My Blog List

Monday, January 16, 2006

UCHAGUZI NA ODA KUTOKA JUU NANI ATANGAZWE MSHINDI

Hili nataka nilieleze kama nilivyolipata kupitia tetesi zilizozagaa mitaani pale Moshi mjini baada ya uchaguzi wa ubunge ambapo mgombea wa Chadema, Mzee Ndesamburo alimshinda yule wa CCM, Mama Elizabeth Minde. Nitaeleza mara baada ya kuweka wazi wasiwasi wangu juu ya hali ya usalama pale Moshi.

Kwa kipindi cha wiki tatu nikiwa Moshi mjini nilishuhudia hali ambayo kwangu ilinitia wasiwasi sana. Eti siku hizi ujambazi umeongezeka sana Tanzania hasa Moshi na utawala umeamua kwamba askari polisi lazima wapite mitaani wakiwa na silaha kuhakikisha usalama. Kwa kweli mitaa imejaa askari ila katika hali ya kunishangaza sikujiona salama kabisa. Niwachekeshe: katika matembezi yangu nilikutana na kijana, charafu, hajachana nywele, amevaa suruali ya jeanse chafu sana ambayo imechanwa sehemu mbalimbali na amebeba bunduki( short gun). Nusura nianguke manake nikajua huyu ni jambazi bahati nzuri watu wengine wakaniambia ni askari yuko kazini.

Nililoliona hapa ni kwamba tofauti ya jambazi na askari haionekani manake usalama unakuwa haupo, raia hawezi kumjua askari ni yupi.Nidhamu ya askari haipo kabisa hili nitalizungumzia siku nyingine kwani nina mifano mingi tu.

Basi nieleze juu ya uchaguzi pale jimbo la Moshi manispaa hasa kuhusu tetesi ambazo kama waswahili walisema: “lisemwalo lipo na kama halipo…….”.Mwaka jana mara baada ya CCM kuteua wagombea wake wa ubunge nilieleza uvumi uliokuwa umezagaa kule Moshi. Mgombea wa chama hicho, Mama Minde, ni wazi alikuwa ni chaguo bovu kwa wapiga kura.

Nilikuwa Moshi wakati ule na nikasema hatashinda huyu mama. Na kweli imekuwa hivyo; ila nilipokuwa huko hivi karibuni nilikusanya tetesi zingine ambazo nafikiri ni vizuri wanablogu mnisaidie kuchambua.

Ni hivi: uchaguzi wa Tanzania uliokwisha hivi karibuni umesifiwa sana na wanahabari na hata waangalizi mbalimbali. Kwa wapinzani umekuwa ni bumbuwazi kubwa sana. Ila kwangu naomba nijibiwe hili:

Kwa mfano, pale Moshi manispaa, inasemekana msimamizi wa uchaguzi, mkurugenzi wa manispaa, alichelewa sana kutangaza matokeo mara baada ya hesabu kukamilika. Eti ilimbidi afanye mawasiliano na wakubwa ili aruhusiwe kuyatangaza. Habari aisizothititishwa ni kwamba ilikuwa ni janja ya kumtangaza mgombea wa CCM kama mshindi. Ila hapa ilishindikana kabisa. Wigo wa kura ulikuwa mkubwa sana na inasemekana hata hizo alizopata mwanamama sizo zilizotangazwa kuondoa aibu. Je huu ndio uchaguzi ulio huru na haki?

Inasikitisha sana hizi sera za Mao hazifai kabisa.

No comments: