My Blog List

Sunday, April 27, 2008

AJALI YA NDEGE - MOSHI

Nilikuwepo ndege ilipoanguka Moshi maeneo ya jirani na kiwanda cha mafuta BP. Watu wawili walipoteza maisha yao: Rubani (Mbongo) na Mzungu mmoja. Wengine wawili walijeruhiwa.Ilikuwa ni Januari mwaka huu.

VYOO VYA USWAHILINI

Hiki choo kimebomoka lakini kinatumika, ndio mambo ya walalaho wa kitanzania. Nusu kimetoboka na jamaa akija kujisevu hapa inabidi awe makini asije tumbukia.

HILI NALO BAFU


TUONE NA MABAFU YA KUOGEA YA MTANZANIA WA KAWAIDA

Mtanzania wa kawaida ambaye kwake maisha ni magumu na haoni vijisenti hata kidogo. Yeye huwa anaoga mahali kama hapa. Chini ni mchanga tu, hakuna mlango na ujenzi wa bafu ni makaratasi na magunia. Haya yakitokea, wengine wanakomba mafedha "vijisenti" na wala hawachukuliwi hatua. Wanalazimishwa kujiuzulu tu.

HEBU TUJIONEE VYOO VYA WATANZANIA

Hapo chini ni hali halisi ya vyoo vya mtanzania wa kawaida ambaye vijisenti kwake ni ndoto. Mambo ya uswahilini hayo.

Saturday, April 05, 2008

UFISADI HADI JESHINI UGANDA

Wakati ufisadi umetawala Tanzania,kule Uganda hakuna tena woga, mafisadi ambao zamani walikuwa jeuri sasa mkono wa sheria unawakumba. Kuna Jemedari wa jeshi sasa kawekwa jela kwa kosa la ufisadi jeshini. Hebu msome anavyojitetea dhidi ya ufisadi alioufanya.
Majenerali wengine wanaendelea kukanusha ufisadi. Wakati jeshi letu liko Comoro, Waganda nao wako Somalia na kuna tetesi za ufisadi zaidi jeshini.

Tuesday, April 01, 2008

MAJENERALI UGANDA MATUMBO MOTO

Kwa wale masekretary wa vibosile basi wajifunze ni jinsi gani kazi hiyo imejaa ufisadi kutoka kwa sekretary wa Museveni.
Kuna skandali kubwa dhidi ya maafsa wa jeshi la Uganda kwa kuajiri askari hewa: unalijua? Msome pia kinara wa skandali hilo Jenerali James Kazini, ni yule aliyewahi kushtakiwa na Umoja wa Mataifa kwa kuibia DRC rasilimali.

Tuesday, March 18, 2008

YOWERI MUSEVENI NA AJENDA YA KIFALME

Muammar Ghadafi amemuhimiza Museveni aendelee kuitawala Uganda milele.

Saturday, March 15, 2008

NRM NA MADHILA KWA WAGANDA

Unataka kuijua NRM, ni chama dume, tawala kama kilivyo CCM, lakini madhara yake ni makubbwa sana kwa watu wake.

Thursday, March 13, 2008

TANZANIA NA MFUMO WA KIOLIGACHI KAMA URUSI

TANZANIA NA MFUMO WA KIOLIGACHI KAMA URUSI

Wiki hii nimeshawishika kuchangia juu ya mwono wangu kuhusu hili skandali la wizi wa fedha kule benki kuu: BoT maarufu kama EPA. Kwanza nimevutwa na mchango wa jumapili iliyopita kutokana na makala ya Bw. Tambwe Hiza: “Fedha zetu ni muhimu kuliko mashitaka” Tanzania Daima, Jumapili, Machi 09, 2008. uk. 21. Kwangu makala ile imenifanya nijiulize hivi kweli elimu ya Tanzania inafundisha watu kufikiri hasa?

Kwanza niseme tu nampongeza mwandishi kwa mtizamo wake huu ambao una tija moja tu: nayo ni fedha zote kurudishwa. Haya ni mawazo mazuri sana ambayo kwangu yananipa wasiwasi kama tunafurahia kurudishwa kwa fedha kwa kuwabembeleza wahalifu. Siamini kuwa kashfa hii imetufikisha mahali tuwaogope hawa mafisadi hadi kuwalinda na kuwahakikishia usalama wao mara watakaporudisha dhidi ya mkono wa sheria.

Pili, mwandishi alitumia mifano hai kuonesha jinsi gani matatizo katika nchi mbalimbali yalivyotatuliwa kwa njia nje ya mkondo wa kisheria. Nina wasiwasi kuwa kama tunawaepusha mafisadi na mkondo wa kisheria basi tunajenga mustakabali mbaya (wrong precedence) kwa mwelekeo wa Taifa hili changa kidemokrasia. Mwandishi alitahadharisha eti kama tutafuata mkondo wa kisheria basi itatugharimu sana kuwapata mafisadi ambao watakimbilia ughaibuni. Hili si kweli kabisa: moja, mfano jirani zetu Kenya kumekuwa na kashfa kubwa kama ile ya Anglo Leasing ambapo mabilioni ya dola yalichotwa kama EPA.

Baada ya watuhumiwa kujulikana hasa vigogo, tumeona serikali kama za Marekani na hata Uingereza zikiwanyima hata visa (hati za kusafiri na kuzuru nchi zao). Matokeo yake baadhi ya vigogo wa serikali ya Kibaki hawaruhusiwi kuitembelea Marekani. Mbili, sisi hapa hata kuwataja tunaogopa na hii inawaruhusu wawe huru kutoroka huko ambako Bw. Tambwe anakohofu itatugharimu kuwapata. Usiri huu kwa nia ya kubembelezana wahalifu nadhani ndio utakaotugharimu zaidi kuliko tungeamua kukazia kwenye mkondo wa kisheria.

Tatu, mwandishi wa makala ile alidai kuwa: “Binafsi nitafurahi endapo rais atashauriwa kusaini ‘Presidential Decree’ ya kuwasamehe waliorejesha fedha na watakaozirejesha”. Hii inanirejesha pale awali niliposema juu ya ‘wrong precedence’. Kama kweli ndio mawazo ya serikali yetu basi ni kusema kuwa Taifa letu limetupwa kwa mambwa. (thrown to the dogs). Ni kielelezo tosha cha tatizo la kielimu na kifikra miongoni mwa watanzania walio wengi hasa katika nyadhifa za juu. Haingii akilini eti watu Flani wanachukua kiasi cha fedha cha Taifa na kuzifanyia biashara zao alafu uchumi wan chi unaathirika vibaya hasa thamani ya shilingi yake nab ado kuna watu wana mawazo eti tuwasamehe na kuwapa upendeleo Fulani dhidi ya mkono wa sheria.

Ni wazi woga wote huu wa serikali katika kupambana na hili ni kwasababu tu Taifa letu limejaa mafisadi wa hali ya juu. Watu wasioshikika kirahisi wenye mitandao hadi ikulu na hata katika idara zote nyeti za nchi. Kule Urusi ya Putin wanawaita hawa watu ni “Oligarchy”. Ni watu wenye hila, wasio na huruma na maisha ya binadamu wenzao hata kidogo. Kwa kawaida hawa wanalindwa na dola katika ufisadi wao. Hawa hukamatwa tu pale ambapo wameamua kuwa maadui wa dola kwa kuanzisha harakati dhidi ya dola. Na ndio maana watu kama “Khodokosky” yule tajiri wa kampuni ya mafuta ya ‘Yukos’ anaozea jela baada ya kuanza kumpinga Putin.

Hapa kwetu kile anachotetea Bw. Tambwe ni katika kuendeleza mfumo wa kioligarchy kama ilivyo kule Urusi. Kama alivyokiri mwenyewe hajatumwa na mtu; lakini kama mtu una akili inayojali kuwajibika kimaadili kwa kila utendalo basi kwa Bw. Tambwe nadhani kwake maadili si hoja maadam hela zinarudi zote. Hivi kuna maana gani kuwa na Taifa ambalo watu ama viongozi wake wanakuwa huru kuiba fedha na baadae kuzirudisha baada ya kuzitumia kwa matumizi yao binafsi? Tena wanazirudisha wakati zimeshapoteza thamani ya kipindi walipozichota alafu tunasema hela imerudi.

Alafu pia tunajenga Taifa ambalo viongozi wake hawana mfumo maalum wa kitabia katika ofisi za umma (code of conduct). Ni hatari manake ni lazima tuwe na taratibu za kisheria za kuadhibu makosa na wala si kubembelezana.

Ningependa pia nipinge mifano kadhaa ambayo Bw. Tambwe aliitoa katika kuhimiza hoja zake; na hasa ni juu ya jinsi kule Kenya mfumo wa kisheria ulivyoachwa na mazungumzo yakaleta faraja. Naamini kama tunafananisha na Kenya kwa hili la BoT basi ile naiona kama mfanano usio sahihi (wrong analogy). Labda tu nimkumbushe Bw. Tambwe kuwa kwa Kenya bado ni mapema sana kudhani kuwa siasa za Kenya zitatulia. Kuna suala moja nyeti sana wakenya wameliacha nalo ni Haki (justice). Ni usanii tu pale kwani haiwezekani mtu ashinde kwa kuiba kura alafu wafanye kazi pamoja na aliyeibiwa kirahisi. Ni usanii tu; kwani siamini kuwa miaka mitano serikali hii ya Muungano (grand coalition) itadumu. Kuna tofauti za kimsingi kati ya ODM na PNU ambazo bila kuzingatia haki haziwezi kusawazishwa.

Ni katika mfanano huo wa Kenya ambao siamini unatufaa katika hili la EPA. Masuala ya kimaadili hayawezi kutatuliwa kwa kisiasa; haya ni mambo yenye kuathiri uchumi na maendeleo ya nchi na kama tunafanya makubaliano na hawa maoligarchy wa kitanzania basi ni kutangaza Tanzania kama Taifa la viongozi kuwa huru kuiba kwani watarudisha. Kwa mtizamo wa Bw. Tambwe, kitaalamu ni kuwa hii ni nchi ya ustahimivu wa maovu wa hali ya juu (highest impunity) kwa watawala.

Mawazo ya Bw. Tambwe yalikuwa ni mazuri kusikiliza na kihisia (emotionally) lakini unapoyaingiza ndani ya ubongo ni ya hatari kwani ni kweli fedha zitarudi lakini ndio utakuwa ni mwanzo wa kuwaruhusu watawala kutumia ofisi za umma kuiba bila kushtakiwa kwani wanarudisha. Na kwa mantiki hiyo, serikali itatumika kama mkopeshaji bila riba kwa vigogo kama ilivyokwisha jionesha kwani pesa zinarudishwa bila riba. Hii ni hasara kwa nchi; na i ikiachwa iendelee basi zitaibiwa nyingi sana kitu ambacho ni hatari sana.

Mwisho niseme ni vyema tukumbuke kila mtu ana haki ya kutoa maoni ila tukae chini tufikiri kwa mapana kimantiki na si kihisia kabla hatujazungumza. Nalisema hili kwani umasikini mkubwa unaoikumba Tanzania na hata Afrika ni kwasababu tumegeuka kuwa watu wa mashiko ya kihisia zaidi kuliko kufikiri. Tanzania ya leo hakuna tofauti ya kimawazo kati ya msomi wa hadhi ya mwanasheria mkuu dhidi ya msomi wa elimu ya msingi linapokuja suala la kuwajibika na kutoa mawazo ya kifikra yanayohitaji kufikiri hasa.

Kwani wenye mawazo kama haya ya Tambwe basi kuna tatizo la ubinafsi hasa pale mtu anapochagua hatua ambazo hazitamuumiza panapohitaji kuwajibika. Kimaadili tunasema ni ‘ethical relativism’. Kuepukana na hili zinahitajika bongo kufanya kazi kwelikweli. Na kwasababu kwa Tanzania hili ni tatizo kubwa basi ufisadi na mafisadi wataendelea kutesa hasa.

Saturday, March 08, 2008

SIKU YA AKINA MAMA TANZANIA

Ni siku ya wanawake duniani; na hatuna budi kutafakari.

Ulimwengu wa leo umejaa “ngano” nyingi sana ambazo kwa kiasi kikubwa ni chanzo cha tamaduni na ustaarabu usio makini miongoni mwa waafrika na hasa watanzania kwa ujumla wetu. Katika siku hii ya wanawake duniani, nasema hivi huku nikijiuliza bila majibu maswali kadhaa:

Mosi, hivi siku hii ya wanawake duniani ni changamoto zipi tulizonazo kama watanzania? Kwangu nadhani ni wakati muafaka kwa jamii ya wanawake kujiuliza hivi ni kwa vipi bado wanaishi katika “ngano”: yaani bado kuamini wao si bora zaidi ya wanaume? Badala yake mwelekeo wa uongozi wa nchi hii umebakia na wanawake wasindikizaji, yaani wanaoridhika na vyeo tu. (sycophants). Hawa hawana hoja mbadala kwa bwana mkubwa; na ndio maana katika hii dhahama yote ya ufisadi (ufisadizesheni) iliyoikumba nchi yetu hakuna wanawake hasa wasomi wakionesha hisia zao kimaandishi ama kimdomo.

Pili, ni wakati akina mama kujiuliza hivi ni lini wataamua kukataa kutumiwa kama chombo cha kustarehesha (enticing object)? Hili naliona kwani ni ukweli halisi kuwa ufisadi mwingi nchini Tanzania unachangiwa sana na tamaa ya akina baba wengi kutamani mafedha katika kile kuwaridhisha wapenzi ama wake wao waishi raha mustarehe. Ni wakati akina mama waamue la sivyo ufisadi hautakwisha.

Tatu, kuna huu upendeleo maalum kuwainua wanawake (affirmative action): nakumbuka tamko la Beijing (Platform for Action) ilihimiza kuwainua wanawake katika nyadhifa za kiuongozi dhidi ya mfumo dume (partriarchy). Kwa Tanzania nadhani rais Jakaya Kikwete katimiza hili. Ila nadhani kaenda mbali sana manake kuna wanawake wengi tu nchini mwetu wana nyadhifa zisizolingana na kiwango cha elimu walichonacho na wanapwaya sana pale mambo yanayohitaji mtu atumie bongo hasahasa. Hili nalisema wazi kuwa nadhani upendeleo maalum naukubali lakini usitumiwe kama zawadi kwa mtu ama ahsante kama tunavyoshuhudia kwa sasa.

Kwa Tanzania, nimeshangazwa sana kuona bunge letu limejaa hawa wabunge wa viti maalum ambao wengine hata elimu ya sekondari hawana ama wameishia kidato cha nne na vikozi kama vya vyeti vya utunzaji ofisi (secretary). Siamini kabisa katika ulimwengu wa leo, mbunge wa aina hii anaweza kutoa mijadala ya kimantiki katika kujenga nchi yetu; wengi wao hawajui hata sera za kiuchumi za nchi zikoje ama hata mpangilio wa kidunia ukoje (World Order). Ni katika mtizamo wa aina hii hata hizi kashfa kama za Richmond, EPA – BoT na zingine nyingi zimetufikisha hapa tulipo leo bila kuhojiwa huko Bungeni. Ni wazi wabunge wengi wa viti maalum ni mzigo kwa walipa kodi wa nchi hii.

Tufike pahali tukomeshe huu mfumo wa uwakilishi wa viti maalum. Ikibidi tuige nchi kama Uganda kwa mfano, wabunge wanawake wote ni lazima wagombee na wapigiwe kura na wananchi na si kama hapa kwetu ambapo mara nyingi njia chafu kama rushwa za kila aina mara nyingine hata za ngono zinatumika miongoni mwa vigogo wa vyama vya siasa ili mabibi warembo fulani wawe wabunge. Pia hata Kenya hivi majuzi tumeona ni jinsi gani wanawake wamejikakamua kuhakikisha wanagombea na wanaume na kushindana kwa hoja badala ya kusubiri kuhonga kamati za chama / vyama ili vikupitishe kupitia vitandani na hongo nyingine nyingi za kila aina hasa za aibu.

Nne, tukiacha mambo ya mustakabali wa nchi yetu kisiasa, pia kifamilia tayari tujiulize mambo kadhaa: mojawapo ni hili la wanawake kujikomboa katika mtizamo wa kujilinganisha na wanaume ukiachilia mbali tofauti za kimaumbile (anatomy) na hata kimajukumu (roles). Katika hili kundi (radical feminists) naliona kama hatari sana katika Tanzania ya leo. Hawa ni wale wanawake wasomi kabisa na kwa mantiki hiyo ubinafsi umewajaa kwa kiwango kikubwa (highest ego) na matokeo yake hawawezi kudumu katika ndoa ama hata kama wanadumu wanaishi katika ndoa zilizofeli (failed marriages). Hawa ndio walioshindwa kuwa mifano bora kwa jamii; na wengi wana nafasi kubwa katika jamii wakibadilisha wanaume – vigogo kama njugu ili kuhakikisha wanaishi raha mustarehe. Wengi wao wanaishi wakiwa wamechanganyikiwa (frustrated).

Nimalizie kwa kumbushia nasaha za wanafalsafa wawili: mmoja ni Jeremy Benthamy, ambaye alikataa kata kata kuwa hatambui nafasi yeyote ya mwanamke katika jamii. Alisema: “Wife should submit to husband”, yaani mke shuruti awe chini ya utawala wa mume. Wako wanawake wengi ambao bado wana hisia za bwana huyu na ndio maana wamewafanya wanaume ni miradi yao. Mwanafalsafa wa pili ni John Stuart Mills, yeye anajulikana kama “Male feminist” yaani mwanaume – mke. Alipinga mwanamke kunyanyaswa kabisa. Alishawishi sana kwa wanawake kuruhusiwa kupiga kura nchini Uingereza wakati wa maisha yake. Tunaweza kurejea pale alipoandika juu ya mke wake – Harriet Taylor.

Basi siku hii ya leo itufanye hasa kwa wale wanawake kufuata mawazo ya wanafalsafa hawa wawili kwa kuchagua mmoja. Kazi kwenu sijui mtachagua yupi kwani tukikosea tuataendelea kuishi maisha yaliyojaa hisia na imani potofu za kijinsia (stereotypes). Tufike pahali wanawake waamue kikwelikweli na si kimzaha mzaha kushiriki katika nyanja mbalimbali za maisha nchini Tanzania na kuachana na kuishi kwa unafiki ilimradi wanapata upendeleo kuwawezesha kupata mkate wa kila siku. Nashangazwa sana hadi leo bado wanawake wengi sana nchini mwetu na Afrika kwa ujumla wako tayari kujidhalilisha ilimradi wapate vyeo, upendeleo, na raha za kila aina kutoka kwa wanaume.

Ni katika mtizamo huu; bado wanawake wa Tanzania bado wako kizani hasa kama wanafikiri wameshajikomboa. Manake hata wengi wa wanaharakati si mfano bora kimaadili linapokuja swali la mahusiano bora ya kijinsia. Tujiulize je siku ya wanawake imetusaidia kubadili mwelekeo wetu? Au ni usanii kama kawaida?

Wednesday, February 27, 2008

ZIARA YA BUSH—NA UFISADI WA FIKRA ZETU

Mwezi wa februari utabakia wa kukumbukwa kwangu binafsi kwa matukio kadhaa ya kukumbukwa. Kwanza, tarehe ya pili tu nilimpoteza bibi yangu, Emilia aliyefariki akiwa na umri wa miaka tisini na sita (96). Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Tarehe saba wakati nikiwa nimesimama pembeni ya jeneza la bibi siku ya mazishi, ndugu yangu mmoja ananiuma sikio kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa amejiuzulu.

Ukiacha hayo mawili, lingine ambalo kwangu naliona la kukumbuka ni ziara ya Rais George Bush nchini Tanzania. Imenishangaza sana huyu bwana kapata mapokezi makubwa sana barani Afrika kitu ambacho ni tofauti katika mabara mengine ambapo anachukiwa sana. Kwangu nadhani ina mafunzo mengi sana kwetu kama wananchi na hasa kwa viongozi wetu. Labda niseme pia siungi mkono hata kidogo kelele na pingamizi nyingi ambazo zilioneshwa na baadhi ya watanzania—waislamu wachache na jumuiya ya wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Nasema hivi kwani siamini kabisa kuwa rais Bush anazo sera zake binafsi ila kila kinachofanywa na serikali ya Bush ni matokeo ya sera ya nje ya serikali ya Marekani ikihanikizwa na imani za kihafidhina za Chama cha Republican.

Tatu, sijui kama Magaidi wasingeivamia Marekani September kumi na moja kama kweli leo majeshi ya Marekani yangekuwa Iraq na Afghanistan. Lakini pia sijui kama kweli kuna njia gani ya mazungumzo ingetumika kuleta mabadiliko ya kiutawala ya kidhalimu chini ya Matalebani ama Saddam Hussein. Si kura hata kidogo ingeumaliza udikteta wa Saddam ila kujitoa mhanga wa maisha ya watu—yaani damu kumwagika ili kuleta mabadiliko kutoka mfumo dhalimu. Kama hatutaki kuamini hivyo, basi tuangalie Kenya kama itatulia iwapo Kibaki atakuwa rais kwa miaka mitano ijayo. Kuna nyakati vita haiepukiki ili kuleta mabadiliko kwani hata nchi yetu ilibidi ipigane vita kumng’oa Iddi Amin ili kuung’oa udikteta wa Amin Uganda.

Kwa kuzingatia mwelekeo wa uchumi wa kileo duniani, na hata kihistoria, Taifa kubwa limejiimarisha kwa njia nyingi mojawapo ikiwa ni vita. Hivyo basi, Bush si wa kwanza kuendesha vita. Hata Nyerere aliendesha vita kwa maslahi ya nchi yake (Tanzania) kitu ambacho anafanya Bush. Hivyo basi, kumkataa Bush asitembelee nchi yetu si hoja yenye mashiko sana kiuhalisia leo hii; kwani kama asingekuja na hata alivyokuja, hakuna kitu amepoteza. Nguvu ya kujieneza ya Taifa kubwa kama Marekani haizuiliki; hivyo basi kimtizamo kelele za pale Mlimani zilikuwa zimejaa mantiki ya kitaaluma ambayo kwangu sina hoja kupinga uhalali wake kimaadili na katika suala zima la uadilifu unaotakikana kwa mwanadamu.

Lakini katika hali halisi ya dunia si hoja muafaka manake inaonekana maisha ya mwanadamu na mtanzania wa leo yamejaa matendo mengi ambayo si ya kimaadili lakini ndiyo yamefanywa haswa kama utamaduni. Hata Raisi Kikwete alimwambia Bush kuwa kwetu watanzania hatuana shida nae japo zipo serikali nyingine ambazo zina mitizamo tofauti na sera zake.

Kwa maana nyingine mtanzania anaongozwa na mbinu nyingi za kifisadi kufikia malengo yake; na ndio maana ziara ya Bush ilikuwa ya mapokezi mazuri sana sidhani kama amewahi kufanyiwa hivyo ugenini hata siku moja. Tanzania ni Taifa linalojiendesha kifisadi fisadi sana na ndio maana ni wananchi wachache sana waliokuwa na muda wa kutafakari hoja za wasomi wetu kule Mlimani. Watanzania na serikali yao hawajali jambo fulani linapatikana kwa njia gani ilimradi tu lina tija katika kutatua matatizo yao. Ni nchi ambayo kama kweli una elimu yako nzuri na ya juu kama vile Dr. Msabaha alivyofanya kwenye skandali ya Richmond, lazima uachane na kile unachokiamini ndio sahihi na ufuate matakwa ya utawala. Labda nieleze ni kwanini watanzania na serikali yao hawakuona haja ya kusikiliza busara za kisomi:

Moja, ziara hii imetoa msaada mkubwa kwa nchi yetu katika sekta ya afya na miundombinu. Japo nina mashaka na mafisadi hawataziacha salama, ila ni kielelezo kuwa Bush ana nia njema na nchi yetu. Na katika kutia shime vita dhidi ya ufisadi, Bush alisema baada ya kusaini mkataba kuwa fedha za Marekani si kwa mafisadi. Na kusisitiza kuwa moja ya masharti ya Mfuko wa Millenia ni serikali yetu kuzingatia “Utawala Bora”, vita dhidi ya ufisadi na kwa ujumla serikali inayojali watu wake.

Pili, ziara hii imeonesha ni jinsi gani Raisi Bush na mkewe walivyo watu wa kujitolea (compassionate)hata huruma ya kujali watu wa kawaida. Kwa viongozi wetu wamejifunza ni jinsi gani wanapaswa kuishi na kujichanganya na watu hohehahe kama walivyo watanzania wengi. Viongozi wetu wengi wa Afrika, kwa mfano, si rahisi mtu atembelee hospitali na umwone akikumbatiana na kukaa karibu kabisa kwa kujichanganya na wagonjwa. Hili Bush katoa funzo; nilitegemea kule hospitali ya Mount Meru nione makachero wakiwa karibu na Raisi wakimwongoza wapi apite na ashikane na nani mkono au hata kuwazuia watu wasimkaribie bwana mkubwa. Hili sikuliona ila niliona Raisi Bush akijiweka sawa na binadamu wengine na kukaa hata karibu nao kabisa, wala si kwenye kiti maalum bali viti vya kawaida wanavyokalia wagonjwa kwenye foleni. Wakubwa wetu watataka sofa maalum tofauti na walalahoi.

Kimavazi pia imekuwa ni funzo kwa viongozi na vigogo wetu. Unakwenda kuwatembelea watu masikini ni lazima angalau ufanane nao. Kwa Bush hili alilizingatia hasa na wala sikuona akiwa ndani ya suti, siku ile yenye joto ambalo lingemfanya achemke kwa joto na aogope kujichanganya. Nadhani ndio maana kulikuwa hamna haja ya wanausalama kumzuia kuwa karibu na watu kwani vigogo wetu inabidi makachero kuzuia watu ili bwana mkubwa apate hewa kwani mara nyingi unakuta watu wamevaa misuti. Hapa katukumbusha mavazi rahisi (simplistic). Hili nalo ni funzo gumu kwa vigogo wa kiafrika kulimeza.

Wakati akiitembelea shule ya sekondari maalum kwa wasichana wa kimasai kutoka mazingira magumu alinigusa hasa. Labda niseme mwaka jana Raisi Jakaya Kikwete alifungua shule moja ya sekondari kule Moshi. Ilikuwa ni ziara ya saa moja kufungua shule rasmi; na mara alipowasili pale shuleni si walimu wala wanafunzi waliopata muda wa kumfariji na kumpokea rais wao. Kilichotokea nilishangaa kuona makada kibao wa CCM pamoja na vigogo wa serikali kutoka mkoani na wilaya za jirani wakihangaika kugombania kujipanga mstari ili tu kushikana mkono na bwana mkubwa. Walimu waliokuwa wamejipanga sehemu maalum walifunikwa na wala hawakuweza kupata nafasi hiyo. Wala raisi hakuwa na muda wa kusalimiana ama kuzungumza sana na wanafunzi zaidi ya kupiga kejeli za kisiasa katika hotuba yake. Nadhani angeteta na wanafunzi kadhaa na kusikia hisia zao ingependeza zaidi.

Lakini kwa Bush tumeoneshwa nini maana ya kuwa kiongozi na nini cha kujali wakati unapotembelea sehemu. Raisi Bush alisalimiana na watoto wote wa shule ile pale Arusha; pia alisalimiana na hata kucheza ngoma na wamasai waliokuwa wakiburudisha ikiwa ni pamoja na kuwakumbatia baadhi yao. Hapa kwetu na Afrika kwa ujumla sivyo inavyokuwa, wanausalama hawaruhusu hili kabisa. Hivi huwa najiuliza kila Rais wetu anapokuwa mahali utaona mlinzi wake/ msaidizi wake kasimama nyuma. Hivi hiyo ndio kumaanisha ulinzi wa rais ni imara? Mbona watu kama akina Bush si hivyo na ulinzi ni imara? Nadhani ziara hii iwe mwanzo wa kuiga jambo kwa wanausalama na kwa ujumla wale watu wa karibu wa bwana mkubwa.

Labda niungane na waziri Dr. Jumanne Maghembe aliponukuliwa na ITV katika ziara ya Bush kule Arusha: “Marekani ni Taifa kubwa na tajiri na lina fursa nyingi. Ni vizuri tukashirikiana nayo na kudumisha urafiki na udugu na Taifa hili”. Nikiwarudia wale walionesha kutokutaka ziara hii: Hasa wasomi wa Mlimani, wajameni hivi tunajua kuwa wahenga waliwahi kusema kwa kiingereza tafsiri isiyo rasmi: “Every black has its white”, kuwa kila cheusi kina weupe wake pia”. Hapa namaanisha pamoja na uovu na unyama unaoambatanishwa na haiba ya Raisi George Bush, huyu ni mwanadamu mwenye pande mbili. Na kwa kutilia mkazo kwenu mabaya yake naamini mlighafilika tu; na mashiko ya kihisia yalitawala zaidi ya busara, mbona hamkutizama upande wa pili wa Bush?. La sivyo wala msingefikia hatua hiyo ya kutaka kuandamana.

Ziara ya Bush imetuonesha upande wa pili Bush mwanadamu. Mpaka kaondoka sijasikia akiongelea habari za Africom kama wasomi wetu walivyokazia kuwa anatafuta mahali pa kujenga kambi za kijeshi. Pia nadhani kilio chenu kingine kuwa kumkaribisha Bush ni kuonesha serikali yetu imeamua kuacha marafiki wa zamani na kufuata mabepari kama hatua isiyo muafaka si sahihi. Tumefuata sera za marafiki zetu kama Cuba, China na wengine wengi kwa miongo minne kwa mafanikio sana ya kiuchumi. Dunia ya leo tusiogope sana juu ya hali ya baadaye ila tutumie fursa zinazojitokeza hasa kama zina mwelekeo wa kukuza uchumi wetu.

