My Blog List

Tuesday, May 04, 2010

DU! RAIS JK AMEKASIRIKA KWA HOJA NYEPESI

Hatimaye Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliamua kuhutubia Taifa mwisho wa mwezi wa Aprili kwa kutumia mtindo tofauti na mazoea. Hapa alibadili hadhira, badala ya kuhutubia Taifa, Raisi Jakaya Kikwete aliamua kuwahutubia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam. Wengi wao walionekana ni wanachama wa CCM kwa mavazi yao hali ambayo sidhani kama iliwakilisha taswira ya utaifa kwa mtu yeyote makini.

Raisi wa nchi anapoamua kubadili hadhira, ni wazi anazo sababu za msingi na ndio hapa binafsi nadhani ukakazi unakoanzia kwa kuzingatia yote aliyoyasema katika hotuba ile huku akishangiliwa kwa kelele na makofi lukuki. Ushangiliaji huu wa kishabiki hata katika mambo ya msingi kabisa unatia shaka dhamira ya dhati ya raisi pamoja na watu wake wa karibu kwa ustawi wa Taifa letu. Ninasema hivi kwa maono yangu kwani kuna kila sababu ya kufikiri kwa kina ambayo imenifanya niione hotuba ile kama lengo lake kuu ilikuwa ni kuwajibu TUKTA dhidi ya azma yao ya kuwahamasisha wafanyakazi kugoma.

Moja ya wasiwasi wangu kuhusu dhamira ya kiongozi wetu mkuu ni ile hali iliyojitokeza kwa yeye kutumia muda mrefu kuponda na kukebehi madai ya TUKTA kutaka kima cha chini kiwe ni shilingi laki tatu. Binafsi kwa serikali yetu ninayoifahamu ni kweli haiwezi kulipa kiwango hicho kamwe lakini naamini inaweze kulipa kiwango cha juu zaidi ingawa chini ya hapo kama kima cha chini. Raisi hawatendei haki TUKTA kwa kuwaponda ilihali wamejaribu kumuamsha kutoka lindi la udhaifu wa serikali yake katika kukusanya kodi. Naamini kama kweli nchi hii kodi itakusanywa kwa dhati ni wazi serikali yetu ina uwezo wa kulipa wafanyakazi wake kwa mujibu madai ya TUKTA.

Serikali yetu haikusanyi kodi kuendana na rasilimali na biashara zilizopo; serikali yetu inasamehe sana kodi, mtu makini arejee taarifa ya CAG iliyotolewa hivi majuzi, angalia misamaha ya kodi inavyoathiri mapato ya serikali yetu. Raisi anapotuambia kuwa mapato ya serikali ni madogo sana nashindwa kumuelewa kabisa. Angalia viongozi wa ngazi za juu wanavyoikwangua hazina ya nchi yetu kupitia wabunge, mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya kwa malipo lukuki ya posho mbalimbali ambazo hazilipwi kodi lakini mfanyakazi wan chi hii anakatwa kodi katika kila apatacho. Hapa nadhani Raisi wa Jamhuri angekuwa anapaona na ana dhamira ya dhati ya kupagusa ili kuleta haki na usawa wa kugawana keki ya Taifa basi asingelithubutu kung’aka kama alivyokuwa katika hotuba yake.

