My Blog List

Monday, January 16, 2006

KUTOKA TANZANIA HADI UGANDA

Mara ya mwisho niliaga kwamba sitakuwepo ulingoni mwaka jana. Nilikwenda mapumzikoni kule kwetu Moshi. Niliondoka hapa Uganda nikiacha hali ya kisiasa ikiwa ya vurugu, vitisho na udikteta ukiashiria kila hali ya zari kama sio dhahama ama kasheshe. Nimerudi hapa Uganda; ni wiki moja imekwisha sasa na hali imebadilika haswa kinume na nilivyokuwa nimetabiri kwamba hatima ya Besigye kisiasa. Nitaeleza baadaye.

Niwapashe wanaglobu wenzangu ni nini nilikikuta huko Moshi, uchagani katika wilaya ya Moshi Vijijini, jimbo la uchaguzi la Vunjo. Nilifika tu na Raisi mpya akatangazwa. Hii haikuwa tashwishwi kwangu kufuatilia kwani dhahiri nilijua JK angeshinda. Ila uchaguzi wa ubunge ulinikuna sana.

Baada ya miaka kumi ya utawala wa mbunge wa chama cha upinzani hatimaye jimbo langu la Vunjo likamchagua mbunge kutoka CCM kwa mara ya kwanza tangu siasa za vyama kurejeshwa. Hili lilinifurahisha kwani hawa jamaa wa upinzani wameirudisha Vunjo nyuma sana. Nasema hivi kwani katika eneo ninaloishi, kijiji cha Uparo, Kirua Vunjo, palw maeneo ya Kawawa Road ni dhihirisho tosha.

Nyumbani pale hakuna maji ya bomba tangu uhuru saa. Umeme ndio usiseme hakuna kabisa. Barabara ya kwenda Kirua Vunjo haifai kabisa; ikinyesha mvua inabidi magari yasubiri jua litoke ili pakauke ndio watu waweze kusafiri. Kuhusu mambo ya elimu ndio usiseme: eneo la Kawawa Road kwa mfano halina shule ya sekondari wala msingi na lina makaazi ya watu wasiopungua elfu tano. Watoto inawabidi kutembea kwa miguu zaidi ya kilomita saba kwenda shule kama za Pakula Sekondari, Mashingia na Uchira Sekondari. Hii ni hatari sana sasa tuone hawa CCM watafanya nini.

Niliposikia Kikwete na ari yake mpya, nguvu mpya na kasi mpya sikumwelewa sana ila nampa matarajio kama mkazi wa Kawawa Road kwani tumempa mbunge labda matatizo yetu yatapungua. Nafikiri mheshimiwa mbunge anajua hili.

Sasa niwarejeshe hapa Uganda: Mnakumbuka Museveni aliamua kumweka jela mpinzani wake mkuu Dr. Kiiza Besigye. Chama cha Besyigye kikaweka ukinzani wa hali ya juu. Nakwambea imesaidia sana , hali ya siasa ya Uganda kwa sasa ni shwari hata mimi nashangaa. Besigye yuko nje kwa dhamana ila kampeni in kama kawa. Vitisho dhidi ya fyombo vya habari na wapinzani vimekomeshwa; wale wanajeshi waliozoeleka kujazana mitaani hawapo tena.

Museveni kabadilika sana; uchaguzi utakuwa shwari kama hali itaendelea hivi. Nitaendelea kuwapasha zaidi ila tu Besigye anatuhumiwa kubaka na kesi inaendelea na imejaa vituko kwelikweli.

No comments: