My Blog List

Monday, May 25, 2009

Leo naamua kujikita katika soka mchezo niupendao sana. Soka la Tanzania liko nyuma sana lakini siku za karibuni jamaa wanapiga kelele sana juu ya huyu Maximo. Wiki iliyopita kwa mfano makala moja katika gazeti la Raia Mwema ilisema: MAXIMO ANAKOSEA KUTOWEKA WAZI UTOSAJI WACHEZAJI: Mimi nina mawazo tofauti:

MAXIMO HAKOSEI KUTOWEKA WAZI UTOSAJI WA WACHEZAJI
Nikiwa kama msomaji wa magazeti yote makini hasa yale yanayotolewa mara moja kwa wiki, nimeguswa na makala zenye ushawishi na hisia kali dhidi ya mtaalam wa soka Tanzania, Marcio Maximo. Sina hakika kama kuna kampeni ya kumng’oa huyu kocha wa Taifa Stars lakini ni dhahiri wapenda soka wa Tanzania wamemchoka kwa sasa.

Binafsi kama mtanzania na mpenda soka asilani sijafikia hatua hiyo kwani bado sikuwa na matarajio makubwa ya Tanzania kufanikiwa kwa haraka aambayo wadau wengi wana itaka. Kwan chi kama ya kweu kufiia mafanikio ya soka ya kufuzu fainali za Afrika ama zile za Kombe la Dunia sidhani kama ni uhalisia wa dhahiri kwa kipindi kifupi ambacho Maximo amekuwa na timu yetu. Nimesoma makala kibao zinazoonesha kuwa wafuatiliaji wengi wa soka la Tanzania hawampendi Maximo na wanadhani hana jipya. Kwa mfano, wiki iliyopita magazeti ya wiki matatu yaliamua kumjengea hoja chafuzi kocha huyu.

Napenda kugusia juu ya makala ya Ibrahim Mkamba juu ya “Maximo anakosea kutoweka wazi anapomtosa mchezaji”. Nadhani ni vyema nianze kwa kusema kuwa ni vyema tumuache amalize mkataba wake na ikiwezekana afungashe virago lakini tusimtimue wala kumlazimisha afuate ushauri wa wadau, wapenzi wala waandishi kwani naamini mkataba wa kiuweledi ambao alisaini na serikali kupitia wizara inayosimamia michezo hautoi nafasi ya wadau kumshawishi juu ya uchaguaji au upangaji wa timu.

Mosi nianze na suala la Maximo kulalamikiwa kwa kuwatosa baadhi ya wachezaji kipenzi kwa mashabiki nchini. Si ajabu golikipa mahiri anayeaminiwa hapa nchini Juma Kaseja ni kinara ambaye amesababisha Maximo kuchukiwa na mashabiki. Siwezi kujua hasa ni kwanini Maximo kamtosa Juma Kaseja ila naweza nikasema pia sipati taabu sana kila anapomuacha.

Kwanini sipati taabu? Nitoe mifano, mwaka 1998, kocha wa Ufaransa Aime Jacqet, wakati akiiandaa timu ya Taifa kwa kombe la Dunia aliwaacha mastaa vipenzi vya mashabiki kama Eric Cantona, Leslandes na Davidi Ginola nje ya “Le Blue” na kupigiwa kelele za kufa mtu kuwa wenyeji wangeaibishwa nyumbani bila nyota hao. Kocha alikaa kimya pamoja na benchi lake la ufundi akiamini utaaalam na imani yake kwa wachezaji Fulani ni zaidi ya mapenzi ya mashabiki ambao mara nyingi hawazingatii hali halisi ya kutawala wachezaji ili uweze kuwa na timu.

Bw. Mkamba ametoa mfano mwingine kuwa makocha wanapomtosa mtu wanatoa taarifa kwa chama cha soka ama bodi za timu zao kuwa mchezaji Fulani harekebishiki. Mimi naamini waajiri wa Maximo yaani serikali na TFF wanajua kwanini wachezaji wakongwe kama Kaseja na akina Boban wametoswa na ndio maana wako kimya. Lakini nikumbushe pia wako wadau wakubwa wa soka nchini tena waliowahi kuwa vigogo wa FA, ambao walizoea kuitumia Kamati ya Utendaji ya TFF kupendekeza line up kwa kocha wa timu ya taifa. Hata walilazimisha kocha amchague mchezaji gani. Leo hii wanataka kocha afanye kazi kwa mtindo huo.

Maadam mkataba wa Maximo hatuufahamu na ninavyoamini Bodi za utawala za vilabu huko Ulaya pia huwa hazimpangii meneja nini cha kufanya ila zinachotaka ni meneja kuwasilisha mahitaji ya kifedha yatakayomuwezesha kufanikisha Bodi inachotaka ikiwa ni pamoja na aina ya wachezaji anaotaka kusajili. Lakini hata siku moja Bodi hailazimishi ama haikatai ushauri wa kitaalam kwa kupinga mchezaji asisajiliwe. Na ndio maana makocha huko Ulaya huwajibika ama kuwajibishwa pale matokeo yanapokuwa mabaya kulingana na kushindwa kutimiza malengo tarajiwa. Basi ni lazima tujue katika mkataba wa Maximo alitakiwa atufikishe wapi kisoka? Je ni kufuzu kwenda Kombe la Dunia ama kufuzu kombe la Afrika kwa kipindi cha miaka miwili? Kama ndio hivyo basi tufungue mlango aende. Tusipige kelele kuwa ni nani aitwe au apangwe katika kikosi anachochagua. Tukifanya hivyo inakuwa haina maana ya kuwa na kocha basi tuache TFF waongoze timu hiyo.


Ninasema hivi kwani ninaamini kwa nchi kama Tanzania wachezaji wetu ni wa kiwango kinachokaribiana sana. Si Kaseja, Chuji ama Boban na wengine ambao ni wakongwe wamefanikiwa sana kisoka. Kwa mfano, hawa ni wachezaji ambao wamecheza mechi kibao za kimataifa kuanzia kwenye vilabu vyao hasa vya Simba na Yanga. Wamekumbana na vilabu vikubwa barani Afrika kama Zamalek, Estional Al Ahly, Enyimba, Santos, Mamelodi Sundowns na vingine kama hivyo katika uchezaji wao. Je msaada wao uliwezesha kuzishinda timu hizi? Na je kwanini kupata kwao nafasi kucheza katika mechi kama hizi hakukuvutia mawakala wa timu hizo angalau kufanya majaribio?

Ni wazi tuwatizame wanasoka wetu katika mwelekeo wa kiuchezaji na tutafute tofauti yao na wachezaji wengine ndipo tupige kelele kama kweli tuna nyota wa kutisha nchini mwetu. Nakubaliana na wazo la Mkamba kuwa kama ilivyo kwa wenzetu walioendelea kisoka, wakongwe huondoka taratibu na chipukizi kuchukua nafasi zao taratibu pia. Kwa upande wa Maximo hili sioni ni tatizo kwani wakongwe wamekuwepo na hata sasa wamebakia wachache ila naamini kama kuna wakongwe wameondoka basi ni kwa kupoteza sifa za mwalimu Maximo anazotaka mchezaji awe nazo. Na ndipo hapa hatupaswi kumlazimisha Kocha Maximo kufanya kazi na watu wasiokuwa tayari kufuata anachotaka eti kwa kisingizio kuwa Maximo awe kama mzazi, hawa ni vijana wadogo ambao wanakosa kama binadamu wengine.

Hivi jamani, Mkamba mtu kama Kaseja, Chuji ama Boban ni watu wanaotakiwa waangaliwe kama Baba na Mtoto na Maximo? Mtu mwenye mke na mtoto achukuliwe katika malezi ya baba na mtoto? Huyu ni mtu mzima anayepaswa kujua madhara ya kila jambo analofanya hasa kwa kuzingatia wakati tuliopo katika dunia ya leo. Professionalism (weledi) ina misingi yake ambayo wachezaji na wapenzi na watu waelewa kama Mkamba mnapaswa kuielewa. Kwa hili Maximo aachwe na asiongozwe na matakwa ya mashabiki kabisa.
Ni wazi hatutaweza kuifikisha nchi yetu mahali popote katika nyanja mbalimbali kama bado kuna mtanzania anafikiri visingizio kama “hakuna mwanadamu asiyekosea” basi makosa yavumiliwe ni ndoto.

Lazima tuzingatie kanuni na kuacha hisia za kimaono (emotion) kuongoza matendo na maamuzi yetu. Umefika wakati wanamichezo wetu waelewe kuwa kila fani ina kanuni zake na hawa makocha wenye utaalam wanatumia sana kanuni kwani ndio msingi wa mafanikio. Unapoona Ferguson hajali sana hisia za mashabiki kupenda Tevez abakie Man United basi tuelewe timu ni zaidi ya mtu mmoja na pia maamuzi ya kocha yaheshimiwe.

Kabla sijamalizia makala yangu nadhani watanzania tunapaswa kuelewa kuwa timu ya Taifa si ya kila mchezaji, ni timu ya wale tu watakaokidhi matakwa ya kocha yaani watakaowezesha mwalimu aweze kuwa na timu. Si matakwa ya mashabiki ama wadau wa soka. Ndio maana hata nchi ya jirani ya Kenya sasa hivi kuna matatizo katika kambi ya timu hiyo jijini Nairobi ambapo kocha Antoine Hey amewatimua wachezaji mahiri wa Harambee Stars huku wakikabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Nigeria.

Naamini hakuna kocha makini hasa hawa maproffessinal ambaye atakuwa tayari kuendeshwa kama tunavyotaka iwe. Ni mwalimu gani ambaye atapenda kukaa darasani na kuongozwa na mwanafunzi wake ama wazazi wa mwanafunzi Fulani wamlazimishe mwalimu kutenda kitu Fulani kwa watoto wao hasa kuhusu suala la ubora wa mwanafunzi?
Mwisho, kwa mantiki ya maslahi ya timu bila kufuata mashiko ya mashabiki wenye matarajio yasiyo na uhakika wala uhalisia kamwe nchi yetu haitaweza kuendana na taratibu na misingi ya soka la kisasa. Maximo ataondoka ama pia atafukuzwa lakini mwisho wa siku kama kocha atakuwa ni mgeni basi hii kutoswa toswa kwa wachezaji haitakwisha hadi tutakapotambua umuhimu wa kujifunza na misingi yake na si kuvimba kichwa kwa baadhi ya wachezaji na kutegemea kubebwa na hisia za mashabiki ama upenzi na hisia za wadau wa soka. Roger Milla aliitwa na raisi Paul Biya wa Cameroon kujiunga na timu ya Taifa licha ya kustaafu kwani alikuwa ni mchezaji maalum “special” hapa kwetu hatuna mchezaji wa aina hiyo kabisa

No comments: