiulize kwa kina: Nacho ni hivi kauli ile ya Chacha ilikuwa na ukweli wowote? Nilipomsikia Wangwe akidai kuwa ni chama cha wachaga sikupata taabu kabisa. Nilimwelewa akimaanisha kuwa ile safu ya uongozi ya juu kabisa, safu ya wadhamini wa chama ndicho alichokuwa analenga. Nani anaweza kubisha kwa muundo wa vyama vya siasa hapa Afrika tangu mageuzi yaanzishwe vimeegemea kwenye nguvu ya kiuchumi ya ama mtu mmoja au kikundi cha watu ambao ndio wenye ushawishi katika Chama? Hili lipo karibu kila nchi ya Afrika kwa mfano: Uganda, NRM ilianzishwa na watu wa magharibi ya Uganda alikozaliwa Museveni. PNU ya Kibaki kule Kenya imeegemea zaidi kabila la Wakikuyu ambako Kibaki katokea. Hapa Tanzania mambo ni hay ohayo, hebu tizama chama kama UDP iko chini ya John Cheyo na yeye ndie mshika dau mkuu pamoja na ukoo wa Cheyo.

Ni katika hali kama hii ambapo nadhani kwa mwanademokrasia wa dhati kama marehemu Wangwe asingeweza kuwa ndani ya Chadema ambacho mhimili wake mkuu ni watu wa kabila la mwenyekiti . Na hata uongozi wa Chadema nani asiyejua kwa mfano wabunge wa kuteuliwa wengi wao ni wa kabila moja na ama wamepata nafasi hizo kwa kigezo cha urafiki ama undugu na baadhi ya wadhamini wa chama? Isitoshe, wabunge baadhi wa kuteuliwa ni ndugu wa karibu wa baadhi ya wadhamini? Ni katika mtizamo huu ambapo ninaamini marehemu Wangwe alikosea mwenyewe kutambua juu ya mifumo ya uundaji wa vyama vya siasa. Nani atakayebisha kuwa kama hao wote ambao Wangwe aliwatuhumu kabla ya kusimamishwa kuwa ni wa kabila fulani ndio mhimili wa Chama? Na kama wakiamua waondoke katika chama hicho na wamwachie marehemu akiendeshe basi chama kitayumba?

Wazungu wana msemo “to go too far” yaani kwenda mbali zaidi. Kwa marehemu Chacha kutuhumu Chama ni cha Kabila fulani ilikuwa sio hatua muafaka kufanywa na mbunge kama yeye ingawa alilotetea ni la ukweli. Matokeo yake Chama kimepatwa na mitikisiko ambayo kwa vyovyote vile kama marehemu Chacha angetafakari kwa kina, nadhani hata kifo chake kisingehusishwa na Chadema. Mara nyingine binadamu ana kasumba tofauti lakini kwa wale wote wenye tabia na kasumba za akina Wangwe; yaani misimamo thabiti isiyoyumbishwa kwa hali yeyote ile inakuwa vigumu sana kuelewana na watu wengi. Watu kama akina Wangwe hawafai kuwa wanasiasa kwani siasa ni mchezo uliojaa unafiki. Na Wangwe na jamii ya watu kama yeye si wanafiki sasa inakuwa taabu sana kuweza kuhimili mizengwe ya kisiasa. Kama Wangwe angekuwa mwanasiasa nina hakika kabisa asingeliwahi kuzua mambo ambayo yalipelekea kusimamishwa uongozi.

Katika hali kama niliyoielezea nadhani tatizo la vyama vyetu ni la kimfumo tulioamua kujiwekea wenyewe ambapo demokrasia ya kweli kwa maana ya kutoa maoni yako mbele ya viongozi wako hayaruhusiwi na yanaonekana ni dharau. Mpaka hapo tutakapoamua kuendesha vyama vya siasa ambavyo havitegemei ruzuku kutoka kwa wenye chama kama kikundi basi tujue migogoro ya aina ya Chacha itaendelea. Ni katika hali hiyo basi umefika wakati tujitizame kama jamii ya watanzania makini na tuamue kuwa na kanuni za kuendesha siasa ambazo zitawekwa kama sheria. Hii itasaidia sana kuwa na vyama kwa maslahi ya nchi na wala si chombo cha kutetea maslahi ya wananchi kijujuu huku wakati huo huo vyama vya siasa vikitumika kama vyombo ama nyenzo za kusaidia ndugu na jamaa ya viongozi kujipatia maslahi ya kazi na maisha yao.

Na tunapokuwa na vyama hivi tulivyonavyo leo hii basi watu wote wa aina ya Wangwe kamwe hawataweza kuishi bila kukumbana na mikasa ya kusimamishwa, kufukuzwa na hata kuonywa mara kwa mara. Si hayo tu, pia kwa zile nchi zenye udikteta watu wa aina hii huuawa ( elimination) ili kuwaondoa katika uso wa kisiasa wa nchi husika. Na ndio maana hadi leo kuna watu wamefariki na kuacha maswali bila majibu. Hawa ni kama vile: Horace Kolimba, Imran Kombe, Amina Chifupa, Ipyana Malecela kwa hapa Tanzania na akina Litvnenko kule Russia, Robert Ouko kule Kenya na wengine wengi ambao wamekufa na watu wakawa na hisia wemeuawa bila kuwa na ushahidi wa dhati kabisa.

Mwisho, binafsi ninaamini kabisa kuwa Wangwe amekufa na baada ya kushindwa kuthibitisha risasi ilitumika basi ni wakati wa kukubali kuwa ilikuwa kazi ya Mungu kwani pamoja na maadui wengi aliokuwa nao bado tumeshindwa kuthibitisha. Lililo mbele yetu ni kuwa umefika wakati kuhakikisha tunaimarisha taasisi za mfumo wa kisiasa Tanzania hasa jinsi gani vyama vya siasa vinapaswa kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia misingi ya demokrasia ya kweli bila kuweka uzandiki. Tukishindwa haya basi tujue kuwa kila mwaka hasa wakati wa bajeti tutarajie mbunge fulani mwenye misimamo isiyoyumba atatutoka hapa duniani katika mazingira tata ambayo mara nyingi tutashindwa kuthibitisha kama kweli ni kazi ya Mungu.