My Blog List

Wednesday, December 19, 2007

ZUMA AANZA HARAKATI ZA KUWA RAISI WA BONDENI

The image “http://www.mg.co.za/ContentImages/328066/zuma.jpg” cannot be displayed, because it contains errors.

Bado nina hisia mchanganyiko manake kuchaguliwa kwa Zuma kuiongoza ANC ni matokeo ya demokrasia. Ila mara nyingine demokrasia ina matatizo yake; hili ni tatizo kwa Afrika ya kusini kabisa.

Vijana wa ANC nao wana mashaka sana na uchaguzi wa Zuma kwani hana haiba nzuri ya kiongozi.

Wednesday, December 12, 2007

SIASA ZA BONDENI ZINACHEKESHA

Yaani mara nyingine inafikia wakati mtu anaamini kuwa siasa zetu zimebakwa na wanasiasa. Pia huko somalia, amechaguliwa waziri mkuu mpya je, ataweza kazi yake?

UHURU NA AKILI MGANDO ZA BAADHI YA WATAWALA

Taifa letu lilitimiza miaka arobaini na sita (46) tangu lizaliwe; jumapili iliyopita ilikuwa ni kumbukumbu ya siku ya uhuru kwa maana nyingine. Kama mtanzania, na mzalendo sina budi kuchukua kalamu na kutafakari kwa kina miongo kadhaa kama Taifa ni changamoto gani tumezikabili na zipi inatubidi tupandishe soksi (pull up socks) ili kuendeleza nchi yetu. Binafsi, naamini kama tutafanyia kazi changamoto ya “Utawala Bora” basi uhuru wetu utakuwa na maana sana. Mada yangu itaegemea sana hapa tu.

Kabla ya kujadili, nitoe pongezi kwa watanzania wote tangu raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na kwa ujumla watu wa kada zote hapa nchini kwa kuadhimisha siku hii.

Bila ubishi kabisa, nchi yetu imefanikiwa sana katika nyanja mbalimbali tangu uhuru hasa ukilinganisha na nchi nyingine za dunia ya tatu. Hapa ieleweke hata kama tungekuwa tumefanikiwa kiuchumi kama vile Wachina ama Wajapan bado kungekuwa tu na matatizo. Hivyo si vyema kubeza kuwa labda kila kitu ni mrama; yapo mafanikio kama vile umoja wa kitaifa ambao ni mfano dunia nzima. Binafsi nimekutana wa watu kadhaa kutoka pande mbalimbali za dunia wanaposikia umetoka Tanzania watasifia Umoja wetu. Hii yote ni heshima za mwasisi wa Taifa, hayati Mwalimu Nyerere.

Kuendana na mfumo wa kiutawala duniani, yapo mapungufu mengi ambayo nadhani ni vigumu kujikwamua nayo hasa ukizingatia mfumo mzima wa biashara ulimwenguni ni wa upendeleo na ukandamizaji kwa sera za mashirika makubwa ya kiuchumi na kibiashara ulimwenguni. Hapa nazungumzia sera za Mfuko wa Kimataifa wa Fedha (IMF), Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Biashara Ulimwenguni (WTO) mwanzoni likijulikana kama GATT.

Ndio maana kama mtu anafuatilia hata yale majadiliano kibiashara ya kule DOHA yamekwama kabisa na ni wazi watawala wa dunia hawataki kabisa kukubali baadhi ya hoja ambazo zitalikwamua bara la Afrika kutoka umasikini usiokwisha. Hata hivi majuzi, Taifa letu limesaini makubaliano mapya ya mashirikiano ya kiuchumi na Jumuiya ya Ulaya (EU) yajulikanayo kama (EPA) kwa kutumia mgongo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ni wazi yameshinikizwa na hayatailetea nchi yetu tija sana kinyume na inavyodhaniwa na wale waliosaini. Inajulikana wazi tumelazimishwa kwa kuharakisha kusaini kabla ya ule mkataba wa Cotonou kumalizika hapo December 31 mwaka huu. Nisijadili hili zaidi labda siku nyingine.

Ni katika mchakato huu wa changamoto hizi za mabepari basi hata kama watawala wetu wanao utashi inakuwa vigumu kuweza kusimamia maslahi yenye tija kwa nchi zetu. Kwani mara nyingine watawala wetu wanapokuwa na utashi wa dhati basi mambo kama yanayomkuta Robert Mugabe hayazuiliki kwani wanaishia kufanya maamuzi kwa pupa, bila kufikiri kwa mpangilio na kwa logiki ambayo yanagharimu maisha na uchumi wa nchi zao. Ndio changamoto za “Uhuru” ambazo kwangu ni jinamizi tu; kwani, tunaposherehekea siku hii lazima tuelewe inawezekana kabisa siku ile ilikuwa ni mwanzo wa kipindi cha giza. Ningependa nielezwe hivi Mwalimu Nyerere alipokwenda kule Lancaster alikwenda kusaini mambo gani? Manake inatia shaka huenda ndio ulikuwa wakati wa kujitia kitanzi badala ya kuwa huru. Kwani nina mashaka sana kama kweli tuko huru.

Na ndio maana bado tuna changamoto nyingi sana za kutafakari na kujiuliza tufanye nini? Kwa mtizamo wa serikali ya awamu ya nne, ni wazi changamoto kuu ambayo lazima ifanyiwe kazi ni hii ya “utawala bora”. Hii imebaki kuwa ngonjera na kama hatubadiliki kwa hili basi kamwe hatutapiga hatua yeyote. Nasema hivi kwani naamini pamoja na changamoto za jinamizi la uhuru linaloongozwa na sera dhalimu za kimataifa bado tuna mengi ya kufanya kwa hapa nyumbani ambayo yatatuwezesha tuwe bora tu mbali na mashinikizo dhalimu ya mabepari.

JE TUFANYE NINI?

Tunahitaji kufikiri zaidi ya kuongea sana; hii itatuwezesha kuwekeza katika kuwajibika kwa bidii (hardworking) badala ya kupiga siasa kwa muda mrefu zaidi. Ni wazi hadi leo hii, bado utendaji wetu umetawaliwa na mashiko ya kisiasa zaidi kuliko nidhamu ya kazi katika nyanja mbalimbali. Hasa katika chombo kama Bunge, ni lazima tubadilike; miaka arobaini na sita itufanye tuamue sasa ni mwisho wa siasa za upande mmoja usiozingatia maslahi ya umma. Njozi za chama kushika hatamu zisipoachwa basi hatufiki popote kama Taifa la miongo hii minne na ushehe.

Kwa watawala wetu, lazima kung’amua kuwa kama mhimili wa utawala (executive) unakuwa na nguvu kubwa dhidi ya mihimili mingine basi hatufiki. Pamoja na nguvu ya kikatiba ya taasisi ya uraisi, Uhuru unakuwa na maana kama kiongozi mkuu wa nchi atang’amua hili na kuruhusu utendaji unaoruhusu majadiliano ya vyama vyote vya mitizamo tofauti ndani ya bunge badala ya kuzingatia tu upitishaji wa maamuzi yenye kuegemea uchama na si umma.

Ingawa demokrasia inasema ‘wengi wape’, lakini nadhani pia tuangalie mfumo wetu wa upigaji kura na maamuzi ya upitishaji sheria ama maamuzi bungeni ukoje? Je unaruhusu upigaji kura wa wabunge wa chama tawala unaozingatia uhuru wa mawazo ya mbunge au ni kushurutisha kwa kuegemea maslahi ya chama yaliyofichwa ili kulinda maslahi ya vigogo wa chama tawala bila kutoa sababu za msingi kuhusu jambo fulani ili kulinda maslahi ya nchi.Uhuru unaweza usiwe na maana sana kama mfumo wa maamuzi ndani ya chombo kama Bunge unambana mbunge mwenye mawazo tofauti.

Hata ndani ya vyama vya siasa, ni changamoto pia kujiuliza hivi kuna uhuru wa mawazo wa mbunge katika kujadili mambo na hata kuhoji ndani ya chama? Yaani kwa miaka yote hii arobaini na sita, bado ni kosa la jinai ndani ya chama tawala kwa mtu kujadili hisia zake kwa uwazi inavyoonekana na hata kupinga ama kupiga kura ni udikteta tu (intra-party disagreement, debate and even voting is still a crime). Hapa lazima watawala wakumbuke hili ndilo linalokwamisha maendeleo yetu na hapana budi tuweke mizani ya usawa (strike a balance) katika utendaji wa serikali dhidi ya mihimili mingine miwili hasa ule wa Bunge tukianzia ndani ya vyama vya siasa.

Kwa mfano, kama tutazingatia utawala bora, basi lazima tubadili mitizamo yetu (mentality): yaani serikali iwe kwa ajili ya umma na si kama jamvi la kuficha mafisadi kama ilivyokwishajidhihirisha kwa watuhumiwa wa ufisadi kutajwa hadharani na wao kuamua kukaa kimya bila kujisafisha. Hata mamlaka yenye uwezo wa kuwawajibisha nayo haikuchukua hatua zozote. Ndio hapa bado inaonesha tunawaza zaidi katika kulinda maslahi ya kisiasa kuliko ya umma. Yote hii inashawishi mtu mwenye akili timamu kuwaza na kuamini labda ni kwa sababu ya utawala mbovu. Mfumo wa “Check and Balance” uko likizo ili tu kulinda maslahi ya kisiasa ya chama kinachotawala. Huu ni ugonjwa mkubwa barani Afrika na kama hatubadili mtizamo “Uhuru” unakuwa hauna maana.

Ninaamini kama watanzania, tuna bahati ya kuwa na raisi wa nchi ambaye ana karama ya kuongoza kwa kujali demokrasia; kwani anajitahidi kujumuisha pande na hisia mbalimbali za kisiasa katika utendaji wake. Mashaka yangu bado nadhani waliomzunguka raisi wetu mitizamo yao imepitwa na wakati na si endelevu. Ni mitizamo ya kusisitiza zaidi ‘umilele-chama’ (party-omnipresence) kuwa na woga labda chama kitaangushwa madarakani kwa kile wasichokijua. Na hii ndio chanzo cha madhila kadhaa zinazoisumbua serikali ya awamu hii.

Ni changamoto nzuri za kumfanya raisi na wasaidizi wake kuliona hili na kuamua kubadilika. La sivyo tuna hatari ya kubakiwa na “Kiongozi mwenye karama asiye na mwelekeo” (a charismatic leader without a cause). Mwelekeo wa sasa kwa nchi huru unatia shaka kwani uwezo wa kufikiri wa vigogo wengi ni mdogo sana na ni wazi unasababishwa na tamaa ya fedha na ulafi wa kila aina. Kitu woga kwa viongozi wetu ndio chanzo cha udhaifu wa viongozi wetu kuanzia juu.

Siku ya leo tujiulize ni kwa jinsi gani utawala wa shaghala baghala ulivyogharimu taifa letu kwa kipindi chote cha uhuru. Tunaweza tukalaumu sana na kusingizia mfumo wa kidunia (world order) ambao nimeuelezea awali, lakini kama tuna akili timamu ni wazi kwa nafasi yetu kwa mambo ya hapa nyumbani tuna mapungufu pia ambayo lazima tuamue kwa dhati kuyafanyia kazi. Ndio maana hata Raisi wetu majuzi alisikika akisema na kukiri hata hii mikataba ya madini ni sisi wenyewe wa kujilaumu mbele ya Waziri Mkuu wa Canada mheshimiwa Stephen Harper.

Kama Taifa, miaka arobaini na sita ya Uhuru haina maana sana kwani tumeshindwa kukabili changamoto za ndani kabisa. Inakuwa vigumu kukabili zile za nje manake watawala wa dunia wanatumia udhaifu wetu huu kutulaghai kwa kila hali. Kama hatubadiliki kwa kuruhusu kukosoana ndani ya vyama vyetu, bunge letu na kila mahali ili kulinda maslahi ya umma basi kamwe sioni maana sana ya uhuru. Ninachokiona ni sana sana ni juhudi kubwa tena hasi (highest retrogressive endeavour) za watawala na wanasiasa katika kuirudisha nyuma nchi yetu kwa kasi.

Uhuru bila ‘utawala bora’ ni kwa wachache na si kwa umma wa watanzania. Kama siku ya Jumapili, leo nitamwomba Mungu aizindue akili ya watawala na wanasiasa kwa ujumla wao kubadili mitizamo. Tuachane na akili mgando ndio uhuru utakuwa na maana. Miaka arobaini na sita ya Uhuru ije na mtimzamo (mentality) mpya kuhusu utawala wa Taifa hili. Hii ndio tafakuri yangu ya siku hii ya uhuru kwa leo.

MAWAZIRI NAO HAWALIPI BILI YA MAJI MPAKA WAKATIWE?

Kama unataka kuamini kuwa ni vigumu kwa nchi ya Tanzania kuendelea basi amini kwa haya ya vigogo wa serikali tena mawaziri eti hawalipii kodi ya maji mpaka wakatiwe.
Ni wazi hatuwezi kuendelea kama hata mawaziri hawako makini kiasi hiki. Sasa kama waziri halipi bili ya maji je wananchi wa kawaida watalipa? Nakwambia bado tuko kwenye lepe la ujamaa ambapo kila kitu kilifanywa na serikali.
Hebu soma habari hii alafu ushangae ni vigogo gani hao?

Mawaziri wasiolipia maji watajwa

::Yumo Waziri wa Maji, Msola, Hawa Ghasia
::jumbe wa vitisho watumwa DAWASCO


na yasmine protace

MAJINA ya mawaziri sita, ambao ni miongoni mwa wateja wa Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO), waliokatiwa maji baada kushindwa kulipia ankara, yametajwa.

Mawaziri hao wanaoishi eneo la Masaki, jijini Dar es Salaam, pamoja na wakazi wengine wa eneo hilo, walikatiwa maji wiki iliyopita.

Kabla ya kuwakatia maji, DAWASCO kupitia Ofisa Mtendaji Mkuu wake, Alex Kaaya, iliwaomba wateja wanaodaiwa kulipia ankara wanazodai.

Katika maombi hayo kwa wateja, DAWASCO ilitoa siku tatu wateja hao kulipia ankara hizo, hata hivyo ni wachache tu waliotii.

MTANZANIA imefanikiwa kupata baadhi ya majina ya mawaziri wanaodaiwa ankara, ambao ni pamoja na Waziri wa Maji, Dk. Shukuru Kawambwa.

Wengine wanaodaiwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mizengo Pinda na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Anthony Diallo.

Katika orodha hiyo, Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msolla, naye ametajwa, pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, naye ni mmoja wa mawaziri hao.

Akizungumzia kilichomsibu hadi kushindwa kulipia ankara zake kwa kipindi kirefu, Waziri Ghasia alidai kuwa tangu aanze kuishi katika nyumba hiyo amekuwa hapati huduma ya maji.

Alisema amekuwa akinunua maji kutoka kwa wafanyabiashara binafsi na si kampuni ya DAWASCO.

“Kwa hili jambo ni la binafsi mno. Lakini hata hivyo, lakini sikuwahi kupata huduma ya maji ya DAWASCO na zaidi sikuwahi kupata hizo bili. Sikuwahi kuletewa bili hadi leo,” alidai Waziri Ghasia.

MTANZANIA pia iliwasiliana na Waziri Msolla kwa simu, ambaye alikiri kudaiwa, lakini akadai kuwa hakuwa akifahamu taratibu za kupata ankara na malipo.

“Ni kweli kwamba hilo suala (la kudaiwa) lilikuwapo, nami sikuwapo nchini… lakini last week (wiki iliyopita) tulipata bili na tumekwishalipia,” alisema Prof. Msolla, ambaye hakuwa tayari kuzungumza zaidi kutokana na kile alichodai yupo katika mkutano.

Waziri Simba hakuweza kupatikana, baada ya kuwasiliana naye kupitia simu yake ya mkononi. Majibu kutoka kwa aliyepokea simu hiyo yalieleza kuwa waziri huyo yuko safarini Marekani.

Waziri wa Maji, Dk. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Anthony Diallo, Waziri wa TAMISEMI, Mizengo Pinda, hawakupatikana, baada ya simu zao za mkononi kuita kwa muda mrefu bila kujibiwa.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, DAWASCO imesita kuzungumzia majaliwa ya viongozi hao kurejeshewa huduma ya maji.

Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo, Badra Masoud, alisisitiza kwamba, walichokifanya ni kukata maji kwa wadaiwa.

“Tunadai fedha nyingi sana Masaki, hivyo tunataka tuendelee kutoa huduma bora kwa wateja wetu ambao wanalipa na wasiolipa tumewakatia mpaka hapo watakapolipa,’’ alisema.

Eneo jingine lililokatiwa maji mbali na Masaki ni Mbezi Beach. Hata hivyo, tofauti na Masaki, wateja wa Mbezi Beach wamekuwa wakijitokeza kulipia ankara zao.

Katika hatua nyingine, DAWASCO imedai kupokea vitisho baada ya kuwapo kwa operesheni hiyo ya ukataji maji.

“Watu wananipigia simu na kunitaka niwarudishie maji eti sijafanya vizuri, lakini mimi nimesema kwamba maji yatarudishwa kama watumiaji watalipia ankara zao,’’ alisema.

Aliongeza kwamba pamoja na kupigiwa simu, pia amekuwa akitumiwa ujumbe wa maneno ya kashfa kutoka kwa watu asiowafahamu.

Takwimu za DAWASCO zinabainisha kuwa, eneo la Masaki lenye wateja 1,270 linadaiwa Sh milioni 574, wakati Mbezi Beach kuna wateja 1,271 wanaodaiwa Sh milioni 578.

Eneo la Ada Estate lenye wateja 475 wanadaiwa Sh milioni 527, Mwenge wateja 733 wakiwa wanadaiwa Sh milioni 463 na Regent kwenye wateja 222 wanadaiwa Sh milioni 200,’’ alisema.

Ni kwa misingi hii jamani tutaendelea kama tunakuwa na viongozi makupe?Yaani kwao kila kitu bure tuu? Ni wazi hata kodi nyingine nadhani hawalipi?Pafanyike uchunguzi hapa.

Saturday, December 01, 2007

TANZANIA BILA UKIMWI INAWEZEKANA?

Siku ya Ukimwi duniani; ni wakati wa kila mtu hasa mwafrika kutafakari juu ya balaa hili ambalo limeshachukua roho za watu lukuki. Wakati naandika makala hii mara nasikia redioni kuwa huko Mbagala Kizuiani kuna jamaa mmoja kaamua kujiua baada ya kuthibitishiwa kuwa ana virusi mwilini mwakeMwingine kaamua kumuua mkewe huko Mbeya baada ya kusikia mkewe kapima bila ruhusa yake

.Ni habari za kusikitisha lakini ni lazima tujiulize hivi kweli hizi kampeni za upimaji ndio jibu la dhahama hili? Na pia tujiulize kwanini tunahofu juu ya kuambiwa tumeathirika?Je hatupo tayari kuwajibika na matokeo ya tabia zetu za ngono zembe?

Napenda niseme kuwa hizi kampeni za upimaji ukimwi zinanitia wasiwasi kama kweli ndio muarobaini wa gonjwa hili. Nasema hivi kwani ni zaidi ya miaka ishirini sasa tangu nimeanza kusikia habari za ugonjwa huu. Na kwa muda wote huo kampeni mbalimbali za kuhamasisha na kuelimisha kuhusu ugonjwa huu zimekuwepo. Ndio maana leo hii katika kampeni hizi za rais Jakaya Kikwete, hakuna jipya linalosemwa. Nimesikiliza, kutizama na hata kuhudhuria semina juu ya gonjwa hili kwa kweli sijaona kipya chochote juu ya elimu ya gonjwa hili.

Nikirejea kwenye mafunzo yatolewayo shuleni: msingi, sekondari na hata katika vyuo kupitia mitaala mbalimbali, nadhani watanzania kama jamii tuna tatizo. Ni jamii isiyojishughulisha kabisa kusoma na kujielimisha binafsi. Habari juu ya gonjwa hili zimesambaa kila kona kwa miaka ishirini iliyopita: vitabuni, majarida, vibwagizo, kwenye mitandao ya intaneti na magazetini, lakini watanzania hatujishughulishi kupata mafunzo lakini tunataka semina, makongamano na hata vipindi vya redio na televisheni visivyo na jipya juu ya gonjwa hili kila kukicha. Kuna haja ya watanzania kuamka katika kujali umuhimu wa kujua mambo yanayohusu maisha yao. Bila hivyo sidhani kama tutafika popote katika vita ya gonjwa hili.

Hivi kweli inaingia akilini kuwa hadi leo hii watanzania watu wazima kwa vijana hatuna uelewa wa gonjwa hili?Miaka yote tumeishi na gonjwa hili yaani hatulifahamu? Nisingetegemea tuwe na kampeni kubwa kama ya sasa na ambayo hatima yake bado ni kutokupungua kwa maambukizi kwani kuna kila dalili watu wengi wameziba masikio.

Nashangazwa na upimaji kwa siri: mosi, hivi kama napima kama nina virusi alafu nasema ni siri yangu, na sitaki watu wajue kama nimeathirika, si kuwa ninataka kuendelea kujichanganya visivyo na watu wengine ili niwaambukize? Kwanini tusiwe na utaratibu wa kistaarabu wa waathirika kuhimizwa kwa ushauri nasaha ili wajiweka wazi na hata kujiunga kwa uwazi na taasisi za waathirika kwani kwa sasa wengi wao ni kwa siri sana. Hapa siongelei unyanyapaa, ila ni vyema watu wawe huru kutambuliwa kwani kama usiri utaendelea kutiliwa maanani zaidi, basi hii kampeni haitatusaidia sana kwani kuna kila shaka ya kuendeleza uambukizi zaidi.

Uwazi huu pia ungeoneshwa hata kwa wanajamii vinara: wabunge, mawaziri, na viongozi mbalimbali wa jamii. Kwa mfano, kama tungejulishwa angalau taarifa za upimaji kule bungeni, je wangapi walipima, wangapi walionekana kuathirika ama kutoathirika. Lakini kupambana na ukimwi kwa usiri hakutakomesha ukimwi kamwe.

Pia nashangazwa na hizi juhudi za upimaji hazijaonekana sana katika taasisi za elimu hasa elimu ya juu. Huku kuna vijana lukuki na ingekuwa vyema hapa watu wapimwe manake ndio viongozi wa kesho tunaowatarajia na tukiwaacha ngono mbele kwa mbele basi tujue kuna mahali ambapo paangaliwe manake kwa muono wa karibu ni sehemu ambapo maambukizi yanawezekana kuwa kwa kasi sana.

Linalonishangaza sana ni kuwa Ukimwi umekuwa ni mradi mkubwa kwa baadhi ya watu flani na vitaasisi vyao vyenye utegemezi wa wafadhili. Ni wazi kuna watu wanafurahi sana ongezeko la wagonjwa wa ukimwi na hata yatima. Bila gonjwa hili watu wengi hawataajiriwa na wengine wangekuwa masikini kabisa. Najua siku hizi imani za kidini ni kiini macho kwa wengi kutokana na matendo yao. Ni kwa misingi hii vita ya gonjwa la Ukimwi inaonesha kama vile hakuna Mungu.

Ukimwi bado ni kiini macho kupambana nao kwani hadi leo bado watu wanaugua gonjwa hili lakini utasikia eti wamekufa kwa vigonjwa vingine ama wamelogwa na mambo mengine ambayo mtu mwenye akili inashangaza sana. Kuna haja mtu anaugua gonjwa hili awe tayari kusema nilikuwa naugua gonjwa hili bila aibu. Tunazika watu wengi hata wasomi kabisa ambao wakati wa kuugua anaonekana anaugua Ukimwi ila siku ya kufa utasikia eti anaumwa sijui kansa, presha na kadhalika. Ni usiri wa kijinga tunauendekeza na ambao hatima yake ni kiini macho cha vita ya ukimwi. Umefika wakati tuache usiri bila hivyo ni vifo bila mabadiliko.

Mwisho, nadhani kwa mwenendo wa sasa, “Tanzania bila Ukimwi” haitawezekana kama raisi wetu anavyotusihi. Usiri huu kwa kisingizio cha kuzuia unyanyapaa ni chanzo cha janga hili kuendelea. Siamini nchi yetu inaweza kuendelea, ni wazi gonjwa hili litaendelea kudumaza na kuwamaliza wasomi wa nchi yetu. Ni mwaka wa ishirini na saba tangu gonjwa hili livamie nchi yetu na bado watanzania wengi hawajaamua kuacha ngono zembe, ni mwanzo wa kiama Tanzania.

Thursday, November 29, 2007

MALKIA ALIVYOFURAHIA UGANDA

Leo nataka tuone ni wapi Malkia Elizabeth alilala na ni jinsi gani aliandaliwa na kufurahi maisha ya kiafrika alipokuwa nchini Uganda.

KAMATI YA MADINI--NI SARAKASI ZA KISIASA ZISIZO NA TIJA SANA

Katika makala yangu ya mwezi September, tarehe 9, mwaka huu,katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili: “Bunge letu ni jumba la Sanaa”, ukurasa wa 12—13 , nilieleza kuwa demokrasia ya Tanzania ni ya kipekee duniani na kusema hivi: “kwa misingi kwamba tuna serikali isiyozingatia mihimili mitatu: Watawala, Bunge na Mahakama. Tanzania ya leo, serikali inaendeshwa kwa mihimili miwili: watawala na mahakama.” Hapa nilionesha wasiwasi wangu jinsi gani Bunge linafanya kazi ya kubariki na kuisemea serikali (rubber stamping) mijadala ya serikali badala ya kuihoji.

Hii niliona kama chanzo cha Bunge, kupitia wabunge wengi (majority) wa CCM walivyohakikisha wanaizima hoja ya Zito Kabwe na kumfungia kama adhabu kwa kile walichodai ni uzushi na utafutaji wa umaarufu kirahisi (cheap popularity).

Leo nataka niendelee nilipokomea kwani kutokana na mada ile ile ya Zitto Kabwe, rais Kikwete kaja na mpya. Kuunda kamati ya raisi kuchunguza ama kuipitia mikataba ya madini ni jambo zuri japo ninapata wasiwasi na utashi wa kweli wa hatua yake. Yaani raisi kama mkuu wa mhimili wa utawala na pia sehemu ya Bunge, ni wazi maamuzi ya awali ya kumuadhibu Zitto hayakuanzia tu kwa wabunge bali yalipangwa na raisi pia kupitia baraza la mawaziri, alafu waziri mkuu akawafunda wabunge wa CCM na maamuzi yakawa jinsi ilivyokuwa.

Mpango mzima wa kuzima madai yale ulishindwa na ukaleta matokeo isivyotarajiwa (backfire) na ikadhihirisha aibu kubwa ya kifikra kwa wabunge wa CCM na serikali kwa ujumla. Raisi anapong’amua hili alafu anawageuka wabunge baada ya kuwaaibisha kwa kuwashurutisha wafikiri visivyo. Ni kichekesho kikubwa; hebu fikiri Bunge letu limejaa wasomi, maprofesa, madaktari wa falsafa lukuki wa fani mbalimbali. Ni hatari kwa nchi kubwa kama yetu yaani mafanikio yote haya ya kitaaluma hawawezi kufikiri sahihi wala kusoma alama za nyakati.

Ukiacha hilo, raisi anajaribu kukiuka ahadi yake ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya. Raisi anaturudisha kulekule kufanya mambo kwa mazoea kitu ambacho amekuwa akikipinga. Uundwaji wa tume ya raisi wala si ya Bunge unanifanya nianze kukosa imani na raisi kwa hili. Swali: Inakuwaje Bunge, linaamua kufanya kazi ya mhimili wa watawala na kuacha wajibu wake wa kuhoji au kuchunguza madai halali ya Zitto kwa kisingizio cha Spika eti tungepoteza pesa bure baada ya kupoteza zile za tume ya madai ya Mengi awali. Pili, hivi hii tume ya raisi ya leo hii haitumii pesa?

Wajuzi wa masuala ya kiuchunguzi wanasema tume ya raisi haina meno kisheria kama ile ya kibunge. Ni wazi raisi anajaribu kutuchezea mchezo wa kisiasa katika kujaribu kuifuta ile kashfa ya Buzwagi. Hoja ya Kabwe ilikuwa juu ya uvunjaji wa taratibu kusaini mkataba wa Buzwagi kule hotelini Churchil. Raisi kaiteka nyara ile hoja na akageuza kuunda kamati kuchunguza mapitio ya mikataba yote ya madini. Hapa nashangazwa na utashi wa kupambana na ufisadi kama ni kiini macho tu. Najiuliza: hivi zile juhudi zote sa Spika na Wabunge wa CCM kutumia kanuni halali za Bunge na kuzima kwa msisitizo mkubwa hoja ya Buzwagi zilikuwa za kuwalinda akina nani?

Kuna harufu ya rushwa hapa, kwani kama tunapitia sheria zote za madini basi labda tunataka kuondoa akili ya watanzania wote kutoka Buzwagi na kuzika madai ambayo Spika ama kwa utashi wake ama kwa maagizo hakutaka kabisa iundwe kamati ya Bunge.

Hata hii kamati ya Bunge ya kuchunguza mkataba wa Richmond inatia wasiwasi sana juu ya utashi wa kweli kama upo. Ukifikiri sana unajiuliza: kwanini imeundwa leo hii na si wakati ule ambapo ilipingwa kwa nguvu zote? Hata taasisi nyeti ya uchunguzi wa rushwa (Takukuru) ilishaisafisha Richmond lakini mara tunaona mabadiliko ya bunge letu (U-turn) na sasa bunge linakubali kamati ya Bunge iundwe. Hapa nina wasiwasi sasa wahusika wameshaandaa nakala-vielelezo mpya za kufuta ushahidi wa rushwa na maadam wameshajihami basi wana hakika Kamati ya bunge itawakuta ni wasafi.

Jambo lingine kwenye hii kamati ya raisi kupitia sheria za madini: vipi miongoni mwa wajumbe wa tume ya raisi ni wabunge wawili wa CCM ambao kwa nguvu kubwa walipiga makelele kwa kupiga meza katika kuzima kabisa hoja ya Buzwagi? Kama hawakuona kabisa utata katika mkataba ule hivi kweli ni watu wenye utashi wa kuchunguza mikataba ya madini? Hapa ndio pananitoa imani na uamuzi huu wa kuunda kamati ya raisi.

Wasiwasi wangu mwingine, nakumbuka wakati anaongea na Sauti ya Amerika (VOA) akihojiwa na Shaka Sally kupitia kipindi cha Straight Talk Afrika kutoka Chamwino Dodoma, raisi alisema mikataba yote ya madini imeshapitiwa na sasa inaendana na viwango vinavyokubalika kimataifa. Nakumbuka alizungumzia mambo kama ya mirabaha inayolipwa na kampuni za madini na hata lile suala nyeti la mgawanyo wa kodi wa asilimia 3% kwa 97% na akasema sasa ni 30% kwa 60% kama sijakosea kukunukuu. Sasa kuunda kamati kupitia tena sheria za mikataba kunamaanisha alikuwa anadanganya? Nilitegemea raisi aunde kamati kuchunguza Buzwagi—kiini cha madai ya Zitto. Sasa hii upitiaji wa mikataba ambayo raisi amewahi kusema imepitiwa na wataalamu ni nini tena?

Hapa raisi mimi binafsi nadhani tumwamini kwa maamuzi yake japo utashi unatutia wasiwasi. Nampa imani ya kidhahania tu (benefit of doubt) na tusubiri tuone kweli kama tume yake itapendekeza nini na kama atafanyia kazi mapendekezo hayo. Mambo haya ya kufunikafunika ni mbinu za kisiasa zilizopitwa na wakati. Nina wasiwasi raisi hajui kuwa nchi yetu ipo katika kipindi cha kiongozi mkuu kufanya maamuzi magumu la sivyo umaarufu wa chama na serikali yako utagharimika sana. Ni wakati wa “Utawala Bora” kuachiwa ufanye kazi. Mihimili mitatu ya dola isipoachiwa ifanye kazi kwa kujitegemea bila kuingiliwa na watawala basi ndio tunashuhudia usanii kila kukicha hasa tangu awamu ya nne ianze.

Ule wakati wa kuwachukulia watanzania kama watu wa mawazo finyu (gullible) umekwisha. Ni wazi kama rais na chama chake hawakutaka kamati ya bunge kuchunguza Buzwagi ila anaamua kuunda kamati chini ya mamlaka yake. Lengo linaweza kuwa ni kuweza kudhibiti uchafu wote utakaoibuliwa usishughulikiwe kwa mujibu wa sheria. Tume aliyoiunda inawajibika kwake na wala haina nguvu za kisheria kuwezesha mapendekezo yake yafuate mkondo wa kisheria iwapo itathibitika kuna haja ya kuwawajibisha vigogo fulani.

Ndio maana ikiwa tume itawakilisha ripoti kinyume na matarajio ya Raisi, tusishangae yale yaliwahi kumkumba Jaji Robert Kisanga wakati wa enzi za uwazi na ukweli yakamkumba pia Jaji Mark Bomani. Binafsi nimeitafakari hatua ya kuunda kamati ya raisi na si ya Bunge kama sarakasi za raisi katika kufunika kashfa ya Buzwagi. Ni dhihirisho jinsi Bunge lilivyotekwa na mhimili wa watawala (executive’s hijack of the legislature). Raisi anafanya kila juhudi kuendeleza hali tata iliyopo (Status Quo) yaani kuzuia mabadiliko ya kifikra na hata jinsi mpya ya kiutendaji ili kuikwamua nchi yetu katika umasikini wa kujitakia.

Kwa mwendo huu kama viongozi wa bara la Afrika hawataki kuruhusu mfumo wa utawala bora ufanye kazi basi katu haisaidii juhudi za kujikwamua na umasikini. Haya ndio yananifanya niwe na wasiwasi na tume ya raisi; hebu tusubiri tuone kama itakuwa na tija. Lakini ningekumbusha mbona tunaizika kashfa ya Buzwagi? Hii ni sarakasi ya raisi; je itafanikiwa? Tusubiri tuone.

Saturday, November 17, 2007

LEO JUMAMOSI

Profesa Mazrui kaandika juu ya mapambano ya mwafrika; na pia kama kawaida napenda sana kujijuza mambo ya nyakati za Iddi Amin.

Wednesday, November 14, 2007

RAIS KIKWETE ADHIHIRISHA JINSI BUNGE LISIVYOJALI MASLAHI YA NCHI

Sijui niuite ni ukinyonga au niseme nini ila kama kuna siku rais Kikwete kanichekesha ni pale niliposikia kuwa ameunda tume ya kuchunguza na kupitia mikataba ya madini. Mshangao ulinipata baada ya kusikia eti na mheshimiwa Zito Kabwe nae ni miongoni mwa wajumbe wa tume. Kwangu hii ilikuwa ni faraja kusikia hili la kumjumuisha mpinzani ndani ya shughuli kama hii. Zaidi kumjumuisha Zito Kabwe lilinichekesha sana.

Zitto Kabwe ndie mwaanzilishi na mpiga filimbi mkuu aliyethubutu kujitoa mhanga na hatimaye kupewa adhabu ya kutohudhuria kikao cha Bunge kinachoendelea sasa ili kutaka tume ya Bunge iundwe kuchunguza haya rais anayoyaundia tume. Kama mtu unafikiri na si kimgandomgando, unapata hisia kuwa raisi Jakaya Kikwete amelipiga bunge mwereka kimawazo. Ni katika msingi huu Bunge letu hasa vinara wake: Waziri Mkuu na Spika pamoja na wabunge wote waliounga mkono Zitto apewe adhabu wanafanywa ni wajinga ajabu.

Saturday, November 10, 2007

MSONGO WA MAWAZO TATIZO KUBWA UGANDA

Jamani watu wengi wana msongo mkubwa w a mawazo au wana tatizo la kisaikolojia; Uganda eti watu wengi wamechanganyikiwa. Pia ziara y a Museveni Marekani imekuwa gumzo juu ya uswahiba m p ya na Joji Kichaka.

MUSEVENI NA UTUNZI WA VITABU

Museveni ni rais mahiri kwani huwa anaandika vitabu na hata makala magazetini. Karibuni kaandika kitabu na kimeshangaza kidogo kimtazamo. M useveni anaaminika kama kiongozi bora ila kuna haja ya mabadiliko kwa mujibu wa jaji maarufu. Pia tujiulize je Big Brother ni muhimu sana?Pia benki zimeanza kuhimiza ndoa unazijua?
Pia tunajuzwa zaidi ni vipi Iddi A min alivyowapendelea watu wa kabila lake.

Kumbe John Garang aliuawa na serikali ya Uganda? Kumbe pia uzazi bila mpango ni chanzo cha Ukimwi kuenea kwa kasi? Mwisho kabisa hii ni kali yaani kuna kesi kubwa ya aina yake nchini Uganda.Unamjua mtuhumiwa wa wizi wa f edha za Gl obal Fund?Na ugonjwa wa m araisi wa Afrika je?

Monday, November 05, 2007

KWANINI VIGOGO WANAPENDA HOSPITALI ZA MAJUU?

Ama kweli bongo kuna vituko, huwezi amini eti madaktari wanaweza kosea namna hii; mambo kama haya yanawezekana bongo tu. Inawezekana ndio maana vigogo wanaziogopa hospitali za bongo.

Saturday, November 03, 2007

IDDI AMIN MZIMU BADO HAI

Kwanza kabisa leo tukumbushane juu ya Iddi Amin; alafu tutizame waasi wa LRA Uganda wanavyojaribu kujirudi.
Alafu kuna hili gonjwa la kisukari linakuwa sugu, hali ni mbaya Uganda.

Na kwa wale mapedeje, mnajua gharama zake?

Saturday, October 27, 2007

DR. JAMES WATSON NA MALUMBANO YA AKILI ZA MTU MWEUISI

Je akili za waafrika ni sawa na za wazungu? Ushindi wa urais bora kwa Chisano una ujumbe gani kwa maraisi wengine?
Mambo ya siasa ni kuwa eti kiranja wa bunge la Uganda ni mvunjaji sheria mkubwa.

Thursday, October 25, 2007

KWAHERI MAMA MBATIA

Ni habari za kusikitisha Naibu waziri wa wizara ya Maendeleo ya Wanawake, Jinsia na Watoto amefariki kwa ajali ya gari jana huko mkoani Iringa. Picha hii ni dhihirisho la ubaya wa ajali hiyo.
Huu ni mwaka wa ajali nyingi sana hasa kwa viongozi wetu, ni wazi kuna tatizo kubwa katika matumizi bora dhidi ya watumiaji wa vyombo vya moto.

Saturday, October 20, 2007

DUBE MWANAMAPINDUZI HALISI

Lucky Dube katutoka; ni jambo la kusikitisha sana. Mungu amlaze pema peponi. Dube alifahamika kila kona ya Afrika hasa wakati wa kipindi cha makaburu. Aliimba kuhamasisha dhidi ya ukaburu; sitamsahau.
\Pia tunakumbushwa kujali njia ya ABC dhidi ya Ukimwi na pia je unawajua Waganda wenye akili sana?

Tuesday, September 25, 2007

SHIRIKISHO LA AFRIKA MASHARIKI KUREJESHA ENZI ZA FALME YA BUNYORO KITARA

KUTOKA "FAST TRACKING HADI DOUBLE TRACKING"--SHIRIKISHO LA AFRIKA MASHARIKI KATIKA MCHAKATO MPYA.

Hivi majuzi jumuiya ya Afrika Mashariki ilipigwa butwaa baada ya kuripotiwa kuna juhudi za kichinichini kuanzisha shirikisho kati ya Uganda na Kenya na kuiacha Tanzania kwani inaonekana kuzuia mawazo ya rais Yoweri Museveni ya kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki ifikapo mwaka 2013. Ghafla kama wiki mbili zilizopita kumeripotiwa eti Museveni anaendeleza ushawishi na Kenya ili Uganda iungane na iunde Shirikisho na kuiacha Tanzania ambayo inaonekana bado inasita kwa mujibu wa ripoti ya kamati ya maoni ya wananchi wake.

Asilimia 80% ya watanzania hawakuunga mkono wazo la Shirikisho kuharakishwa ingawa asilimia 97% waliunga mkono wazo la Shirikisho hatua kwa hatua. Habari hizi za juhudi za chinichini za Museveni hazikunishangaza hata kidogo bali zimenisukuma kuandika makala ya leo hii.Leo nataka tushirikishane ndugu wasomaji wetu ni kwa vipi haiba ya rais Museveni inaashiria ni mtu wa kuburuza mambo yake yafanyike hata pale inapohitaji watu kushirikiana na kuheshimu maamuzi ya pamoja. Ningependa tutafakari kama kweli Museveni ana malengo yenye tija kwa watu wa Afrika Mashariki au ni janja ya maslahi binafsi? Je watanzania tunamfahamu mtu huyu hasa au ni jujuu tu?Pia ni lazima tuone kama kweli mtindo wake wa uongozi wa Uganda kwa miaka zaidi ya ishirini unampa sifa kutuongoza katika utengamano? Nitaanza kwa maoni juu ya kikao cha mwisho cha viongozi wetu pale Arusha mwezi uliopita.

Kwanza kabisa, viongozi wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walipokutana Arusha mwezi uliopita walifanya maamuzi kamambe ili kuokoa juhudi za ufufuaji wa jumuiya ambapo ilishaanza kupingwa na wananchi katika kura za maoni hasa Tanzania. Kubwa lilikuwa juu ya kuharakisha uundaji wa shirikisho ifikapo mwaka 2013.

Nilipokea maamuzi ya viongozi wetu kama tukio la aina yake kwa viongozi wetu kwa mara ya kwanza baada ya maberamu dhidi ya kuharakisha shirikisho kuzidi sana wameamua waanze kusikiliza sauti ya watu. Nakumbuka niliwahi kuwafananisha na kondoo ambaye anapelekwa machinjioni asiyejua kuna kifo katika makala yangu ya tarehe 26/08/2007 dhidi ya uharakishaji huu. Viongozi wetu walikubaliana kubaki na lengo la kufikiwa kwa Shirikisho ila kwa sasa ni lazima taasisi nyeti ziundwe kwanza. Kwa maana nyingine tuanze kuungana kiuchumi--kibiashara na shughuli kadhaa za kijamii. Ila serikali moja si wakati muafaka. Mimi ni muumini wa hili waliloamua kule Arusha mwezi uliopita. Yaani muungano wa Ushuru wa Forodha, Soko la Pamoja na hata Sarafu Moja, uhuru wa watu kuvuka mipaka kama wafanyabiashara, wafanyakazi na hata bidhaa bila vipingamizi visivyo vya lazima pamoja na mambo mengi chungu mbovu ambayo tayari yanafanyika hadi sasa.

Binafsi, ninaamini kabisa Shirikisho halina tija kwa jamii ya Afrika Mashariki ila tu mashirikiano ya kiuchumi ndiyo yenye tija. Tukiharakisha shirikisho bila kuwa na taasisi (institutions) zenye nguvu kukabili nyanja mbalimbali za mahusiano ni bure na ndio hapa panaponifanya niamini kuna mizengwe ya wazito fulani wenye mkakati binafsi usiozingatia maslahi ya wananchi kwa ujumla wao. Malengo ya utawala bora katika nchi zetu bado hayajafikiwa hasa nchini Uganda sasa je kweli mtu ambaye hajafanikiwa kuleta utawala bora ana nini kipya katika Shirikisho? Je ni kwanini nina wasiwasi sana na juhudi za raisi Museveni?

KUTOKA MCHAKATO MMOJA HADI MIWILI (FAST TRACKING TO DOUBLE TRACKING)
Baada ya kikao kile cha Arusha, tarehe 20, August 2007, ni wazi mwelekeo wa muundo wa Shirikisho umekumbwa na wimbi jipya. Raisi Museveni inaripotiwa, na gazeti la 'Sunday Monitor' la tarehe 23, September 2007, alimtuma mjumbe maalum kwa mwenzake wa Kenya akimhimiza rais Kibaki kuunda Shirikisho jingine lisilojumuisha Tanzania lakini litakalotoa mwanya kwa Tanzania kujiunga itakapokuwa tayari. Ni mchakato mpya ambao wachunguzi wa mambo ya siasa za jumuiya ya Afrika Mashariki, wanadai ni mpango utakaoendeshwa kwa staili tofauti ya uharakishaji kutoka ile ya "Fasttracking hadi Double Tracking". Serikali ya Uganda haijakanusha haya kwa hivyo ni wazi juhudi hizi ni za kweli. Hapa Museveni anaonesha ni jinsi gani asivyopenda kusikiliza maoni ya watu wengi; au kwa maana nyingine anamaanisha lile zoezi zima la ukusanyaji maoni halikustahili labda. Watu wameamua sivyo na yeye anaamua kuja na mkakati mpya.

Kwa maana nyingine, Kenya na Uganda zinatangulia na Shirikisho wakati Tanzania nayo ikija kwa mwendo wa pole.(Double Tracking). Tayari jina la Shirikisho hilo limebuniwa, nalo ni "Muungano wa Wenye Nia" (Coalition of the Willing). Hata makao makuu mapya inasemekana yanatajwa kama yatakuwa ya muda kule Entebbe Uganda wakati wakisubiri ya kudumu kule katika mji wa vilima wa Tororo Uganda. Hii yote inaaminika itashinikiza Tanzania kufikiri na kubadili msimamo. Wachunguzi wa jinsi juhudi za Museveni zinavyohakikishwa zinafanikiwa, ni kwamba baada ya ugunduzi wa mafuta katika ukanda wa eneo la ziwa Albert (Albertine) basi inapanga kutumia nguvu ya fedha ya mafuta hayo kuhakikisha siku za usoni ndio inakuwa na ushawishi mkuu katika eneo zima la maziwa makuu. Mafuta yatatumika kama rungu ama silaha ya kidiplomasia kuhakikisha mradi wowote wa mashirikiano ukibuniwa na Uganda unafanikiwa kwa vyovyote vile.
Binafsi Museveni kaamua kuihujumu Tanzania kiaina kwani kama kweli ana nia njema ni kwanini tayari wana mawazo ya makao makuu mapya? Na kama ni kweli wamefikia hatua hii ina maana tayari Museveni alikuwa na mipango tayari kwani si mambo rahisi tu kuamua ni wapi pa kujenga makao makuu ya muda na pia ya kudumu bila kuhusisha maamuzi ya taasisi kama Bunge.

MASLAHI YA NCHI NDANI YA SHIRIKISHO
Inaripotiwa pia kuwa katika kuishawishi Kenya iunde Shirikisho jipya-Wenye Nia-Uganda imeihakikishia Kenya itafaidika 'kiuchumi' kwa kupanua soko la bidhaa zake hadi Rwanda, Burundi, Uganda, Sudan ya Kusini na hata Kongo-DRC. Kwa upande wa Uganda, yenyewe imebainisha maslahi yake ni ya 'kisiasa' ikimaanisha hapa ni wazi Museveni anawaza zaidi utawala. Ni katika mtizamo huu najiuliza je kama Tanzania tunajiunga na mchakato huu wa Shirikisho, je maslahi yetu ni nini?
Ni wazi iwe isiwe, Kenya ina uchumi mkubwa na imara kuliko nchi zote na ndio itakayofaidika zaidi. Lakini sisi kama Tanzania ili tuamue kujiunga na wenye nia, ni lazima tuwe makini na tujue maslahi yetu ni yapi la sivyo hakuna haja ya sisi kuwa kwenye shirikisho.

WASIWASI--CHUKI ZA KIKABILA UGANDA
Kuna tatizo kubwa sana la chuki kali sana za kikabila nchini Uganda na ni vizuri ieleweke kuwa hii ni sababu ya kihistoria katika nchi hiyo kwa kiasi fulani. Ikumbukwe kuwa Uganda ilipata uhuru wake Waziri mkuu wake wa kwanza na baadaye Raisi alikuwa ni Dr. Milton Obote mzaliwa wa Kaskazini mwa Uganda. Huyu aliwajaza jeshini wazaliwa wa kaskazini kwani ndio waliokuwa wakitumika shughuli za jeshi tangu wakati wa ukoloni. Baadaye alipinduliwa na Iddi Amin ambaye alitoka kaskazini pia na akaendeleza utawala wa watu wa kaskazini katika kila nyanja.
Hadi anakuja kupinduliwa na majeshi ya Tanzania yakisaidiana na wakombozi wa Uganda chini ya watu kama Yoweri Museveni na wengine Uganda ilikwishatawaliwa na watu wa kaskazini kwa miongo zaidi ya mitatu tangu uhuru. Obote alirudi madarakani kwa uchaguzi uliojaa mizengwe ya kitanzania inavyodaiwa ambayo ilimfanya Yoweri Museveni kuamua kurudi msituni kwani alidai uchaguzi kuendeshwa kimizengwe. Ikumbukwe aligombea urais wakati huo-1980 na kushindwa vibaya. Ila baadaye Obote alipinduliwa na Tito Okello; hali yote hii ikiendeleza utawala wa watu wa kaskazini. Tito Okello akapinduliwa mwaka 1986 na Yoweri Kaguta Museveni akachukua hatamu kuifufua nchi ambayo ilikwisha poromoka kiuchumi hadi kufikia hatua mbaya (failed state).
Kwa umahiri mkubwa kabisa Museveni akaweza kuifufua nchi na kuisimamisha hadi kuwa sawa na majirani zake kwa sasa. Ni jambo ambalo atajivunia hadi kaburini; ila uongozi wake ulikuwa wa mabavu, yaani mfumo wa "vuguvugu-movement"ambao haukuruhusu vyama vya siasa. Katika kipindi chake cha uongozi ni wazi serikali ya NRM imekuwa ikiongozwa chini ya viongozi kutoka makabila ya magharibi (westerners) katika nyadhifa zote za juu. Hali hii imejenga chuki kati ya watu wa kaskazini na kusini kwani inaaminika baada ya Museveni kuingia madarakani basi ulikuwa ni mwisho wa wakati wa watu wa kaskazini kutesa.
Hisia hizi pia ziko kwa watu wanaounga mkono hata ule uasi wa LRAkule kaskazini. Hali inamfanya Museveni kuwa mwoga na maisha baada ya urais na hivyo kuharakisha uundwaji wa Shirikisho ili aendelee kuwa kwenye hatamu za uongozi wa juu na asiyeweza kuguswa na vyombo vya sheria.

Kama sijakosea ni wazi wazo la kuharakishwa kwa shirikisho lilianzishwa na Rais Museveni na mara moja aliweza kuwashawishi wenzake na likapewa kipaumbele na ndio ikaundwa kamati ya kukusanya maoni ambayo kwangu ulikuwa ni ubadhirifu mkubwa iwapo ni kweli Museveni anaishawishi Kenya kuendelea na juhudi za kuharakisha baada ya Tanzania kutokuunga mkono wazo lake. Inaonekana alitegemea serikali ya Tanzania ingefanya mizengwe na kutosikiliza sauti ya wananchi.

Moja ya udhaifu wa Museveni ni mtu anayependa ubabe na anapokuwa na nia ni lazima itekelezwe. Kwa mfano, amekwamisha suluhu ya vita ya LRA kwani anawafananisha na majangili (thugs) akidai ni kikundi kidogo cha wahuni lakini la kushangaza ni miaka zaidi ya ishirini ameshindwa kuwamaliza. Wakosoaji wake wanadai hawajali sana watu wa kaskazini dhidi ya mateso ya vita na hapa pamemjengea chuki kubwa dhidi ya watu wa kaskazini. Binafsi nina marafiki kadhaa wanaotoka kaskazini mwa Uganda ukiwasikiliza hawafichi chuki zao dhidi ya makabila ya magharibi na kusini kama ndio chanzo cha madhila ya kaskazini. Ikumbukwe tangu Museveni aingie madarakani, Uganda iko chini ya watu wa magharibi wanaojulikana kama (westerners): wanyankole, watooro, wachiga, na wanyoro. Niliwahi kuzungumza na jamaa mmoja wa kabila la la magharibi 'mtooro', akaniambia "acha jamaa wateseke, walitutesa sana nyakati za Amin na Obote". Ni wazi kuna chuki za kisirisiri dhidi ya watu wa sehemu fulani ya nchi (xenophobia) ambapo Museveni hajafanya juhudi za kutosha kuziondosha ingawa ana uwezo huo. Ni nadra sana kwa watu wa kaskazini kuoana na watu wa magharibi.
Kwa mantiki hii, Rais Museveni lazima abebe lawama kama mtu asiye na haiba ya kuunganisha jamii kuishi kwa utengamano; na ndiye mtu anayedai anaweza kuiongoza Shirikisho la nchi tano kuishi kwa utangamano. Ni kiroja na siamini kama kweli anatufaa.

KUCHIPUA KWA MBEGU YA CHUKI

Baada ya mapinduzi ya mwaka 1986, mbegu ya chuki za kikabila ndipo ilipoanza kuchipua hasa. Museveni akampindua Tito Okello; askari wa Okello walikimbilia Kaskazini wakipita Jinja, Tororo hadi Lango na Acholi--kaskazini na kuanzisha uasi ambao hata hivyo haukuwa na nguvu. Baadaye Museveni aliwashawishi waasi na kukaa mezani na baadhi ya makamanda wao wakakubali yaishe na wakazawadiwa nyadhifa serikalini. Mmojawapo alikuwa Jenerali Moses Ali ambaye alikuwa mmoja wa vigogo wa vyeo vya juu kabisa hadi uchaguzi wa mwaka jana. Askari ambao hawakutaka suluhu walibaki msituni na ndio ukawa mwanzo wa uasi chini ya mama Alice Lakwena na baadaye Joseph Kony hadi leo.

Wote hawa wamekuwa na madai mengi mojawapo kuchukizwa na 'unyanyapaa' dhidi ya makabila ya kaskazini. Kuthibitisha haya, taasisi zote nyeti za serikali na idara zake ziko chini ya watu kutoka magharibi-kusini ukiacha spika wa Bunge. La kushangaza kama ni wasomi waliobobea wengi wanatoka Kaskazini na Mashariki--Lango, Pakwach, Acholi, Pader, Teso, Tororo n.k. Hawa wapo nchi za nje kama Marekani, Canada, Uingereza, Australia huku kukiwa na tetesi miongoni mwao ni wafadhili wakubwa wa LRA.
Kwa maelezo hapo juu, hii ndio jamii iliyo chini ya mtu anayetaka kwa nguvu za ushawishi mkubwa tuunde Shirikisho; tujiulize je kweli ana jipya kama kashindwa kuunganisha nchi yake? Je nchi tano ataziweza? Ni wazi ni kiongozi anayeongoza sehemu moja ya nchi kama vile eneo lililotekwa kivita (conquered territory). Yaani watu wa kaskazini kwa miongo kadhaa wamekuwa wakiishi katika makambi (IDPs) chini ya hali ya hatari kwa muda wote. Kisa ni serikali kukosa busara za kumaliza vita; yaani kushindwa kukang'amua njia bora ya kutatua tatizo la LRA na badala yake kusisitiza njia za kijeshi ambazo zimeshindwa kabisa. Ni hivi majuzi baada ya uchaguzi ambao ulionesha mgawanyiko mkubwa wa wananchi ndipo angalau Museveni akakubali kukaa mezani japo inaonekana huenda akarudi msituni.

JE NI LAZIMA AWE RAIS WA KWANZA WA SHIRIKISHO?
Ukiacha sababu ya woga wa maadui asiyewafahamu (paranoia), Rais Museveni ana tabia ya usaliti kwa wale anaoshirikiana nao hasa watu makini wenye misimamo. Hii inajionesha wazi baada ya Museveni kuwaahidi wanachi mwaka 2001 kuwa alikuwa akigombea kwa mara mwisho alikuja kugeuka na kuwahonga wabunge shilingi millioni tano kila mmoja ili wabadili katiba kuondoa ukomo wa rais kugombea vipindi viwili vya miaka mitano.

Hii ilimruhusu kugombea kipindi cha tatu maarufu kama "third term" kitu ambacho kilimtenganisha na watu waliokuwa nae karibu sana tangu harakati za msituni. Wale wote katika baraza la mawaziri ambao hawakumuunga mkono aliwafukuza kazi kwa kisingizio cha kutokuheshimu utendaji kazi wa pamoja(collective responsibility). Kwa mfano, alikuwepo mtu wake wa karibu tangu utotoni, Eriya Kategaya, ambaye alikuwa waziri mkuu na ambaye sasa hivi amemrudisha tena kama waziri wa Afrika Mashariki na naibu waziri mkuu. Meja Amanya Mushega, katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki aliyepita pia alifukuzwa uwaziri na amekuwa akisimamia misimamo thabiti ya kidemokrasia. Hali hii ni kitu kilichompotezea marafiki wa karibu kwa kipindi kuelekea uchaguzi mkuu uliopita.

Pili, uchaguzi mkuu uliopita aligombea kwa mara ya tatu baada ya kubadili katiba na upinzani ulikuwa mkali ajabu ambao ulihitaji mahakama ya kijeshi "Court Martial" iliyokuwa chini ya Jenerali Elly Tumwine, mzaliwa pia wa kabila moja na rais kutumika kumuundia mashtaka ya bandia mpinzani wake mkuu. Hii ilimnyima mpinzani wake kupata muda wa kutosha kupiga kampeni na badala yake kukimbizana na kesi muda wote. Hali hii iliongeza ukinzani au mbinyo wa mataifa wafadhili kwa Museveni. Ni wakati huu alipoona ndoto ya kuendelea kung'ang'ania madaraka siku za usoni itakuwa ngumu sana na akaanzisha wazo la kuharakisha shirikisho "fasttracking". Inawezekana kabisa anaamini atakapomaliza uraisi wake 2011, atakuwa na mwaka mmoja wa kampeni na mwaka unaofuata anachukua hatamu za uongozi.

Tatu, kuna kanuni ya hila "conspiracy theory" inayodai kuwa Museveni kama mtoto wa chifu wa kabila la Wanyankole-Hima, ana tabia za kutawala kwa kujitanua kupitia uvamizi wa mataifa jirani "expansionism". Hii ni tabia ambayo ameshaionesha tangu asaidie kuikomboa Rwanda, na baadae akaivamia Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo. Utaona baada ya kusaidia juhudi za ukombozi alitaka pia kuzitawala nchi hizo kwa kuwageuza viongozi wa nchi hizo kama vikaragosi wake (puppets) kitu ambacho kilimgombanisha na watu kama raisi Kagame na hata sasa hana uhusiano mzuri na rais Kabila. Kwani anajulikana anaunga mkono mpinzani mkuu wa Kabila, Jean Pierre Bemba. Ni hisia hizi zinadhaniwa na wengi labda ndizo zinazomsukuma ili atakapokuwa chifu wa Shirikisho si ajabu akatunisha misuli yake na kuteka nguvu za serikali za nchi shirika. Kitu ambacho kinaweza kuja leta matatizo sana.

Kanuni hii ya hila za Museveni inachangiwa na muundo halisi wa serikali yake kama nilivyokwisha eleza awali imejaa watu wa kabila lake hasa. Mwandishi mmoja, aliwahi kusema ni serikali inajionesha katika mantiki ya muungano wa kikabila yaani akaiita "Kinyoro Kitara Kingdom". Ikumbukwe kihistoria Bunyoro Kitara ilikuwa falme kubwa ilijomuisha makabila kadhaa chini ya Mfalme mmoja. Makabila haya ni kama Wanyankole (kabila la Museveni), Watooro, Wabusoga, Wanyoro, Karagwe na hata Wabaganda. Katika mtizamo huu si ajabu historia inaweza kujirudia kupitia kinara mkuu--Museveni. Ni kama serikali ya kifalme hivi kwani hata vigogo wa juu kabisa ni ndugu wa damu. Kwa mfano, binti wa Museveni kaolewa na kijana wa Waziri wa mambo ya nje--Sam Kutesa. Kwa mujibu wa tamaduni zao, watoto wa vigogo wanaoana wao kwa wao kutoka kabila moja: wanyankole. Ni kama serikali ya kifalme hivi (monarchy)

Jambo lingine ni hatua ya mama Janet Museveni, mke wa Museveni, kugombea ubunge uchaguzi mkuu uliopita. Inasemekana Museveni alipinga sana hatua za mkewe kugombea ubunge japo familia nzima iliunga mkono. Tetesi ni kuwa Mama anajiandaa kurithi nafasi ya mzee alafu na yeye ajikite kwenye shirikisho. Kwa maana nyingine familia itakamata hatamu za nchi na shirikisho kwa ujumla. Kama si hivi basi inahisiwa mtoto wake pekee wa kiume, Meja Kainerugaba ambaye sasa yupo masomoni majuu anaandaliwa kumrithi baba yake. Kwani amekuwa akipelekwa kuhudhuria masomo ya kijeshi katika vyuo maarufu vya kijeshi Uingereza na Marekani. Hadi anakwenda masomoni mwaka jana ndie aliyekuwa mkuu wa kikosi cha ulinzi wa rais (Presidential Guard Brigade).

SHIRIKISHO KWA NJIA YEYOTE ILE
Awali nimesema kuwa siku za karibuni Raisi Museveni karipotiwa kuanzisha juhudi mpya kwa siri za kuishawishi Kenya iungane na Uganda na kuikacha Tanzania ambayo bado haiko tayari. Mimi naiona hatua hii kama kiashirio cha dhati kuwa Museveni anatafuta mahali pa kutokea "Exit Strategy" na iliyobakia ni Shirikisho kuharakishwa.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la Uganda, Museveni aliwahi kunukuliwa hapo November 29, 2005 akiwahutubia waandishi wa habari: "Tutakapokuwa kwenye awamu yangu ya tatu (third term) sala yangu kuu ni kuanzishwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki. Ifikapo mwaka 2010, tuwe na uraisi wa kupokezana na 2013 tuwe na raisi mmoja wa kuchaguliwa. Kama msomaji una akili timamu lazima ujiulize suala la muda hapa (timing) . Aliongeza zaidi: "Hilo likitokea utaona mtu aking'ang'ania kustaafu hata kama mnaleta tingatinga kunilazimisha nibakie madarakani, nitaenda kuchunga ng'ombe". Inaonekana hapa si kwamba Museveni alimaanisha kustaafu siasa za Uganda ataenda kijijini, ila atapenda ahamishe ikulu yake kutoka pale "Nakarero" hadi Arusha. Hii kwenda kuchunga ng'ombe kijijini kwake kule 'Rwakitura' wilayani Mbarara ni janja tu.
Mwisho, jambo la msingi ni wazi kuwa rais Museveni ni kiongozi shupavu na mwenye kuthubutu kufanya mambo makubwa bila kujali mbinyo wa wapinzani. Hii ni sifa ambayo viongozi wengi hawana na ni silaha yake kubwa. Ila tu tatizo mara nyingi maamuzi yake si kwa ajili tu ya nchi bali maslahi binafsi.
Wasiwasi wangu unaanzia hapa: Mwanzoni alidai Shirikisho kwa misingi ya 'Wigo mpana wa Soko', kutokana na idadi ya watu wa nchi tatu na baadaye tano. Sasa anapoiacha Tanzania, tena yenye watu wengi kuliko nchi mwanachama yeyote.
Tujiulize: je wigo wa soko unaongezeka au unapungua? Hapa ananiacha hoi; kama si ukubwa unatafutwa ni nini hasa? Nitaendelea kuwajuza siku zijazo.

Saturday, September 22, 2007

MUSEVENI NA HILA DHIDI YA TANZANIA?

Museveni mambo yalivyo ikulu ni vituko, yaani katibu wa rais ndio kama Makamu wa Rais.Pia kuonesha kuwa Museveni ana roho ya kwanini, ukikosana naye, anakufuatilia mpaka uliko hata nchi za nje ili usiajiriwe.
Pia hebu tujionee ni vipi Uganda na Kenya zina mbinu za kichinichini dhidi ya Tanzania juu ya Shirikisho?

Saturday, September 15, 2007

KENYA UGANDA KUUNDA SHIRIKISHO-EAC

Museveni kaanza tena kuonesha ni jinsi gani alivyopania kuwa Raisi wa kwanza wa EAC-Shirikisho. Huyu ni kiongozi shupavu ambaye ana malengo, sasa kaashauri Uganda ijiunge na Kenya. Pia hebu jisomee jinsi gani Nyerere alivyompindua raisi wa zamani Uganda, Binaisa.

Saturday, September 01, 2007

MFUMO WA KISIASA TANZANIA NI MBOVU SANA

MARA NYINGINE NAFIKIRI WABUNGE WA CCM WANAGEUZA BUNGE KUWA"NATIONAL THEATER'

Tusipobadili katiba hatufiki popote hata kama CCM itashindwa.

Leo nikiandikia ndani ya "Tanzania Daima" napenda nigusie juu ya mfumo wetu wa kisiasa niuonavyo nadhani una tatizo na tusipoweka tafakuri za kina sio ajabu tukawa tunalaumu wanasiasa wetu--hasa wabunge wa chama tawala-- na baadaye kitakapokuja shinda chama kingine mambo yakawa kama sasa. Naliona bunge letu kama si chombo kinachotekeleza yale yaliyokusudiwa; yaani mhimili wa kutunga na kuipa changamoto serikali bila kuingiliwa na serikali. Labda nianze kwa kuonesha wasiwasi wangu juu ya uhuru wa kusema usivyozingatiwa hasa na taasisi hii.
Ni wazi, kuwa jamii huru ni ile abayo maoni pinzani yanazingatiwa au kuvumiliwa hata kama ni machungu kiasi gani. Kama mtu kasoma somo la fizikia, kuna kanuni isemayo kuwa: 'kila tendo lifanyikalo kuna matokeo sawa kutoka pande mbili zinazotofautiana' (tafsiri isiyo rasmi). Yaani: "for every action there is an equal and opposite reaction".

Kanuni hii inanisukuma kueleza hisia zangu juu ya tatizo kubwa la mfumo wetu wa kisiasa ambao nadhani una madhara mengi sana juu ya udhaifu wa Bunge letu. Nina fikra kuwa kwa ujumla watawala wetu bado hawajaweza kutoka katika fikra za umungu mtu; yaani kuwa tayari kusikiliza mawazo ya upande mwingine kwa moyo wa dhati. Bali yanayotokea mengi inaonekana ni 'bezo' kila serikali ama taasisi zake zinapokosolewa. Hawajui bado kama kwa kila watakachosema lazima kitapata wazo mbadala. Masikini, wamesahau hiyo kanuni ya fizikia!

Ni katika muono wangu huu wa kifizika ninaamini ingawa tumekuwa chini ya mfumo wa kisiasa wa vyama vingi ila bado hatujaweza kufaidi matunda ya mfumo huo kwa kiasi cha kukidhi haja ya kisiasa kuiletea nchi yetu utawala bora. Je ni kwanini nimeona hivyo? Nitaanza moja kwa moja kuangalia mfumo wetu wa kisiasa na kuoanisha na mambo kadhaa ambayo yanatokea nchini kwetu kuthibitisha kuwa bado tuna mambo ya msingi kuyafanyia kazi ili tufikie angalau demokrasia yenye tija kwa maendeleo ya nchi na wananchi wetu.

Mfumo wa siasa unaweza kuwa ule wa Chama kimoja, vyama vingi, au hata usio na vyama vya siasa bali wa kikundi cha askari (junta) kama uliokuwa nchini Uganda kipindi cha nyuma kidogo yaani ule wa vuguvugu-movement. Katika mifumo yote hii kama uhuru wa kusema na kuvumiliana hauzingatiwi basi jamii haiwezi kupiga hatua katika maendeleo. Ni katika mtizamo huu, kikao cha bunge la bajeti kilichomalizika hivi karibuni kwa kiasi kikubwa kimedhihirisha kuwa taasisi nyeti kama Bunge haizingatii sana uhuru wa kusema na kuvumiliana.

Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania la awamu ya nne lilianza na kauli mbiu za Spika Samweli Sitta eti litakuwa la 'viwango na kasi' na kutupa faraja watanzania wengi kama mimi. Ninasikitika mijadala ya hivi karibuni bungeni imeonesha badala ya kwenda mbele tumeamua kurudi nyuma (reverse gear); kuna dalili kubwa za uoza wa kujadili; na inaonesha bunge sasa ni taasisi isiyofaa (irrelevant) hasa mtu unapozingatia mambo ya uzalendo au maslahi ya Tanzania. Spika wa Bunge ndio chanzo cha uoza kwa kiasi fulani kwani jinsi anavyoadhibu wabunge inatia shaka. Anafikia kusema mbunge fulani anahitaji ushauri nasaha kwa hiyo asamehewe pale alipotenda kosa; mtu unajiuliza ni kanuni gani inasema haya unashangaa manake sidhani kama bunge letu lina watoa ushauri nasaha.

Ila ukiangalia hili la majuzi la mheshimiwa Zitto Kabwe, maamuzi ya bunge letu yanakanganya. Napata hisia spika kazidiwa na hisia za chama chake-CCM anapokuwa anataka kutoa maamuzi na anashindwa kutumia busara kama alivyoweza kuzitumia na kusema mbunge wa chama chake anahitaji ushauri nasaha. Natambua kwa kanuni za Bunge, ambazo hata Spika amekiri mara nyingi zimepitwa na wakati, kuna uhalali wa mheshimiwa Zitto Kabwe kuadhibiwa. Ila nashangaa kwanini busara haikutumika hapa? Ina maana hoja alizotoa mheshimiwa Zitto Kabwe hazina chembe ya kuona umuhimu wa kuunda kamati kuchunguza mambo yenye maslahi kwa nchi? Hivi kama ni kweli mkataba ulisainiwa nje ya nchi tena ndani ya hoteli ya Churchil na wala si angalau ubalozi kwetu London, kwani tusichunguze kama sheria zilifuatwa?

Hivi wabunge wa maeneo yenye migodi kama huko Buzwagi, Bulyanulu, North Mara, Mwadui na Nzega hawashangai ni kwanini watu wao bado wako nyuma kimaendeleo katika nyanja nyingi wakati wana utajiri mkubwa? Historia itawahukumu wabunge wa mikoa yenye rasilimali zinazoibiwa na wao kubariki bungeni kwa kile kinajionesha kama mapenzi ya chama zaidi ya wananchi waliowachagua. Hapa upande mmoja ninawalaumu wabunge wa sehemu hizo lakini kwa upande mwingine sitaki walaumiwe kabisa na ndio ningependa nizungumzie kuwa tuna tatizo. Tangu mwaka 1992, tumeanzisha mfumo wa vyama vingi tukiiga uendeshaji wake kutoka nchi za magharibi kama Marekani. Mfumo wetu naamini ni tatizo na unawalazimisha waheshimiwa wabunge wa chama tawala kuzima mfumo wa kufikiri waliojaliwa na maulana wanapokuwa bungeni.

Ninadhani bunge, kama mhimili muhimu katika kuhakikisha dola inakuwa na tija, lina tatizo na inabidi lirekebishwe sana maana kwa hali ilivyo sasa kuna hatari hiki ni chombo au kinaelekea kuwa ni chombo kisichokuwa cha maslahi yeyote kwa nchi, bali kwa maslahi ya vigogo wachache na marafiki zao wenye mitaji kutoka nje ya nchi. Kuna athari kadhaa lazima tuzing'amue kama watanzania ili tuweze kuja na mkakati hasa wakati wa kupiga kura. Tuna mfumo wa siasa wenye chama kimoja chenye maguvu mengi kutokana na kuwa na wabunge wengi. Madhara yake tunakuwa na demokrasia ya vyama vingi wenye bunge dhaifu na butu; ni Bunge lisilofanya kazi kama mhimili unaojitegemea bali linalowakilisha watawala.

Kwa maana nyingine demokrasia ya Tanzania ni ya aina yake na kipekee duniani kwa misingi kwamba tuna serikali ya awamu ya nne isiyozingatia mihimili mitatu: 'watawala, bunge na mahakama'. Tanzania ya leo, serikali inaendeshwa kwa mihimili miwili: watawala na mahakama. Bunge kupitia chama tawala limejikita katika kufanya kazi za watawala kwa kuisemea na kubariki (rubber stump) mijadala ya serikali badala ya kuihoji. Ni mfumo ambao ama unaambatana na shuruti kwa wabunge wa chama tawala au ni utashi wao kutenda watendavyo, mimi nashindwa kuelewa ila nionavyo tuna tatizo la mfumo wa kisiasa.

Nionavyo labda tunahitaji mfumo wa vyama vingi wenye chama tawala dhaifu, kwa maana kisicho na viti vingi sana ndani ya Bunge. Yaani, chama tawala ambacho kinaweza kushindwa kwa kura na wabunge wengine wa upinzani linapokuja suala lenye kuhitaji watu kufikiri kwelikweli kama la kupigia kura maamuzi kadhaa kama haya ya juzi ya kumuadabisha Zito Kabwe.
Ni kutokana na kuwa na bunge la chama kimoja chenye wabunge lukuki, bunge letu sasa limebakia kama "Sanaa za maonesho-majukwaani za kitaifa" (Nationa Theatre). Nathubutu kusema kama mtu amefuatilia kikao cha bunge hivi karibuni kwenye televisheni ni wazi tulikuwa mara kwa mara tunashuhudia sanaa za maonesho. Kwanini ninasema hivi?

Mosi, kwa mfumo wa demokrasia tulionao ni wazi wabunge wanajumuika katika makundi yao tofauti yaani kambi (CAUCUS). Kabla ya kujadili jambo bungeni, wabunge katika kambi zao wanakuwa wameshajadili ni vipi watajadili au hata kupigia kura hoja ili zipite au la. Kwa mantiki hii tunachoshuhudia pale Bungeni ni marudio ya kile kilichokwishajadiliwa ndani ya vikao vya kambi (caucus) za wabunge. Kwa maana nyingine kwa mfumo huu Bunge linakuwa chombo cha kisanii kwani ni sawa na kupoteza fedha za umma wa watanzania wengi masikini kuja kukaa na kujadili mambo ambayo yameshajadiliwa na kuamuliwa uamuzi ndani ya vikao maalum vya kambi ya chama tawala (caucus) na upinzani pia. Napata hisia wanachi tunaibiwa na wabunge kwani hakuna cha maana wanachofanya. Ingekuwa bora Spika akishirikiana na kila kiranja (Chief whip) wa kambi hizo mbili bungeni wawakilishe maamuzi, idadi ya kura za wabunge kama zilivyopigwa ndani ya kambi (caucus) zao badala ya watu wazima, wasomi waliobobea kwenda kupasha viti moto na kula fedha za walipa kodi wa nchi hii bila jasho.

Pili, ndio maana kwa mfumo huu wa kujali zaidi nidhamu ya chama na kupuuza maslahi ya kitaifa basi ni bora hata watoto wadogo wa chekechea, mangumbaru (wasio na elimu ya kiwango cha kutoa maamuzi ya msingi) waruhusiwe kuwa wabunge. Binafsi nadhani Bunge letu limefikia mahali nalifananisha na kusanyiko la watoto wa chekechea. Pamoja na ukweli kuwa serikali inaongozwa kwa kuzingatia ilani ya uchaguzi ya CCM, kinachogomba ni kwanini utekelezaji hauzingatii kanuni za msingi za uwajibikaji kwa wanachi na Taifa kwa ujumla? Hoja za wabunge wa chama tawala katika sakata la Zitto Kabwe zilionesha kabisa ilikuwa ni katika kutekeleza agizo la chama na si utashi wa dhati wa wazungumzaji. Na ndio maana wale wabunge makini wa CCM hawakuchangia hoja; inaonekana hawakuwa tayari kutuonesha ni kwa jinsi gani mfumo wa bunge ulivyoteka (hijack) akili zao.

Tatu, pamoja na spika kusisitiza kanuni mpya zinakuja karibuni, ni wazi huu si muarubaini kwani bila katiba mpya hatufiki mahali. Kuna haja ya watanzania tuwe na kongamano la kitaifa tujadili namna tunavyoweza kujiundia taratibu mpya za mustakabali wa Taifa letu bila kuzingatia sana hii mifumo ya kisiasa ya kimagharibi. Demokrasia ya magharibi kwa kiasi fulani nadhani ina matatizo kwa mazingira ya kiafrika hususan Tanzania. Nikiangalia jinsi bunge letu linavyoendeshwa na linavyotumiwa kufanya kazi za mhimili wa utawala (executive) badala ya wajibu wake halisi (legislative) nashindwa kumlaumu mbunge yeyote manake naamini kwa mfumo tulionao hata kama chama cha upinzani kinashika hatamu leo, sanaa za maonesho hazizuiliki. Nimejaribu kuitizama hii kasheshe ya hivi majuzi ya mheshimiwa Zitto Kabwe, binafsi, napata hisia kuwa mfumo wetu wa demokrasia ya vyama vingi wa kimagharibi labda pia ni tatizo.

Kuna mambo yanayoambatana na mfumo huu ambayo inabidi tuyafanyie mabadiliko katika sheria zetu. Kwa mfano, ukizingatia mfumo tulionao wa kibunge wa jumuiya ya madola: yaani unaruhusu chama chenye wabunge wengi kiamue kila kitu bila kujali hata nadhiri binafsi (conscience) ya wabunge. Yaani chama tawala kinakuja na hoja inayotetea maslahi ya chama na viongozi wake wala si Taifa. Na wabunge wa chama hicho wanaagizwa na kushinikizwa kwa mfumo wa nidhamu ya chama (party discipline) kuunga mkono jambo kama hilo hata kama nafsini mwao sivyo wanavyofikiri basi ni hatari sana. Yaani mfumo wa kisiasa tulionao unaruhusu taasisi nyeti kama Bunge kutumika kama chombo cha kuvunja Katiba; kwani, ibara ya kumi na nane (18) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa haki ya uhuru wa mawazo katika vipengele vyake vinne: a, b, c na d. Bunge letu haliheshimu vipengele viwili hapa:

Kwa mfano, kifungu (a) kinazungumzia: 'uhuru wa mtu kuwa na maoni na kueleza fikra zake', lakini Bungeni kwetu mfumo unaruhusu maamuzi ya wabunge katika kambi (caucus) zao hata kama yana upofu basi lazima yapitishwe bila kuhojiwa kwa uchambuzi makini. Kinyume cha hapo mbunge ataadhibiwa na kamati ya nidhamu ya chama husika pindi akijaribu kuhoji au kuonesha kutoridhishwa na jambo husika. Mfumo huu ndio tunaotakiwa tuondokane nao, la sivyo kama tutaiga kila kitu kutoka demokrasia ya nchi za magharibi basi nchi yetu haitatoka katika lindi hili la wabunge waliotekwa fikra. Na hii haijali tunatawaliwa na CCM au chama kingine chochote.

Kifungu cha (d) kinazungumzia: 'haki ya mtu kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii'. Tukizingatia mjadala wa Zitto Kabwe juu ya kuundwa kwa kamati ya uchunguzi ya Bunge napata hisia mheshimiwa alikuwa akiegemea haki ya kikatiba ambayo imeainishwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Yaani waziri anaweza kusaini mkataba bila kutaarifu Bunge kama taasisi ya uwakilishi wa wananchi. Hili ni suala muhimu kwa jamii kwa hivyo kama lina utata ni vyema uchunguzi ungefanywa. Ila mfumo wetu una mwanya wa kuruhusu katiba ivunjwe kutokana tu na "uwingi wa wabunge wa chama tawala" ambao inawalazimu wafuate agizo la chama kupitia kambi (caucus).

Wabunge wa chama tawala wanajinyima haki ya kupewa taarifa juu ya suala muhimu la jamii kwa kuunga mkono hakuna haja ya uchunguzi wa madai ya mheshimiwa Zitto. Hii ni sababu ya mfumo wa siasa tulionao unawalazimisha wabunge wenye akili timamu wasizitumie pale inapobidi. Sitaki niwalaumu wabunge wa chama tawala manake naona mfumo wa kisiasa unatoa mwanya na kuwalazimisha wasihoji na waunge mkono maamuzi ya chama ambayo si yakinifu. Na usipohoji unaadhibiwa na chama chako.


Hapa inamaanisha wabunge wengi wa chama tawala kwa ishu kama ile ya Karamagi na Zitto naamini si wote walikuwa na msimamo waliouchukua kuunga mkono adhabu iliyotolewa. Ila naamini tayari kulikuwa na agizo ndani ya kambi ya chama tawala kuamua vile. Ni wazi wabunge wetu wametekwa kiakili, yaani chama cha Mapinduzi kinawasaidia kufikiri na kuamua mambo kadhaa yenye maslahi kwa umma na kuwafanya wayaamue kwa kufuata maelekezo ya watawala. Na hapa maamuzi yanakuwa si kwa ajili ya umma bali dhidi ya wachache, yaani wanasiasa mafia fulani ambao ni wateule wanaostahili kufaidi keki ya nchi hii.

Ndio maana mwanataaluma mmoja hivi karibuni katika gazeti la 'The Citizen' tarehe 22 August 25, 2007, kanena kuwa yaliyomkuta Zitto ni Bunge kutenda kosa la "Crime against Logic", yaani "Kosa/hatia dhidi ya Kufikiri sahihi". Pamoja na lawama zinazoelekezwa kwa wengi wa vigogo hasa kule bungeni kama Spika na wabunge kadhaa na hata mheshimiwa Karamagi, nadhani maoni yangu tukae chini kama Taifa tuunde demokrasia ya kitanzania, yenye kuzingatia maslahi ya nchi ambayo itakuwa na Bunge lisiloruhusu mwanya wowote wa mbunge kufungwa mdomo hata kama anatoka kwenye chama kinachotawala. Ikibidi tusiwe na mawaziri ambao ni wabunge au hata wakuu wa mikoa ambao ni wabunge. Mianya inayoingilia uhuru wa mbunge wa kufikiri inatokana na mfumo wa kibunge unaowapa wabunge wengi (majority) bungeni kutuamulia mambo kama watoto wa chekechea.

Tukiachia mfumo tulionao wa kibunge wa Jumuiya ya Madola uendelee basi hata kama siku za usoni kitashinda kwa kishindo chama kingine zaidi ya CCM, bado kitatumia mianya iliyopo sasa kupitisha na kujadili maamuzi katika hali ya kitoto kama tunavyoshuhudia sasa. Wanasiasa wetu waanzie kwenye vyama vyao kuweka taratibu za uwazi na uhuru wa viongozi na wabunge wanaowakilisha vyama wawe huru kuzungumzia hata mambo yanayogusa maslahi ya vyama vyao na kukinzana na maslahi ya Taifa bila kubanwa na kamati za nidhamu za vyama vyao. Tusipoacha mfumo wa kuadabishana ndani ya vyama vyetu, hata Bungeni hatutaruhusu wabunge wetu wazungumze kwa uwazi. Na ndio kinachotokea kwa sasa.

Na ndio tatizo lililotufikisha hapa tulipo leo ambapo Bunge la bajeti lililokwisha majuzi lilikuwa sawa na 'Sanaa ya Maigizo', mahali ambapo wabunge kwa ujumla wao na kwa makusudi kabisa hawajali maslahi ya nchi ila tu kujali fedha na posho, huu ni ulafi wa hali ya juu (collective greed of the highest degree) kuunga mkono na kupitisha maamuzi kadhaa yasiyozingatia maslahi ya nchi yetu na wananchi kwa ujumla wao. Inanikumbusha mwanafalsafa wa kifaransa, Jean-Francois Bayart anavyoiona hali kama hii kama siasa za tumboni (politics of the belly) akihusisha na mkakati wa wanasiasa kujitajirisha pamoja na kuimarisha utamaduni wa kung'ang'ania madarakani tu. Ni kama vile kwao wanaangalia maslahi yao na chama chao tu; wananchi na nchi kwa ujumla si hoja. Nionavyo hii inasababishwa na mfumo holela wa kiunyanyasaji (irregular coercive mechanism) tulionao ambao tunafikiri ndio demokrasia makini kumbe ni mfumo wa vyama vingi wa hali ya chini sana (primitive multipartism)

Nahitimisha kama nilivyoanza makala hii juu ya kukubali kukosolewa hata kama kunauma kiasi gani lazima kukubaliwe kama changamoto. Kukichukuliwa ni kama kudhalilisha utawala ama ni kudanganya basi ujue maendeleo ya jamii husika hayatafikiwa. Ni wakati tubadili mfumo wetu wa kisiasa ili uendane na wakati na mahitaji ya wote na si wachache tu kwa kuondoa mianya yote inayotulazimu tufikiri kama watoto katika maamuzi ya kimsingi ya nchi yetu na kutuadabisha pindi tunapojaribu kufikiri kwa umakini.

Tukibadili mfumo wetu wa kisiasa tutaweza kuondoa ile nguvu ya chama tawala kuwa na nguvu ya kudhibiti Bunge kama ilivyo sasa hata kama kuna wingi wa wabunge. Hii ni lazima ianzie kwenye vyama vya siasa; manake leo ni CCM kesho ikiwa DP au Chadema kwa mfumo huu wa kibunge wa jumuiya ya Madola sitashangaa kumwona mtu kama Zitto au Mtikila akifanya kwa mbwembwe ndani ya Bunge haya haya yaliyokuwa yakifanywa na wabunge wa chama tawala bila aibu.

Kama tunadhani tuna mfumo bora wa kidemokrasia barani Afrika, ni wakati wa kutafakari; la sivyo tutakuwa tunatupiana lawama bila sababu za msingi kwani mfumo wa kisiasa unaruhusu taasisi ya Bunge kuonekana kama tamthiliya kwa yeyote mwenye uchungu na nchi yetu. Na tujiulize: Ili ile kanuni ya fizikia izingatiwe bila kukwepeka, je wabunge wenye kutoa hoja zinazofanana na watoto wa chekechea, je ni nani wa kulaumiwa, wabunge hasa wa chama tawala au ni mfumo mzima wa kisiasa?

Wednesday, August 15, 2007

VITA YA MAFUTA CONGO DRC--UGANDA?

Unajua vita ya mafuta inakaribia kuanza kati ya Uganda na Kongo-DRC?Je Uganda itaweza kupigana vita nyingine na huku pia ikipimwa kama ni dola iliyofeli?(failed state)
Kama ni kweli mafuta ni chanzo cha ugomvi na Kongo, je ni nini nafasi ya Uganda katika biashara ya mafuta barani Afrika.
Ni lazima watu tutambue kuwa Ituri ni eneo lenye utajiri wenye balaa sana kwani ni chanzo cha mgogoro wa sasa kati ya nchi hizi mbili.

Saturday, August 11, 2007

SHIRIKISHO LA AFRICA MASHARIKI-- SI HATUA MUAFAKA

Leo nigusie tena juu ya hii jumuiya yetu ya Africa Mashariki (EAC) ambayo watanzania wengi wameikataa kwa kutoa maoni yao kwa tume ya Profesa Wangwe. Nianze kwa kuwafananisha wote wenye ndoto ya kuundwa ama kuharakisha (Fast Tracking) uundaji wa Shirikisho la Africa Mashariki (EAF) hawana tofauti na wapigania haki wa uhuru watanguliziwa bara la Afrika ambao ndoto yao ya Shirikisho la Afrika mpaka leo ni kiinimacho.

Baadhi ya wanaofuatilia mtizamo wangu ni wazi nimekuwa napinga Shirikisho la Afrika Mashariki ila nikiunganga mkono hatua ya Jumuiya tu kwani naamini Shirikisho la Afrika Mashariki itakuwa ni hatua ya kisiasa isiyokuwa na manufaa yeyote kwa mwanachi wa kawaida.

Mmoja wa watu wanaotaka Shirikisho la Afrika Mashariki liharakishwe ni Yoweri Kaguta Museveni--Rais wa Uganda. Aliweza hata kubadili katiba ya Uganda kwa kuwahonga wabunge Shilingi Millioni Tano za Uganda (chini ya shilingi milioni tano za Tanzania) kila mmoja ili tu wapitishe mabadiliko ya kuondoa "ukomo" wa vipindi viwili vya miaka mitano mitano cha mtu kuwa rais wa nchi. Lengo inasemekana na wachunguzi wengi wa siasa za Uganda likiwa ni ili aendelee kuwa madarakani hadi pale mchakato mzima wa Shirikisho utakapowadia ambapo ataweza kuwa Rais wa kwanza wa Shirikisho la Afrika Mashariki ifikapo 2013.

Museveni anaamini Shirikisho ndio njia pekee iliyobakia kutuletea umoja Afrika Mashariki; anafikiri ni rahisi namna hiyo; mwenyewa kwa miaka ishirini na ushehe sasa ameshindwa kuinganisha Uganda sijui Afrika Mashariki itawezekanaje. Hapa pananipa utata sana manake viongozi (wanasiasa) wetu kuna nyakati wanafanya mambo kikondoo sana. Hebu nivute hisia nikumbushe historia ya bara letu la Afrika, ambapo ndoto za waanzilishi wake za kuunda Shirikisho la Kisiasa mpaka leo zimebakia katika vitabu vya historia tu kwa visababu ambavyo hapa kwetu Afrika Mashariki navyo vipo pia.

Moja, mwaka 1958, Osagyefo Kwame Nkrumah alifanya juhudi sana kuinganisha Afrika kwa kuanzia na Ghana na Guinea, ikafuatiwa na Ghana-Guinea-Mali ambazo zote hazikudumu. Pili, kukaja Shirikisho la Senegambia kati ya mwaka 1981 na 1989. Zote hizi hazikudumu sana wala kuweza kusimama; kwa ujumla mashirikisho ya kisiasa yaliyojaribiwa katika karne iliyopita hayakufanikiwa pia si tu Afrika bali hata sehemu nyingine za ulimwengu na mifano ipo mingi: kwa mfano, Shirikisho la India Magharibi (West Indies Federation) kati ya mwaka 1952 hadi 1962.

Nyingine ikawa ni Shirikisho la Kijamaa la Mataifa ya Kiarabu (Federation of Socialist Arab States) kati ya mwaka 1972 hadi 1977 ambapo msisitizo ulikuwa wa kizalendo yaani Pan Arabinism; alafu likawepo lile shirikisho la Yugoslavia kati ya mwaka 1945 hadi 1992; na mfano wa mwisho kabisa ni lile shirikisho kubwa kubwa kabisa la kisiasa wakati wa vita baridi la Urusi ( Union of Socialist States of Russia) la mwaka 1922 hadi 1991.

Unaweza kuona mashirikisho niliyoyataja hapo juu yalianza na kufa kwa sababu mbalimbali ambazo pia zipo hapa Afrika Mashariki. Lakini pia mtu anaweza kujiuliza mbona yapo mashirikisho ya kisiasa ambayo bado wamo na yanaendelea? kwa mfano, Shirikisho la Nigeria lenye watu takriban millioni mia moja na kumi (110) au lile la Ethiopia lenye wakazi takriban milioni sabini na nane (78). Kama kweli Mashirikisho haya mawili ya kiafrika yana tija hasa kwa wananchi wa kawaida ni kwanini basi nchi zote hizi mbili bado ziko katika kundi la nchi zinazoendelea na si nchi zilizoendelea?

Hii ni sababu inayonifanya mimi kutokuunga mkono wazo la Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki. Nikihakikishiwa ni dawa ya kutuondoa kutoka katika nchi zinazoendelea, au zile masikini sana ulimwenguni (LDCs) basi nitaunga mkono; ila kwa hali ya sasa nafikiri shirikisho halina maslahi makini ukiacha matakwa binafsi ya wachache.

Nimejaribu kutizama pia lile shirikisho ambalo nadhani ni mfano wa mafanikio ulimwenguni, nalo ni ule Muungano wa Mataifa ya Amerika ( United States of America) ambalo kisiasa ni mfano wa kuigwa kimafanikio. Je hiki ni kielelezo cha Shirikisho la Afrika Mashariki kufikiwa? Mimi sioni kama ni kweli kabisa: nikumbushe kihistoria ilihitajika takriban miaka mia moja (100)--1776 hadi 1865 pamoja na vita kali na kubwa ya kiraia ya mwaka 1861 hadi 1865 ndipo Marekani ikakomaa na kuweza hata kustawi kama taifa lenye nguvu kabisa ulimwenguni.

Ni wazi kuundwa kwa Shirikisho sio mchakato wa kuharakishwa kama akina Museveni, Kibaki na Kikwete wanavyotaka. Kuna mambo mengi ya kuzingatia hasa ukiangalia EAC ni jumuiya yenye nchi zenye historia ya kupiganapigana katika kila jambo la kisiasa.

Labda nisisitize kuwa si Marekani tu ambapo mambo hayakuwa rahisi kama vile maraisi wetu wanavyotaka tuharakishe kufikia Shirikisho. Niwapeleke katika jumuiya ya Ulaya--(European Union). Kuanzia juhudi za mwanzo kabisa pale uliposainiwa mkataba wa Roma- 1957, kuanzisha Jumuiya ambayo mpaka leo mchakato wa kuunda Shirikisho la Kisiasa umebaki kiini macho. Mwaka juzi tu wanachi wa Ufaransa na Uholanzi walikataa kuunga mkono Katiba mpya ya Jumuiya ya Ulaya kwenye kura ya maoni, ambapo lilikuwa ni pigo katika kukwamisha mchakato mzima wa kufikia Shirikisho la Kisiasa. Tunaweza kuona ni miaka zaidi ya hamsini sasa Ulaya inashindwa kuunda Shirikisho la Kisiasa.

Mambo yote haya niliyoyataja yananifanya niamini kuwa muungano ya kiuchumi ni hatua muafaka ambayo itatufaidisha kiuchumi baada ya kipindi fulani. Nionavyo, Shirikisho la Kisiasa halitaweza kwa jinsi yeyote kuleta faida yeyote kwa mwananchi wa kawaida zaidi ya kuwafaidisha wanasiasa wetu. Wanasiasa wetu waache mawazo eti ile kuwa tu na idadi kubwa ya watu basi utakuwa na soko kubwa ambayo ni kielelezo cha nguvu za kiuchumi. Kwa Jumuiya yetu kweli soko litakuwa kubwa ila ni dhaifu sana kiuchumi; ni soko la wateja wengi ila ni masikini sana na ndio hapa nadhani zifanyike juhudi kuendeleza wananchi kielimu na kiuchumi hasa kiujasiriamali (entreprenuership) ndipo tutegemee soko lenye tija. Kinyume chake, hii "uharakishaji" ni usanii mwingine wa watawala kama walivyowahi kujaribu hapo nyuma na kutofanikiwa.

Mwisho ni vyema tuangalie historia ya mashirikisho ya kisiasa katika sehemu kadhaa za dunia ili tuweze kung'amu tufanye nini katika juhudi zetu za kujumuika kimataifa; lisiwe suala la kuharakisha bila kujiuliza je ni kwa maslahi ya nani? Je watawala wanawaza juu ya mwananchi wa kawaida katika jumuiya? Mimi nashangazwa sana na hili zoezi la kukusanya maoni juu ya Shirikisho kufanyika wakati tayari wameshatia saini kuruhusu "kuharakisha mchakato" mzima wa kuunda Shirikisho. Zoezi zima la kukusanya maoni naamini ilikuwa ni ufujaji wa fedha kwani viongozi wetu walishaamua jambo walilotaka kutuuliza; sasa sijue kwanini wanakusanya maoni kwa kitu walichokwisha kitolea maamuzi. Ama kweli tusipokuwa makini tutaburuzwa bila kutafakari.