Raisi ameonesha kung’ang’ania sana mambo madogo katika kutia nguvu hoja yake na akaacha mambo makubwa ambayo ndiyo msingi wa wafanyakazi wa nchi hii kudai haki yao. Kwa mfano, sidhani kama ni sahihi sana kwa raisi kuongelea kuwa TUKTA inadai kima cha chini cha laki tatu kwa wafanyakazi wa majumbani (house girls) au kwenye mabaa (bar maids). Hivi kwa kazi wafanyakazi hawa wazifanyazo, ina maana hawastahili kulipwa malipo stahili kuliko wanayolipwa sasa? Sioni mantiki kama mtu ni tajiri, anakwenda kijijini anamchukua mtoto wa masikini ambaye ameshindwa kupelekwa shule alafu anakuja kumfanyisha kazi kwa kipato ambacho si haki kibinadamu. Hapa raisi ameonekana kuwatetea sana matajiri; kwake wenye viwanda kwa mfano alionekana kusisitiza kiwanda cha Maji, hapa nachukulia mtu kama Mengi, eti ukimlazimisha alipe kima cha chini cha juu hatapata faida. Inatia shaka inawezekana raisi ana ubia na watengeneza maji mpaka anajua faida yao, kwani mie naamini biashara ya Maji kwa sasa ina faida kubwa sana.

Raisi ameonekana kutowajali wafanyakazi wa Tanzania kabisa kwa kuwatisha eti kama mtu hataki kazi aache kuna wengine watajiunga. Hapa imeonesha jinsi gani raisi kama mwajiri mkuu asivyojua kabisa misingi ya utawala wa wafanyakazi. Ukiwa kama meneja mkuu, Raisi hapaswi kutumia kauli kama ile kwani moja kwa moja raisi analazimisha kuwa na wafanyakazi wa umma wanaofanya kazi bila msukumo chanya, waliokatishwa tamaa, wanafanya kazi bora liende. Ni katika mfumo huo, sitegemei maendeleo ya kweli kufikiwa katika kipindi tunaongozwa na sera za vitisho na kutojali. Ina maana raisi wetu haelewi madhara ya kisaikolojia watakayoyapata wafanyakazi ambao kwa ukweli wanafanya kazi kwa vipato vidogo sana lakini wanaona serikali yao ikisema haina fedha huku ikiruhusu mabilioni ya fedha kuliwa na vijikundi vidogovidogo vya mafisadi kupitia kashfa kama “Richmond, Meremeta, IPTL, mikataba ya Rites na vijimambo vingi ambavyo kamwe watanzania wamebaki gizani huku fedha zikipotea alafu watu wanaambiwa hatuna uwezo wa kulipa mnachotaka.

Raisi alizungumza jambo zuri sana kuwa kama serikali italipa kwa mujibu wa madai ya TUKTA, basi ina maana wafanyakazi 355,000 wa serikali watakuwa wanawanyonya wananchi wapatao milioni 39. Raisi anafikiri ukilipa wafanyakazi hao aliowataja basi inaishia hapo, kiuchumi hapa kuna “domino effect”, naamini kwa idadi ya wafanyakazi wa serikali wanategemewa sana na watu wengi. Malipo yao yanakwenda mpaka kwa watoto, wajukuu na hata wazee wa wafanyakazi hawa. Hapa naona raisi alighafilika kidogo lakini hapaswi kubeza idadi ya wafanyakazi eti ni ndogo. Kama kweli ana dhamira ya kuondoa unyonyaji basi asitumie wafanyakazi wa serikali bali atumie kundi dogo tu ambalo ndilo msingi wa unyonyaji hapa nchini. Nitaeleza:

Kundi hili ambalo naamini linatumia fedha nyingi sana ambayo kama ikidhibitiwa kwa utaratibu mzuri unaojali haki sawa katika jamii ya kitanzania ni kundi la wateule wachache wa nyadhifa mbalimbali za kitaifa pamoja na wawakilishi wa wananchi. Hapa naongelea wabunge takriban mia tatu na ushehe, nina hakika hawa ni mzigo kwa Taifa letu. Wengi wao hawana chochote wanachochangia bungeni ni kupiga usingizi, ama kukaa kimya na kila siku kujichukuliwa posho ambazo nadhani hazikatwi kodi. Nina wasiwasi hata kama mbunge hajahudhuria kikao bado analipwa. Siamini katika kipindi tunaelekea katika uchaguzi ni vyema wabunge wanaomaliza muda wao wakalipwa mafedha lukuki ya Mfuko wa Jimbo (CDF) kama si matumizi mabaya? Busara ingekuwa kuwasubiri wachaguliwa wapya, je kwa nini tusiamini kuwa hii itakuwa fedha ya uchaguzi? Bado tena mbunge huyuhuyu atalipwa mafao yake ya miaka mitano, mamilioni ya shilingi ambayo yanazidi kabisa mafao ya mfanyakazi wa serikali aliyeitumikia nchi hii kwa miaka zaidi ya thelathini. Hivi Mheshimiwa Raisi anajua vipaumbele vyetu halisi ni vipi?

Orodha ya wanyonyaji ni ndefu ikijumuisha waheshimiwa mbalimbali wa ngazi za kitaifa, wizara, mikoa hadi wilayani. Mtindo ni mmoja tu, kazi kidogo mapato ni makubwa tena bila kodi. Kama kweli Raisi angelikuwa ni muungwana basi angelijadili hili tuone mtizamo wake badala ya kutuletea mambo madogo kama ya “mahouse girls na mabar maids”. Nasema hivi nikitambua kuwa kama hili tabaka la viongozi ambalo ni mzigo kwa hazina yetu “parasitic class” kama litaangaliwa na serikali basi angalau itasaidia kuwezesha serikali kuwalipa wafanyakazi wake mshahara wenye heshima na utu. Hapa lazima niseme wazi kuwa sidhani kama mshahara wa laki tatu na kumi na tano ndio ulipwe kwani hata mie nadhani kwa maisha ya Kitanzania hii inaweza chochea mfumoko wa bei kama wa Zimbabwe. Naamimi panahitajika kiasi zaidi ya kinacholipwa kwa sasa.

Hapa lazima nimkumbushe Raisi kuwa alijisahau na hili angelizungumzia basi wafanyakazi wangeliridhika. Hakuwa na haja ya vitisho kwani mwisho wake Raisi anakuwa ndio chanzo cha tabaka la wafanyakazi wa umma ambao hawana tija kwani wanafanya bila kupenda wakifanyacho. Kwa maana nyingine, Raisi kupitia hotuba yake amedhoofisha ari ya wafanyakazi wake.

Nilipokuwa ninamsikiliza mheshimiwa Raisi JK, nilijikuta nikitafuta nakala ya magazeti ya nyuma ambayo iligusa ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) ya mwaka 2009 nakwambia nilijiuliza hivi raisi anapoongea na wananchi kweli anakuwa anatafakari mapungufu ya serikali yake katika kuhakikisha fedha za serikali zinatunzwa na kutumiwa vizuri ambapo kwa kiasi fulani ingesaidia kuboresha maslahi ya wafanyakazi? Kwa mfano ripoti hiyo inaonesha kuwa kwa mwaka 2009, serikali kupitia TRA ilitoa misamaha ya kodi shilingi 752.4 bilioni. Hii ni sawa na asilimia 18% ya mapato ya serikali yalisamehewa. Hapo hapo taarifa inaonesha kuwa TRA ilishindwa kukusanya kodi kwa kutimiza lengo kwa shilingi bilioni 426.4. Hapa ni wazi uwezo wa kukusanya kodi una walakini na ukiongeza na misamaha kuna kama takriban shilingi Bilioni moja inaachwa tu kupotea. Kwa ufupi taarifa hiyo naweza nikainyumbulisha kama ifuatavyo:

i) Matumizi ya hovyo kununua magari: 4 bilioni.
ii) Upotevu wa fedha katika manunuzi (procurements):12.9 bilioni
iii) Fedha zilizotumika nje ya bajeti iliyokusudiwa: 67. 4 bilioni
Ukitazama mashirika ya umma ndio hatari pia:
i) Bodi ya mikopo Elimu ya Juu (HESLB) imegeuka kuwa chombo cha kutoa zawadi kwa watanzania. Kwa mfano, taarifa inaonesha kuwa kutoka 1994 – 2004/05, imekopesha wanafunzi 113,240 lakini haijaweza kufuatilia fedha zake kwa wengi ni wachache sana wameanza ama wamerudisha mikopo. Bodi imetumia shilingi 51.1 bilioni ambazo kinadharia zinakuwa kama zawadi kwa walengwa, hakuna ufuatiliaji.
ii) Kuna hili la wafanyakazi hewa ambapo kutokana na udhaifu katika usimamizi wa malipo, shilingi bilioni 3 zilipotea mwaka 2009.

Kwa mtizamo wa haraka, kuna kama shilingi 890.8 bilioni, karibu Trilioni moja zimepotea katika kipindi cha mwa ka wa 2009. Kwa mantiki hii, nilipomsikiliza rais akilalama kama vile serikali yake ni masikini sana, ripoti ilinijia nikajiuliza labda ingelikuwa vyema kwa raisi kuwapa picha halisi ya changamoto zinazoikabili serikali yake na angeliwaomba wafanyakazi wajitoe mhanga ili kuepusha upotevu wa mapato ili serikali iboreshe makusanyo ndipo TUKTA ifikirie suala la kuomba maslahi. Badala ya kuwalaumu akina Mgaya, angeliwaomba wamsaidie kuwafunda wafanyakazi juu ya kujali kazi zao kwani upotevu mkubwa wa mafedha hayo au kutofikiwa kwa lengo la makusanyo ni matokeo ya wafanyakazi kuzembea majukumu yao. Ndio maana naamini kabisa raisi Kikwete pamoja na hotuba yake ndefu bado hakuwa na mantiki kabisa siku ile. Ile si hotuba ya Kitaifa, kama ni kwa wazee tu basi ilikuwa muafaka lakini kwa wafanyakazi ambao wengi wao wana akili na wanaona mapungufu kibao serikalini, rais hakututendea haki wafanyakazi.

Pamoja na mapungufu yote ya hotuba ile ya Raisi, lakini lazima nikiri kuwa, ni wajibu wa kiongozi wa serikali kama raisi kuhakikisha nchi haikumbani na migomo. Serikali haina budi kuwazoesha watu wake na masuala ya migomo kama njia ya kutatua matatizo yao. Katika kutimiza hili, raisi amefanikiwa kwani naamini kabisa hakuna mtu atakayegoma kama TUKTA wataendelea kuitisha mgomo mwingine baada ya kusitisha huu wa sasa. Hakuna mtanzania ambaye yuko tayari kufukuzwa kazi au kuandamana akumbane na rungu la dola. Kufanikiwa huko kuepusha mgomo ni ushindi kwa raisi lakini tija na weledi miongoni mwa wafanyakazi vitabakia vikishuka badala ya kuboreka.

Mwisho nimalizie kwa kusema tu kuwa Raisi alipoamua kuzungumza na wazee labda kwa kuwa wote wale enzi zao zimepita labda aliamua aongee katika lugha watakayoilewa ndio maana akaamua kujadili hoja kwa kutumia dhana nyepesi ambazo kimsingi hazikuwa madai makuu ya TUKTA. Naamini kama niliwasikiliza vizuri viongozi wa TUKTA, yapo mambo matatu ya msingi ambayo sikuona Raisi akiyagusa. Mambo hayo ni: Kodi kubwa kwa Makato ya Mishahara, Mishahara midogo sana, Mazingira bora ya Kazi. Hebu fikiria, kuna wafanyakazi lukuki wa serikali wanalazimika kufanya kazi zaidi ya muda wa saa za kazi lakini hawalipwi stahili zao kwa mujibu wa utaratibu.

Na ndipo hapa pamenifanya nijiulize: “Hivi kweli, Raisi wetu anajua athari za kisaikolojia za kauli zake hasi dhidi ya wafanyakazi na viongozi wake katika kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye mafanikio kutoka kwa wafanyakazi wake? Naachia hapa lakini niseme tu hii ni “ Food for Thought”.

No comments: