My Blog List

Wednesday, February 27, 2008

ZIARA YA BUSH—NA UFISADI WA FIKRA ZETU

Mwezi wa februari utabakia wa kukumbukwa kwangu binafsi kwa matukio kadhaa ya kukumbukwa. Kwanza, tarehe ya pili tu nilimpoteza bibi yangu, Emilia aliyefariki akiwa na umri wa miaka tisini na sita (96). Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Tarehe saba wakati nikiwa nimesimama pembeni ya jeneza la bibi siku ya mazishi, ndugu yangu mmoja ananiuma sikio kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa amejiuzulu.

Ukiacha hayo mawili, lingine ambalo kwangu naliona la kukumbuka ni ziara ya Rais George Bush nchini Tanzania. Imenishangaza sana huyu bwana kapata mapokezi makubwa sana barani Afrika kitu ambacho ni tofauti katika mabara mengine ambapo anachukiwa sana. Kwangu nadhani ina mafunzo mengi sana kwetu kama wananchi na hasa kwa viongozi wetu. Labda niseme pia siungi mkono hata kidogo kelele na pingamizi nyingi ambazo zilioneshwa na baadhi ya watanzania—waislamu wachache na jumuiya ya wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Nasema hivi kwani siamini kabisa kuwa rais Bush anazo sera zake binafsi ila kila kinachofanywa na serikali ya Bush ni matokeo ya sera ya nje ya serikali ya Marekani ikihanikizwa na imani za kihafidhina za Chama cha Republican.

Tatu, sijui kama Magaidi wasingeivamia Marekani September kumi na moja kama kweli leo majeshi ya Marekani yangekuwa Iraq na Afghanistan. Lakini pia sijui kama kweli kuna njia gani ya mazungumzo ingetumika kuleta mabadiliko ya kiutawala ya kidhalimu chini ya Matalebani ama Saddam Hussein. Si kura hata kidogo ingeumaliza udikteta wa Saddam ila kujitoa mhanga wa maisha ya watu—yaani damu kumwagika ili kuleta mabadiliko kutoka mfumo dhalimu. Kama hatutaki kuamini hivyo, basi tuangalie Kenya kama itatulia iwapo Kibaki atakuwa rais kwa miaka mitano ijayo. Kuna nyakati vita haiepukiki ili kuleta mabadiliko kwani hata nchi yetu ilibidi ipigane vita kumng’oa Iddi Amin ili kuung’oa udikteta wa Amin Uganda.

Kwa kuzingatia mwelekeo wa uchumi wa kileo duniani, na hata kihistoria, Taifa kubwa limejiimarisha kwa njia nyingi mojawapo ikiwa ni vita. Hivyo basi, Bush si wa kwanza kuendesha vita. Hata Nyerere aliendesha vita kwa maslahi ya nchi yake (Tanzania) kitu ambacho anafanya Bush. Hivyo basi, kumkataa Bush asitembelee nchi yetu si hoja yenye mashiko sana kiuhalisia leo hii; kwani kama asingekuja na hata alivyokuja, hakuna kitu amepoteza. Nguvu ya kujieneza ya Taifa kubwa kama Marekani haizuiliki; hivyo basi kimtizamo kelele za pale Mlimani zilikuwa zimejaa mantiki ya kitaaluma ambayo kwangu sina hoja kupinga uhalali wake kimaadili na katika suala zima la uadilifu unaotakikana kwa mwanadamu.

Lakini katika hali halisi ya dunia si hoja muafaka manake inaonekana maisha ya mwanadamu na mtanzania wa leo yamejaa matendo mengi ambayo si ya kimaadili lakini ndiyo yamefanywa haswa kama utamaduni. Hata Raisi Kikwete alimwambia Bush kuwa kwetu watanzania hatuana shida nae japo zipo serikali nyingine ambazo zina mitizamo tofauti na sera zake.

Kwa maana nyingine mtanzania anaongozwa na mbinu nyingi za kifisadi kufikia malengo yake; na ndio maana ziara ya Bush ilikuwa ya mapokezi mazuri sana sidhani kama amewahi kufanyiwa hivyo ugenini hata siku moja. Tanzania ni Taifa linalojiendesha kifisadi fisadi sana na ndio maana ni wananchi wachache sana waliokuwa na muda wa kutafakari hoja za wasomi wetu kule Mlimani. Watanzania na serikali yao hawajali jambo fulani linapatikana kwa njia gani ilimradi tu lina tija katika kutatua matatizo yao. Ni nchi ambayo kama kweli una elimu yako nzuri na ya juu kama vile Dr. Msabaha alivyofanya kwenye skandali ya Richmond, lazima uachane na kile unachokiamini ndio sahihi na ufuate matakwa ya utawala. Labda nieleze ni kwanini watanzania na serikali yao hawakuona haja ya kusikiliza busara za kisomi:

Moja, ziara hii imetoa msaada mkubwa kwa nchi yetu katika sekta ya afya na miundombinu. Japo nina mashaka na mafisadi hawataziacha salama, ila ni kielelezo kuwa Bush ana nia njema na nchi yetu. Na katika kutia shime vita dhidi ya ufisadi, Bush alisema baada ya kusaini mkataba kuwa fedha za Marekani si kwa mafisadi. Na kusisitiza kuwa moja ya masharti ya Mfuko wa Millenia ni serikali yetu kuzingatia “Utawala Bora”, vita dhidi ya ufisadi na kwa ujumla serikali inayojali watu wake.

Pili, ziara hii imeonesha ni jinsi gani Raisi Bush na mkewe walivyo watu wa kujitolea (compassionate)hata huruma ya kujali watu wa kawaida. Kwa viongozi wetu wamejifunza ni jinsi gani wanapaswa kuishi na kujichanganya na watu hohehahe kama walivyo watanzania wengi. Viongozi wetu wengi wa Afrika, kwa mfano, si rahisi mtu atembelee hospitali na umwone akikumbatiana na kukaa karibu kabisa kwa kujichanganya na wagonjwa. Hili Bush katoa funzo; nilitegemea kule hospitali ya Mount Meru nione makachero wakiwa karibu na Raisi wakimwongoza wapi apite na ashikane na nani mkono au hata kuwazuia watu wasimkaribie bwana mkubwa. Hili sikuliona ila niliona Raisi Bush akijiweka sawa na binadamu wengine na kukaa hata karibu nao kabisa, wala si kwenye kiti maalum bali viti vya kawaida wanavyokalia wagonjwa kwenye foleni. Wakubwa wetu watataka sofa maalum tofauti na walalahoi.

Kimavazi pia imekuwa ni funzo kwa viongozi na vigogo wetu. Unakwenda kuwatembelea watu masikini ni lazima angalau ufanane nao. Kwa Bush hili alilizingatia hasa na wala sikuona akiwa ndani ya suti, siku ile yenye joto ambalo lingemfanya achemke kwa joto na aogope kujichanganya. Nadhani ndio maana kulikuwa hamna haja ya wanausalama kumzuia kuwa karibu na watu kwani vigogo wetu inabidi makachero kuzuia watu ili bwana mkubwa apate hewa kwani mara nyingi unakuta watu wamevaa misuti. Hapa katukumbusha mavazi rahisi (simplistic). Hili nalo ni funzo gumu kwa vigogo wa kiafrika kulimeza.

Wakati akiitembelea shule ya sekondari maalum kwa wasichana wa kimasai kutoka mazingira magumu alinigusa hasa. Labda niseme mwaka jana Raisi Jakaya Kikwete alifungua shule moja ya sekondari kule Moshi. Ilikuwa ni ziara ya saa moja kufungua shule rasmi; na mara alipowasili pale shuleni si walimu wala wanafunzi waliopata muda wa kumfariji na kumpokea rais wao. Kilichotokea nilishangaa kuona makada kibao wa CCM pamoja na vigogo wa serikali kutoka mkoani na wilaya za jirani wakihangaika kugombania kujipanga mstari ili tu kushikana mkono na bwana mkubwa. Walimu waliokuwa wamejipanga sehemu maalum walifunikwa na wala hawakuweza kupata nafasi hiyo. Wala raisi hakuwa na muda wa kusalimiana ama kuzungumza sana na wanafunzi zaidi ya kupiga kejeli za kisiasa katika hotuba yake. Nadhani angeteta na wanafunzi kadhaa na kusikia hisia zao ingependeza zaidi.

Lakini kwa Bush tumeoneshwa nini maana ya kuwa kiongozi na nini cha kujali wakati unapotembelea sehemu. Raisi Bush alisalimiana na watoto wote wa shule ile pale Arusha; pia alisalimiana na hata kucheza ngoma na wamasai waliokuwa wakiburudisha ikiwa ni pamoja na kuwakumbatia baadhi yao. Hapa kwetu na Afrika kwa ujumla sivyo inavyokuwa, wanausalama hawaruhusu hili kabisa. Hivi huwa najiuliza kila Rais wetu anapokuwa mahali utaona mlinzi wake/ msaidizi wake kasimama nyuma. Hivi hiyo ndio kumaanisha ulinzi wa rais ni imara? Mbona watu kama akina Bush si hivyo na ulinzi ni imara? Nadhani ziara hii iwe mwanzo wa kuiga jambo kwa wanausalama na kwa ujumla wale watu wa karibu wa bwana mkubwa.

Labda niungane na waziri Dr. Jumanne Maghembe aliponukuliwa na ITV katika ziara ya Bush kule Arusha: “Marekani ni Taifa kubwa na tajiri na lina fursa nyingi. Ni vizuri tukashirikiana nayo na kudumisha urafiki na udugu na Taifa hili”. Nikiwarudia wale walionesha kutokutaka ziara hii: Hasa wasomi wa Mlimani, wajameni hivi tunajua kuwa wahenga waliwahi kusema kwa kiingereza tafsiri isiyo rasmi: “Every black has its white”, kuwa kila cheusi kina weupe wake pia”. Hapa namaanisha pamoja na uovu na unyama unaoambatanishwa na haiba ya Raisi George Bush, huyu ni mwanadamu mwenye pande mbili. Na kwa kutilia mkazo kwenu mabaya yake naamini mlighafilika tu; na mashiko ya kihisia yalitawala zaidi ya busara, mbona hamkutizama upande wa pili wa Bush?. La sivyo wala msingefikia hatua hiyo ya kutaka kuandamana.

Ziara ya Bush imetuonesha upande wa pili Bush mwanadamu. Mpaka kaondoka sijasikia akiongelea habari za Africom kama wasomi wetu walivyokazia kuwa anatafuta mahali pa kujenga kambi za kijeshi. Pia nadhani kilio chenu kingine kuwa kumkaribisha Bush ni kuonesha serikali yetu imeamua kuacha marafiki wa zamani na kufuata mabepari kama hatua isiyo muafaka si sahihi. Tumefuata sera za marafiki zetu kama Cuba, China na wengine wengi kwa miongo minne kwa mafanikio sana ya kiuchumi. Dunia ya leo tusiogope sana juu ya hali ya baadaye ila tutumie fursa zinazojitokeza hasa kama zina mwelekeo wa kukuza uchumi wetu.

Tukiwa bado tuna marafiki zetu wa zamani hakuna ubaya kama tunaongeza mwingine bila kuwapoteza wa zamani. Hii ndio hisia ninayoipata kwa ugeni wa Bush. Ziara hii kupitia mkataba wa Millenium Challenge naamini ni fursa ambayo tusingepaswa tuiache kwani ina tija sana hasa kama “mafisadi” watadhibitiwa wasiweke pua zao hapa. Tukumbuke hata jirani yetu Yoweri Museveni alikuwa na uswahiba na Bush na hata enzi za Clinton na kwa sasa wamemtupa kiana na kwa kipindi chote Uganda haikuwahi kuathiriwa kijeshi na Marekani ingawa kwa sasa kuna makampuni kibao ya Marekani yakianza kuchimba mafuta nchini humo.

Funzo lingine la ziara ya Bush kwangu ni pale kung’amua kuwa kweli nchi yetu ni masikini sana. Yaani bado hatuna uwezo wa kujikinga na Malaria? Yaani Bush anatununulia chandarua watanzania? Yaani watanzania walio wengi hawana uwezo wa kununua chandarua? Kwa maana nyingine watanzania wengi tu wachafu hatuwezi kuishi kwenye mazingira safi yasiyoruhusu mbu kuzaliana. Hatujui wajibu wa kiafya kusafisha mazingira yetu ili kuondoa mazalia ya mbu. Ni aibu lakini tufanyeje? Mpaka aje Bush atununulie chandarua. Hili linanipa shida sana kwani nadhani fedha ya malaria ni nyingi na ingefaa itumike kwenye sekta kama ya elimu. Sidhani kama unamzuia mtu asiugue malaria lakini hapo hapo humpi elimu bora kama unamsaidia sana. Bado umasikini hautoki kwa njia hii.

Ukimwi pia ingawa ni janga ambalo binafsi limeniathiri sana; ila ni wakati tujiulize kuwa hivi kama tukiweza kujihadhari na maambukizi, hizi fedha zote za Bush si zingefanya mambo mengine? Napata mashaka sana kama tunaendelea kupata ufadhili hasa wa kurefusha maisha na kwa wakati huo huo hatuna utaratibu wa kuwalinda wale ambao hawajaambukizwa ambao kwa kujichanganya kwao na waathirika wengi ni hatari.Ni wazi waathirika Fulani wana hasira sana na lengo lao kubwa ni kuondoka na wengine. Sisemi hili kwa kunyanyapaa ila ni lazima tufike mahali tujiulize hii misaada mikubwa ya kulinda maisha ya waathirika ina matokeo mazuri? Ni kwa vipi tuifanye tuwe na mazingira mapya kiutaratibu wa maisha ili tupate tija. La sivyo Taifa zima litaangamia na mamilioni ya dola za Bush.

Mwisho, nimalizie kama nilivyoanza: wakati nikiwa pale pembeni ya jeneza la bibi yangu baada tu ya kunong’onezwa na ndugu yangu kuwa Waziri Mkuu kajiuzulu, mara moja nilichoropoka nikaingia ndani nikafungua kiredio changu kidogo, radio sauti ya Ujerumani na nikakutana na sauti yake ikisema: Nimefadhaishwa, nimesononeshwa, …..mengine nimeyasahau manake yalinishangaza kwanini sasa kaamua kujiuzulu. Taifa linapotekwa nyara na mafisadi mtu hushangai pale hata busara za wasomi kama wale wa pale Mlimani zinapoonekana ni kejeli.

Nilisikitika tu pale jeshi la polisi lilipokataa kiaina kutoa ulinzi kwa maandamano ya wasomi wa mlimani kupinga ziara ya Bush. Ingawa sikuwa naunga mkono hoja zao, nadhani walinyimwa haki yao ya msingi kuandamana kupinga ujio wa Bush. Kweli February sitaisahau kama wakati muafaka wa mapinduzi ambayo sina imani sana kama yatabadilisha mwelekeo wa Taifa letu dhidi ya ufisadi. Hii ni nchi inaathiriwa na tabia na hulka ya kubebana, kupendeleana na utapeli wa kila aina. Na ndio maana baada ya Raisi kukabidhiwa ripoti ya Ernst & Young iliyokwishagundua kila ufisadi ndani ya BoT bado anaunda kamati nyingine ya uchunguzi. Lengo ni kulindana tu. Nimeshangazwa pia na mtuhumiwa mmojawapo wa ufisadi karudi kwa wapiga kura wake na kupokewa kwa shangwe na hata kupewa baraka za Askofu wa kanisa lake. Kweli kwa Tanzania ya leo bila ufisadi labda maisha ya wengi yatasimama.