MAXIMO NA WABRAZIL NA KIELELEZO CHA UCHANGA WA SOKA LA BONGO
Nimeitizama mechi ya Taifa Stars dhidi ya Brazil iliyochezwa tarehe 7/06/2010 siku ya jumatatu na ikanifurahisha sana. Furaha yangu si kufungwa bao 5 – 1 kwani tangu awali nilitarajia tungefungwa 3 – 0 lakini matarajio yangu hayakuwa hivyo. Ilikuwa ni mechi ya mwisho kwa Marcio Maximo na zawadi nzuri ya kocha huyo kuonesha kielelezo cha kazi aliyoifanya takriban kwa miaka isiyopungua mitatu na ushehe.
Marcio Maximo alianza kazi yake kwa kupokea timu ambayo ilikuwa haina misingi yeyote ya soka la kisasa. Ni timu iliyokuwa inaendeshwa kienyeji sana, timu ambayo nina hakika ilikuwa haina tofauti na timu za vijijini hapa Tanzania. Kimsingi timu hii kwa kipindi chote cha Maximo imekuwa katika kujengwa ingawa wadau wengi wa soka wamekuwa wakimlaumu kocha huyo mbrazili kuwa hana mafanikio yeyote. Kimsingi hawajui kuwa kujenga timu yenye wachezaji wa kiwango cha chini kama ya kwetu inahitaji kizazi “generation” kuandaliwa tangu utotoni katika timu za makundi tofauti ya umri ili kufikia timu kamili ya kisasa.
Wadau wengi walisahau kuwa Maximo amekuta timu ya kuokoteza mitaani ya wachezaji wasiojua kuwa kwenye mpira kuna nidhamu ya mpira ili uweze kufanikiwa. Wadau wetu wa soka hawakuzingatia mambo mengi ya msingi ambayo Maximo kailetea nchi yetu lakini ukweli utabakia pale pale kuwa huyu bwana kwa kiasi kikubwa kawafumbua macho watanzani na TFF juu ya jinsi ya kuendesha timu ya soka kisasa. Lililobakia ni kazi hiyo kuendelezwa na mrithi wake kutoka Dernmak ambaye ametangazwa hapo jana.
Kilichoonekana katika kipigo cha jana ni kielelezo tosha kuwa wachezaji wetu bado sana. Ni wachezaji ambao kimpira bado wako chini sana, uwezo wao kiufundi ni mdogo sana. Ni wachezaji ambao naweza kusema kuwa hawafundishiki kirahisi na wala hawajifunzi. Inashangaza kuwa pamoja na kuwa na kocha wa hadhi ya Maximo, bado wachezaji hawa wanapata fursa nyingi za kutizama mechi kupitia runinga lakini sidhani kama wanajifunza kitu. Ndio maana nasema Tanzania inahitaji kizazi kipya cha soka kiandaliwe ili kuweza kufikia angalau mafanikio ya timu kama Ivory Coast.
Kama watanzania tutaendelea kutaka kushawishi na kuwapangia makocha wachezaji wa kuita kambini kamwe hatutafika popote. Umefika wakati tuheshimu kazi kitaalamu badala tu ya kufuata hisia zetu mioyoni mwetu. Kama tutafanya hivyo ni lazima tu soka letu litapiga hatua.
Jambo pekee ambalo ningetaka kumshauri kocha mpya ni kuwa kuna haja ya kuibua vipaji vya soka kutoka mikoani. Ninaamini kuna vipaji vya soka vimejificha mikoani na haviibuliwi kwani soka letu limebakia ni la Dar es salaam tu. Makocha wa mikoani wanatakiwa kuwatambulisha vipaji vilivyopo huko mikoani.
Mwisho, naamini soka ya Tanzania inaelekea kuzuri, nimshukuru Maximo kwa kututoa tongotongo.
No comments:
Post a Comment