My Blog List

Monday, July 28, 2008

MSIBA BUNGE LA TANZANIA TENA

TANZIA – SASA IMEKUWA ZAMU YA CHACHA WANGWE


Ni saa nne na dakika arobaini na saba, mara nikitizama taarifa ya habari ya ITV usiku nashanga mstari mweusi wa maneno unakatiza katika runinga na maneno: “mbunge wa Tarime, mheshimiwa Chacha Wangwe amefariki dunia usiku kwa ajali ya Gari” habari zaidi fuatilia redio one.

Na kweli ninazima runinga yangu na kuanza kusikiliza redio one. Ninakutana na mahojiano kati ya watangazaji: Asia Mohamed na Jerry Muro akiripoti kutoka Dodoma. Wanahojiwa waheshimiwa mbalimbali kwa masikitiko bado wanaonekana kutaharuki. Mtangazaji anadai eti nyakati za mchana mheshimiwa Chacha alionekana akiteta na mheshimiwa Mudhihir, hii inanikumbusha huyu ni mhanga mwingine wa ajali katika bunge hili. Hisia fulani zinanijia akilini lakini sisemi kitu najinyamazia.

Nikiwa nimekwishaamini kuwa mheshimiwa huyu katutoka, navuta hisia kadhaa juu ya bwana huyu na mara moja nautambua Umachachari wake, ubishi wake hata pale pasipo na Mantiki lakini kwa yote , kauli ya John Cheyo inanikuna akihojiwa na Jerry Muro. Anasema: “Chacha alikuwa na msimamo ambao wengi wetu hatunao” . Nakubaliana na mheshimiwa Cheyo na ninaendelea kusikitika.

Mara ninaamua kumtumia mtu wangu wa karibu sms akiwa Dar es salaam nikimsihi afuatilie habari kuna tukio la kifo cha mbunge mashuhuri. Pia katika message yangu nampa hisia yangu kuwa sasa “ Chadema itachafuka hasa kwani kifo hiki kitatumiwa na wanazi kuonesha kukolimbana hakuko tu CCM”. Ninapoituma message ile mara napata message kutoka kwa rafiki mwingine akinihabarisha juu ya kifo cha Chacha. Ninamrudishia nikimsihi kuwa “Siasa za Afrika ni mchezo mchafu, nina hisia lazima kuna mkono wa mtu awe wa kambi ya marehemu ama kule tulikozoea kukolimba watu wabishi kama Wangwe”.

Hapo hapo napokea message nyingine ambayo inanijibu ile niliyotuma Dar es salaam: “Sio Chadema ni CCM walileta mgogoro alafu wamemuua ili tuone Chadema nao wana mchezo kama wao! Tunaelekea pazuri sana. Tutashuhudia mengi na ukweli utadhihirika mwisho”. Mie sijui kwanini watu wana maoni ya aina hiyo ila ndio jamii ya kitanzania ilipofikia sasa.

Inapofika saa sita na dakika kumi na sita usiku hisia zangu zinashangaa: Jerry Muro, mwandishi wa ITV anaongea na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, mheshimiwa Lukuvi ambaye anasema kuwa gari la Wangwe limepata ajali ya kuanguka baada ya kupasuka gurudumu. Lukuvi anamnukuu rafiki wa Wangwe ambaye alikuwa ndani ya gari la Wangwe na amepata michubuko tu. Anasema gari lenyewe lilibiringika mara nyingi sana na ndipo Israel akachukua roho ya mheshimiwa Chacha. Moja kwa moja hapa ninajenga kanuni za kihisia na chonganishi (conspiracy theories) kadhaa:

Moja, kwanini gari la mbunge kama tuyajuavyo ni magari imara , mazuri na nina hakika yanafanyiwa matengenezo bora, itakuwaje lipasuke tairi tena nyakati za usiku pasipo na joto sana la kupasha hiyo chubu? Inawezekana kirahisi namna hiyo? Au tuseme Chacha anatembelea ulimu?
Pili, hili Bunge letu lina matatizo gani? Ni balaa ama ni nini? Kwanini kila kikao kinapokutana hasa cha bajeti lazima Mbunge afe?
Tatu, kwanini katika bunge hili ukiacha mbunge mmoja tu, wote waliokufa kulikuwa na hali ya kuwa na maadui hasa juu ya misimamo ya marehemu hawa?
Nne, kwanini wabunge wa bunge hili wanapatwa na madhila kama ajali ama vifo mara baada ya kuwa ni watu wenye misimamo yenye kutetea maslahi ya umm a sana ama kudhoofisha maslahi ya umma?

SHUHUDA WA AJALI

Saa sita na dakika thelathini na sita, redio one inaripoti kuwa ndio mwili wa Chacha Unaingia hospitali ya Dodoma kutoka eneo la ajali huko Kongwa. Gari ni Land Cruiser namba: SM.4297 la Halmashauri ya Kongwa. Jerry Muro anaongea na Rafiki wa mheshimiwa Chacha ambaye alikuwa akisafiri na mheshimiwa Chacha, ndugu Deus Mallya, rafiki wa karibu wa Chacha, anaeleza walitoka Dodoma wakienda Dar, anasema alisikia kishindo kikubwa sana kabla ya ajali, ninapata hisia sio ajabu inawezekana gari hilo lilikuwa limetegwa bomu labda, na gari liliruka juu na kufuatiwa na mbiringiko mkubwa sana.

Kuhusu mwendo wa gari Deus Mallya anasema kuwa Mheshimiwa Wangwe hana hakika kama alifunga mkanda. Yeye alifunga mkanda, lakini kimazingira inaonekana marehemu alibanwa kwa hiyo napata hisia alikuwa amefunga mkanda la sivyo kwa mbiringiko huo lazima angerushwa nje.
Je mheshimiwa Wangwe alikuwa kwenye hali gani? Mwanzoni nilidhani ni Land Cruiser, kumbe sio, ila ni gari dogo. Alikuwa anaendesha gari aina ya Corola na anapoulizwa kama marehemu alikuwa mlevi anasema hadhani ila asubuhi alisema alikuwa na malaria.
Je hali ya gari ilikuwaje? Gari limekuwa kama kopo lililofinyangwa. Mheshimiwa Wangwe alikuwa katika hali gani baada ya ajali? Aliumia maeneo ya kichwani na kifuani.
Deus Mallya yeye anasema ameumia mguu wa kushoto kama ameteguka tu na ana maumivu kichwani. Haamini kama amepona, ndio maajabu ya Mungu.

Mwisho, Mkuu wa mkoa wa Dodoma anasema baada ya mwili kuingia Dodoma tusubiri maelezo ya Spika kesho asubuhi. Nami naamua kwenda kulala nitamsubiri Spika aseme zaidi asubuhi.

Binafsi niseme tu, kifo hiki kimenisikitisha na ndio maana nikaamua kuandika makala hii usiku huu wakati nikufuatilia habari zaidi za kifo hiki. Nimalizie kwa maneno ya rafiki yangu katika message yake ambayo yameingia sasa hivi wakati namaliza : “ Aise inasikitisha ubunge sio kazi nzuri kwa sasa afrika hakuna la maana wanalofanya bali kuadhibiana kiainaaina, ngoja tuone mengi yanaweza kufichuka”. Mie nabaki nikijiuliza sijui ni nani atafuata manake nina hakika kabisa kwa mtiririko huu basi kuna mbunge mwingine atakufa kikao kijacho cha bajeti. Kazi kwenu wabunge.

Nimalizie kwa kusema: “ Chacha tulimpenda sana lakini Mafisadi walimchukia sana”. Mungu amlaze mahali pema peponi, Amina.

No comments: