My Blog List

Friday, August 04, 2006

YALIYONIVUTIA LEO

Wakati bado timu yetu haijaanza maandallizi ya kwenda huko Ghana mwaka 2008, Uganda tayari kocha waao kaanza mambo. Tunaambiwa hata sex inataka maadili fulani yazingatiwe, unazijua?
Kuhusu politiki ni kuwa Museveni kaishiwa hana hela, rushwa imezidi na sasa chama tawala kinabidi kifunge shughuli katika ngazi za chini. Athari za Chama dola ndio hizi. Nikiwa kama bachela mzoefu basi mambo ya mapishi ni vyema niyapitie.
Angalia ukubwa wa Afrika ulivyo, hapa rais anapopita anaweza akasababisha hata mauaji.Alafu ligi ya Uingereza ndio inakaribia.
Kama unamjua Joseph Kony pata undani wa maisha yake ya sasa. Je ilikuwaje Mapinduzi yakatokea Uganda?

Saturday, July 15, 2006

SALA KUONDOA RUSHWA?

Kweli sala na mafungo ndio dawa ya Rushwa?Pia mambo ya imani yapo kweli?Na siasa mwanzo wake je?
Mpira huu ni mwaka wa Chelsea tena?Je kashfa kubwa mpirani?

Friday, July 14, 2006

KONY ATAELEWEKA?

Mambo ya Kony?

UGANDA KUNASEMAJE?

Baada ya kimya kirefu leo niangaze yanayojiri nchini Uganda: kuna huyu bwana anatuhumiwa kuuwa mkewe. Katika kesi yake anaonekana kujiamini sana kitu kinachowashangaza wengi. Alafu kama ilivyo kawaida, siku hizi tunawaza pesa tu haswa wengi wetu. Matokeo yake hata kazi zetu kwa mfano wachapishaji wa magazeti maadili ya kazi yameshuka sana. Pia nchi ya Uganda inatamani kuwa na mafuta lakini inakumbushwa kuwa hiyo ni balaa kwa Afrika na ni hatari kwa demokrasia.
Baada ya kombe la dunia hebu tujue ni nini kinasemwa pia kuhusu kosa la Zidane? Alafu kuna Padri wa Kikatoliki uzalendo umemshinda na kaamua kuvunja sheriia za useja. Pia tunakumbushwa juu ya ongezeko la ugonjwa wa moyo. Nini kifanyike?
Mwisho vipi kuhusu Kony?

Thursday, June 08, 2006

VIROJA KATIKA VIAPO UGANDA

Hebu ona jinsi mawaziri wapya walivyoonesha manjonjo wakati wakiapishwa wiki iliyopita.Pia unaweza ukasoma uswahiba kati ya mmojawapo wa mawaziri walioteuliwa na Museveni hivi majuzi.

Wednesday, May 24, 2006

BARAZA LA MAWAZIRI LA MUSEVENI HILO!

Hatimaye Rais Museveni kachagua baraza la mawaziri na kama ilivyotarajiwa kamchagua mdogo wake ambaye ni ofisa wa jeshi aliyeishia kidato cha sita kuwa waziri wa fedha. Huko nyuma Museveni aliwahi kumtimua kazini kwa kisingizio cha ulevi kupindukia.
Mambo ya ufalme labda ndiyo yanaanza hebu tusubiri. Maajabu ni huyu Eliya Kategaya ambaye alimpinga sana juu ya kung'ang'ania madaraka sasa kawa waziri.
Yamesemwa mengi juu ya sababu za uteuzi wa mawaziri mbalimbali. Pia kama kawaida ya Uganda, uongozi umekwenda kwa watu wa mashariki, yaani kule alikozaliwa Museveni. Hata jamaa mmoja kadai eti anaota mji mkuu wa Uganda ukahamia "RWAKITURA" kijijini kwa Museveni siku chache zijazo.
Mawaziri ni wapya wengi na hasa vijana.

Monday, May 22, 2006

Thursday, May 18, 2006

MARAISI "SUPA GLUU"-AFRIKA

Kuna malalamishi ambayo yanafurahisha juu ya hatua ya marais wa Afrika kuunga mkono wenzao wanaong'ang'ania madaraka.
Mwandishi mmoja kalaani ni kwa nini hata JK wetu alihudhuria kuapishwa kwa Museveni?
Alafu Obasanjo alifika Uganda baada ya Museveni kuapishwa inasemekana alikuja kumfunza Museveni jinsi ya kutawala ukiwa haupendwi. Demokrasia bado inaendelea kuchezewa hapa na Museveni kwani sasa hivi yuko tayari kutumia hela za walipa kodi kumfunga mpinzani wake.

MARAISI "SUPA GLUU"-AFRIKA

Kuna malalamishi ambayo yanafurahisha juu ya hatua ya marais wa Afrika kuunga mkono wenzao wanaong'ang'ania madaraka.
Mwandishi mmoja kalaani ni kwa nini hata JK wetu alihudhuria kuapishwa kwa Museveni?
Alafu Obasanjo alifika Uganda baada ya Museveni kuapishwa inasemekana alikuja kumfunza Museveni jinsi ya kutawala ukiwa haupendwi. Demokrasia bado inaendelea kuchezewa hapa na Museveni kwani sasa hivi yuko tayari kutumia hela za walipa kodi kumfunga mpinzani wake.

Saturday, May 13, 2006

IGIZO LA KIAPO CHA MFALME MUSEVENI WA UGANDA

Kama ilivyotarajiwa jana Rais Kaguta Museveni aliapishwa na jaji mkuu kwa mara nyingine kuendelea na ngwe nyingine ya miaka mitano katika viwanja vya Kololo jijini Kampala. Ametoa rai kwa vyama vya upinzani viwe makini ili kuweza kushirikiana naye.
Pia alipata wasaa wa kuelezea mipango ya baadaye na hata mafanikio aliyoyapata kwa miaka ishirini iliyopita.Katika sherehe za jana vyama vya upinzani hasa vile vyenye wafuasi wengi havikuhudhuria katika kile kinachoonekana kama kutomkubali Museveni kama rais halali. Pamoja na kung'ang'ania madaraka kwa Museveni lakini huwezi kuamini hadi leo ni miaka miwili Uganda ina mgao wa Umeme usiokwisha na watu wanaanza kumlalamikia sana.
Mwanzoni kabla ya kula kiapo ilisemekana hata rais Hu Jintao wa China angehudhuria katika kile kinachodaiwa kama mkakati mpya wa Museveni katika kujikita katika siasa za nchi za ukanmda wa maziwa makuu.

Sunday, May 07, 2006

J 2 YA LEO

Kama kawaida kila jumapili ninaangaza magazeti ya hapa Uganda na kwingineko. Kwa akina mama wajawazito ipo makala ya jinsi ya kujipendezesha. Alafu kuna hili la mameneja wa kiume kuongoza kwa kuwachukulia wafanyakazi wao kama wanawake.

Saturday, May 06, 2006

WAGOMBEA BINAFSI WAJA

Kwa mara nyingine mahakama nchini Tanzania imeruhusu wagombea binafsi. Huu ni ushindi wa demokrasia lakini sina hakika kama una mantiki yeyote ukizingatia demokrasia yetu changa.
Wengi wamefurahia ila ni lazima turuhusu muda tuone kwani hata nchini Uganda katika uchaguzi uliokwisha hivi majuzi pia wamechaguliwa wagombea binafsi.

Friday, May 05, 2006

HAKUNA MABADILIKO?

Kweli ukoloni unatumaliza au ni porojo tu?

UNAMJUA RAIS AJAYE WA UGANDA?

Huku Uganda ikiwa inasubiri kwa hamu kuapishwa kwa Rais wa Maisha, Yoweri Kaguta Museveni hapo wiki ijayo ni wazi mtu huyu hapendwi ila king'ang'anizi tu.
Naona ni hivyo kwani kwa sasa hadithi kubwa ni juu ya nani atamrithi Museveni atakapoamua kung'atuka. Wako wengi ila huyu waziri wa ulinzi ndiye anayeonekana atakuwa rais ajaye wa Uganda.
Si haya tu ya kumrithi ila inaonekana bado serikali ya Museveni inatumia kila mbinu hata zile chafu kabisa kumtia hatiani mpinzani wake Kiiza Besigye. Hapo jana serikali iliamua kumleta mahakamani mmoja wa makamanda wa jeshi la waasi wa LRA kuja kutoa ushahidi. Nakwambia hii inaonekana ni hatua ya ajabu kabisa. Kwani hapa hata serikali inatumia wauaji ili kumtia hatiani bwana Besigye. Mawakili hawakuwa tayari kuendelea na kesi na wanataka kwanza shahidi asimamishwe juu ya koti ili ajibu mashtaka ya mauaji na ugaidi. Hali hii inafanya wanazuoni kuhoji labda hii vita ya waasi wa LRA haishi kwani kuna mkono wa serikali. Kuwatumia waasi kutoa ushahidi mahakamani kunachukuliwa kama dhihirisho la kuwepo na uhusiano kati ya serikali na waasi kwa kiasi fulani. Mwenyewe Rais Museveni hivi karibuni kazungumza kinagaubaga juu ya mzozo huu wa miaka ishirini.
Ni wazi ingawa Museveni alishinda uchaguzi majuzi, kwasasa ana kazi kubwa kuunda serikali yenye mvuto. Sasa ameanza kuwashawishi baadhi ya wanasiasa waliokuwa naye wakati akipambana msituni ambao walimkimbia na wengine aliwafukuza pale, walipopinga kampeni yake maarufu kama "EKISANJA" ya kubadili katiba ili aendelee kuwa rais wa maisha, anataka wajiunge serikali mpya atakayounda baada ya kuapishwa wiki ijayo.
Familia nzima ya Museveni sasa imeamua kujikita kwenye siasa za nchi hii kiasi kwamba kuna kila dalili hapa ni mambo ya kurithishana yatafuata pale Museveni atakapokuwa amemaliza muda wake. Kwa mfano, hata mwanaye wa kiume Museveni, ambaye afisa wa jeshi la hapa sasa kaanza kuandika makala za kisiasa hasa akiunga mkono shirikisho la Afrika Mashariki, kitu ambacho kinapigiwa upatu sana na Museveni.

Sunday, April 30, 2006

SHERIA DHIDI YA WABAKAJI YAKWAMA-KENYA

Wiki iliyopita mbunge mmoja mwanamama aliamua kupeleka muswaada bungeni ili kudhibiti ubakaji nchini humo. Matokeo yake inaonekana kagonga mwamba manake wabunge wanaume wamekuja juu na inasemekana muswaada hautapitishwa kuwa sheria.
Mwanamama mmoja kasema hii ni sababu za umangimeza wa wanaume wa Afrika. Ila kuna sababu imetolewa ni kwanini Wabunge waliamua kuzichachamalia hoja mbalimbali ndani ya muswaada huo. Vifungu mbalimbali vya muswaada huo vilikuwa na utata. Mkwamo huu dhidi ya kuwaadhibu wabakaji kwa kiasi kikubwa unachangiwa na kutobadilika kwa jamii nyingi za kiafrika hususan nchini Kenya ambapo wengine wanaamini hawawezi kuishi bila kufuata mila zenye kukandamiza wanawake kwani mababu wa zamani watachukia.

URAFIKI WA TZ NA CHINA UMEFIFIA?

Mambo yamebadilika dunia ya leo. Sijui kama kuna umuhimu sana kwa Tanzania kutembelewa na kiongozi wa China ila niseme tu ziara ya rais Hu Jintao huko Nigeria na katika kituo chake cha mwisho nchini Kenya imenifanya niwaze vipi, kulikoni Tanzania.
Si tulikuwa washirika wakubwa sana wa China wakati wa Mwenyekiti Mao?Jibu nimelipata eti mwelekeo umebadilika duniani na China ya ujamaa sio hii ya leo. Zipo sababu kwanini China ni mshirika mzuri kwa nchi kama Kenya.
Kwa Wachina ziara ya hii Hu sehemu mbalimbali ni muhimu sana na hatuna haja ya kusikiliza kelele za Magharibi. Unajua kwa mfano sekta ya mafuta barani Afrika ambayo ilitawaliwa na magharibi sasa China nayo imeamua kuingia kwa nguvu hasa barani Afrika.

LEO MAGAZETINI

Leo kuna mambo ya lugha yameandikwa jinsi jamii ilivyogawanyika na kama mtu hauko makini unaweza shindwa muelewa mwenzako katika mazungumzo. Alafu Madaraka Nyerere anatukumbusha juu ya hii dhahama ya silaha za nyuklia kati ya Marekani na Iran na anasema kuwa na silaha hizi ni sababu ya kupunguza mizozo duniani. Mwanazuoni Ali Mazrui anatukumbusha jinsi ilivyo vigumu kwa nchi za Afrika kuungana. Ugomu ambao umejionesha pia katika muungano wa Tanzania ni dalili ya ugumu wa kuunganisha bara la Afrika ukiachilia mbali hii gumzo ya kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki ambapo mwandishi mmoja kaonya nini labda kifanyike ili kufikia mafanikio.
Hapa Uganda tatizo ni umeme hakuna na hakuna mtu anayejali. Ila inasemekana ziko sababu kwanini kwa waganda hili sio tatizo la kulalamikiwa. Si umeme tu ila Uganda ina mambo kwelikweli: kwa mfano, Uganda inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa nchi za jumuiya ya Madola mwakani ambapo Malkia wa Uingereza atakuwa ndio mgeni mkubwa kabisa. La kushangaza kuna juhudi kubwa za baadhi ya Wapinzani za kupinga mkutano huo kufanyika hapa kabisa. Ila yuko Bibie mmoja kaandika labda ni nini kinagaubaga juu ya hili.
Mwisho ni hili la hiki kitabu Da Vince Code, mengi ya msingi yameandikwa juu ya ubishi ambao umegubika toleo hili. Pia tunaulizwa hivi ni kwanini tunasoma?

Friday, April 28, 2006

JOJI KICHAKA MAMBO MRAMA?

Leo nimesoma blog moja kutoka huko Amerika kwa Joji Kichaka. Kwa mfano hata hili shirika la ujasusi, CIA, mambo si shwari kwani Joji Kichaka kamfuta kazi bosi wa shirika hilo. Halafu hali ya mzozo wa silaha za nyuklia na Iran ndio inafanya mambo yawe magumu kwa Kichaka.

Tuesday, April 25, 2006

Ile sheria kandamizi-TAKRIMA-dhidi ya makabwera imefutiliwa mbali na mahakama ya katiba nchini Tanzania. Sijui watu kama Fredrick Sumaye na Andrew Chenge watakuwa na mawazo gani. Unajua nilifuatilia hotuba zao bungeni wakati wa kuundwa sheria hii nikachukizwa sana na maoni yao.
La msingi nimefurahi sana kwani angalau maana ya demokrasia inajionesha. Kuna utafiti nimefanya kuhusu hali ya kisiasa ya jimbo la Vunjo kule Moshi Tanzania ninatarajia kuuweka mtandaoni siku chache zijazo na pia nimejadili madhara ya sheria hii.

TFF NA SOKA LA TANZANIA USINGIZINI.

Wakati bado TFF haijampata kocha wa kuinoa timu ya Taifa-Taifa Stars-hapa Uganda viongozi wapya wa shirikisho la soka hapa Uganda-FUFA- tayari wamemleta mwalimu mpya wa timu hiyo kutoka Serbia. Kocha huyo ni Tomislav Sicic kutoka Serbia.
Viongozi wapya wa FUFA wameingia madarakani mapema mwaka huu tu na tayari wanafikiria juu ya safari ya timu hiyo ya Kombe la dunia na lile la Mataifa ya Africa.
Kama tunavyojua TFF walishaadiwa ushirikiano na Rais JK. Nataka tuwaulize hawa mabwana mbona wamelala? September si mbali wajameni. Nataka niangalie hii mikakati Tenga anayodai ipo je itafanikiwa?
Si soka tu ila Tanzania chini ya JK ni lazima ichukue hatua madhubuti ili kuendeleza michezo. Mimi ninaamini kama tutaendeleza michezo basi tutawainua vijana wengi ambao hawana ajira na hawatakaa waipate kutokana na fursa chache. Ninaunga mkono juhudi za serikali kufanikisha ziara ya timu ya ndondi wiki hii kwenda nchini Uhispania.
Hii ifanyike pia kwenye soka kwani ikiwa kombe la dunia litafanyika hapa Afrika hatuna budi tuanze leo kama wenzetu wa Uganda. Hainifurahishi kwa viongozi wa TFF kutuambia eti timu inakwenda Ushelisheli kwa mechi za kirafiki baada ya kualikwa huko. Pia eti Malawi imetualika kwa michezo ya kirafiki. Nasema hivi kwani inaonesha kwamba labda TFF hawana mipango madhubuti ila wanasubiri mialiko na kama isipokuja itakuwaje? Pia nataka nitoe rai ya makocha wazalendo hawakidhi haja ni muhimu tukawa na makocha kutoka Ulaya kwani tunahitaji mambo ambayo watanzania wenzangu hawana katika suala zima la kuiandaa timu ya Taifa. Kwa mfano, nina hakika kwa aina ya makocha tulionao nchini Tanzania si makini sana kwenye masuala ya kudhibiti wachezaji kinidhamu. Nidhamu ni msingi wa wachezaji kutekeleza wajibu wao na kama wachezaji wetu hawakai kambini na kufuata taratibu za kambi tusitarajie kufuzu kwenda Ghana au Afrika kusini 2010. Tayari hata katibu mkuu wa TFF, Tenga kakiri wachezaji wa Stars ni kama "chokaraa". Sijafurahishwa kabisa na hali ya sasa ambapo inabidi Tenga awakumbushe makocha akina Msola juu ya kutoa ruhusa. Hivi kweli tuna makocha wenye taaluma ya kutosha kuongoza timu ya Taifa? Jibu ni hatuna, hebu tujaribu kufuatilia timu kadhaa zitakapoanza kupiga kambi kwa ajili ya kombe la dunia kama utakuwa unasikia mchezaji kaomba ruhusa eti akachukue begi lake nyumbani kama wachezaji wetu wanavyofanya.
Alafu ni lazima tucheze na wapinzani wenye kutumia staili ya uchezaji kama ya wale tunaotarajia kukutana nao.Nionavyo mimi hii TFF bado ni kama FAT ya akina Rage na Ndolanga kwani bado sioni mabadiliko yenye kasi na ari mpya.

Sunday, April 23, 2006

RUBANI MLEVI--CHANZO CHA AJALI KENYA

Wajameni eti ile ajali ya ndege kule Kenya siku chache zilizopita ilisababishwa na ulevi wa rubani. Hii inaonesha ni jinsi gani sisi waafrika siku hizi hatujali nidhamu ya kazi. Inawezekanaje rubani mlevi aruhusiwe kupanda ndege?

HABARI ZA JUMAPILI YA LEO

Kila jumapili napata wasaa wa kupitia magazeti mbalimbali na kuangalia kuna nini cha maana. Leo nimeona mengi: moja, kuna hili la wabunge kupenda kulipwa mishahara mikubwa, mwandishi mmoja katuhusia kuwa hili ni janga kwa mataifa ya kiafrika kama Kenya. Nafikiri pia hata kwa Tanzania makala hii itakuwa ina maana.
Pili pia kutoka Kenya, mara baada ya ajali ya ndege ambayo iliyamaliza maisha ya wabunge kadhaa wiki mbili zilizopita, mara Rais Kibaki anatangaza siku maalum ya maombi kwa Taifa.Mwandishi anatuhabarisha zaidi kunani mpaka maombi kwenye mambo ya kiserikali? Alafu kama ulinifuatilia wiki iliyopita niligusia juu ya ile Injili mpya ya Yuda Iscariot, yule anayedaiwa kuwa alimuuza Yesu kristu kwa fedha.Mwandishi anatuambia hata mapadri wamebaki kimya juu ya hili kama kweli Yuda ni msaliti au shujaa.
Alafu lililonifurahisha kabisa ni hii ziara ya Rais wa China huko Marekani na hasa juu ya nishati ya Nuklia ambayo inasemekana China ni mshikadau anayepaswa kuzingatiwa. Nafikiri ukisoma makala hii ni muhimu; utaelewa haya mambo ya mashindano ya silaha hizi kwa undani.
Kuna pia hili la maraisi wa Afrika kutaka kugombea urais zaidi ya kipindi kilichowekewa ukomo ili kukaa madarakani mpaka kifo.Iko habari moja huko Marekani, jamaa wanajiuliza vipi tena hivi hata kama hujawahi kuwa Raisi pia kuna ukomo wa kugombea.Jamani simnajua watu kama akina Mrema na Lipumba na akina Maalim Seif wataendelea kugombea sijui mpaka lini.
Hapa Uganda, inasemekana vyama vya upinzani vimeshindwa kutekeleza yale ambayo vinapaswa kufanya. Hali hapa si tofauti sana na upinzani wa kule Tanzania.
Mwisho kabisa nimeshangazwa kiasi fulani eti vijana wengi wa Kimarekani hawana habari na mambo ya msingi ya serikali yao. Hii imenifanya nivute pumzi na kuangalia huku kwetu na kwa kiasi fulani hata kwetu Tanzania na hata hapa hali ni moja tu.

Sunday, April 16, 2006

NI PASAKA-ETI YUDA HAKUMSALITI YESU?

Nimepitia habari leo jumapili ya pasaka nikakunwa kuhifadhi haya: Moja Eti Yuda Eskarioti, yule mtume wa Yesu inasemekana ni shujaa na hakuna haja sisi waumini kumfikiria kama msaliti.bonyezahapa Eti inasemekana kuna injili ya Yuda ambayo kanisa limeikataa ambayo inaeleza kinagaubaga juu ya hili. Papa Benedict tayari ameikana ripoti iliyotolewa hivi karibuni juu ya injili ya Yuda. Nakwambia haya mambo mtu unaweza usiwe muumini wa dini yoyote. Sijui wanaglobu mnasemaje, mmeshafikiria hili? bonyeza hapa
Pia nikamsoma Papa Benedict-16 ana ujumbe gani leo hii. Ameushangaza umma kwa kubadilika kama kinyonga kinyume na alivyodhaniwa atakuwa Papa Ngangari.bonyeza
Pili, kuna huyu mtoto wa Mwalimu Nyerere, basi nikaamua nimsome nijue anaandika juu ya nini unajua inawezekana ana falsafa za baba yake. bonyezahapa
Alafu nikakunwa na umuhimu wa kuheshimu na kuilewa demokrasia, mwanamama mmoja kaandika kweli hapa Uganda. bonyeza

TUNAHITAJI SHIRIKISHO LA AFRIKA MASHARIKI?

Jumuiya ya Afrika Mashariki imeingia katika hatua ya kuwa shirikishio. Ili kujua ni nini kinatarajiwa kufanyika, bonyezahapa ili umsome mwanamama ambaye atatuletea shirikisho. Pia kuna machache aliyoyasema Katibu mkuu wa jumuiya Bw Mushega wakati akiaga ili kuhitimisha muhula wake. Amemponda sana Bw Njonjo, waziri wa zamani wa Kenya kwa kuiponda jumuiya.Hebu soma mahojiano kamili ya mwanadiplomasia huyo aliyemaliza muda wake.Pia kuna ripoti maalum ambayo itatolewa hivi karibuni juu ya kama kweli hii jumuiya inawezekana.Hapa nataka tusome taarifa tangulizi ya ripoti hiyo.
Mimi sio muungaji mkono sana Shirikisho ila tu jumuiya manake najua ni ndoto. Hata JK bado anaweka msisitizo zaidi kwenye SADC. Ila kwa baadhi ya wananchi wana wasiwasi juu ya hizi nchi za Rwanda na Burundi kwani zitatuletea balaa.

Friday, April 14, 2006

TANZANIA KUWA BORA KULIKO UGHAIBUNI--JK.

Unajua mara nyingi nikisoma anayosema JK kila anapopewa nafasi huwa ninacheka alafu ninajaribu kufikiri hivi kweli itawezekana?
Leo anaripotiwa eti ataondoa ile kasumba ya wasomi kukimbilia ughaibuni.somahapa
Haya hebu ngoja tuishi kwa matumaini manake huyu jamaa anafurahisha sana. Ila nimefurahishwa na makala moja hapa Uganda juu ya tatizo la utegemezi wetu waafrika huko ughaibuni.Nimeona ni vizuri tulinganishe yaliyojadiliwa hapa na hayo JK anayosema alafu tuamue je kweli JK ataweza kuboresha na kuzuia tamaa ya kwenda Ughaibuni?somahapa

Sunday, April 09, 2006

MTANZANIA KASHIKWA UGONI HOTELINI NA MWANABALOZI

Ni wiki moja sasa ambapo mwanadiplomasia mmoja wa Rwanda alizusha sekeseke kama sio kasheshe pale alipokamatwa ndani ya hoteli moja ya kitalii akijinjiri na mwanamama mmoja ambaye ni mke wa mtu. somahapa
Mengi yamesemwa ila pia kumekuwa na utata juu ya kukamatwa kwa mwanadiplomasia anavunja sheria za nchi ikimaanisha ni kuvunja mkataba wa Vienna.Ila hili limefanunuliwa vizuri na msomi mmoja hapa Uganda somahapa
Sina hakika kama ninavunja Azimio la Dodoma, ila napenda nieleze kushtushwa kwangu eti mwanamama huyo alikuwa ni Mtanzania.
La msingi nataka nitoe hoja na ijadiliwe: Hivi kuwa mwanabalozi ndio tiketi ya kufanya maovu? Eti ukifanikiwa kuhodhi au kumiliki kile kitambulisho cha uanadiplomasia basi ndio mwisho wa kubughudhiwa na wakora-mapolisi na wanausalama wengine?
Serikali ya Rwanda imelalamika sana juu ya kukamatwa mwanadiplomasia wao. Ila zaidi ni kwamba kuna hali tete sana katika tukio hili: Unajua kuna uadui mkubwa sana kati ya Museveni na Kagame na hali hii imepelekea mwanamama, ndugu yetu mtanzania mwenzetu kuhusishwa katika kuendeleza sokomoko kati ya wakubwa wawili hawa.
Unaambiwa udikteta wa Museveni sasa unaingilia starehe za watu bonyezahapa na kuzihusisha katika kuaibishana kati ya serikali hizi mbili. Mambo si mambo hapa. bonyeza hapa

MPASUKO WA KISIASA PEMBA

Nimesoma makala moja kwenye IPP Media ikanikuna sana. Unajua hii siasa ya Pemba watanzania wengi hatuifahamu kabisa. Ule MPASUKO wa kisiasa JK aliodai upo eti inasemekana hata yeye hajui kuuziba.
Kujua zaidi hebu soma makala hii: bonyeza
Zaidi ya hapo, mwandishi kaongeza makala yake katika sehemu ya pili akichambua zaidi hasa baada ya kiongozi wa chama pinzani, CUF, kufika pia Pemba na kumsifia JK. bonyezahapa
Lakini inafurahisha zaidi kwani JK kasifiwa na wasomi wa Bongo juu ya jinsi ambavyo analifuatilia suala la Muungano.

Sunday, April 02, 2006

JK SIKU 100

Eti rais Jakaya Kikwete kafikisha siku mia moja madarakani. bonyeza hapa Binafsi nafikiri anastahili pongezi.
Ila leo kanifurahisha zaidi katika kupambana na majambazi kwani kaanzisha kikosi maalum dhidi ya ujambazi; bonyezahapa ni hatua ya muhimu nainga mkono.
Ila tahadhari imetolewa leo hii juu ya utendaji mzima wa serikali ya JK kama inataka iendeleze mafanikio zaidi ya haya yaliyotokea kwa siku mia moja. somahapa

Sunday, March 19, 2006

HABARI ZA LEO MAGAZETINI

Katika pitiapitia yangu ya habari leo nimekunwa na jinsi wanaume wa siku hizi wanavyochagua wanawake wanaowapenda wawe wenza wao. Mwandishi kaandika kwelikweli na akaonya sana juu ya makosa tufanyayo sisi wanaume. somahapa . Kuna hili la haki za ukombozi wa wanawake: inasemekana wengine wamejisahau na wakavuka mipaka. soma
Habari nyingine ni kuwa eti dunia ya leo mambo ya elimu sio tena msingi wa kufanikiwa kimaisha. Ukisoma mwandishi wa makala ile ameniacha nikipigwa butwaa ni kwanini ninasoma sasa? bonyezahapa
Alafu ningependa tumsome raisi wa hapa Yoweri Museveni katika mahojiano yake ya kwanza tangu achaguliwe kuwa raisi hivi majuzi. bonyeza

Saturday, March 18, 2006

HISTORIA KUJIRUDIA KOMBE LA MABINGWA ULAYA?

Arsenal ndio timu pekee kutoka ligi kuu ya Uingereza iliyobakia katika ligi ya mabingwa Ulaya. Sikutarajia hili kabisa ila napenda niwasifu wapiga bunduki wa London kwa hili. Waingereza huwa wanasema ‘due credit’.
Hii siyomara ya kwanza Arsenal kufikia hatua hii ya robo fainali ila emeweka rekodi ya ulaya kuiondoa Real Madrid. Hii, kwa kuzingatia misingi ya kihistoria katika soka la Ulaya, Arsenal itafika fainali kama kweli historia hujirudia. Nimechambua historia ya mashindano haya inaonesha kila timu iliyoweza kuondoa Real Madrid ilifika fainali. Hebu tujitahidi kukumbuka Bayern Munich, AC Milan, Juventus na Monaco katika miaka kadhaa michache iliyopita.
Ushindi wa Benfica dhidi ya Liverpool ni historia nyingine katika soka la Ulaya. Sio tu ni timu ya kwanza kuiondoa Liverpool katika vikombe vya Ulaya bali pia ni timu ya kwanza barani Ulaya kuifunga Liverpool ugenini na nyumbani tangu mwaka 2001/ 2002. Hii inanifanya niamini kuwa timu yeyote yenye uwezo wa kuiondoa Man United na Liverpool katika mashindano ni bora kufikia fainali. Labda hapa niwakumbushe kuwa Bayer Leverkusen iliiondoa Liverpool mwaka 2001/ 2002 na ikatinga fainali. Porto chini ya mtaalam Mourinho iliiondoa Man United mwaka 2003/ 2004 na wakafika fainali na kushinda.
Hadi sasa Arsenal wana rekodi bora kabisa ya kufungwa magoli mawili tu na ni timu pekee pamoja na Barcelona hazijapoteza mchezo wowote. Timu imebadilika ikicheza kwa umoja na nidhamu ya mchezo katika kulinda na kushambulia.
Kwa upande wa Chelsea, iliaminika na wengi kwamba ingeondolewa tu. Barcelona ni timu yenye vipaji asili (natural) pamoja na ufundi wa hali ya juu. Ukizingatia timu ya Mourinho inayotegemea ufundi wa kisayansi—yaani mtizamo wa kibinadamu (artificial) niwazi njia za asili zingeshinda tu. Kushinda ligi ya mabingwa unahitaji wachezaji wenye vipaji vya asili ambavyo vituvizidi vile vya kufundishwa na walimu wa timu pinzani. Mourinho alikosa jibu la Lionel Messi na Ronaldino katika timu yake.
Liverpool haina wafungaji magoli na ndio maana ikatolewa. Unapopata nafasi nyingi za kufunga alafu hufungi magoli ninachoweza kusema ni kuwa timu ni mbovu. Magoli ndio kiashirio cha ushindi na wala sio chati ya vielelezo vya umilikaji au majaribio mangapi timu imefanya golini mwa timu pinzani.
Mwisho, Liverpool kuondolewa katika ligi ya mabingwa ni sheria wala sio jambo la kustaajabisha. Hakuna bingwa mtetezi aliyewahi kutetea kombe hili. Arsenal wanalihitaji kombe hili na inaonekana matumaini yapo. Kwani nina hakika Juventus watapata shida sana kuenda na kasi na ari ya Arsenal. Hebu tusubiri robo fainali tuone.

Thursday, March 16, 2006

MKAPAISIM--LEGASI YA AWAMU YA TATU

Mimi ni mmoja wa watanzania wachache sana ambao wakati JK anaingia madarakani sikuwa namwamini kabisa. Unajua nimezaliwa nikakuwa nikiona wanasiasa wa CCM wakituongoza kwa migengwe ya kila aina. Ndio maana niliwahi kuandika JK Anatania tu. SOMA
Kama nilivyosema katika makala ile, kuwa JK anawafahamu walarushwa waliojikia mizizi ndani ya dola. Na nikahisi ataendeleza sera ya kulindana ya aliyemtanglia, mheshimiwa Mkapa. Nafurahi kusema kwa ninayoyaona sasa, JK kadhihirisha kuwa nilikosea. Kwa kiasi fulani ninaanza kuona Kasi Mpya. Na hii ni wazi kwangu ni juu ya suala la “Ujambazi”.
Ninasoma habari jinsi ambavyo serikali imewavalia njuga baadhi ya matajiri ambao wanalea majambazi nikafurahi sana. Imani yangu imeanza kumea kwani nataka niseme baadhi ya matajiri waliokamatwa ni watu ambao wamekuwa wakitawala tetesi kuwa ni majambazi tangu nikiwa mtoto nasoma shule ya msingi. Kwa hiyo mimi nimefurahishwa na hatua ya serikali.
Labda nimkumbushe kamanda Saidi Mwema kuwa tafadhali hakikisha dola inajua shughuli za wenye fedha wote. Kuna umuhimu wa serikali kujua baadhi ya wafanyabishara wanapata wapi mitaji mikubwa ya kuendeshea miradi yao feki. Utandawazi isiwe ndio mwanzo wa watu kuachiwa huru kujifanyia chochote watakacho. Nikumbushe pia hawa wafanyabiashara wanajihusisha na vigogo wa serikali; hivyo ni muhimu na vigogo kadhaa waanze kuhoiwa kama kweli tunataka kupambana na ujambazi kwa ari mpya na kasi mpya. Hii mambo ya kuhamisha baadhi ya maofisa polisi na kuwapeleka jijini makao makuu nataka niseme ni doa katika hii vita ya ujambazi. Yaani mtu anahamishwa eti kutoka mkoa unaosemekana ni kitovu cha ujambazi alafu anakwenda makao makuu? Kwa nini tusiwastaafishe watu kama hawa kwa manufaa ya umma? Hapa nimechanganyikiwa kabisa.
Katika gazeti la Nipashe toleo la tarehe 10/3 nilisoma eti kuna afisa wa polisi eti akaunti zake zimesimamishwa. Hakutajwa kwa jina na mimi naona nisimtaje ila walipoandika eti anatoka mikoa ya kaskazini hisia zangu zilinicheza. Unajua Tanzania watu wa kawaida wanaishi na kuzungumza tetesi nyingi sana. Ila tatizo ni kwamba hasa kipindi cha Mkapa alikuwa akipiga tetesi kabisa. Alikuwa anasisitiza eti wananchi walete ushahidi. Dhihirisho la jinsi ambavyo alivyokuwa anapenda kulea watendaji wake, wengi wao wakiwa wala rushwa na mafisadi wakubwa. Hii madhila ya jeshi la polisi ni dhihirisho la sera mbovu za uongozi mbovu wa awamu iliyopita.
Madhila ya ujambazi tunayoyaona leo ni matokeo ya sera: MKAPAISM—kuficha maovu, wala rushwa, mafisadi na kutochukua hatua dhidi ya maafisa wakubwa wa serikali pale walipokwenda mrama. Hii ilipelekea kwa mfano jeshi la polisi likafika mahali haliheshimu hata raia. Jeshi linaendeshwa kama mali ya mtu binafsi bwana. Nakumbuka kila mara ninapokuwa kule Moshi huwa nashangaa sana. Sina hakika kama ni watu wote wanashangaa kama mimi pale unapoona askari polisi wa usalama barabarani wanasimamisha vipanya navyo havisimami na unasikia kondakta akitumwa akawaone hawa mabwana. Huko nasikia huwa anapeleka noti ya shilingi 1500 au 2000. Huwa nabaki kujiuliza je hawa ni wafanyakazi wa umma au wakusanya ushuru? Kama unataka kuyaona haya nenda karibu na kituo cha mabasi Moshi Mjini sehemu inaitwa BORA, kuna nguzo ya umeme na utakuta askari kasimama pale mida ya asubuhi.
Hapa kamanda Saidi Mwema atajiju kwani jeshi letu la polisi lilikuwa likiendeshwa bila maadili, kizamani na kila aina ya michezo michafu. Mwisho, niulize: polisi imewatia kizuizini matajiri kadhaa lakini nikumbushe kitu kimoja: wataalam wa sosholojia wanasema wanawake pia wanajihusisha sana na uhalifu. Mbona hamjawatia lupango Wabejing? Wanalea majambazi sana pia.
Pamoja na kumkandia Mkapa na "Mkapaism yake" nafikiri ni bora pia tujue anaendeleaje na mapumziko yake. Hebu bonyeza hapa uone.

Sunday, March 12, 2006

USHOGA KUKUBALIKA KAMA DESTURI HIVI KARIBUNI

Nimekutana na makala moja ambayo imenikuna sana juu ya ushoga.
Ama kweli hivi majuzi katika nishani za Oskar kule kwa Joji Kichaka, walifikia mahali na kuitunza filamu ya ushoga.
Kwa kweli nina wasiwasi sasa si muda mrefu 'Ushoga utakuwa sio dhambi'. Jamani mimi nimechanganyikiwa manake sasa wazungu wanatuwekea viwango kwenye kila kitu. Na wakishapitisha kwamba kitu fulani ni bora ndio hivyo tena sisi makabwela tunaona ni fasheni. Bonyeza hapa uone yuko mzungu mmoja hapa Uganda ana maoni fulani.

NCHI INAPOMILIKISHWA KWA MTU BINAFSI

Ama kweli kuna viongozi wanaopenda kumiliki nchi kama mali yao. soma hapa

Tuesday, March 07, 2006

MAMBO YA LUGHA NA FRED MACHA

Makala ya Fred Macha imenikosha na nimeona niifadhi ili tuisome na tujikumbushe umuhimu wa kulea lugha yetu. soma

UGANDA BAADA YA UCHAGUZI

Kama kawaida hapa Uganda mambo ya siasa yanaendelea kuchacha. Museveni kashinda uchaguzi kwa mbinde. Leo mahakama kuu imetoa hukumu soma dhidi ya Dk Besyige kuwa hana hatia ya ubakaji. soma
Ni aibu kwa Museveni tena lakini yeye anaendelea kujitapa katika makala aliyoiandika mwenyewe leo magazetini hapa soma. Pia leo imeandikwa makala juu ya udhalimu wa serikali ya Museveni kutumia jeshi kwa manufaa yake binafsi na kuvunja katiba. Hebu soma uone udikteta ulivyokomaa.
Ni wazi majaji wa hapa wako makini kwani serikali inapoteza kila kesi si kawaida lakini ndio hali halisi bonyeza

Monday, February 27, 2006

UCHAGUZI SAFI KWA VIWANGO VYA KIAFRIKA

Leo nimeona niwape habari za ushindi wa Museveni. Niseme tu kwa nilivyouona uchaguzi huu hakuna tofauti na chaguzi za Tanzania au Kenya.
Wapinzani wanalalamika lakini ndio kawaida yetu tumezoea. Sikutarajia Uganda inaweza kufanya uchaguzi kwa ustaarabu niliouona.
Dosari ni kule Museveni kubadili katiba; ila ameonesha alishawasoma watu na akagundua asilimia 59 wanampenda. Sasa kashinda ila swali ni: Demokrasia ni nini kweli? Je ni ipi demokrasia ya kweli ya Magharibi au ya kifalme kama hii ya Museveni? Wananchi wa hapa wametoa jibu hebu soma matokeo kamili hapa
Basi hebu tuangalie mambo yatakuwaje?

