My Blog List

Monday, January 30, 2006

JK ANATANIA TU.

Nakumbuka mzee kifimbo alipong’atuka mwaka 1985, nchi yetu ilikuwa hoi kiuchumi. Mzee Ruksa alikuja kama mkombozi. Wakati huo nasoma shule ya msingi, basi redio Tanzania ilizoea kucheza nyimo kuonesha mwelekeo mpya; nakumbuka kibao kimoja: ‘Usiopowajibika Ole Wako, Utakumbwa na Fagio la Chuma’. Pia kulikuwepo tangazo katika redio kila mara redioni eti: Mdudu rushwa ni hatari na anapiga na anaua’.

Hii yote ilikuwa kuonesha eti Mzee Ruksa kaja na ari mpya dhidi ya rushwa. Matokeo yake utawala wake uliikumbatia rushwa hadi mzee Kifimbo kumkemea kiana wakati Fulani pale Kilimanjaro Hoteli.Baadaye akaja Mkapa na kauli mbiu ilikuwa ‘Uwazi na Ukweli’. Kinyume chake huyu bwana hakupenda uwazi kabisa; ukweli ndio usiseme, waandishi wa habari watakuwa mashahidi hapa.

Sasa kaja Kikwete na kauli mbiu—Ari mpya, Kasi mpya na Nguvu mpya. Hisia zangu zinaniambia hivi: Kuna hatari haya majigambo tu. Katika uteuzi wake anaonekana kuja na sura mpya nyingi tu. Hii ni habari njema isipokuwa utendaji wao sidhani kama utafanikiwa.

Hii ni kwasababu raisi anapaswa, nafikiri analijua hili kwamba CCM imejaa wala rushwa wakuu nchi hii. Vyombo vya dola, mfano jeshi la polisi limejaa wala rushwa na huu ni utamaduni ndani ya chombo hiki inavyoonekana.

Nilipokuwa natizama hotuba ya JK ya ufunguzi wa bunge niligundua mambo mengi. Wapo wabunge kadhaa walionesha sura za woga na chuki dhidi ya maneno ya raisi. Wengi wa wabunge wazee pamoja na wabunge wanawake kadhaa walionekana kuogopeshwa na hotuba ile.

Kwa mtu yeyote aliyezoea kuishi kiujanjaujanja aliogopa sana. Nani asiyejua wabunge wengi wanalitumia bunge kama tanuri ya utajiri? Nani asiyejua wabunge wengi ni vihiyo ambao hata hawafahamu nchi yao kwa dhati. Mheshimiwa JK anaongea kama vile hajui wapo wazee, vigogo ambao hawashikiki nchini mwetu (untouchable) wamejazana bungeni ili kulinda maslahi yao. Hawa ni kikwazo kwa Ari mpya, Kasi mpya na Nguvu mpya.

Mwisho niseme tu ninamuunga mkono mheshimiwa JK, ila nina hakika itakuwa vigumu kwake kuleta mabadiliko tunayoyatarajia. Kutamba kwa majambazi ni kielelezo cha kwanza. Ila itabidi raisi awe mkweli tu kuwaridhisha watanzania. Kama waswahili walivyonena: “Bahari haiishi Zinge” nami ninene: JK anatania tu.

Monday, January 16, 2006

UCHAGUZI NA ODA KUTOKA JUU NANI ATANGAZWE MSHINDI

Hili nataka nilieleze kama nilivyolipata kupitia tetesi zilizozagaa mitaani pale Moshi mjini baada ya uchaguzi wa ubunge ambapo mgombea wa Chadema, Mzee Ndesamburo alimshinda yule wa CCM, Mama Elizabeth Minde. Nitaeleza mara baada ya kuweka wazi wasiwasi wangu juu ya hali ya usalama pale Moshi.

Kwa kipindi cha wiki tatu nikiwa Moshi mjini nilishuhudia hali ambayo kwangu ilinitia wasiwasi sana. Eti siku hizi ujambazi umeongezeka sana Tanzania hasa Moshi na utawala umeamua kwamba askari polisi lazima wapite mitaani wakiwa na silaha kuhakikisha usalama. Kwa kweli mitaa imejaa askari ila katika hali ya kunishangaza sikujiona salama kabisa. Niwachekeshe: katika matembezi yangu nilikutana na kijana, charafu, hajachana nywele, amevaa suruali ya jeanse chafu sana ambayo imechanwa sehemu mbalimbali na amebeba bunduki( short gun). Nusura nianguke manake nikajua huyu ni jambazi bahati nzuri watu wengine wakaniambia ni askari yuko kazini.

Nililoliona hapa ni kwamba tofauti ya jambazi na askari haionekani manake usalama unakuwa haupo, raia hawezi kumjua askari ni yupi.Nidhamu ya askari haipo kabisa hili nitalizungumzia siku nyingine kwani nina mifano mingi tu.

Basi nieleze juu ya uchaguzi pale jimbo la Moshi manispaa hasa kuhusu tetesi ambazo kama waswahili walisema: “lisemwalo lipo na kama halipo…….”.Mwaka jana mara baada ya CCM kuteua wagombea wake wa ubunge nilieleza uvumi uliokuwa umezagaa kule Moshi. Mgombea wa chama hicho, Mama Minde, ni wazi alikuwa ni chaguo bovu kwa wapiga kura.

Nilikuwa Moshi wakati ule na nikasema hatashinda huyu mama. Na kweli imekuwa hivyo; ila nilipokuwa huko hivi karibuni nilikusanya tetesi zingine ambazo nafikiri ni vizuri wanablogu mnisaidie kuchambua.

Ni hivi: uchaguzi wa Tanzania uliokwisha hivi karibuni umesifiwa sana na wanahabari na hata waangalizi mbalimbali. Kwa wapinzani umekuwa ni bumbuwazi kubwa sana. Ila kwangu naomba nijibiwe hili:

Kwa mfano, pale Moshi manispaa, inasemekana msimamizi wa uchaguzi, mkurugenzi wa manispaa, alichelewa sana kutangaza matokeo mara baada ya hesabu kukamilika. Eti ilimbidi afanye mawasiliano na wakubwa ili aruhusiwe kuyatangaza. Habari aisizothititishwa ni kwamba ilikuwa ni janja ya kumtangaza mgombea wa CCM kama mshindi. Ila hapa ilishindikana kabisa. Wigo wa kura ulikuwa mkubwa sana na inasemekana hata hizo alizopata mwanamama sizo zilizotangazwa kuondoa aibu. Je huu ndio uchaguzi ulio huru na haki?

Inasikitisha sana hizi sera za Mao hazifai kabisa.

KUTOKA TANZANIA HADI UGANDA

Mara ya mwisho niliaga kwamba sitakuwepo ulingoni mwaka jana. Nilikwenda mapumzikoni kule kwetu Moshi. Niliondoka hapa Uganda nikiacha hali ya kisiasa ikiwa ya vurugu, vitisho na udikteta ukiashiria kila hali ya zari kama sio dhahama ama kasheshe. Nimerudi hapa Uganda; ni wiki moja imekwisha sasa na hali imebadilika haswa kinume na nilivyokuwa nimetabiri kwamba hatima ya Besigye kisiasa. Nitaeleza baadaye.

Niwapashe wanaglobu wenzangu ni nini nilikikuta huko Moshi, uchagani katika wilaya ya Moshi Vijijini, jimbo la uchaguzi la Vunjo. Nilifika tu na Raisi mpya akatangazwa. Hii haikuwa tashwishwi kwangu kufuatilia kwani dhahiri nilijua JK angeshinda. Ila uchaguzi wa ubunge ulinikuna sana.

Baada ya miaka kumi ya utawala wa mbunge wa chama cha upinzani hatimaye jimbo langu la Vunjo likamchagua mbunge kutoka CCM kwa mara ya kwanza tangu siasa za vyama kurejeshwa. Hili lilinifurahisha kwani hawa jamaa wa upinzani wameirudisha Vunjo nyuma sana. Nasema hivi kwani katika eneo ninaloishi, kijiji cha Uparo, Kirua Vunjo, palw maeneo ya Kawawa Road ni dhihirisho tosha.

Nyumbani pale hakuna maji ya bomba tangu uhuru saa. Umeme ndio usiseme hakuna kabisa. Barabara ya kwenda Kirua Vunjo haifai kabisa; ikinyesha mvua inabidi magari yasubiri jua litoke ili pakauke ndio watu waweze kusafiri. Kuhusu mambo ya elimu ndio usiseme: eneo la Kawawa Road kwa mfano halina shule ya sekondari wala msingi na lina makaazi ya watu wasiopungua elfu tano. Watoto inawabidi kutembea kwa miguu zaidi ya kilomita saba kwenda shule kama za Pakula Sekondari, Mashingia na Uchira Sekondari. Hii ni hatari sana sasa tuone hawa CCM watafanya nini.

Niliposikia Kikwete na ari yake mpya, nguvu mpya na kasi mpya sikumwelewa sana ila nampa matarajio kama mkazi wa Kawawa Road kwani tumempa mbunge labda matatizo yetu yatapungua. Nafikiri mheshimiwa mbunge anajua hili.

Sasa niwarejeshe hapa Uganda: Mnakumbuka Museveni aliamua kumweka jela mpinzani wake mkuu Dr. Kiiza Besigye. Chama cha Besyigye kikaweka ukinzani wa hali ya juu. Nakwambea imesaidia sana , hali ya siasa ya Uganda kwa sasa ni shwari hata mimi nashangaa. Besigye yuko nje kwa dhamana ila kampeni in kama kawa. Vitisho dhidi ya fyombo vya habari na wapinzani vimekomeshwa; wale wanajeshi waliozoeleka kujazana mitaani hawapo tena.

Museveni kabadilika sana; uchaguzi utakuwa shwari kama hali itaendelea hivi. Nitaendelea kuwapasha zaidi ila tu Besigye anatuhumiwa kubaka na kesi inaendelea na imejaa vituko kwelikweli.

Saturday, December 10, 2005

MSUMARI WA MWISHO KATIKA JENEZA LA DR. BESIGYE

Kama nilivyokwisha tabiri siku kadhaa zilizopita hatimaye serikali ya Uganda imegongelea msumari wa mwisho katika jeneza--na kuthibitisha kuwa Dr. Kiiza Besigye hatagombea uraisi katika uchaguzi mkuu ujao hapo mwakani.
Nimeona niwaletee barua maalum iliyoandikwa na mwanasheria mkuu wa Uganda ili mjue kabisa sasa ile ndoto ya kumuondoa dikteta hapa Uganda imekwisha. SOMA
Ninachokiona hapa ni kwamba itakuwaje sasa manake sasa tuturajie mapambano na sijui yatakuwa ya aina gani manake yale ya kisheria inaonekana chama cha upinzani kimeshapoteza kabisa.

TUTAONANA BAADA YA WIKI MBILI

Kwa ufupi tu niseme kwamba kesho ninaanza safari ya kwenda nyumbani-Tanzania pale Moshi.Hivyo sitakuwa hewani kwa wiki moja na nusu hivi kwani ninapitia Tororo hapa Uganda na nitakaa kwa siku kama tisa hivi na nina hakika pale hakuna huduma yeyote ya tarakilishi hivyo sitaandika kabisa. Ila nitakapofika tu Tanzania nitaandika niliyoyaona katika safari yangu.
Kumbuka nitadodosa ya kule Tororo hasa juu ya siasa za hapa Uganda, alafu nikiwa Kenya kwa siku moja nitajaribu kuangalia kuna nini cha maana kuandika alafu nitakapofika Tanzania ujue wakati huo ndio uchaguzi utakuwa umekwisha. Hivyo nitaangazia nini kinajiri najua kutakuwa kuna mengi.
Basi niseme tutaonana.
Waziri wa afya wa Tanzania, Anna Abdallah alipokuwa akizindua rasmi kiwanda cha dawa za kusaidia kuongeza maisha kwa waathirika wa ukimwi, waya,mtandao,ngoma) Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd, DSM.

Sasa kiwanda cha madawa ya kuongeza muda wa maisha ya mgonjwa wa ukimwi kimezinduliwa rasmi Tanzania. SOMA Kuna watu wamefurahia hatua hii sana kwani kwao vifo vya ugonjwa huu vitapungua. Kwangu mimi nawaza vingine kabisa. Kwani naona ndio mwanzo wa maambukizi mengi hebu tusubiri tuone athari za kiwanda hiki kuwepo nchini mwetu.
Wabongo wengi tulivyo ni kwamba sasa mapenzi ni mbele kwa mbele na kwa maana hiyo tutakwisha zaidi. Na kama ilivyo kawaida Bongo, tutaanza kuuziwa dawa za kufoji na hapo ndio utaona utitiri wa maambukizi. Watanzania ni maskini na wapo wajanja sana ambao huu ni mwanya mzuri kwao kujipatia fedha na ndipo hapo tutakapokufa na kufaana.
Nia yangu sio kuponda ila nathubutu kusema hii ni hatua nzuri katika kupambana na janga hili ila tujiandae kwa madhara.

Thursday, December 08, 2005

UHUSIANO NA AKINA MAMA-- KIZUIZI CHA URAISI AFRIKA

Kama unataka kuwa rais wa nchi yeyote Afrika lazima uwe kati ya wale wateule la sivyo uwe mtakatifu. Nasema uwe mtakatifu kwani ni lazima uwe hajawahi hata kuwa na uhusiano na binti au mwanamama yeyote katika maisha yako. Kinyume na hapo kesi za ubakaji au udhalilishaji wa wanawake zitakukumba na ndoto yako ya kuwa rais itakwisha. Jacob Zuma, anakubali kuwa alifanya mapenzi na mwanamama fulani kwa makubaliano lakini anashangazwa na tuhuma za rushwa. somahapa
Haya ndio yanayowakumba Dr. Kiiza Besigye na Zuma wa huko Afrika kusini. Hadi sasa ni tuhuma lakini kwa hali ilivyo inanifanya niamini kuna ukweli ila hila zinatumika kubadili uhusiano wa makubaliano kati ya watu wawili kuwa ni ubakaji. Hebu soma hii habari ya mashtaka ya Zuma ujionee mwenyewe. soma

Wednesday, December 07, 2005

KIKWETE MZALENDO KWELI?

Nimekutana na makala moja ambayo imenifanya nijiulize maswali mengi sana. Unajua hivi kweli ni sawa kumpima mtu kama kiongozi bora kwa kuangalia ni wapi watoto wake wanasoma? Hivi majuzi mtoto wa rais mtarajiwa, Mh Kikwete alihitimu katika chuo kikuu cha Dar es salaam; baadhi ya watu wanachukulia hiki kama kitendo cha kizalendo.
Hebu jaribu kusoma hapa alafu useme mwenyewe.

Sunday, December 04, 2005

MBOWE ANAVYOANDAMWA NA WA-TWAWALA

Freeman Mbowe anataka kuingia Ikulu; na inavyosemekana anawakilisha kizazi kipya(sio wanamuziki wa bongo flava) katika siasa za Tanzania.
Huyu bwana inasemekana anawapa maumivu ya kichwa sana waheshimiwa wa chama cha wa-twawala(CCM). Hevu soma hapa uone ni jinsi gani ukijaribu kupambana na wa-twawala wakati wewe huna tabia zao watapambana na wewe sawasawa. Inasemekana Mbowe anaipata fresh.

MKAPA ASIFIWA HAPA UGANDA

Wakati watu wote makini hapa Uganda wakiwa wamesikitishwa na hatua ya rais Museveni kung'angania madaraka, magazeti mengi yamekuwa yakimsihi Museveni afuate mfano wa rais Mkapa.
Ila leo ndio ilikuwa fungakazi manake gazeti moja hapa liliandika tahariri kumsifu raisi Mkapa kama mfano mzuri wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki. somahapa
Kwa Museveni yeye kasema kila nchi ni tofauti na hakuna haja ya kufananisha mifano kwani kila mtu ana njia zake binafsi za kutatua matatizo. Mnasemaje hapo?

Saturday, December 03, 2005

HAWA NDIO WASHIKA DAU.

MAJENERALI WA UGANDA: (L-R) David Tinyefuza, Salim Saleh and Elly Tumwine : Hawa ndio washika dau wakuu hapa Uganda. Hakuna cha wanasiasa, hapa lazima uwe mwanajeshi ndio uweze kuwa mshika dau katika siasa.
Anayeonekana kulia ndio jaji wa mahakama ya kijeshi inayomshtaki Dr.Kiiza Besigye. Wa katikati ni mdogo wake rais Museveni na inaaminika ni kati ya watu matajiri sana hapa na ni askari shupavu.

MAGAZETI YAFUNGIWA TANZANIA

Hapa Uganda mambo yamepoa kiasi fulani kuhusu siasa.Inavyoelekea Museveni ni mbabe vya kutosha na hakuna njia ya kumdhibiti.
Kiiza Besigye ni wazi hatagombea uraisi nionavyo;kwani inaonekana kuna migongano ya muda mrefu ya kibinafsi kati yake na Museveni pamoja na maofisa wengine wa serikali hasa wanajeshi. somahapa Kwa hali hiyo hawataruhusu agombee na kama atagombea ninaona hali mbaya baadaye kama atakuwa rais.
Lakini labda tusubiri tuone.Leo niangaze Tanzania manake sasa Mkapa naye kaanza kufungia magazeti.somaSina hakika kama ni halali kulifungia gazeti ila nafikiri hii sio dawa manake kama serikali ingaling'amua nguvu ya mtandao basi isingechukua hatua hii.
Lakini kuna udhaifu sana Tanzania juu ya matumizi ya mtandao, manake sioni magazeti yetu mengi mtandaoni. Hapa Uganda ukifungia gazeti linaendelea kuchapisha mtandaoni.
Nataka niulize hivi kama gazeti linaandika kashfa ya kigogo ambayo inaisumbua familia yake ni makosa ya gazeti au kigogo mwenyewe?Nani alaumiwe hapa?

Saturday, November 26, 2005

NITAKAMATWA SIKU YOYOTE KUANZIA LEO

Nataka niseme kwa sasa niko hatarini kukamatwa wakati wowote. Unajua kuanzia juzi serikali imepiga marufuku kuandika, kuzungumza juu ya Dr. Kiiza Besyige, mpinzani wa Museveni ambaye yuko lupango.Kama mnavyojua hapa kila kitu ni kijeshi tu kwa hiyo mkisikia nimetiwa korokoroni msishangae kabisa.
Lakini kabla hayo hayajanikumba labda niseme tu kwamba bado hali sio shwari. Jana Besyige kapewa dhamana bonyezahapa ila bado anabakia ndani ya lupango. Kujua zaidi hebu bonyezahapa. La kushangaza zaidi hapa polisi ndio hao hao wanajeshi na kuna wanajeshi wengi sana Kampala onahapa
Katika kuhakikisha uhuru wa kusema, kuandika na kutangaza unadhibitiwa, serikali imemteua mwanajeshi bonyeza kuongoza bodi ya gazeti la serikali-New Vision. Hii inatafsiriwa kama kuhakikisha hata gazeti la serikali linamchafua mpinzani yeyote na haliandiki habari njema kumhusu.
Kwa Museveni hii ndio demokrasia.

Friday, November 25, 2005

KISA CHA WA-TWAWALA WETU

Ile stori ya wa-twawala wetu wanavyowanyonya walalahoi inaendelea kudhihirika. Huko Kenya, rais Mwai Emilio Kibaki amelifuta kazi baraza la mawaziri.
Bonyeza hapa uone ni jinsi gani walalahoi wanavyonyonywa.Hivi kweli bara la Afrika ni masikini au tunatania?Mimi nashindwa kujua wala kuamini ila inanifanya niulize wenzangu: Kwa mfano jinsi serikali ya Tanzania inavyohangaishana na madaktari je ni kiasi gani kinatumika kwa wanasiasa wetu? Je ni busara kutumia mabilioni kwenye siasa na kuwasahau madaktari wetu?

Thursday, November 24, 2005

DALILI ZA UDIKTETA ZAJIONESHA JANA KAMPALA

Watu wanasema Museveni kawa dikteta; na leo nataka niwaoneshe haswa ni kwa vipi huyu bwana kweli ameamua kuitupa demokrasia kapuni.
Jana ile kesi ya mpinzani wake mkuu, Dr.Kiiza Besigye ilikuwa itajwe na kulikuwa kumepangwa maandamano makubwa ya wafuasi wake.Kinyume chake serikali ilitumia wanajeshi na kuwavisha nguo za polisi wakiwa na magari makubwa ya kijeshi katika kona mbalimbali za kampala. Soma hapa ujione mwenyewe udikteta unavyomea.

Wednesday, November 23, 2005

MKAPA ANAVYOSHAMBULIA WAZUNGU

Haya, leo Mkapa naye ameamua kuwachachamalia hawa jamaa wa magharibi. Anadai wanapokosoa nchi zetu wanaingilia sana mambo yetu kwa maslahi yao.SOMA

Tuesday, November 22, 2005

WIVU WA WAZUNGU

Eti wamarekani na waingereza wanashangaa kwanini China inawekeza kwa kasi Afrika?soma
Jamani huu sio wivu? Naomba tuelezane je China kuwekeza Afrika ni habari njema kwetu waafrika au balaa jingine?

JAMANI HII "THANKS GIVING NI NINI?"

Hii nataka mheshimiwa Ndesanjo asome na ikiwezekana anipe muangaza. Nasikia huko Amerika kuna hii sikukuu iitwayo: Thanksgiving, hebu niambie inamaanisha nini?
Joji Kichaka kong'oli hapa nimeona akitoa salamu za siku hii.Hapa ninaishi na Wamarekani miongoni mwao ni waalimu wangu basi siku tayari wameshaanza kutoa udhuru hawatahudhuria darasani. Ni nini msingi wa siku hii?

Monday, November 21, 2005

HATARI KWA UHAI WA GLOBU

Haya wanablogu jamani mimi sasa natishika. Hivi kama mmefuatilia huu mkutano wa vyombo vya mawasiliano ya kompyuta kuna habari sasa wa-twawala wanataka wadhibiti mitandao ya intaneti.
Sijui mnalionaje manake natishika sasa hapa.Kuna hatari habari zinazotokea huku zikadhibitiwa, tunaelekea wapi? Nimesoma habari bonyeza
nikashtuka sasa ule uhuru wa mawasiliano uko hatarini.Jamani tutuwaweza wa-twawala?