Namaliza nikisema: "Shirikisho si hatua muafaka"; ila Jumuiya inahitajika kwa sasa yaani mambo ya sarafu moja, umoja wa forodha ni mambo ya msingi yatakayotusaidia kuendeleza wananchi wetu kwa miongo kadhaa labda na ndipo tufikiri Shirikisho tutakapokomaa vya kutosha.

UMOJA WA AFRIKA--USA NI NDOTO NYINGINE ZA ALINACHA

Mwaka 1963, tarehe 25, mwezi Mei, Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ulianzishwa rasmi chini ya hekima za muasisi mkuu Asagyefo Kwame Nkrumah. Lengo lake lilikuwa ni kulifanya bara la Afrika kama nchi moja kubwa ambayo aliamini itakuwa na nguvu ulimwenguni dhidi ya hujuma zozote za mabeberu. Julius Kambarage Nyerere, 'mchonga meno' alimpinga vilivyoo kwa hoja yake ya miungano ya kimkoa (regional blocks).

Leo hii, karibu miongo mitano, bado tuko palepale hatujaweza kuamua tufuate hoja ya Asgyefo au Julius. Mwaka 2002, October 15, ikiwa ni miaka 38 ya OAU, viongozi wetu walikutana Durban, Afrika Kusini na kuunda Umoja wa Afrika (AU) mbadala wa OAU. Ilikuwa ni hatua moja mbele kuongeza nguvu za kisiasa na kiuchumi kama hatua moja kuelekea muungano kamili. Mapema mwezi Julai, viongozi wetu wamekutana Accra-Ghana ili sasa waunde Shirikisho la Afrika. Raisi wa Libya akawa kinara na kuivalia njuga hoja ya Nkrumah kuunda Shirikisho la kisiasa (USA).

Mkutano wa maraisi wa Afrika kule Accra unezua tofauti na hali ya sintofahamu sana baina ya viongozi wetu. Kwa mfano, raisi Muammar Ghadafi alikazia sana kuwa shirikisho liharakishwe; yaani, kuanzishwa kwa wizara ya mambo ya nje na ulinzi ifikapo January 2008. Hali hii haikuwapendeza viongoz wengine wengi: Moja, raisi Umaru Yar'Adua alipinga hali ya kuharakisha na akaungana na Nyerere kwenye hoja ya "Mashirikiano ya Kimkoa"(regional blocks).

Mwishoni mwa mkutano ule, ni wazi ilijionesha wazi kuwa Umoja wa Afrika (AU) tulionao umefeli kabisa. Raisi wa kamisheni ya AU, Alpha Oumar Konare wa Mali alikiri kuwa ni chombo kisichokuwa na nguvu kabisa. Alisema lengo ni kufikia shirikisho ila 'mpango barabara' (road map) ya kufikia hapo ni kuwa tumechanganyikiwa na hatujui tufanye nini.

Je tumuenzi Julius Nyerere au Kwame Nkrumah? Hadi sasa wazo la Nyerere linaungwa mkono na wengi wa viongozi waliokutana kule Ghana.

YAWEZEKANA RAISI KIKWETE NI MWOGA!


Kama sijakosea Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwoga katika kuwachukulia hatua watendaji kadhaa pale panapotokea tuhuma zenye kustahili mtu kuadhibiwa. Hii kusema bei ya mafuta kushindwa kudhibitiwa na serikali ni udhaifu wa Ewura kunanitia wasiwasi sana, kwani raisi anajaribu kutupa mpira. Ninahisi wauza mafuta ni kundi linaloendesha mambo kimafia mafia hivi na lina uswahiba na baadhi ya vigogo wenye nguvu (untouchables).

Serikali inaogopa kuwagusa na inarusha mpira kwa Ewura iwashughulikie situ ambacho nadhani Ewura hawataweza. Kuna uwezekano serikali yetu imeshanunuliwa na hawa mafia wa mafuta ndio maana wanaogopwa na wanajipangia bei watakavyo. Kama sivyo, basi serikali ijaribu kufanya yale iliyofanyiwa Shirika la ndege la Uingereza wiki hii kwa kupigwa faini dhidi ya kupanga bei ghali kuwanyanyasa wasafiri. Nitaeleza juu ya muono wangu huu wa labda raisi wetu ni mwoga mwishoni mwa waraka wangu wa leo; ila kwanza nigusie hisia zangu kadhaa pale nilipobahatika kumuuliza Raisi Kikwete maswali mawili wakati akihojiwa na shirika la utangazaji la VOA la Marekani hivi majuzi.

Kwa miaka sita sasa nimekuwa mfuatiliaji wa kipindi cha mahojiano cha redio na televisheni "Straight Talk Africa" kinachorushwa na shirika la utangazaji la Sauti ya America (VOA) na kuendeshwa na mtangazaji Shaka Sally. Hivi karibuni pia nimekuwa pia mshiriki na nimepata nafasi kutoa ama kuuliza maswali juu ya mada zilizokuwa zikijadiliwa. Wiki hii, yaani tarehe 1/8/2007, Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa ndiye mgeni akihojiwa kutoka Dodoma. Washiriki tulitakiwa tutume maswali mapema kwa barua pepe. Nilifanya hivyo ili nipate nafasi ya kipekee kumuuliza Raisi swali juu ya mustakabali wa nchi yetu. Na kwa bahati nzuri kabisa, maswali mawili ya kwanza yalitoka kwangu; yalihusu wasiwasi wangu juu ya mchango wa sekta ya madini kwa uchumi wetu. Mheshimiwa Raisi alinijibu na nikaridhika hasa swali la kwanza ila sehemu ya pili kidogo kutokana na uhariri uliofanywa na Shaka Sally, sikuridhika na jibu la mheshimiwa Raisi.

Swali langu la kwanza nilitaka mheshimiwa Raisi lilikuwa ni kwa vipi ametimiza ahadi yake ya kuipitia upya mikataba ya madini iliyosainiwa na serikali iliyopita ili sasa ituletee tija? Raisi alijibu vyema kwa maoni yangu na napenda nimshukuru sana kwani alieleza makubaliano kati ya serikali na makampuni mawili: Barrick Gold na Resolute Mines, kuwa sasa yanalipa kwa takriban asilimia 33% ya kodi ikijumuisha pia na mrabaha.Na akasema kuwa kiwango cha dunia au kimataifa ndio hicho kinachotumika katika nchi nyingine. Raisi aliahidi kuwa kuanzia sasa mchango wa makampuni ya madini itakuwa asilimia 33% na si tena yale mambo ya 3%.

Swali langu la pili ambalo mheshimiwa Raisi Kikwete hakuniridhisha kwa majibu na ningependa kama inawezekana atoe ufafanuzi zaidi pindi akipata wasaa niliuliza: Je ni kweli Tanzania hatuna uwezo wa ndani wa kuweza kuzalisha madini hadi hatua ya mwisho na badala yake tunauza nje madini katika hatua ya malighafi?

Raisi alijibu kuwa hatuna nibu la ndani kwa hili na imetubidi tutegemee mitaji ya nje ya kimataifa kama hali halisi inavyodhihiri. Binafsi, nilitegemea ajibu hivyo kwani si mara ya kwanza kusikia viongozi wetu wakisema hivyo. Jibu hili linanisumbua sana na litaendelea kuniuma roho labda mpaka atakapotokea mtu anipe maelezo fulani ambayo sidhani kama huwa yanazingatiwa tunaposema eti nchi ya miaka arobaini na zaidi ya uhuru haina uwezo wa kuuza rasilimali zake katika thamani stahili kupata faida halisi. Je ni kwanini nasema hivi?

Ili nimtendee haki Raisi Kikwete, labda nioneshe swali langu ambalo Shaka Sally alilihariri lilikuwa hivi: Je ni kweli Tanzania hatuna uwezo wa teknolojia au kitaaluma kutengeneza madini ya nchi yetu hadi hatua ya mwisho? Kama ni kweli, ni nini maana ya kuwa na idara ya Geolojia kwa mfano pale Chuo Kikuu cha Dar es salaam? Ina maana kwa miaka yote ya uwepo wa idara hii imekua ikifanya nini kama imeshindwa kutupatia wataalam katika sekta ya madini?

Manake kwa hoja ya kutegemea mitaji kutoka nje, inamaanisha chuo chetu kimeweza tu kutuzalishia wataalamu wa kusaini mikataba bila kuzingatia maslahi ya nchi, hii ni hatari kwa elimu yetu kwani haikidhi haja ya kuzalisha wasomi wazalendo, kweli tumekwisha. Nimpongeze mheshimiwa Raisi alishang'amua hili alipokuwa ziarani kule nchi za Nordic.

Nikiacha maswali ambayo niliyazua binafsi, niseme tu mahojiano ya Raisi yalikuwa mazuri sana na ya uwazi wa dhati. Kwa mfano, Raisi Kikwete akijibu swali la Juma Iddi, juu ya "Kupaa kwa Uchumi Wetu", Raisi aliweka wazi kuwa kwa sasa tuko kwenye mchakato tu na kusema Uchumi unapaa ni mapema sana. Alitumia kauli: "We are yet to see the trickle down". Hapa Raisi Kikwete aliifunga ile hoja ya majibizano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na waandishi kadhaa katika gazeti hili la Tanzania Daima.

Raisi aliulizwa na Shaka Sally juu ya Visheni yake kwa Taifa: Alisema lengo lake kuu ni kuona Tanzania inaondoka kutoka kundi la nchi masikini kabisa (Least Developed Countries) hadi kuwa kati ya nchi za pato la kati (Middle Income) mara moja ifikapo 2010. Hapa mkazo ataweka kwenye Kilimo na Miundo Mbinu. Na ndio hapa Raisi Kikwete alipoungana na akina Padri Kitambo, Mwanakijiji na Malera kuwa kusema 'uchumi unapaa si kweli kabisa'. Kwa visheni ya Raisi Kikwete, tutegemee ndege itaanza kuwasha injini zake ifikapo 2010; kwa sasa iko gereji ikishughulikiwa.

Shaka Sally alitaka kujua kuwa tangu Raisi Kikwete awe raisi ni jambo gani au uamuzi gani mkubwa na muhimu anaweza kujivunia kati ya mengi aliyokwishafanya? Alisema ni upanuzi wa elimu ya sekondari ambapo asilimia 96% ya wanafunzi wameandikishwa shuleni. Ila alikiri kiwango cha elimu kinachotolewa hakina viwango madhubuti. Na alikiri ni changamoto iliyobakia kuboresha ubora (quality) akitumia neno 'tall order'. Hapa raisi Kikwete alinikuna kwa kuwa mkweli kwani ni kweli kabisa kunahitajika kazi ya ziada; yaani walimu bora na zana bora.

Jambo lingine Raisi Kikwete aliulizwa: je ni nini kinaichoisumbua sana roho yake tangu awe Raisi katika majukumu yake? Jibu la Raisi lilinipa hisia mchanganyiko; kwani raisi alisema kuwa pale anapomuondoa mtu kutoka kwenye madaraka yake amegundua imekuwa ikiambatana na habari za uzushi zaidi na si ukweli. Kwa maana nyingine majungu ni mengi sana anayofikishiwa Raisi wetu. Na ndio maana amesisitiza katika kikao cha NEC kilichomalizika hivi karibuni kuwa tuhuma zozote dhidi ya watendaji ziambatane na ushahidi.

Hapa napata hisia raisi wetu labda hajui kwa nafasi aliyopo majungu lazima yawepo mengi sana; ila kwa kiongozi ni lazima mtu ujifunze kuamini hisia zako pale unapopata jambo na kulitafakari. Kwenye mambo ya utawala kuna kitu kinaitwa "INTUITION" yaani hali ya kung'amua jambo lisilohitaji kufikiri sana na kiongozi unachukua hatua stahili.

Raisi amenishtua kidogo labda hana karama za kiuongozi za kutosha. Kwani kama ni kweli anaumia roho kwa kugundua baadhi ya mabadiliko ya viongozi aliyofanya hayakustahili kwa ajili ya majungu; basi inamaana kuwa hii kuongezeka kashfa kila kukicha na Raisi anakaa kimya labda pia anaumia roho?

Nitoe mifano michache ambapo kashfa zisizohitaji hata mtu kufikiri na kuchukua hatua dhidi ya wahusika: hivi waliosaini Richmond, Kashfa ya Minara ya BOT au hii ya hivi majuzi mtu kwenda kusaini mkataba na kampuni ya madini huko ughaibuni kinyume na taratibu tulizojiwekea ni mambo ya majungu kweli? Raisi Kikwete acha woga, usiumwe roho; chukua hatua, bila maamuzi magumu hasa kutoka kwako nchi hii haitajengwa wala kwenda mbele.

Visheni yako haitafikiwa hata kidogo ukiumia roho kwa kupima majungu, wajibisha watu kwa ujasiri. Angalia hisia za wananchi juu ya kashfa mbalimbali alafu chukua maamuzi kuwaadhibu waliokuzunguka ambao wanakosa kila kukicha wakijua hawafanywi kitu. Woga wako utalifikisha Taifa hili katika siasa za kiushirika vikundi (patronage au cronyism) kama utajaribu kupima uzito wa majungu yanayoambatana na kashfa kadhaa. Si ulishasema huna ubia na mtu; sasa ukiumia roho dhidi ya maamuzi yako hii itapalilia "ubia".

Mwisho, nitoe hongera kwa mheshimiwa Raisi kwa mahojiano yale na VOA; Mungu Ibariki Tanzania iwe na viongozi majasiri wasio waoga na wenye kutenda badala ya kutoa sababu kwa kila jambo lililo ndani ya uwezo wao.