Saturday, February 25, 2006

KANDANDA LEO

Siku nyingi sijaandika juu ya soka.Kama baadhi yenu mnavyojua mimi ni mnazi wa Liverpool. Wiki hii tulipoteza mechi dhidi ya Benfica ila nina matumaini tutashinda mechi ijayo.
Leo nataka nizungumzie juu ya Manchester United kwani leo ndio wanamaliza msimu.Huwezi kuamini siku hizi ni faraja kwa Manchester kushindani kwa nguvu vikombe vidogo kama hili la leo la Carling.Siku za nnyuma Ferguson alikuwa akidharau mashindano haya ila leo hii ni shida hata kushinda kikombe hiki.
Klabu hii imeporomoka kwa kila kitu: kocha mzee, wachezaji dhaifu na wasio na ujuzi wa kutosha.Rooney na Ronaldo walisemekana kama kizazi cha baadaye.Inavyoonekana sivyo kwani hata sifa ya kuwa kiongozi hawana. Mara nyingi utawaona wakishindwa hata kujidhibiti wenyewe.Sasa ligi ya Uingereza ni ya Liverpool na Chelsea kama klabu imara.
Arsenal pamoja na kuifunga Real Madrid wiki hii naweza kusema sio klabu imara. Real Madrid wajinga kweli. Huwezi cheza na Arsenal alafu ukawaruhusu wacheze katika kiungo. Ni hatari sana na ndio maana walifungwa. Niionavyo Arsenal haiwezi kufurukuta kwa timu kama Chelsea au Liverpool.
Nitoe ushauri kwa Ferguson astaafu na pia klabu isainishe wachezaji wapya.
Mwisho kuhusu Tanzania, kama mjuavyo, wiki hii nchi yetu ilipangwa katika makundi ya michuano ijayo ya kandanda ya Afrika. Senegal, Burkinafaso sio mchezo kabisa,sidhani kama tutafika mahali.Kwa ufupi tusahau fainali hizi manake bado sijaona program yeyote ya vijana chini ya TFF.Hatuwezi kushinda katika mazingira kama hayo.

UHURU WA HABARI KAPUNI?

Mwezi wa kwanza, tarehe ya 16 niliandika makala juu ya jinsi gani uchaguzi mkuu kule Moshi ulivyoendeshwa.
Nilijaribu kugusia juu ya hisia mbalimbali za watu mara baada ya uchaguzi ule na nikaonesha ni jinsi gani kwa kiasi fulani demokrasia ilifanyiwa mchezo mchafu.
Nilisisitiza kwamba ilikuwa ni hisia zaidi za watu.Nahisi jamaa kadhaa hawakufurahishwa na makala ile.Kwani nadhani wameamua kuizuia makala hiyo isisomeke kabisa.
Nawaomba radhi wanaglobu ila niseme tunalo tatizo la uhuru wa habari katika nchi yetu.Siku za usoni nitaandika ni kwanini hali iko hivyo hasa nikijaribu kufananisha na kile kinachotokea hapa.

Thursday, February 23, 2006

UCHAGUZI UGANDA LEO

Kwanza kabisa niwaombe radhi kwa kupotea kwa muda mrefu. Unajua tena mihangaiko ya maisha. Tatizo kubwa hapa Uganda ni umeme kwani kuna mgao wa umeme hatari sana. Huwezi kuamini hapa tunapata umeme kila baada ya masaa ishirini na nne.
Kwa hali hii mara nyingi mchana huwezi pata mahali pa kufanyia kazi kwa kutumia umeme. Kwa wananchi wao ni kawaida kwani hii japo imesababishwa na uzembe wa viongozi wao wanaamini eti ni ukame tu.Hayo tuyaache kwani yanakera kweli pale ulafi na rushwa ya wanasiasa wetu zinapoua uchumi wa nchi alafu wanasingizia eti hali mbaya ya hewa.
Leo kutwa nzima nimekuwa nikipitia vituo mbalimbali vya kura hapa Jinja na kufuatilia yanayojiri huko Kampala. Kwa ufupi kura zimepigwa shwari na ni dhahiri bwana Besigye anaongoza mijini. Ngoma imebaki huko vijijini kwani Yoweri ndio ngome yake.
Watu wanafurahi dikteta atashindwa ila mimi siamini manake ni vigumu. Hebu tusubiri tuone.

Thursday, February 02, 2006

KWANINI MUSEVENI NDIO PEKEE KINARA?

Haya tena sasa ni mwezi ambao nchi ya Uganda itafanya uchaguzi wake mkuu.
Baada ya kukaa kimya kwa kipindi nikiwajulisheni siasa za hapa leo narejea tena. Kama inavyoeleweka na wengi ugombea wa rais ambaye alitarajiwa kumaliza muda wake umekuwa na utata sana hasa baada ya kubadili katiba kidemokrasia kupitia wabunge kuondoa ukomo wa vipindi vya kukaa madarakani.
Leo Rais Museveni kaandika makala maalum somahapa kuelezea ni kwa nini wananchi wanamkubali na kuwa ilikuwa ni sahihi kubakia madarakani.

Monday, January 30, 2006

JK ANATANIA TU.

Nakumbuka mzee kifimbo alipong’atuka mwaka 1985, nchi yetu ilikuwa hoi kiuchumi. Mzee Ruksa alikuja kama mkombozi. Wakati huo nasoma shule ya msingi, basi redio Tanzania ilizoea kucheza nyimo kuonesha mwelekeo mpya; nakumbuka kibao kimoja: ‘Usiopowajibika Ole Wako, Utakumbwa na Fagio la Chuma’. Pia kulikuwepo tangazo katika redio kila mara redioni eti: Mdudu rushwa ni hatari na anapiga na anaua’.

Hii yote ilikuwa kuonesha eti Mzee Ruksa kaja na ari mpya dhidi ya rushwa. Matokeo yake utawala wake uliikumbatia rushwa hadi mzee Kifimbo kumkemea kiana wakati Fulani pale Kilimanjaro Hoteli.Baadaye akaja Mkapa na kauli mbiu ilikuwa ‘Uwazi na Ukweli’. Kinyume chake huyu bwana hakupenda uwazi kabisa; ukweli ndio usiseme, waandishi wa habari watakuwa mashahidi hapa.

Sasa kaja Kikwete na kauli mbiu—Ari mpya, Kasi mpya na Nguvu mpya. Hisia zangu zinaniambia hivi: Kuna hatari haya majigambo tu. Katika uteuzi wake anaonekana kuja na sura mpya nyingi tu. Hii ni habari njema isipokuwa utendaji wao sidhani kama utafanikiwa.

Hii ni kwasababu raisi anapaswa, nafikiri analijua hili kwamba CCM imejaa wala rushwa wakuu nchi hii. Vyombo vya dola, mfano jeshi la polisi limejaa wala rushwa na huu ni utamaduni ndani ya chombo hiki inavyoonekana.

Nilipokuwa natizama hotuba ya JK ya ufunguzi wa bunge niligundua mambo mengi. Wapo wabunge kadhaa walionesha sura za woga na chuki dhidi ya maneno ya raisi. Wengi wa wabunge wazee pamoja na wabunge wanawake kadhaa walionekana kuogopeshwa na hotuba ile.

Kwa mtu yeyote aliyezoea kuishi kiujanjaujanja aliogopa sana. Nani asiyejua wabunge wengi wanalitumia bunge kama tanuri ya utajiri? Nani asiyejua wabunge wengi ni vihiyo ambao hata hawafahamu nchi yao kwa dhati. Mheshimiwa JK anaongea kama vile hajui wapo wazee, vigogo ambao hawashikiki nchini mwetu (untouchable) wamejazana bungeni ili kulinda maslahi yao. Hawa ni kikwazo kwa Ari mpya, Kasi mpya na Nguvu mpya.

Mwisho niseme tu ninamuunga mkono mheshimiwa JK, ila nina hakika itakuwa vigumu kwake kuleta mabadiliko tunayoyatarajia. Kutamba kwa majambazi ni kielelezo cha kwanza. Ila itabidi raisi awe mkweli tu kuwaridhisha watanzania. Kama waswahili walivyonena: “Bahari haiishi Zinge” nami ninene: JK anatania tu.

Monday, January 16, 2006

UCHAGUZI NA ODA KUTOKA JUU NANI ATANGAZWE MSHINDI

Hili nataka nilieleze kama nilivyolipata kupitia tetesi zilizozagaa mitaani pale Moshi mjini baada ya uchaguzi wa ubunge ambapo mgombea wa Chadema, Mzee Ndesamburo alimshinda yule wa CCM, Mama Elizabeth Minde. Nitaeleza mara baada ya kuweka wazi wasiwasi wangu juu ya hali ya usalama pale Moshi.

Kwa kipindi cha wiki tatu nikiwa Moshi mjini nilishuhudia hali ambayo kwangu ilinitia wasiwasi sana. Eti siku hizi ujambazi umeongezeka sana Tanzania hasa Moshi na utawala umeamua kwamba askari polisi lazima wapite mitaani wakiwa na silaha kuhakikisha usalama. Kwa kweli mitaa imejaa askari ila katika hali ya kunishangaza sikujiona salama kabisa. Niwachekeshe: katika matembezi yangu nilikutana na kijana, charafu, hajachana nywele, amevaa suruali ya jeanse chafu sana ambayo imechanwa sehemu mbalimbali na amebeba bunduki( short gun). Nusura nianguke manake nikajua huyu ni jambazi bahati nzuri watu wengine wakaniambia ni askari yuko kazini.

Nililoliona hapa ni kwamba tofauti ya jambazi na askari haionekani manake usalama unakuwa haupo, raia hawezi kumjua askari ni yupi.Nidhamu ya askari haipo kabisa hili nitalizungumzia siku nyingine kwani nina mifano mingi tu.

Basi nieleze juu ya uchaguzi pale jimbo la Moshi manispaa hasa kuhusu tetesi ambazo kama waswahili walisema: “lisemwalo lipo na kama halipo…….”.Mwaka jana mara baada ya CCM kuteua wagombea wake wa ubunge nilieleza uvumi uliokuwa umezagaa kule Moshi. Mgombea wa chama hicho, Mama Minde, ni wazi alikuwa ni chaguo bovu kwa wapiga kura.

Nilikuwa Moshi wakati ule na nikasema hatashinda huyu mama. Na kweli imekuwa hivyo; ila nilipokuwa huko hivi karibuni nilikusanya tetesi zingine ambazo nafikiri ni vizuri wanablogu mnisaidie kuchambua.

Ni hivi: uchaguzi wa Tanzania uliokwisha hivi karibuni umesifiwa sana na wanahabari na hata waangalizi mbalimbali. Kwa wapinzani umekuwa ni bumbuwazi kubwa sana. Ila kwangu naomba nijibiwe hili:

Kwa mfano, pale Moshi manispaa, inasemekana msimamizi wa uchaguzi, mkurugenzi wa manispaa, alichelewa sana kutangaza matokeo mara baada ya hesabu kukamilika. Eti ilimbidi afanye mawasiliano na wakubwa ili aruhusiwe kuyatangaza. Habari aisizothititishwa ni kwamba ilikuwa ni janja ya kumtangaza mgombea wa CCM kama mshindi. Ila hapa ilishindikana kabisa. Wigo wa kura ulikuwa mkubwa sana na inasemekana hata hizo alizopata mwanamama sizo zilizotangazwa kuondoa aibu. Je huu ndio uchaguzi ulio huru na haki?

Inasikitisha sana hizi sera za Mao hazifai kabisa.

KUTOKA TANZANIA HADI UGANDA

Mara ya mwisho niliaga kwamba sitakuwepo ulingoni mwaka jana. Nilikwenda mapumzikoni kule kwetu Moshi. Niliondoka hapa Uganda nikiacha hali ya kisiasa ikiwa ya vurugu, vitisho na udikteta ukiashiria kila hali ya zari kama sio dhahama ama kasheshe. Nimerudi hapa Uganda; ni wiki moja imekwisha sasa na hali imebadilika haswa kinume na nilivyokuwa nimetabiri kwamba hatima ya Besigye kisiasa. Nitaeleza baadaye.

Niwapashe wanaglobu wenzangu ni nini nilikikuta huko Moshi, uchagani katika wilaya ya Moshi Vijijini, jimbo la uchaguzi la Vunjo. Nilifika tu na Raisi mpya akatangazwa. Hii haikuwa tashwishwi kwangu kufuatilia kwani dhahiri nilijua JK angeshinda. Ila uchaguzi wa ubunge ulinikuna sana.

Baada ya miaka kumi ya utawala wa mbunge wa chama cha upinzani hatimaye jimbo langu la Vunjo likamchagua mbunge kutoka CCM kwa mara ya kwanza tangu siasa za vyama kurejeshwa. Hili lilinifurahisha kwani hawa jamaa wa upinzani wameirudisha Vunjo nyuma sana. Nasema hivi kwani katika eneo ninaloishi, kijiji cha Uparo, Kirua Vunjo, palw maeneo ya Kawawa Road ni dhihirisho tosha.

Nyumbani pale hakuna maji ya bomba tangu uhuru saa. Umeme ndio usiseme hakuna kabisa. Barabara ya kwenda Kirua Vunjo haifai kabisa; ikinyesha mvua inabidi magari yasubiri jua litoke ili pakauke ndio watu waweze kusafiri. Kuhusu mambo ya elimu ndio usiseme: eneo la Kawawa Road kwa mfano halina shule ya sekondari wala msingi na lina makaazi ya watu wasiopungua elfu tano. Watoto inawabidi kutembea kwa miguu zaidi ya kilomita saba kwenda shule kama za Pakula Sekondari, Mashingia na Uchira Sekondari. Hii ni hatari sana sasa tuone hawa CCM watafanya nini.

Niliposikia Kikwete na ari yake mpya, nguvu mpya na kasi mpya sikumwelewa sana ila nampa matarajio kama mkazi wa Kawawa Road kwani tumempa mbunge labda matatizo yetu yatapungua. Nafikiri mheshimiwa mbunge anajua hili.

Sasa niwarejeshe hapa Uganda: Mnakumbuka Museveni aliamua kumweka jela mpinzani wake mkuu Dr. Kiiza Besigye. Chama cha Besyigye kikaweka ukinzani wa hali ya juu. Nakwambea imesaidia sana , hali ya siasa ya Uganda kwa sasa ni shwari hata mimi nashangaa. Besigye yuko nje kwa dhamana ila kampeni in kama kawa. Vitisho dhidi ya fyombo vya habari na wapinzani vimekomeshwa; wale wanajeshi waliozoeleka kujazana mitaani hawapo tena.

Museveni kabadilika sana; uchaguzi utakuwa shwari kama hali itaendelea hivi. Nitaendelea kuwapasha zaidi ila tu Besigye anatuhumiwa kubaka na kesi inaendelea na imejaa vituko kwelikweli.

Saturday, December 10, 2005

MSUMARI WA MWISHO KATIKA JENEZA LA DR. BESIGYE

Kama nilivyokwisha tabiri siku kadhaa zilizopita hatimaye serikali ya Uganda imegongelea msumari wa mwisho katika jeneza--na kuthibitisha kuwa Dr. Kiiza Besigye hatagombea uraisi katika uchaguzi mkuu ujao hapo mwakani.
Nimeona niwaletee barua maalum iliyoandikwa na mwanasheria mkuu wa Uganda ili mjue kabisa sasa ile ndoto ya kumuondoa dikteta hapa Uganda imekwisha. SOMA
Ninachokiona hapa ni kwamba itakuwaje sasa manake sasa tuturajie mapambano na sijui yatakuwa ya aina gani manake yale ya kisheria inaonekana chama cha upinzani kimeshapoteza kabisa.

TUTAONANA BAADA YA WIKI MBILI

Kwa ufupi tu niseme kwamba kesho ninaanza safari ya kwenda nyumbani-Tanzania pale Moshi.Hivyo sitakuwa hewani kwa wiki moja na nusu hivi kwani ninapitia Tororo hapa Uganda na nitakaa kwa siku kama tisa hivi na nina hakika pale hakuna huduma yeyote ya tarakilishi hivyo sitaandika kabisa. Ila nitakapofika tu Tanzania nitaandika niliyoyaona katika safari yangu.
Kumbuka nitadodosa ya kule Tororo hasa juu ya siasa za hapa Uganda, alafu nikiwa Kenya kwa siku moja nitajaribu kuangalia kuna nini cha maana kuandika alafu nitakapofika Tanzania ujue wakati huo ndio uchaguzi utakuwa umekwisha. Hivyo nitaangazia nini kinajiri najua kutakuwa kuna mengi.
Basi niseme tutaonana.
Waziri wa afya wa Tanzania, Anna Abdallah alipokuwa akizindua rasmi kiwanda cha dawa za kusaidia kuongeza maisha kwa waathirika wa ukimwi, waya,mtandao,ngoma) Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd, DSM.

Sasa kiwanda cha madawa ya kuongeza muda wa maisha ya mgonjwa wa ukimwi kimezinduliwa rasmi Tanzania. SOMA Kuna watu wamefurahia hatua hii sana kwani kwao vifo vya ugonjwa huu vitapungua. Kwangu mimi nawaza vingine kabisa. Kwani naona ndio mwanzo wa maambukizi mengi hebu tusubiri tuone athari za kiwanda hiki kuwepo nchini mwetu.
Wabongo wengi tulivyo ni kwamba sasa mapenzi ni mbele kwa mbele na kwa maana hiyo tutakwisha zaidi. Na kama ilivyo kawaida Bongo, tutaanza kuuziwa dawa za kufoji na hapo ndio utaona utitiri wa maambukizi. Watanzania ni maskini na wapo wajanja sana ambao huu ni mwanya mzuri kwao kujipatia fedha na ndipo hapo tutakapokufa na kufaana.
Nia yangu sio kuponda ila nathubutu kusema hii ni hatua nzuri katika kupambana na janga hili ila tujiandae kwa madhara.

Thursday, December 08, 2005

UHUSIANO NA AKINA MAMA-- KIZUIZI CHA URAISI AFRIKA

Kama unataka kuwa rais wa nchi yeyote Afrika lazima uwe kati ya wale wateule la sivyo uwe mtakatifu. Nasema uwe mtakatifu kwani ni lazima uwe hajawahi hata kuwa na uhusiano na binti au mwanamama yeyote katika maisha yako. Kinyume na hapo kesi za ubakaji au udhalilishaji wa wanawake zitakukumba na ndoto yako ya kuwa rais itakwisha. Jacob Zuma, anakubali kuwa alifanya mapenzi na mwanamama fulani kwa makubaliano lakini anashangazwa na tuhuma za rushwa. somahapa
Haya ndio yanayowakumba Dr. Kiiza Besigye na Zuma wa huko Afrika kusini. Hadi sasa ni tuhuma lakini kwa hali ilivyo inanifanya niamini kuna ukweli ila hila zinatumika kubadili uhusiano wa makubaliano kati ya watu wawili kuwa ni ubakaji. Hebu soma hii habari ya mashtaka ya Zuma ujionee mwenyewe. soma

Wednesday, December 07, 2005

KIKWETE MZALENDO KWELI?

Nimekutana na makala moja ambayo imenifanya nijiulize maswali mengi sana. Unajua hivi kweli ni sawa kumpima mtu kama kiongozi bora kwa kuangalia ni wapi watoto wake wanasoma? Hivi majuzi mtoto wa rais mtarajiwa, Mh Kikwete alihitimu katika chuo kikuu cha Dar es salaam; baadhi ya watu wanachukulia hiki kama kitendo cha kizalendo.
Hebu jaribu kusoma hapa alafu useme mwenyewe.

Sunday, December 04, 2005

MBOWE ANAVYOANDAMWA NA WA-TWAWALA

Freeman Mbowe anataka kuingia Ikulu; na inavyosemekana anawakilisha kizazi kipya(sio wanamuziki wa bongo flava) katika siasa za Tanzania.
Huyu bwana inasemekana anawapa maumivu ya kichwa sana waheshimiwa wa chama cha wa-twawala(CCM). Hevu soma hapa uone ni jinsi gani ukijaribu kupambana na wa-twawala wakati wewe huna tabia zao watapambana na wewe sawasawa. Inasemekana Mbowe anaipata fresh.

MKAPA ASIFIWA HAPA UGANDA

Wakati watu wote makini hapa Uganda wakiwa wamesikitishwa na hatua ya rais Museveni kung'angania madaraka, magazeti mengi yamekuwa yakimsihi Museveni afuate mfano wa rais Mkapa.
Ila leo ndio ilikuwa fungakazi manake gazeti moja hapa liliandika tahariri kumsifu raisi Mkapa kama mfano mzuri wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki. somahapa
Kwa Museveni yeye kasema kila nchi ni tofauti na hakuna haja ya kufananisha mifano kwani kila mtu ana njia zake binafsi za kutatua matatizo. Mnasemaje hapo?

Saturday, December 03, 2005

HAWA NDIO WASHIKA DAU.

MAJENERALI WA UGANDA: (L-R) David Tinyefuza, Salim Saleh and Elly Tumwine : Hawa ndio washika dau wakuu hapa Uganda. Hakuna cha wanasiasa, hapa lazima uwe mwanajeshi ndio uweze kuwa mshika dau katika siasa.
Anayeonekana kulia ndio jaji wa mahakama ya kijeshi inayomshtaki Dr.Kiiza Besigye. Wa katikati ni mdogo wake rais Museveni na inaaminika ni kati ya watu matajiri sana hapa na ni askari shupavu.

MAGAZETI YAFUNGIWA TANZANIA

Hapa Uganda mambo yamepoa kiasi fulani kuhusu siasa.Inavyoelekea Museveni ni mbabe vya kutosha na hakuna njia ya kumdhibiti.
Kiiza Besigye ni wazi hatagombea uraisi nionavyo;kwani inaonekana kuna migongano ya muda mrefu ya kibinafsi kati yake na Museveni pamoja na maofisa wengine wa serikali hasa wanajeshi. somahapa Kwa hali hiyo hawataruhusu agombee na kama atagombea ninaona hali mbaya baadaye kama atakuwa rais.
Lakini labda tusubiri tuone.Leo niangaze Tanzania manake sasa Mkapa naye kaanza kufungia magazeti.somaSina hakika kama ni halali kulifungia gazeti ila nafikiri hii sio dawa manake kama serikali ingaling'amua nguvu ya mtandao basi isingechukua hatua hii.
Lakini kuna udhaifu sana Tanzania juu ya matumizi ya mtandao, manake sioni magazeti yetu mengi mtandaoni. Hapa Uganda ukifungia gazeti linaendelea kuchapisha mtandaoni.
Nataka niulize hivi kama gazeti linaandika kashfa ya kigogo ambayo inaisumbua familia yake ni makosa ya gazeti au kigogo mwenyewe?Nani alaumiwe hapa?

Saturday, November 26, 2005

NITAKAMATWA SIKU YOYOTE KUANZIA LEO

Nataka niseme kwa sasa niko hatarini kukamatwa wakati wowote. Unajua kuanzia juzi serikali imepiga marufuku kuandika, kuzungumza juu ya Dr. Kiiza Besyige, mpinzani wa Museveni ambaye yuko lupango.Kama mnavyojua hapa kila kitu ni kijeshi tu kwa hiyo mkisikia nimetiwa korokoroni msishangae kabisa.
Lakini kabla hayo hayajanikumba labda niseme tu kwamba bado hali sio shwari. Jana Besyige kapewa dhamana bonyezahapa ila bado anabakia ndani ya lupango. Kujua zaidi hebu bonyezahapa. La kushangaza zaidi hapa polisi ndio hao hao wanajeshi na kuna wanajeshi wengi sana Kampala onahapa
Katika kuhakikisha uhuru wa kusema, kuandika na kutangaza unadhibitiwa, serikali imemteua mwanajeshi bonyeza kuongoza bodi ya gazeti la serikali-New Vision. Hii inatafsiriwa kama kuhakikisha hata gazeti la serikali linamchafua mpinzani yeyote na haliandiki habari njema kumhusu.
Kwa Museveni hii ndio demokrasia.

Friday, November 25, 2005

KISA CHA WA-TWAWALA WETU

Ile stori ya wa-twawala wetu wanavyowanyonya walalahoi inaendelea kudhihirika. Huko Kenya, rais Mwai Emilio Kibaki amelifuta kazi baraza la mawaziri.
Bonyeza hapa uone ni jinsi gani walalahoi wanavyonyonywa.Hivi kweli bara la Afrika ni masikini au tunatania?Mimi nashindwa kujua wala kuamini ila inanifanya niulize wenzangu: Kwa mfano jinsi serikali ya Tanzania inavyohangaishana na madaktari je ni kiasi gani kinatumika kwa wanasiasa wetu? Je ni busara kutumia mabilioni kwenye siasa na kuwasahau madaktari wetu?

Thursday, November 24, 2005

DALILI ZA UDIKTETA ZAJIONESHA JANA KAMPALA

Watu wanasema Museveni kawa dikteta; na leo nataka niwaoneshe haswa ni kwa vipi huyu bwana kweli ameamua kuitupa demokrasia kapuni.
Jana ile kesi ya mpinzani wake mkuu, Dr.Kiiza Besigye ilikuwa itajwe na kulikuwa kumepangwa maandamano makubwa ya wafuasi wake.Kinyume chake serikali ilitumia wanajeshi na kuwavisha nguo za polisi wakiwa na magari makubwa ya kijeshi katika kona mbalimbali za kampala. Soma hapa ujione mwenyewe udikteta unavyomea.

Wednesday, November 23, 2005

MKAPA ANAVYOSHAMBULIA WAZUNGU

Haya, leo Mkapa naye ameamua kuwachachamalia hawa jamaa wa magharibi. Anadai wanapokosoa nchi zetu wanaingilia sana mambo yetu kwa maslahi yao.SOMA

Tuesday, November 22, 2005

WIVU WA WAZUNGU

Eti wamarekani na waingereza wanashangaa kwanini China inawekeza kwa kasi Afrika?soma
Jamani huu sio wivu? Naomba tuelezane je China kuwekeza Afrika ni habari njema kwetu waafrika au balaa jingine?

JAMANI HII "THANKS GIVING NI NINI?"

Hii nataka mheshimiwa Ndesanjo asome na ikiwezekana anipe muangaza. Nasikia huko Amerika kuna hii sikukuu iitwayo: Thanksgiving, hebu niambie inamaanisha nini?
Joji Kichaka kong'oli hapa nimeona akitoa salamu za siku hii.Hapa ninaishi na Wamarekani miongoni mwao ni waalimu wangu basi siku tayari wameshaanza kutoa udhuru hawatahudhuria darasani. Ni nini msingi wa siku hii?

Monday, November 21, 2005

HATARI KWA UHAI WA GLOBU

Haya wanablogu jamani mimi sasa natishika. Hivi kama mmefuatilia huu mkutano wa vyombo vya mawasiliano ya kompyuta kuna habari sasa wa-twawala wanataka wadhibiti mitandao ya intaneti.
Sijui mnalionaje manake natishika sasa hapa.Kuna hatari habari zinazotokea huku zikadhibitiwa, tunaelekea wapi? Nimesoma habari bonyeza
nikashtuka sasa ule uhuru wa mawasiliano uko hatarini.Jamani tutuwaweza wa-twawala?

Sunday, November 20, 2005

MUSEVENI ALIPOCHAGULIWA TENA

UTANDAWAZI HATUWEZANI NAO-WATANZANIA

Rais anayemaliza muda wake amekuwa akisisitiza watu wenye mali Tanzania kukopa benki ili kufanya biashara.Hii ni hatua nzuri isipokuwa kama hakuna usimamizi mzuri wa fedha mambo yatakwenda kombo.
Siku za hivi karibuni ile kampuni ya mabasi Scandinavia soma imeingia katika malumbano ya madai na inavyoonekana mambo si shwari.Huwa nikija huku nasafiri na kampuni hii sasa nasikia inataka kufilisiwa. Jamani watanzania tunani?Tuna udhaifu wa kusimamia shughuli mbalimbali hebu tizama jiji la Dar limekuwa na mgawo wa umeme kwa mwezi sasa.Sio IPTL wala Netgroup Solution imekuwa jibu. soma
Tumekwisha.

Saturday, November 19, 2005

KITENDAWILI CHATEGULIWA

Rais Yoweri Kaguta Museveni hatimaye jana usiku alifanya yale yaliyokuwa yametawala vinywa vya wengi hapa Uganda kwa siku nyingi.Ametangaza rasmi kwamba atagombea urais soma tena baada ya kubadili katiba na kuruhusu agombee kwani alikuwa tayari katimiza vipindi viwili vya miaka 5.
Nilitaraji hili, ila nataka niulize hivi kweli kuna tatizo hata mtu akiitawala nchi yake kwa miaka 50?
Na kama watu, wanachama wa chama chako, tena chenye wafuasi wengi ndani ya nchi wakakusukuma ugombee, ni muhimu kweli kufuata utashi wako?
Hebu pitia makala moja soma hapa ambayo inazungumzia ni njia ipi Museveni ataifuata sasa alafu unaweza ukaelezea hisia zako.
Mimi ninabaki kumshangaa BEN MKAPA eti anaachia ofisi, mbona wenzake bado wamebaki?

EBO! MADAKTARI SI BORA KAMA WANASIASA.

Haya leo turejee Tanzania: somahapa kuna hii kasheshe ya madai ya posho za madaktari. Jamani mimi huwa nachanganyikiwa ninapoona daktari kasoma na akahitimu lakini hana mapato mazuri.
Ukipima kile wanachopata watawala wetu usiombe. Hasa wanasiasa, wabunge na madiwani ndio wanaopata pato kubwa sana. Naomba mniambie wenzangu na mie, hivi ni kwanini tuwalipe mamilioni ya shilingi wabunge alafu madaktari tuwakamue?
Tumekwisha.

Thursday, November 17, 2005

UNG'ANG'ANIZI MPAKA KWA OBASANJO?

Baada ya maneno mengi hapa Uganda, ambayo yalipelekea watu kulalama eti Museveni anang'ang'ania madaraka kwa kubadilisha katiba hatimaye yametimia.
Museveni kachukua fomu somahapa za kuomba kugombea uraisi kwa tikiti ya chama tawala NRMO. Lakini kimefanyika kiroja kimoja cha kisiasa hapa. Wanachama wa chama hicho wameamua kujifanya wamemlazimisha agombee kwani hakuna mtu mwenye kile wanachokiita "visheni" ya kuongoza Uganda.
Ung'ang'anizi huu wa madaraka unanipa wasiwasi juu ya kuwaamini viongozi wanajeshi kwani hata leo asubuhi nimesikia eti hata Obasanjo naye yuko mbioni kubadili katiba.
Jamani naomba maoni yenu nini kifanyike?Manake hawa viongozi ving'ang'anizi wakipata mpinzani wanatuma askari mipakani na wanawakamata alafu wanaigiza eti ni waasi na wanawahusisha na uasi. Ndio yanayomkuta Besigye sasa hivi.

MUSEVENI AANZA KUONESHA DALILI ZA UDIKTETA

Ukisikia hakuna demokrasia basi ndio hapa Uganda. Kweli Museveni amemtia kizuizini mpinzani wake mkuu ambaye amekuwa akidai Museveni ni dikteta.
Huku akiwa jela jana, washtakiwa wengine wanaoshtakiwa naye walipewa dhamana ya bei mbaya: dola elfu sita kwa kila mmoja.Pamoja na kwamba hela hiyo ililipwa lakini hawakuweza kutoka kwani wanajeshi walifika na kuiteka mahakama wakidai wanataka kuwakamata hao jamaa. somahapa Jamaa wakiongozwa na wanasheria wao walikataa kutoka na kuwa huru na wakabaki gerezani kwani haijulikani wanajeshi walitaka kuwapeleka wapi.
Nakwambia dalili za udikteta zimeanza kujionesha hapa.Lakini yote hii imemuongezea umaarufu Dr. Besyige, mpinzani mkuu wa Museveni.
Museveni jana alikutana na mabalozi wa nchi za majuu na akawatisha kwelikweli. Kuna kila dalili ya Museveni kuchokwa na waganda wengi lakini yeye sasa ameamua ni ubabe tu. somahapa
Ila ningependa pia msome makala moja nzuri sana ambayo inaeleza ni kwa vipi kumtia kizuizini Besyige kuna athari kadhaa na ni kwa vipi kunachangia demokrasia ya nchi hii iliyotawaliwa na wanajeshi. somahapa

KIROJA CHA MUSEVENI KUGOMBEA URAISI KWA MARA YA TATU

Haya wajameni, kumekucha hapa Uganda; kama nilivyoeleza mwanzon mwa wiki hii kulikuwa na vurugu sana ila mambo sasa ni shwari.
Leo nataka niwafahamishe kwamba sasa chama tawala hapa kimekuja na staili mpya yaani wajumbe wanajifanya wanamlazimisha Museveni agombee urais.Na yeye atauambia umma wa wananchi kwamba alilazimishwa: hiki ni kiroja cha karne.
Kwa ufupi Museveni kachukua fomu leo soma sasa sijui atarejesha au vipi lakini ndio hali halisi.

Tuesday, November 15, 2005

NJIA NYEUPE KWA MUSEVENI

Kama unakumbuka wakati dikteta wa Nigeria, Sani Abacha alipokuwa anajizatiti madarakani kila aliyekuwa akija mbele yake kama mpinzani aliishia lupango.Hayo yamemkuta mpinzani wa Museveni hapa Uganda jana. soma hapa

Monday, November 14, 2005

VURUGU ZA KISIASA ZATAWALA KAMPALA

Uganda ni vurugu tupu.Ule mradi wa rais Museveni tayari ameanza kuufanyia kazi.Ikitarajiwa wiki hii atajitangaza kama atagombea urais leo hii serikali ya hapa imemkamata na kumshtaki Kiiza Besigye kwa kujihusisha kwake na uasi.
Nakwambia ghasia zililikumba jiji zima la Kampala leo hii.Huu ni mwanzo wa Museveni kutimiza ndoto yake ya ushindi uchaguzi ujao.Kuanzia chuo cha Makerere hadi katikati ya mji ilikuwa ni vurugu tupu. ONA HAPA
Mapema leo katika gazeti moja hapa tayari watu walikuwa wametabiri juu ya kukamatwa kwake na wakatoa sababu kadhaa. soma hapa

Sunday, November 13, 2005

SIASA ZA KIJESHI UGANDA

Hapa Uganda kwa mara nyingine tena inaonekana wanajeshi hawatang'atuka na watafanya kila wawezalo kumlinda bwana Museveni. Wiki iliyopita, Mkuu wa Majeshi hapa alitoa mpya kudhihirisha kuwa Museveni asipingwe na atakayejaribu kumpinga atashughulikiwa.
Leo kuna uchambuzi mzuri wa athari za kauli ya mkuu wa majeshi. Somahapa uone je kweli Uganda inaelekea kwenye demokrasia?

MAALIM SEIF NI WAKUJA UNGUJA

Unaambiwa Zanzibar kama nilivyosema juma lililopita haitakaa itawaliwe na wapemba.Ndio maana nilishauri chama cha CUF kujifute alafu watu wa CUF wajiunge CCM siasa ziendelee, upinzani ndani kwa ndani. Ila leo nimevutwa na maandishi kabambe katika the gurdian la leo. soma hapa
Huyu bwana kanifurahisha nafikiri watanzania wakimsoma huyu mwandishi kuna msisimko fulani utaupata, unaweza kuamini Seif ni wakuja tu pale Unguja?Je ingewezekanaje awe raisi?
Angekubalika kweli?Kamwe nafikiri ndio maana kashindwa kwa mizengwe. Naiona hali sawa tu kwa upande wa Pemba kwani Karume naye hakubaliki huko. soma

Thursday, November 10, 2005

MUSEVENI KUTHIBITISHA KAMA ATAGOMBEA WIKI HII.

Mwishoni mwa wiki hii rais Museveni wa hapa Uganda atahitimisha yale mabishano ya muda mrefu iwapo atagombea urais tena kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.Chama tawala kinatarajia kuteua mgombea uraisi na tutajua je kweli huyu ni mpenda madaraka na je yale mabadiliko ya katiba kuondoa ukomo wa vipindi vya urais yaani miaka mitano mara mbili ilikuwa ni kwa ajili ya maslahi yake au la.bonyeza hapa
Huku umoja wa mataifa ukiwa umethibitisha kuwa kile kikundi cha waasi PRA kinachodaiwa kuongozwa na mgombea uraisi wa upinzani ambaye ni tishio kwa Museveni, inaonekana serikali hapa itamfungulia mashtaka mgombea huyo na hii itaondoa uwezekano wa Besyigye kushiriki uchaguzi.Je hii ni mbinu ya serikali au nini?Soma habari hii BONYEZA uone bonyeza Besigye anasema nini?

MGOGORO WA ZANZIBAR--SIASA MBOVU ZA NYERERE NA KARUME

Mgogoro wa siasa za Zanzibar kwa mara nyingine ni kielelezo kwamba Rais Benjamen Mkapa amefeli kuvirejesha visiwa hivi katika amani iliyopotea kwa muda mrefu.Inavyoelekea tunakwenda kumchagua Kikwete kuwa rais wetu kwa miaka mingine mitano au hata kumi kwani CCM ni utamaduni mtu hang'oki mpaka apige miaka kumi hata kama uchumi unakwenda kombo.
Katika pitia zangu za magazeti basi nikakutana na makala moja ndani ya East African, mwandishi anajaribu kuelezea mchango mkubwa wa hayati Mwalimu Nyerere katika siasa za muungano.Ni makala nzuri bonyezahapa ambayo kwangu imenifanya nione chanzo cha matatizo yote haya ni Mwalimu Nyerere na Karume kutuunganisha katika misingi mibovu.Kama unavyojua ukijenga nyumba katika msingi mbovu basi ujue utakuwa ukifanya ukarabati wa mara kwa mara.
Nimalizie tu kwamba Muungano huu ulijengwa katika msingi mbovu na ndio maana Mwalimu aling'ang'ania Mkapa awe rais ili aendeleze sera zake za kutoruhusu wapemba katika nafasi za uongozi kirahisi.Je Kikwete atafanya nini?Mimi nafikiri ni yaleyale tu.Dawa ni Wapemba waache siasa au wajiunge na CCM ili watoe upinzani wakiwa ndani ya CCM kwani tukumbuke upinzani ndani ya Bunge na Baraza la Wawakilishi ulikuwa mkubwa sana kabla ya siasa za vyama vingi kulinganisha na sasa.
Kweli tumekwisha.

ZANZIBAR--CUF KIJIFUTE CHENYEWE

Uchaguzi Zanzibar umemalizika, kasheshe kama zilivyotabiriwa tumeziona. Kama kawaida ule uadui wa miongo kadhaa umejionesha. Sikuamini wanasiasa wetu ni wajinga kiasi hiki.Nasema hivi kwa sababu pamoja na miafaka kadhaa kati ya vyama vikuu viwili, ambayo ilichukua pesa nyingi za watanganyika na wazanzibara bado imeonesha ilikuwa ni suala la kulipana mafedha tu alafu ghasia mtindo mmoja.
Mengi sitaki kusema ila nawashauri CUF wavunje chama tu manake hawatakaa washinde uchaguzi.Seif inasemekana anataka kuwa rais ona hapa kwa kila hali.Sina hakika kama ni kweli ila nadhani.Baada ya hali ilivyokuwa Zanzibar najiuliza hivi ni kwanini Seif tua au Lipumba tu ndio wagombea wa urais wa CUF kwa mwongo mmoja sasa?Kuna demokrasia ya kweli ndani ya chama au chama ni kama mali ya watu au kikundi fulani?
Wasiwasi wangu unanifanya nisijali sana juu ya mbinu chafu za uchaguzi za CCM huko Zanzibar kwani ni hatari kama Seif angelishinda uchaguzi sio ajabu asingeng'atuka kwa mujibu wa sheria.
Sijui wengine mnasemaje ila nafikiri baada ya uchaguzi huu ni wakati wa Lipumba, Seif, Mrema kupumzika. Inaelekea mtashindwa na hivyo waachieni vijana jamani.
Mwisho sijui nisemeje kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, sina haja ya kumpongeza Karume kwani sidhani kama ni mwanademokrasia halisi lakini ndio hivyo: "Mwenye nguvu mpishe".

Sunday, November 06, 2005

DEMOKRASIA UGANDA NI NDOTO

Pamoja na kwamba mwanasiasa wa upinzani wa Uganda, Dr. Kiiza Besyigye amerudi hapa baada ya kuishi uhamishoni, nchini Afrika kusini kwa miaka minne, tayari kuna wasiwasi baada ya chama chake cha FDC kufanya uteuzi wa viongozi wake na kupanga safu ya uongozi kupambana na Museveni.
Chama tawala hapa NRMO cha Museveni, kimejengwa chini ya jina la mtu kama mali yake na sio kama taasisi ya watu.Ila la kushangaza nimegundua hata hiki chama cha Besyige, FDC, ni kama cha Museveni tu.Soma hapa uone ni kwa jinsi gani Uganda ina safari ndefu kupata demokrasia.

RAISI ANAYEPENDA UJIKO HUYU HAPA

Tunaelekea katika uchaguzi wa hapa Uganda mwaka ujao.Rais Museveni ni dhahiri atashinda, baada ya kufanikisha mradi wake wa kufuta katiba ili awe huru kugombea tena.
Huyu ni mtu mwenye jina haswa hapa Uganda, ingawa siku za karibuni amepoteza sifa na haiba miongoni mwa watu makini baada ya kuonesha dhahiri anapenda madaraka kuliko demokrasia. Sasa hivi ameanza wazi kampeni za kupita na kusalimia wananchi huku binyahapa akiendesha gari mwenyewe. Huwezi kuamini lakini ndio katika njia moja ya kuonesha ukaribu na wananchi.Wengine watasema anajikomba lakini ndio siasa.
Mimi sina maoni sana isipokuwa nilifurahi kuona rais anaendesha mwenyewe, sijawahi kuona kabisa.Nafikiri hii mambo ya kutembea kwa misafara ni utumwa fulani ndio maana nimevutwa na hili.

Thursday, October 27, 2005

MANENO YA MWISHO YA OBOTE KABLA YA KIFO

Hii ni makala muhimu kwa wale wote wanaopenda kumjua halisi hayati Milton Obote, raisi wa kwanza wa Uganda aliyefariki hivi karibuni.Kwa mara ya mwisho kabla ya kufariki aliwahi kufanya mahojiano na kuongelea hisia zake juu ya maisha yake kwa ujumla.
Ukisoma hapa utajua taabu na raha za uraisi katika bara la Afrika.Na ningependa maoni yako msomaji kama kweli huyu bwana ni mwanaafrika halisi au ni ubabaishaji tu.

"MASTAA WA BONGO" KATIKA SIASA

Umuhimu wa wagombea wenye sifa ni jambo la maana sana katika uchaguzi wowote ule.Ndio maana mimi siungi mkono kabisa wasanii na wanamichezo wasio na haiba hasa ya kielimu kuchaguliwa viongozi kupitia mifumo ya kidemokrasia.
Najua ni haki ya kila mtu lakini nafikiri kuchaguliwa ni zaidi ya hapo.Hebu tizama kisa hiki cha wale tunaowaita mastaa wa bongo binya hapa anajaribu pia bahati yake.Jamani naomba mchangie kwa maoni mnaonaje hili?

JE NDESAMBURO ACHAGULIWE TENA MBUNGE--MOSHI?

Nimependa kauli iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro juu ya ukarabati wa hospitali ya Mawenzi. binyahapa Kwa muda mrefu hospitali hii ilikuwa katika hali mbaya ila leo hii inapendeza.
Nilikuwa Moshi miezi minne iliyopita nikatibiwa pale, kwa kweli niliridhika kwa kiasi fulani.Ila kumekuwa na hoja na tambo za wanasiasa eti wao ndio wamehusika na ujenzi wa hospitali ile.Kwa mfano, Mbunge wa Moshi Manispaa aliwahi kununua gari la wagonjwa katika hospitali hii.Na amekuwa akidai kwamba serikali ilishindwa na ni yeye tu anayefaa kuchaguliwa kwani huo ulikuwa ni msaada mkubwa.
Mimi nilikuwa nashangazwa kwa vipi gari moja la wagonjwa iwe ni hoja ya kumfanya mtu achaguliwe kwa miaka mitano?Ninahisi, huyu mbunge inawezekana lipo fungu la kununua gari la wagonjwa lakini yeye ananunua gari binafsi tena lililotumika na mengine anatia ndani.Kama si hivyo basi inawezekana ameshindwa kuihoji serikali, ambapo ni wajibu wake, ili ununuzi wa magari na sio gari la wagonjwa ufanywe.
Haya hebu tusubiri hapo Jumapili kama kweli Bwana Ndesamburo atachaguliwa kwa hoja za zisizo makini kama hizi.

JE NDESAMBURO ACHAGULIWE TENA MBUNGE--MOSHI?

Nimependa kauli iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro juu ya ukarabati wa hospitali ya Mawenzi.BONYEZA HAPAKwa muda mrefu hospitali hii ilikuwa katika hali mbaya ila leo hii inapendeza.
Nilikuwa Moshi miezi minne iliyopita nikatibiwa pale, kwa kweli niliridhika kwa kiasi fulani.Ila kumekuwa na hoja na tambo za wanasiasa eti wao ndio wamehusika na ujenzi wa hospitali ile.Kwa mfano, Mbunge wa Moshi Manispaa aliwahi kununua gari la wagonjwa katika hospitali hii.Na amekuwa akidai kwamba serikali ilishindwa na ni yeye tu anayefaa kuchaguliwa kwani huo ulikuwa ni msaada mkubwa.
Mimi nilikuwa nashangazwa kwa vipi gari moja la wagonjwa iwe ni hoja ya kumfanya mtu achaguliwe kwa miaka mitano?Ninahisi, huyu mbunge inawezekana lipo fungu la kununua gari la wagonjwa lakini yeye ananunua gari binafsi tena lililotumika na mengine anatia ndani.Kama si hivyo basi inawezekana ameshindwa kuihoji serikali, ambapo ni wajibu wake, ili ununuzi wa magari na sio gari la wagonjwa ufanywe.
Haya hebu tusubiri hapo Jumapili kama kweli Bwana Ndesamburo atachaguliwa kwa hoja za zisizo makini kama hizi.

Sunday, October 23, 2005

UGANDA--MARIDHIANO KWELI AU HADITHI ILE ILE?

Baada ya kifo cha Milton Obote, Uganda inaingia katika kipindi cha maridhiano.Ni wakati ambao waganda wameamua kuanza ukurasa mpya: yaani ni marufuku kwa mwanasiasa wa Uganda kuishi uhamishoni.Je hii ni kweli kama raisi Museveni alivyoahidi?
Wiki ijayo yule anatarajiwa kutoa upinzani kwa Museveni, kanali Kiiza Besigye anawasili hapa kuja kujiandikisha ili aweze kushiriki katika uchaguzi huo.Walakini katika maridhiano tayari umeanza kujionesha soma hapa.

TANZIA--KIFO CHA MILTON OBOTE


Dr. Appolo Milton Obote, rais wa zamani na wakwanza wa Uganda amefariki dunia.Amekuwa uhamishoni kwa miongo kadhaa tangu apinduliwe na Generali Tito Okello Lutwa ambaye naye alipinduliwa na Generali Museveni hapo mwaka 1986.Mengi yamesemwa hapa Uganda kwa kipindi cha wiki moja tangu afariki mzee huyu siku moja tu baada ya Waganda kuadhimisha siku ya uhuru.

Katika siku hii rais Museveni aliendelea kumlaani huyu bwana kama chanzo cha madhila kadhaaa zilizowahi kuisibu nchi hii.Alimwita na kunfananisha na nguruwe mwitu wakati wa hotuba yake katika viwanja vya Kololo mbele ya marais Mwai Kibaki na Pierre Nkurunzinza. Kama alivyowahi kusema katka mojawapo ya kauli zake, Shakespeare: “ Binadamu hufa na mazuri yote waliyoyafanya na yale maovu yanabakia kwa muda mrefu baada ya kuondoka kwao”. Ndivyo inavyoonekana hapa kwa mzee Obote; kwani kama ilivyo Sarafu, inazo pande mbili na huyu mzee anazungumzwa katika pande zake mbili yaani ubaya na uzuri.

Nilichogundua hapa Uganda Obote ni baba wa Taifa binyahapa na wala si Museveni. Alipofariki Idi Amia mwaka jana hali ilivyo sasa haikuwa hivi. Watu hawakuvutwa sana na kifo chake na wala hawakukazia aje azikwe hapa nchini mwake. Lakini, kwa Obote, ilibidi baraza la mawaziri likutane kwa saa nane na kuamua kumpa heshima za kitaifa za maziko. Kwa kipindi chote akiwa uhamishoni, mzee huyu amekuwa tishio kwa utawala wa Museveni na anachukuliwa na wengi kama mtu mjuzi sana, mwenye akili nyingi na mwenye dira ya kimantiki kuliko Museveni. Hii imenifanya nitanabaishe baadhi ya nukuu zake alizowahi kuzitoa kama kiongozi na hata zile alizotoa za mwisho mapema mwaka huu.

Umoja wa Afrika

Akihutubia kikao cha uundaji wa OAU mjini Addis Ababa, Mei 22-25, 1963. Alisema: Kama ni urithi kutoka Ukoloni, watu wetu wanakabiliwa na maradhi na umaskini. Tunahitaji katika kikao hiki kuja na azimio la Afrika nzima dhidi ya maradhi, ujinga na umasikini. Tuunde soko la pamoja, sarafu moja na mfumo wa ushirikiano wa ulinzi. Pia tuunde Bunge la pamoja(Pan—African) na serikali ambapo nchi zote ziwe tayari kupoteza baadhi ya hatamu za kiserikali.

Mapinduzi ya kijeshi

Huyu mzee alikumbana na mapinduzi ya kijeshi mara mbili. Sijui ni kwanini, ila labda ni kwasababu mwaka 1968 kabla hata kupinduliwa kwa mara ya kwanza tayari alikwisha onesha chuki dhidi ya tawala za kijeshi. Kwa mfano, aliwahi kumuandikia waraka, rafikiye aishie London ambaye alikuwa mwandishi wa habari, Bw.Colin Legum wa gazeti la Observer kama ifuatavyo:

“Siwezi kukubali mwanajeshi kama mkombozi kwani anatumia kinyume na katiba silaha za Taifa kujifanya mwanasiasa, kazi ambayo sio yake. Hii naichukulia kama ufisadi au rushwa ya hali ya juu.” Akaendelea zaidi eti kwa maoni yake wanasiasa kama Nyerere, Kenyata au Nkrumah waliona uwezekano wa nchi zao kuwa huru wakasota na kujitoa mhanga na kufanikiwa angalau kufikia ndoto zao(kuleta uhuru)

Ni vigumu kwa hawa kuwa wafisadi ama wala rushwa ukilinganisha na wanajeshi ambao hawakushiriki katika kutunga sera mbalimbali wala hawakudhalilishwa na wakoloni zaidi ya wanaharakati kama akina Nyerere. Kwa Obote, wanajeshi hawana uchungu na nchi zao na ni watu ambao watakuwa ni wala rushwa zaidi ya serikali za kiraia.

Kujitegemea

Baada ya kuishi Tanzania, uhamishoni, kwa miaka tisa, Obote alirejea nchini Uganda hapo Mei 27, 1980. Alitua sehemu iitwayo Bushenyi na katika hotuba yake alizungumzia umuhimu wa kujitegemea. Nashiwishika kuhisi labda swahiba wake, Mw. Nyerere, alishampa dozi za sera za ujamaa. Aliwaambia wananchi waliokuja kumpokea:

“Tusisahau kujitegemea, umuhimu wa kujitegemea uwe ni kwa maendeleo yajayo au usalama binafsi. Idi Amin alifanya uharibifu mkubwa wa nchi yetu sawa kabisa na mauaji ya ‘kimbari’. Isipokuwa Tanzania, Zambia, Somalia, Botswana na Sudan hawakukaa na kutizama tu.”

Mara aliilaani OAU eti ilimuenzi huyu fisadi na kumkabidhi uenyekiti wa umoja huo kwa mwaka mmoja katika mkutano wake wa Kampala 1975.Akamalizia hotuba yake kwa kuifagilia Tanzania: “Mwishoni taifa dogo—Tanzania—likiwa na rasilimali chache liliamua kuwajibika na kuamsha hisia za ulimwengu. Liliachwa na kupigana na kugharimia vita hiyo lenyewe.”

Majuto
Katika kufeli kwake, anachukulia kwamba alichemsha sana katika kulidhibiti jeshi. Obote anajutia kumuamini sana Idi Amin kama mkuu wa majeshi.

Kuhusu serikali ya sasa

Pamoja na kukaa uhamishoni kwa muda mrefu, Obote na Museveni hawapikiki kabisa. Katika mahojiano yake ya mwisho na gazeti la monitor mapema mwaka huu huko Lusaka alizungumza mengi: “Kama kwa ajali ya kihistoria nikakutana na Museveni, nitamtandika kama nina fimbo karibu. Hii ndio namna ninavyomchukia huyu bwana” Alijigamba eti chochote watu watakachosema au Museveni atakachosema juu ya Uganda yeye atabakia kama baba wa Uganda. Na kweli hii imedhihirika baada ya kifo chake kwani hata nyumba yake binafsi jijini Kampala ambayo ilikuwa inakaliwa na wanajeshi kwa miaka yote hiyo imebidi irudishwe rasmi kwa familia yake.

Dhidi ya serikali za kifalme

Akihutubia bunge mwaka 1965, alisisitiza kwamba serilkali lazima izingatie matakwa ya watu, utaifa na sio mtu mmoja kuupata uongozi eti kwa sababu ya hadhi ya mababu zake wa zamani.

Kiongozi bora

Kiongozi bora ni lazima atosheke na mfupa kama anapewa na asiangalie ile sehemu yenye mafuta au ile sehemu tamu sana ya nyama. Kwa Obote amefariki akiwa na nyumba yake ya zamani kule kijijini kwake Apac na nyingine hapa Kampala ambayo kwa kipindi kirefu imekuwa ikitumiwa na serikali.

Nimepima hisia za watu hapa bonyeza hapa na picha inayojitokeza ni kwamba huyu bwana kaifanyia nchi yake mambo mengi sana ya kukumbukwa. Doa kubwa kwake ni mauaji ya raia wa kabila la Wabaganda wapatao 300,000 katika sehemu iitwayo Luwero Squire. Hii ilikuwa katika vita kati ya majeshi ya serikali yake na yale ya waasi waliokuwa wakiongozwa na Museveni. Kiundani utaona huyu mzee hakushiriki vita hii ila anawajibishwa kwa makosa ya makamanda wa jeshi ambao walioshiriki mauaji kwa wakati ule. Mtu makini utajiuliza: vita ya makundi mawili iweje upande mmoja unawajibishwa?

Ndio maana sio ajabu wakazi wa Luwero walicheza dansi na kunywa pombe kusheherekea kifo chake.

OBOTE AZIKWA

Kesho jumatatu, raisi wa zamani wa hapa, anazikwa rasmi huko nyumbani kwake kijijini Akokoro, wilayani Apac Lira. Kwa ufupi tu huyu bwana kafariki akiwa na pande mbili za maisha bonyeza hapa yake zinazoshabihiana.

Ni kiongozi aliyefanikiwa kuiletea uhuru nchi hii na kuijenga kitaasisi katika hatua za mwanzo.Ila pia ni kiongozi aliyefeli kabisa na atakumbukwa kama mtu aliyepata nafasi ya kujirekebisha lakini akashindwa kuitumia na hatima yake ilimbidi akimbilie ukimbizini hadi alipofia huko.

Unaweza ukaziona hisia mbalimbali za watu wa hapa Uganda wakijaribu kumhukumu na wengine kumsifu.Wakati wa mazishi ya kiserikali rais Museveni alimsifu Obote kong'oli hapa ikiwa ni siku kumi na nne tu zilikuwa zimepita pale alipomfananisha na nguruwe mwitu aliyesababisha madhila kadhaa za nchi hii.Ama kweli Museveni kigeugeu.Yuko Mzee mmoja kanifurahisha sana na maoni yake kwani yeye alifanikiwa kukutana na maraisi karibu wote waliowahi kuitawala nchi ya bonyeza hapa Uganda na anatoa ushuhuda wake jinsi alivyomfahamu Obote.

JE WASANII NA WANAMICHEZO WANATUFAA KATIKA SIASA?

Imekuwa ni tabia ya kawaida kwa wasanii mbalimbali kujiingiza katika siasa hivi karibuni. Kama tunavyofahamu haka kamchezo kanakoitwa demokrasia imekuwa sasa ni kawaida kila mtu kujaribu bahati yake hata kama hana ujuzi wa kuongoza. Jamii imegeuza uongozi kuwa kama suala majaribio.Yaani mtu amelala nyumbani kwake basi anaota anaweza kuwa mbunge, diwani au hata raisi na kesho yake anachukua fomu na kugombea. Wasiwasi wangu tunakoelekea ni kubaya sana na kama tusipoangalia tutajuta.

Tunapoelekea katika uchaguzi mkuu Tanzania siku chache zijazo, nimeona leo nikumbushie juu ya wasanii na siasa.Huko Liberia, mwanakandada George Weah anatarajia kugombea katika uchaguzi na mwanamama Elen Johnson Sirleaf hapo November 8. Tanzania nako watakuwepo wagombea wengi tuu katika kundi hili la wasanii, wanamichezo ambao kutokana na umaarufu wao michezoni ambao kwa kiasi Fulani haujasaidia sana kuinua hadhi ya nchi yetu wanafikiri wanaweza kutuongoza.

Katika pitia pitia yangu ya mambo wiki hii nimeona nikumbushe juu ya watu kama Weah, Arnold Schwarzneger, Estrada wa Philipines pamoja na yule Ronald Regan.binya hapaWote hawa na wengine ambao utawafahamu kwa mara ya kwanza wameelezewa vizuri sana hapa na jarida la Vision la hapa Uganda. Hebu tuwatizame walifanya nini na nini mchango wao katika siasa. Hapa lazima nikiri kwamba pamoja na kwamba napenda soka sana lakini George Weah sio chaguo langu kabisa.Ningependa mwanamama aibuke mshindi, sijui itakuwaje manake bara la Afrika pia linahitaji mwanamama. Ili tuone nao wana nini cha kulikwamua bara hili.

Saturday, October 22, 2005

Tukiwa tumemaliza kumkumbuka Mwalimu Nyerere hivi majuzi tu, rafikiye wa karibu ambaye inaaminika ni miongoni mwa wale wakombozi wa bara hili, Milton Obote alifariki.Leo sitazungumzia sana kwani mengi nitasema wiki ijayo.
Ila nimevutwa na ile paper ya Profesa Harob Othman aliyowasomea wanafunzi wa Chuo kikuu cha Cape Town juu ya Mwalimu.Wakati nikipitia globu ya PAMBAZUKO sikusita kuiweka katika ukurasa wangu.Kong'oli hapa uisome kama una muda. Namshukuru Nkya kwa kuniwezesha.

Friday, October 14, 2005

MWALIMU NYERERE KUTANGAZWA MTAKATIFU?

Leo kama mtanzania hapa nchini Uganda sina budi kumkumbuka mpendwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.Mengi yamesemwa ila huyu ni mtu wa kipekee kuwahi kutokea katika kizazi cha viongozi wa bara la Afrika.
Ila nimechoshwa sasa na kila mwaka tunapoadhimisha siku kama hii utasikia wanasiasa wakilia eti "Tumuenzi Baba wa Taifa".Sina hakika kama kweli tunamuenzi ipasavyo ila natumaini siku moja tutahukumiwa na kauli zetu.
Hapa nchini Uganda, siku hii imekuja katika wakati ambao swahiba wa Mwalimu, yaani Raisi wa zamani wa nchi hii amefariki dunia akiwa uhamishoni huko nchini Zambia.
Vyombo vya habari hapa vimetawaliwa na habari kumhusu huyu mzee ambaye alipinduliwa mara mbili wakati wa uongozi wake.Tukiwa bado tunasubiri kumzika marehemu Milton Obote,hapa hakuna mengi juu ya Mwalimu Nyerere.Nimesoma Nkya kule Cape Town wameandaa mdahalo maalum juu ya Mwalimu nafikiri ni hatua kubwa na ya kujivunia.Isipokuwa kilichonipa ahueni wiki hii lile gazeti maarufu katika ukanda huu wa Afrika,"The East African" lilichapisha makala kadhaa za kumsifu na kumkukumbuka Mwalimu.
Kuna kitu kimoja ambacho kilinifanya niamini kweli Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi wa kuigwa. Mwanaye wa kwanza, Madaraka Nyerere alichapisha makala nzuri inayoelezea maisha ya Mwalimu baada ya kustaafu.Ni makala ambayo ningependa wanaglobu wote waisome.Hivi mnajua kanisa katoliki nchini Tanzania limeanza kufanya taratibu za Mwalimu kutangazwa "MTAKATIFU"?bofya hapa
Binafsi siungi mkono mtu kuwa mtakatifu kwa vigezo ambavyo huwa vinaangalia upande mmoja ila nadhani hii ni hatua dhahiri kuonesha huyu mtu alikuwa ni kiumbe cha ajabu.
Mimi nimemkumbuka kwa kusoma makala kadhaa katika toleo la The East African wiki hii.

Monday, October 10, 2005

Hongera:Togo,Ghana,Ivory Coast na Angola.

Hatimaye bara la Afrika litawakilishwa katika michuano ijayo ya kombe la dunia na timu nne mpya kabisa:Togo, Ghana,Angola na Ivory Coast.
Kwangu mimi ilikuwa ni raha sana manake hawa jamaa wa Nigeria, Cameroon na Senegal baada ya kupata mafanikio walijiona wao ndio basi na wakajisahau kabisa. Hawa mabwana, ukitoa Senegal, wametuwakilisha mara nyingi bara la Africa bila mafanikio yoyote. Hasa Cameroon sikutaka kabisa ifuzu michuano hii.
Tatizo kubwa la Nigeria na Cameroon ni uongozi mbovu wa michezo pamoja na wachezaji wasiotulia waliolewa mafanikio.Ukienda kwa Angola utaona hii ni nchi iliyotoka vitani karibuni na sasa iko kombe la dunia.Ukilinganisha na Tanzania ni nchi inayosifika duniani kama kisiwa cha amani tangu uhuru lakini haijawahi kutoa hata kikombe hata kimoja cha michuano ya Afrika katika mchezo wowote achilia mbali kufuzu kombe la dunia.
Hivi Tanzania tunani? Hivi wizara inayohusika na michezo ipo kweli? Kuna haja ya kwenda Angola tukapewe somo; wenzetu ni mabingwa wa bara la Afrika katika mchezo wa mikono na wa vikapu.Sasa wamefuzu kwenda kombe la dunia na huenda wakalitwaa kombe la mataifa ya Afrika mapema mwezi januari.
Sasa hivi Tanzania imejaa vijana wengi wasiokuwa na kazi, elimu hakuna ni kuvuta bangi tu.Nasikia hata viwanja vya kuchezea vimeuziwa wenye nazo wakajenga mahekalu;hii ni laana nasema.
Michezo mashuleni imezikwa; haya tuko kwenye kampeni sijasikia sana kuhusu michezo, hivi kweli tunajua michezo ni ngao ya kuunganisha nchi na kujenga umoja ukiachilia mbali kuitangaza nchi?
Naumia roho sijui nisemeje ila nizipongeze na kuzitakia mafanikio timu tano zilizofuzu.