My Blog List

Tuesday, September 25, 2007

SHIRIKISHO LA AFRIKA MASHARIKI KUREJESHA ENZI ZA FALME YA BUNYORO KITARA

KUTOKA "FAST TRACKING HADI DOUBLE TRACKING"--SHIRIKISHO LA AFRIKA MASHARIKI KATIKA MCHAKATO MPYA.

Hivi majuzi jumuiya ya Afrika Mashariki ilipigwa butwaa baada ya kuripotiwa kuna juhudi za kichinichini kuanzisha shirikisho kati ya Uganda na Kenya na kuiacha Tanzania kwani inaonekana kuzuia mawazo ya rais Yoweri Museveni ya kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki ifikapo mwaka 2013. Ghafla kama wiki mbili zilizopita kumeripotiwa eti Museveni anaendeleza ushawishi na Kenya ili Uganda iungane na iunde Shirikisho na kuiacha Tanzania ambayo inaonekana bado inasita kwa mujibu wa ripoti ya kamati ya maoni ya wananchi wake.

Asilimia 80% ya watanzania hawakuunga mkono wazo la Shirikisho kuharakishwa ingawa asilimia 97% waliunga mkono wazo la Shirikisho hatua kwa hatua. Habari hizi za juhudi za chinichini za Museveni hazikunishangaza hata kidogo bali zimenisukuma kuandika makala ya leo hii.Leo nataka tushirikishane ndugu wasomaji wetu ni kwa vipi haiba ya rais Museveni inaashiria ni mtu wa kuburuza mambo yake yafanyike hata pale inapohitaji watu kushirikiana na kuheshimu maamuzi ya pamoja. Ningependa tutafakari kama kweli Museveni ana malengo yenye tija kwa watu wa Afrika Mashariki au ni janja ya maslahi binafsi? Je watanzania tunamfahamu mtu huyu hasa au ni jujuu tu?Pia ni lazima tuone kama kweli mtindo wake wa uongozi wa Uganda kwa miaka zaidi ya ishirini unampa sifa kutuongoza katika utengamano? Nitaanza kwa maoni juu ya kikao cha mwisho cha viongozi wetu pale Arusha mwezi uliopita.

Kwanza kabisa, viongozi wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walipokutana Arusha mwezi uliopita walifanya maamuzi kamambe ili kuokoa juhudi za ufufuaji wa jumuiya ambapo ilishaanza kupingwa na wananchi katika kura za maoni hasa Tanzania. Kubwa lilikuwa juu ya kuharakisha uundaji wa shirikisho ifikapo mwaka 2013.

Nilipokea maamuzi ya viongozi wetu kama tukio la aina yake kwa viongozi wetu kwa mara ya kwanza baada ya maberamu dhidi ya kuharakisha shirikisho kuzidi sana wameamua waanze kusikiliza sauti ya watu. Nakumbuka niliwahi kuwafananisha na kondoo ambaye anapelekwa machinjioni asiyejua kuna kifo katika makala yangu ya tarehe 26/08/2007 dhidi ya uharakishaji huu. Viongozi wetu walikubaliana kubaki na lengo la kufikiwa kwa Shirikisho ila kwa sasa ni lazima taasisi nyeti ziundwe kwanza. Kwa maana nyingine tuanze kuungana kiuchumi--kibiashara na shughuli kadhaa za kijamii. Ila serikali moja si wakati muafaka. Mimi ni muumini wa hili waliloamua kule Arusha mwezi uliopita. Yaani muungano wa Ushuru wa Forodha, Soko la Pamoja na hata Sarafu Moja, uhuru wa watu kuvuka mipaka kama wafanyabiashara, wafanyakazi na hata bidhaa bila vipingamizi visivyo vya lazima pamoja na mambo mengi chungu mbovu ambayo tayari yanafanyika hadi sasa.

Binafsi, ninaamini kabisa Shirikisho halina tija kwa jamii ya Afrika Mashariki ila tu mashirikiano ya kiuchumi ndiyo yenye tija. Tukiharakisha shirikisho bila kuwa na taasisi (institutions) zenye nguvu kukabili nyanja mbalimbali za mahusiano ni bure na ndio hapa panaponifanya niamini kuna mizengwe ya wazito fulani wenye mkakati binafsi usiozingatia maslahi ya wananchi kwa ujumla wao. Malengo ya utawala bora katika nchi zetu bado hayajafikiwa hasa nchini Uganda sasa je kweli mtu ambaye hajafanikiwa kuleta utawala bora ana nini kipya katika Shirikisho? Je ni kwanini nina wasiwasi sana na juhudi za raisi Museveni?

KUTOKA MCHAKATO MMOJA HADI MIWILI (FAST TRACKING TO DOUBLE TRACKING)
Baada ya kikao kile cha Arusha, tarehe 20, August 2007, ni wazi mwelekeo wa muundo wa Shirikisho umekumbwa na wimbi jipya. Raisi Museveni inaripotiwa, na gazeti la 'Sunday Monitor' la tarehe 23, September 2007, alimtuma mjumbe maalum kwa mwenzake wa Kenya akimhimiza rais Kibaki kuunda Shirikisho jingine lisilojumuisha Tanzania lakini litakalotoa mwanya kwa Tanzania kujiunga itakapokuwa tayari. Ni mchakato mpya ambao wachunguzi wa mambo ya siasa za jumuiya ya Afrika Mashariki, wanadai ni mpango utakaoendeshwa kwa staili tofauti ya uharakishaji kutoka ile ya "Fasttracking hadi Double Tracking". Serikali ya Uganda haijakanusha haya kwa hivyo ni wazi juhudi hizi ni za kweli. Hapa Museveni anaonesha ni jinsi gani asivyopenda kusikiliza maoni ya watu wengi; au kwa maana nyingine anamaanisha lile zoezi zima la ukusanyaji maoni halikustahili labda. Watu wameamua sivyo na yeye anaamua kuja na mkakati mpya.

Kwa maana nyingine, Kenya na Uganda zinatangulia na Shirikisho wakati Tanzania nayo ikija kwa mwendo wa pole.(Double Tracking). Tayari jina la Shirikisho hilo limebuniwa, nalo ni "Muungano wa Wenye Nia" (Coalition of the Willing). Hata makao makuu mapya inasemekana yanatajwa kama yatakuwa ya muda kule Entebbe Uganda wakati wakisubiri ya kudumu kule katika mji wa vilima wa Tororo Uganda. Hii yote inaaminika itashinikiza Tanzania kufikiri na kubadili msimamo. Wachunguzi wa jinsi juhudi za Museveni zinavyohakikishwa zinafanikiwa, ni kwamba baada ya ugunduzi wa mafuta katika ukanda wa eneo la ziwa Albert (Albertine) basi inapanga kutumia nguvu ya fedha ya mafuta hayo kuhakikisha siku za usoni ndio inakuwa na ushawishi mkuu katika eneo zima la maziwa makuu. Mafuta yatatumika kama rungu ama silaha ya kidiplomasia kuhakikisha mradi wowote wa mashirikiano ukibuniwa na Uganda unafanikiwa kwa vyovyote vile.
Binafsi Museveni kaamua kuihujumu Tanzania kiaina kwani kama kweli ana nia njema ni kwanini tayari wana mawazo ya makao makuu mapya? Na kama ni kweli wamefikia hatua hii ina maana tayari Museveni alikuwa na mipango tayari kwani si mambo rahisi tu kuamua ni wapi pa kujenga makao makuu ya muda na pia ya kudumu bila kuhusisha maamuzi ya taasisi kama Bunge.

MASLAHI YA NCHI NDANI YA SHIRIKISHO
Inaripotiwa pia kuwa katika kuishawishi Kenya iunde Shirikisho jipya-Wenye Nia-Uganda imeihakikishia Kenya itafaidika 'kiuchumi' kwa kupanua soko la bidhaa zake hadi Rwanda, Burundi, Uganda, Sudan ya Kusini na hata Kongo-DRC. Kwa upande wa Uganda, yenyewe imebainisha maslahi yake ni ya 'kisiasa' ikimaanisha hapa ni wazi Museveni anawaza zaidi utawala. Ni katika mtizamo huu najiuliza je kama Tanzania tunajiunga na mchakato huu wa Shirikisho, je maslahi yetu ni nini?
Ni wazi iwe isiwe, Kenya ina uchumi mkubwa na imara kuliko nchi zote na ndio itakayofaidika zaidi. Lakini sisi kama Tanzania ili tuamue kujiunga na wenye nia, ni lazima tuwe makini na tujue maslahi yetu ni yapi la sivyo hakuna haja ya sisi kuwa kwenye shirikisho.

WASIWASI--CHUKI ZA KIKABILA UGANDA
Kuna tatizo kubwa sana la chuki kali sana za kikabila nchini Uganda na ni vizuri ieleweke kuwa hii ni sababu ya kihistoria katika nchi hiyo kwa kiasi fulani. Ikumbukwe kuwa Uganda ilipata uhuru wake Waziri mkuu wake wa kwanza na baadaye Raisi alikuwa ni Dr. Milton Obote mzaliwa wa Kaskazini mwa Uganda. Huyu aliwajaza jeshini wazaliwa wa kaskazini kwani ndio waliokuwa wakitumika shughuli za jeshi tangu wakati wa ukoloni. Baadaye alipinduliwa na Iddi Amin ambaye alitoka kaskazini pia na akaendeleza utawala wa watu wa kaskazini katika kila nyanja.
Hadi anakuja kupinduliwa na majeshi ya Tanzania yakisaidiana na wakombozi wa Uganda chini ya watu kama Yoweri Museveni na wengine Uganda ilikwishatawaliwa na watu wa kaskazini kwa miongo zaidi ya mitatu tangu uhuru. Obote alirudi madarakani kwa uchaguzi uliojaa mizengwe ya kitanzania inavyodaiwa ambayo ilimfanya Yoweri Museveni kuamua kurudi msituni kwani alidai uchaguzi kuendeshwa kimizengwe. Ikumbukwe aligombea urais wakati huo-1980 na kushindwa vibaya. Ila baadaye Obote alipinduliwa na Tito Okello; hali yote hii ikiendeleza utawala wa watu wa kaskazini. Tito Okello akapinduliwa mwaka 1986 na Yoweri Kaguta Museveni akachukua hatamu kuifufua nchi ambayo ilikwisha poromoka kiuchumi hadi kufikia hatua mbaya (failed state).
Kwa umahiri mkubwa kabisa Museveni akaweza kuifufua nchi na kuisimamisha hadi kuwa sawa na majirani zake kwa sasa. Ni jambo ambalo atajivunia hadi kaburini; ila uongozi wake ulikuwa wa mabavu, yaani mfumo wa "vuguvugu-movement"ambao haukuruhusu vyama vya siasa. Katika kipindi chake cha uongozi ni wazi serikali ya NRM imekuwa ikiongozwa chini ya viongozi kutoka makabila ya magharibi (westerners) katika nyadhifa zote za juu. Hali hii imejenga chuki kati ya watu wa kaskazini na kusini kwani inaaminika baada ya Museveni kuingia madarakani basi ulikuwa ni mwisho wa wakati wa watu wa kaskazini kutesa.
Hisia hizi pia ziko kwa watu wanaounga mkono hata ule uasi wa LRAkule kaskazini. Hali inamfanya Museveni kuwa mwoga na maisha baada ya urais na hivyo kuharakisha uundwaji wa Shirikisho ili aendelee kuwa kwenye hatamu za uongozi wa juu na asiyeweza kuguswa na vyombo vya sheria.

Kama sijakosea ni wazi wazo la kuharakishwa kwa shirikisho lilianzishwa na Rais Museveni na mara moja aliweza kuwashawishi wenzake na likapewa kipaumbele na ndio ikaundwa kamati ya kukusanya maoni ambayo kwangu ulikuwa ni ubadhirifu mkubwa iwapo ni kweli Museveni anaishawishi Kenya kuendelea na juhudi za kuharakisha baada ya Tanzania kutokuunga mkono wazo lake. Inaonekana alitegemea serikali ya Tanzania ingefanya mizengwe na kutosikiliza sauti ya wananchi.

Moja ya udhaifu wa Museveni ni mtu anayependa ubabe na anapokuwa na nia ni lazima itekelezwe. Kwa mfano, amekwamisha suluhu ya vita ya LRA kwani anawafananisha na majangili (thugs) akidai ni kikundi kidogo cha wahuni lakini la kushangaza ni miaka zaidi ya ishirini ameshindwa kuwamaliza. Wakosoaji wake wanadai hawajali sana watu wa kaskazini dhidi ya mateso ya vita na hapa pamemjengea chuki kubwa dhidi ya watu wa kaskazini. Binafsi nina marafiki kadhaa wanaotoka kaskazini mwa Uganda ukiwasikiliza hawafichi chuki zao dhidi ya makabila ya magharibi na kusini kama ndio chanzo cha madhila ya kaskazini. Ikumbukwe tangu Museveni aingie madarakani, Uganda iko chini ya watu wa magharibi wanaojulikana kama (westerners): wanyankole, watooro, wachiga, na wanyoro. Niliwahi kuzungumza na jamaa mmoja wa kabila la la magharibi 'mtooro', akaniambia "acha jamaa wateseke, walitutesa sana nyakati za Amin na Obote". Ni wazi kuna chuki za kisirisiri dhidi ya watu wa sehemu fulani ya nchi (xenophobia) ambapo Museveni hajafanya juhudi za kutosha kuziondosha ingawa ana uwezo huo. Ni nadra sana kwa watu wa kaskazini kuoana na watu wa magharibi.
Kwa mantiki hii, Rais Museveni lazima abebe lawama kama mtu asiye na haiba ya kuunganisha jamii kuishi kwa utengamano; na ndiye mtu anayedai anaweza kuiongoza Shirikisho la nchi tano kuishi kwa utangamano. Ni kiroja na siamini kama kweli anatufaa.

KUCHIPUA KWA MBEGU YA CHUKI

Baada ya mapinduzi ya mwaka 1986, mbegu ya chuki za kikabila ndipo ilipoanza kuchipua hasa. Museveni akampindua Tito Okello; askari wa Okello walikimbilia Kaskazini wakipita Jinja, Tororo hadi Lango na Acholi--kaskazini na kuanzisha uasi ambao hata hivyo haukuwa na nguvu. Baadaye Museveni aliwashawishi waasi na kukaa mezani na baadhi ya makamanda wao wakakubali yaishe na wakazawadiwa nyadhifa serikalini. Mmojawapo alikuwa Jenerali Moses Ali ambaye alikuwa mmoja wa vigogo wa vyeo vya juu kabisa hadi uchaguzi wa mwaka jana. Askari ambao hawakutaka suluhu walibaki msituni na ndio ukawa mwanzo wa uasi chini ya mama Alice Lakwena na baadaye Joseph Kony hadi leo.

Wote hawa wamekuwa na madai mengi mojawapo kuchukizwa na 'unyanyapaa' dhidi ya makabila ya kaskazini. Kuthibitisha haya, taasisi zote nyeti za serikali na idara zake ziko chini ya watu kutoka magharibi-kusini ukiacha spika wa Bunge. La kushangaza kama ni wasomi waliobobea wengi wanatoka Kaskazini na Mashariki--Lango, Pakwach, Acholi, Pader, Teso, Tororo n.k. Hawa wapo nchi za nje kama Marekani, Canada, Uingereza, Australia huku kukiwa na tetesi miongoni mwao ni wafadhili wakubwa wa LRA.
Kwa maelezo hapo juu, hii ndio jamii iliyo chini ya mtu anayetaka kwa nguvu za ushawishi mkubwa tuunde Shirikisho; tujiulize je kweli ana jipya kama kashindwa kuunganisha nchi yake? Je nchi tano ataziweza? Ni wazi ni kiongozi anayeongoza sehemu moja ya nchi kama vile eneo lililotekwa kivita (conquered territory). Yaani watu wa kaskazini kwa miongo kadhaa wamekuwa wakiishi katika makambi (IDPs) chini ya hali ya hatari kwa muda wote. Kisa ni serikali kukosa busara za kumaliza vita; yaani kushindwa kukang'amua njia bora ya kutatua tatizo la LRA na badala yake kusisitiza njia za kijeshi ambazo zimeshindwa kabisa. Ni hivi majuzi baada ya uchaguzi ambao ulionesha mgawanyiko mkubwa wa wananchi ndipo angalau Museveni akakubali kukaa mezani japo inaonekana huenda akarudi msituni.

JE NI LAZIMA AWE RAIS WA KWANZA WA SHIRIKISHO?
Ukiacha sababu ya woga wa maadui asiyewafahamu (paranoia), Rais Museveni ana tabia ya usaliti kwa wale anaoshirikiana nao hasa watu makini wenye misimamo. Hii inajionesha wazi baada ya Museveni kuwaahidi wanachi mwaka 2001 kuwa alikuwa akigombea kwa mara mwisho alikuja kugeuka na kuwahonga wabunge shilingi millioni tano kila mmoja ili wabadili katiba kuondoa ukomo wa rais kugombea vipindi viwili vya miaka mitano.

Hii ilimruhusu kugombea kipindi cha tatu maarufu kama "third term" kitu ambacho kilimtenganisha na watu waliokuwa nae karibu sana tangu harakati za msituni. Wale wote katika baraza la mawaziri ambao hawakumuunga mkono aliwafukuza kazi kwa kisingizio cha kutokuheshimu utendaji kazi wa pamoja(collective responsibility). Kwa mfano, alikuwepo mtu wake wa karibu tangu utotoni, Eriya Kategaya, ambaye alikuwa waziri mkuu na ambaye sasa hivi amemrudisha tena kama waziri wa Afrika Mashariki na naibu waziri mkuu. Meja Amanya Mushega, katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki aliyepita pia alifukuzwa uwaziri na amekuwa akisimamia misimamo thabiti ya kidemokrasia. Hali hii ni kitu kilichompotezea marafiki wa karibu kwa kipindi kuelekea uchaguzi mkuu uliopita.

Pili, uchaguzi mkuu uliopita aligombea kwa mara ya tatu baada ya kubadili katiba na upinzani ulikuwa mkali ajabu ambao ulihitaji mahakama ya kijeshi "Court Martial" iliyokuwa chini ya Jenerali Elly Tumwine, mzaliwa pia wa kabila moja na rais kutumika kumuundia mashtaka ya bandia mpinzani wake mkuu. Hii ilimnyima mpinzani wake kupata muda wa kutosha kupiga kampeni na badala yake kukimbizana na kesi muda wote. Hali hii iliongeza ukinzani au mbinyo wa mataifa wafadhili kwa Museveni. Ni wakati huu alipoona ndoto ya kuendelea kung'ang'ania madaraka siku za usoni itakuwa ngumu sana na akaanzisha wazo la kuharakisha shirikisho "fasttracking". Inawezekana kabisa anaamini atakapomaliza uraisi wake 2011, atakuwa na mwaka mmoja wa kampeni na mwaka unaofuata anachukua hatamu za uongozi.

Tatu, kuna kanuni ya hila "conspiracy theory" inayodai kuwa Museveni kama mtoto wa chifu wa kabila la Wanyankole-Hima, ana tabia za kutawala kwa kujitanua kupitia uvamizi wa mataifa jirani "expansionism". Hii ni tabia ambayo ameshaionesha tangu asaidie kuikomboa Rwanda, na baadae akaivamia Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo. Utaona baada ya kusaidia juhudi za ukombozi alitaka pia kuzitawala nchi hizo kwa kuwageuza viongozi wa nchi hizo kama vikaragosi wake (puppets) kitu ambacho kilimgombanisha na watu kama raisi Kagame na hata sasa hana uhusiano mzuri na rais Kabila. Kwani anajulikana anaunga mkono mpinzani mkuu wa Kabila, Jean Pierre Bemba. Ni hisia hizi zinadhaniwa na wengi labda ndizo zinazomsukuma ili atakapokuwa chifu wa Shirikisho si ajabu akatunisha misuli yake na kuteka nguvu za serikali za nchi shirika. Kitu ambacho kinaweza kuja leta matatizo sana.

Kanuni hii ya hila za Museveni inachangiwa na muundo halisi wa serikali yake kama nilivyokwisha eleza awali imejaa watu wa kabila lake hasa. Mwandishi mmoja, aliwahi kusema ni serikali inajionesha katika mantiki ya muungano wa kikabila yaani akaiita "Kinyoro Kitara Kingdom". Ikumbukwe kihistoria Bunyoro Kitara ilikuwa falme kubwa ilijomuisha makabila kadhaa chini ya Mfalme mmoja. Makabila haya ni kama Wanyankole (kabila la Museveni), Watooro, Wabusoga, Wanyoro, Karagwe na hata Wabaganda. Katika mtizamo huu si ajabu historia inaweza kujirudia kupitia kinara mkuu--Museveni. Ni kama serikali ya kifalme hivi kwani hata vigogo wa juu kabisa ni ndugu wa damu. Kwa mfano, binti wa Museveni kaolewa na kijana wa Waziri wa mambo ya nje--Sam Kutesa. Kwa mujibu wa tamaduni zao, watoto wa vigogo wanaoana wao kwa wao kutoka kabila moja: wanyankole. Ni kama serikali ya kifalme hivi (monarchy)

Jambo lingine ni hatua ya mama Janet Museveni, mke wa Museveni, kugombea ubunge uchaguzi mkuu uliopita. Inasemekana Museveni alipinga sana hatua za mkewe kugombea ubunge japo familia nzima iliunga mkono. Tetesi ni kuwa Mama anajiandaa kurithi nafasi ya mzee alafu na yeye ajikite kwenye shirikisho. Kwa maana nyingine familia itakamata hatamu za nchi na shirikisho kwa ujumla. Kama si hivi basi inahisiwa mtoto wake pekee wa kiume, Meja Kainerugaba ambaye sasa yupo masomoni majuu anaandaliwa kumrithi baba yake. Kwani amekuwa akipelekwa kuhudhuria masomo ya kijeshi katika vyuo maarufu vya kijeshi Uingereza na Marekani. Hadi anakwenda masomoni mwaka jana ndie aliyekuwa mkuu wa kikosi cha ulinzi wa rais (Presidential Guard Brigade).

SHIRIKISHO KWA NJIA YEYOTE ILE
Awali nimesema kuwa siku za karibuni Raisi Museveni karipotiwa kuanzisha juhudi mpya kwa siri za kuishawishi Kenya iungane na Uganda na kuikacha Tanzania ambayo bado haiko tayari. Mimi naiona hatua hii kama kiashirio cha dhati kuwa Museveni anatafuta mahali pa kutokea "Exit Strategy" na iliyobakia ni Shirikisho kuharakishwa.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la Uganda, Museveni aliwahi kunukuliwa hapo November 29, 2005 akiwahutubia waandishi wa habari: "Tutakapokuwa kwenye awamu yangu ya tatu (third term) sala yangu kuu ni kuanzishwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki. Ifikapo mwaka 2010, tuwe na uraisi wa kupokezana na 2013 tuwe na raisi mmoja wa kuchaguliwa. Kama msomaji una akili timamu lazima ujiulize suala la muda hapa (timing) . Aliongeza zaidi: "Hilo likitokea utaona mtu aking'ang'ania kustaafu hata kama mnaleta tingatinga kunilazimisha nibakie madarakani, nitaenda kuchunga ng'ombe". Inaonekana hapa si kwamba Museveni alimaanisha kustaafu siasa za Uganda ataenda kijijini, ila atapenda ahamishe ikulu yake kutoka pale "Nakarero" hadi Arusha. Hii kwenda kuchunga ng'ombe kijijini kwake kule 'Rwakitura' wilayani Mbarara ni janja tu.
Mwisho, jambo la msingi ni wazi kuwa rais Museveni ni kiongozi shupavu na mwenye kuthubutu kufanya mambo makubwa bila kujali mbinyo wa wapinzani. Hii ni sifa ambayo viongozi wengi hawana na ni silaha yake kubwa. Ila tu tatizo mara nyingi maamuzi yake si kwa ajili tu ya nchi bali maslahi binafsi.
Wasiwasi wangu unaanzia hapa: Mwanzoni alidai Shirikisho kwa misingi ya 'Wigo mpana wa Soko', kutokana na idadi ya watu wa nchi tatu na baadaye tano. Sasa anapoiacha Tanzania, tena yenye watu wengi kuliko nchi mwanachama yeyote.
Tujiulize: je wigo wa soko unaongezeka au unapungua? Hapa ananiacha hoi; kama si ukubwa unatafutwa ni nini hasa? Nitaendelea kuwajuza siku zijazo.

