Mara nyingi nawaona watu hasa vijana wakionesha dhamira hasa ya kuwa viongozi wa umma. Leo nimekutana na kijana mwenzangu, wa Chama cha Chadema, anatangaza rasmi kugombea ubunge.
Kwa mazingira ya Tanzania, sina hakika kweli kama dhamira yake itafanikiwa iwapo atachaguliwa. Bado mindset/mawazo mtizamo ya watanzania vijana kwa wazee haitamruhusu mtu wa haiba yake kuweza kufanikisha azma yake kirahisi. Kizazi kipya cha vijana wa Tanzania ya leo kimeamua kurithi mtizamo wa wazazi wao: yaani kufanya mambo kwa kufuata hisia zaidi kuliko kwa kufanya uchambuzi wa kina katika kila jambo. Kwa maana nyingine, kama mtu unafikiri sana katika kila jambo unalofanya kama ninavyomfahamu Bwana Mnyika, sidhani kama kweli Bw. Mnyika ataweza Bunge la Tanzania. Watanzania wa leo ni wavivu sana kutumia ubongo, mara nyingi tunatumia mioyo katika kufikiri. Ni jambo la hatari sana na ndio maana watu kama Mnyika wanaonekana na baadhi ya watu kama vile ni vichaa.
Si kwamba ninamchukia ama sipendi Mnyika awe mbunge, ila nataka ajue tu kuwa itakuwa vigumu sana kufikia malengo yake ya kuleta mabadiliko katika Taifa hili changa la Tanzania. Ninamtakia harakati njema.