Saturday, September 22, 2007

MUSEVENI NA HILA DHIDI YA TANZANIA?

Museveni mambo yalivyo ikulu ni vituko, yaani katibu wa rais ndio kama Makamu wa Rais.Pia kuonesha kuwa Museveni ana roho ya kwanini, ukikosana naye, anakufuatilia mpaka uliko hata nchi za nje ili usiajiriwe.
Pia hebu tujionee ni vipi Uganda na Kenya zina mbinu za kichinichini dhidi ya Tanzania juu ya Shirikisho?

Saturday, September 15, 2007

KENYA UGANDA KUUNDA SHIRIKISHO-EAC

Museveni kaanza tena kuonesha ni jinsi gani alivyopania kuwa Raisi wa kwanza wa EAC-Shirikisho. Huyu ni kiongozi shupavu ambaye ana malengo, sasa kaashauri Uganda ijiunge na Kenya. Pia hebu jisomee jinsi gani Nyerere alivyompindua raisi wa zamani Uganda, Binaisa.

Saturday, September 01, 2007

MFUMO WA KISIASA TANZANIA NI MBOVU SANA

MARA NYINGINE NAFIKIRI WABUNGE WA CCM WANAGEUZA BUNGE KUWA"NATIONAL THEATER'

Tusipobadili katiba hatufiki popote hata kama CCM itashindwa.

Leo nikiandikia ndani ya "Tanzania Daima" napenda nigusie juu ya mfumo wetu wa kisiasa niuonavyo nadhani una tatizo na tusipoweka tafakuri za kina sio ajabu tukawa tunalaumu wanasiasa wetu--hasa wabunge wa chama tawala-- na baadaye kitakapokuja shinda chama kingine mambo yakawa kama sasa. Naliona bunge letu kama si chombo kinachotekeleza yale yaliyokusudiwa; yaani mhimili wa kutunga na kuipa changamoto serikali bila kuingiliwa na serikali. Labda nianze kwa kuonesha wasiwasi wangu juu ya uhuru wa kusema usivyozingatiwa hasa na taasisi hii.
Ni wazi, kuwa jamii huru ni ile abayo maoni pinzani yanazingatiwa au kuvumiliwa hata kama ni machungu kiasi gani. Kama mtu kasoma somo la fizikia, kuna kanuni isemayo kuwa: 'kila tendo lifanyikalo kuna matokeo sawa kutoka pande mbili zinazotofautiana' (tafsiri isiyo rasmi). Yaani: "for every action there is an equal and opposite reaction".

Kanuni hii inanisukuma kueleza hisia zangu juu ya tatizo kubwa la mfumo wetu wa kisiasa ambao nadhani una madhara mengi sana juu ya udhaifu wa Bunge letu. Nina fikra kuwa kwa ujumla watawala wetu bado hawajaweza kutoka katika fikra za umungu mtu; yaani kuwa tayari kusikiliza mawazo ya upande mwingine kwa moyo wa dhati. Bali yanayotokea mengi inaonekana ni 'bezo' kila serikali ama taasisi zake zinapokosolewa. Hawajui bado kama kwa kila watakachosema lazima kitapata wazo mbadala. Masikini, wamesahau hiyo kanuni ya fizikia!

Ni katika muono wangu huu wa kifizika ninaamini ingawa tumekuwa chini ya mfumo wa kisiasa wa vyama vingi ila bado hatujaweza kufaidi matunda ya mfumo huo kwa kiasi cha kukidhi haja ya kisiasa kuiletea nchi yetu utawala bora. Je ni kwanini nimeona hivyo? Nitaanza moja kwa moja kuangalia mfumo wetu wa kisiasa na kuoanisha na mambo kadhaa ambayo yanatokea nchini kwetu kuthibitisha kuwa bado tuna mambo ya msingi kuyafanyia kazi ili tufikie angalau demokrasia yenye tija kwa maendeleo ya nchi na wananchi wetu.

Mfumo wa siasa unaweza kuwa ule wa Chama kimoja, vyama vingi, au hata usio na vyama vya siasa bali wa kikundi cha askari (junta) kama uliokuwa nchini Uganda kipindi cha nyuma kidogo yaani ule wa vuguvugu-movement. Katika mifumo yote hii kama uhuru wa kusema na kuvumiliana hauzingatiwi basi jamii haiwezi kupiga hatua katika maendeleo. Ni katika mtizamo huu, kikao cha bunge la bajeti kilichomalizika hivi karibuni kwa kiasi kikubwa kimedhihirisha kuwa taasisi nyeti kama Bunge haizingatii sana uhuru wa kusema na kuvumiliana.

Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania la awamu ya nne lilianza na kauli mbiu za Spika Samweli Sitta eti litakuwa la 'viwango na kasi' na kutupa faraja watanzania wengi kama mimi. Ninasikitika mijadala ya hivi karibuni bungeni imeonesha badala ya kwenda mbele tumeamua kurudi nyuma (reverse gear); kuna dalili kubwa za uoza wa kujadili; na inaonesha bunge sasa ni taasisi isiyofaa (irrelevant) hasa mtu unapozingatia mambo ya uzalendo au maslahi ya Tanzania. Spika wa Bunge ndio chanzo cha uoza kwa kiasi fulani kwani jinsi anavyoadhibu wabunge inatia shaka. Anafikia kusema mbunge fulani anahitaji ushauri nasaha kwa hiyo asamehewe pale alipotenda kosa; mtu unajiuliza ni kanuni gani inasema haya unashangaa manake sidhani kama bunge letu lina watoa ushauri nasaha.

Ila ukiangalia hili la majuzi la mheshimiwa Zitto Kabwe, maamuzi ya bunge letu yanakanganya. Napata hisia spika kazidiwa na hisia za chama chake-CCM anapokuwa anataka kutoa maamuzi na anashindwa kutumia busara kama alivyoweza kuzitumia na kusema mbunge wa chama chake anahitaji ushauri nasaha. Natambua kwa kanuni za Bunge, ambazo hata Spika amekiri mara nyingi zimepitwa na wakati, kuna uhalali wa mheshimiwa Zitto Kabwe kuadhibiwa. Ila nashangaa kwanini busara haikutumika hapa? Ina maana hoja alizotoa mheshimiwa Zitto Kabwe hazina chembe ya kuona umuhimu wa kuunda kamati kuchunguza mambo yenye maslahi kwa nchi? Hivi kama ni kweli mkataba ulisainiwa nje ya nchi tena ndani ya hoteli ya Churchil na wala si angalau ubalozi kwetu London, kwani tusichunguze kama sheria zilifuatwa?

Hivi wabunge wa maeneo yenye migodi kama huko Buzwagi, Bulyanulu, North Mara, Mwadui na Nzega hawashangai ni kwanini watu wao bado wako nyuma kimaendeleo katika nyanja nyingi wakati wana utajiri mkubwa? Historia itawahukumu wabunge wa mikoa yenye rasilimali zinazoibiwa na wao kubariki bungeni kwa kile kinajionesha kama mapenzi ya chama zaidi ya wananchi waliowachagua. Hapa upande mmoja ninawalaumu wabunge wa sehemu hizo lakini kwa upande mwingine sitaki walaumiwe kabisa na ndio ningependa nizungumzie kuwa tuna tatizo. Tangu mwaka 1992, tumeanzisha mfumo wa vyama vingi tukiiga uendeshaji wake kutoka nchi za magharibi kama Marekani. Mfumo wetu naamini ni tatizo na unawalazimisha waheshimiwa wabunge wa chama tawala kuzima mfumo wa kufikiri waliojaliwa na maulana wanapokuwa bungeni.

Ninadhani bunge, kama mhimili muhimu katika kuhakikisha dola inakuwa na tija, lina tatizo na inabidi lirekebishwe sana maana kwa hali ilivyo sasa kuna hatari hiki ni chombo au kinaelekea kuwa ni chombo kisichokuwa cha maslahi yeyote kwa nchi, bali kwa maslahi ya vigogo wachache na marafiki zao wenye mitaji kutoka nje ya nchi. Kuna athari kadhaa lazima tuzing'amue kama watanzania ili tuweze kuja na mkakati hasa wakati wa kupiga kura. Tuna mfumo wa siasa wenye chama kimoja chenye maguvu mengi kutokana na kuwa na wabunge wengi. Madhara yake tunakuwa na demokrasia ya vyama vingi wenye bunge dhaifu na butu; ni Bunge lisilofanya kazi kama mhimili unaojitegemea bali linalowakilisha watawala.

Kwa maana nyingine demokrasia ya Tanzania ni ya aina yake na kipekee duniani kwa misingi kwamba tuna serikali ya awamu ya nne isiyozingatia mihimili mitatu: 'watawala, bunge na mahakama'. Tanzania ya leo, serikali inaendeshwa kwa mihimili miwili: watawala na mahakama. Bunge kupitia chama tawala limejikita katika kufanya kazi za watawala kwa kuisemea na kubariki (rubber stump) mijadala ya serikali badala ya kuihoji. Ni mfumo ambao ama unaambatana na shuruti kwa wabunge wa chama tawala au ni utashi wao kutenda watendavyo, mimi nashindwa kuelewa ila nionavyo tuna tatizo la mfumo wa kisiasa.

Nionavyo labda tunahitaji mfumo wa vyama vingi wenye chama tawala dhaifu, kwa maana kisicho na viti vingi sana ndani ya Bunge. Yaani, chama tawala ambacho kinaweza kushindwa kwa kura na wabunge wengine wa upinzani linapokuja suala lenye kuhitaji watu kufikiri kwelikweli kama la kupigia kura maamuzi kadhaa kama haya ya juzi ya kumuadabisha Zito Kabwe.
Ni kutokana na kuwa na bunge la chama kimoja chenye wabunge lukuki, bunge letu sasa limebakia kama "Sanaa za maonesho-majukwaani za kitaifa" (Nationa Theatre). Nathubutu kusema kama mtu amefuatilia kikao cha bunge hivi karibuni kwenye televisheni ni wazi tulikuwa mara kwa mara tunashuhudia sanaa za maonesho. Kwanini ninasema hivi?

Mosi, kwa mfumo wa demokrasia tulionao ni wazi wabunge wanajumuika katika makundi yao tofauti yaani kambi (CAUCUS). Kabla ya kujadili jambo bungeni, wabunge katika kambi zao wanakuwa wameshajadili ni vipi watajadili au hata kupigia kura hoja ili zipite au la. Kwa mantiki hii tunachoshuhudia pale Bungeni ni marudio ya kile kilichokwishajadiliwa ndani ya vikao vya kambi (caucus) za wabunge. Kwa maana nyingine kwa mfumo huu Bunge linakuwa chombo cha kisanii kwani ni sawa na kupoteza fedha za umma wa watanzania wengi masikini kuja kukaa na kujadili mambo ambayo yameshajadiliwa na kuamuliwa uamuzi ndani ya vikao maalum vya kambi ya chama tawala (caucus) na upinzani pia. Napata hisia wanachi tunaibiwa na wabunge kwani hakuna cha maana wanachofanya. Ingekuwa bora Spika akishirikiana na kila kiranja (Chief whip) wa kambi hizo mbili bungeni wawakilishe maamuzi, idadi ya kura za wabunge kama zilivyopigwa ndani ya kambi (caucus) zao badala ya watu wazima, wasomi waliobobea kwenda kupasha viti moto na kula fedha za walipa kodi wa nchi hii bila jasho.

Pili, ndio maana kwa mfumo huu wa kujali zaidi nidhamu ya chama na kupuuza maslahi ya kitaifa basi ni bora hata watoto wadogo wa chekechea, mangumbaru (wasio na elimu ya kiwango cha kutoa maamuzi ya msingi) waruhusiwe kuwa wabunge. Binafsi nadhani Bunge letu limefikia mahali nalifananisha na kusanyiko la watoto wa chekechea. Pamoja na ukweli kuwa serikali inaongozwa kwa kuzingatia ilani ya uchaguzi ya CCM, kinachogomba ni kwanini utekelezaji hauzingatii kanuni za msingi za uwajibikaji kwa wanachi na Taifa kwa ujumla? Hoja za wabunge wa chama tawala katika sakata la Zitto Kabwe zilionesha kabisa ilikuwa ni katika kutekeleza agizo la chama na si utashi wa dhati wa wazungumzaji. Na ndio maana wale wabunge makini wa CCM hawakuchangia hoja; inaonekana hawakuwa tayari kutuonesha ni kwa jinsi gani mfumo wa bunge ulivyoteka (hijack) akili zao.

Tatu, pamoja na spika kusisitiza kanuni mpya zinakuja karibuni, ni wazi huu si muarubaini kwani bila katiba mpya hatufiki mahali. Kuna haja ya watanzania tuwe na kongamano la kitaifa tujadili namna tunavyoweza kujiundia taratibu mpya za mustakabali wa Taifa letu bila kuzingatia sana hii mifumo ya kisiasa ya kimagharibi. Demokrasia ya magharibi kwa kiasi fulani nadhani ina matatizo kwa mazingira ya kiafrika hususan Tanzania. Nikiangalia jinsi bunge letu linavyoendeshwa na linavyotumiwa kufanya kazi za mhimili wa utawala (executive) badala ya wajibu wake halisi (legislative) nashindwa kumlaumu mbunge yeyote manake naamini kwa mfumo tulionao hata kama chama cha upinzani kinashika hatamu leo, sanaa za maonesho hazizuiliki. Nimejaribu kuitizama hii kasheshe ya hivi majuzi ya mheshimiwa Zitto Kabwe, binafsi, napata hisia kuwa mfumo wetu wa demokrasia ya vyama vingi wa kimagharibi labda pia ni tatizo.

Kuna mambo yanayoambatana na mfumo huu ambayo inabidi tuyafanyie mabadiliko katika sheria zetu. Kwa mfano, ukizingatia mfumo tulionao wa kibunge wa jumuiya ya madola: yaani unaruhusu chama chenye wabunge wengi kiamue kila kitu bila kujali hata nadhiri binafsi (conscience) ya wabunge. Yaani chama tawala kinakuja na hoja inayotetea maslahi ya chama na viongozi wake wala si Taifa. Na wabunge wa chama hicho wanaagizwa na kushinikizwa kwa mfumo wa nidhamu ya chama (party discipline) kuunga mkono jambo kama hilo hata kama nafsini mwao sivyo wanavyofikiri basi ni hatari sana. Yaani mfumo wa kisiasa tulionao unaruhusu taasisi nyeti kama Bunge kutumika kama chombo cha kuvunja Katiba; kwani, ibara ya kumi na nane (18) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa haki ya uhuru wa mawazo katika vipengele vyake vinne: a, b, c na d. Bunge letu haliheshimu vipengele viwili hapa:

Kwa mfano, kifungu (a) kinazungumzia: 'uhuru wa mtu kuwa na maoni na kueleza fikra zake', lakini Bungeni kwetu mfumo unaruhusu maamuzi ya wabunge katika kambi (caucus) zao hata kama yana upofu basi lazima yapitishwe bila kuhojiwa kwa uchambuzi makini. Kinyume cha hapo mbunge ataadhibiwa na kamati ya nidhamu ya chama husika pindi akijaribu kuhoji au kuonesha kutoridhishwa na jambo husika. Mfumo huu ndio tunaotakiwa tuondokane nao, la sivyo kama tutaiga kila kitu kutoka demokrasia ya nchi za magharibi basi nchi yetu haitatoka katika lindi hili la wabunge waliotekwa fikra. Na hii haijali tunatawaliwa na CCM au chama kingine chochote.

Kifungu cha (d) kinazungumzia: 'haki ya mtu kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii'. Tukizingatia mjadala wa Zitto Kabwe juu ya kuundwa kwa kamati ya uchunguzi ya Bunge napata hisia mheshimiwa alikuwa akiegemea haki ya kikatiba ambayo imeainishwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Yaani waziri anaweza kusaini mkataba bila kutaarifu Bunge kama taasisi ya uwakilishi wa wananchi. Hili ni suala muhimu kwa jamii kwa hivyo kama lina utata ni vyema uchunguzi ungefanywa. Ila mfumo wetu una mwanya wa kuruhusu katiba ivunjwe kutokana tu na "uwingi wa wabunge wa chama tawala" ambao inawalazimu wafuate agizo la chama kupitia kambi (caucus).

Wabunge wa chama tawala wanajinyima haki ya kupewa taarifa juu ya suala muhimu la jamii kwa kuunga mkono hakuna haja ya uchunguzi wa madai ya mheshimiwa Zitto. Hii ni sababu ya mfumo wa siasa tulionao unawalazimisha wabunge wenye akili timamu wasizitumie pale inapobidi. Sitaki niwalaumu wabunge wa chama tawala manake naona mfumo wa kisiasa unatoa mwanya na kuwalazimisha wasihoji na waunge mkono maamuzi ya chama ambayo si yakinifu. Na usipohoji unaadhibiwa na chama chako.


Hapa inamaanisha wabunge wengi wa chama tawala kwa ishu kama ile ya Karamagi na Zitto naamini si wote walikuwa na msimamo waliouchukua kuunga mkono adhabu iliyotolewa. Ila naamini tayari kulikuwa na agizo ndani ya kambi ya chama tawala kuamua vile. Ni wazi wabunge wetu wametekwa kiakili, yaani chama cha Mapinduzi kinawasaidia kufikiri na kuamua mambo kadhaa yenye maslahi kwa umma na kuwafanya wayaamue kwa kufuata maelekezo ya watawala. Na hapa maamuzi yanakuwa si kwa ajili ya umma bali dhidi ya wachache, yaani wanasiasa mafia fulani ambao ni wateule wanaostahili kufaidi keki ya nchi hii.

Ndio maana mwanataaluma mmoja hivi karibuni katika gazeti la 'The Citizen' tarehe 22 August 25, 2007, kanena kuwa yaliyomkuta Zitto ni Bunge kutenda kosa la "Crime against Logic", yaani "Kosa/hatia dhidi ya Kufikiri sahihi". Pamoja na lawama zinazoelekezwa kwa wengi wa vigogo hasa kule bungeni kama Spika na wabunge kadhaa na hata mheshimiwa Karamagi, nadhani maoni yangu tukae chini kama Taifa tuunde demokrasia ya kitanzania, yenye kuzingatia maslahi ya nchi ambayo itakuwa na Bunge lisiloruhusu mwanya wowote wa mbunge kufungwa mdomo hata kama anatoka kwenye chama kinachotawala. Ikibidi tusiwe na mawaziri ambao ni wabunge au hata wakuu wa mikoa ambao ni wabunge. Mianya inayoingilia uhuru wa mbunge wa kufikiri inatokana na mfumo wa kibunge unaowapa wabunge wengi (majority) bungeni kutuamulia mambo kama watoto wa chekechea.

Tukiachia mfumo tulionao wa kibunge wa Jumuiya ya Madola uendelee basi hata kama siku za usoni kitashinda kwa kishindo chama kingine zaidi ya CCM, bado kitatumia mianya iliyopo sasa kupitisha na kujadili maamuzi katika hali ya kitoto kama tunavyoshuhudia sasa. Wanasiasa wetu waanzie kwenye vyama vyao kuweka taratibu za uwazi na uhuru wa viongozi na wabunge wanaowakilisha vyama wawe huru kuzungumzia hata mambo yanayogusa maslahi ya vyama vyao na kukinzana na maslahi ya Taifa bila kubanwa na kamati za nidhamu za vyama vyao. Tusipoacha mfumo wa kuadabishana ndani ya vyama vyetu, hata Bungeni hatutaruhusu wabunge wetu wazungumze kwa uwazi. Na ndio kinachotokea kwa sasa.

Na ndio tatizo lililotufikisha hapa tulipo leo ambapo Bunge la bajeti lililokwisha majuzi lilikuwa sawa na 'Sanaa ya Maigizo', mahali ambapo wabunge kwa ujumla wao na kwa makusudi kabisa hawajali maslahi ya nchi ila tu kujali fedha na posho, huu ni ulafi wa hali ya juu (collective greed of the highest degree) kuunga mkono na kupitisha maamuzi kadhaa yasiyozingatia maslahi ya nchi yetu na wananchi kwa ujumla wao. Inanikumbusha mwanafalsafa wa kifaransa, Jean-Francois Bayart anavyoiona hali kama hii kama siasa za tumboni (politics of the belly) akihusisha na mkakati wa wanasiasa kujitajirisha pamoja na kuimarisha utamaduni wa kung'ang'ania madarakani tu. Ni kama vile kwao wanaangalia maslahi yao na chama chao tu; wananchi na nchi kwa ujumla si hoja. Nionavyo hii inasababishwa na mfumo holela wa kiunyanyasaji (irregular coercive mechanism) tulionao ambao tunafikiri ndio demokrasia makini kumbe ni mfumo wa vyama vingi wa hali ya chini sana (primitive multipartism)

Nahitimisha kama nilivyoanza makala hii juu ya kukubali kukosolewa hata kama kunauma kiasi gani lazima kukubaliwe kama changamoto. Kukichukuliwa ni kama kudhalilisha utawala ama ni kudanganya basi ujue maendeleo ya jamii husika hayatafikiwa. Ni wakati tubadili mfumo wetu wa kisiasa ili uendane na wakati na mahitaji ya wote na si wachache tu kwa kuondoa mianya yote inayotulazimu tufikiri kama watoto katika maamuzi ya kimsingi ya nchi yetu na kutuadabisha pindi tunapojaribu kufikiri kwa umakini.

Tukibadili mfumo wetu wa kisiasa tutaweza kuondoa ile nguvu ya chama tawala kuwa na nguvu ya kudhibiti Bunge kama ilivyo sasa hata kama kuna wingi wa wabunge. Hii ni lazima ianzie kwenye vyama vya siasa; manake leo ni CCM kesho ikiwa DP au Chadema kwa mfumo huu wa kibunge wa jumuiya ya Madola sitashangaa kumwona mtu kama Zitto au Mtikila akifanya kwa mbwembwe ndani ya Bunge haya haya yaliyokuwa yakifanywa na wabunge wa chama tawala bila aibu.

Kama tunadhani tuna mfumo bora wa kidemokrasia barani Afrika, ni wakati wa kutafakari; la sivyo tutakuwa tunatupiana lawama bila sababu za msingi kwani mfumo wa kisiasa unaruhusu taasisi ya Bunge kuonekana kama tamthiliya kwa yeyote mwenye uchungu na nchi yetu. Na tujiulize: Ili ile kanuni ya fizikia izingatiwe bila kukwepeka, je wabunge wenye kutoa hoja zinazofanana na watoto wa chekechea, je ni nani wa kulaumiwa, wabunge hasa wa chama tawala au ni mfumo mzima wa kisiasa?