Tukiwa bado tuna marafiki zetu wa zamani hakuna ubaya kama tunaongeza mwingine bila kuwapoteza wa zamani. Hii ndio hisia ninayoipata kwa ugeni wa Bush. Ziara hii kupitia mkataba wa Millenium Challenge naamini ni fursa ambayo tusingepaswa tuiache kwani ina tija sana hasa kama “mafisadi” watadhibitiwa wasiweke pua zao hapa. Tukumbuke hata jirani yetu Yoweri Museveni alikuwa na uswahiba na Bush na hata enzi za Clinton na kwa sasa wamemtupa kiana na kwa kipindi chote Uganda haikuwahi kuathiriwa kijeshi na Marekani ingawa kwa sasa kuna makampuni kibao ya Marekani yakianza kuchimba mafuta nchini humo.

Funzo lingine la ziara ya Bush kwangu ni pale kung’amua kuwa kweli nchi yetu ni masikini sana. Yaani bado hatuna uwezo wa kujikinga na Malaria? Yaani Bush anatununulia chandarua watanzania? Yaani watanzania walio wengi hawana uwezo wa kununua chandarua? Kwa maana nyingine watanzania wengi tu wachafu hatuwezi kuishi kwenye mazingira safi yasiyoruhusu mbu kuzaliana. Hatujui wajibu wa kiafya kusafisha mazingira yetu ili kuondoa mazalia ya mbu. Ni aibu lakini tufanyeje? Mpaka aje Bush atununulie chandarua. Hili linanipa shida sana kwani nadhani fedha ya malaria ni nyingi na ingefaa itumike kwenye sekta kama ya elimu. Sidhani kama unamzuia mtu asiugue malaria lakini hapo hapo humpi elimu bora kama unamsaidia sana. Bado umasikini hautoki kwa njia hii.

Ukimwi pia ingawa ni janga ambalo binafsi limeniathiri sana; ila ni wakati tujiulize kuwa hivi kama tukiweza kujihadhari na maambukizi, hizi fedha zote za Bush si zingefanya mambo mengine? Napata mashaka sana kama tunaendelea kupata ufadhili hasa wa kurefusha maisha na kwa wakati huo huo hatuna utaratibu wa kuwalinda wale ambao hawajaambukizwa ambao kwa kujichanganya kwao na waathirika wengi ni hatari.Ni wazi waathirika Fulani wana hasira sana na lengo lao kubwa ni kuondoka na wengine. Sisemi hili kwa kunyanyapaa ila ni lazima tufike mahali tujiulize hii misaada mikubwa ya kulinda maisha ya waathirika ina matokeo mazuri? Ni kwa vipi tuifanye tuwe na mazingira mapya kiutaratibu wa maisha ili tupate tija. La sivyo Taifa zima litaangamia na mamilioni ya dola za Bush.

Mwisho, nimalizie kama nilivyoanza: wakati nikiwa pale pembeni ya jeneza la bibi yangu baada tu ya kunong’onezwa na ndugu yangu kuwa Waziri Mkuu kajiuzulu, mara moja nilichoropoka nikaingia ndani nikafungua kiredio changu kidogo, radio sauti ya Ujerumani na nikakutana na sauti yake ikisema: Nimefadhaishwa, nimesononeshwa, …..mengine nimeyasahau manake yalinishangaza kwanini sasa kaamua kujiuzulu. Taifa linapotekwa nyara na mafisadi mtu hushangai pale hata busara za wasomi kama wale wa pale Mlimani zinapoonekana ni kejeli.

Nilisikitika tu pale jeshi la polisi lilipokataa kiaina kutoa ulinzi kwa maandamano ya wasomi wa mlimani kupinga ziara ya Bush. Ingawa sikuwa naunga mkono hoja zao, nadhani walinyimwa haki yao ya msingi kuandamana kupinga ujio wa Bush. Kweli February sitaisahau kama wakati muafaka wa mapinduzi ambayo sina imani sana kama yatabadilisha mwelekeo wa Taifa letu dhidi ya ufisadi. Hii ni nchi inaathiriwa na tabia na hulka ya kubebana, kupendeleana na utapeli wa kila aina. Na ndio maana baada ya Raisi kukabidhiwa ripoti ya Ernst & Young iliyokwishagundua kila ufisadi ndani ya BoT bado anaunda kamati nyingine ya uchunguzi. Lengo ni kulindana tu. Nimeshangazwa pia na mtuhumiwa mmojawapo wa ufisadi karudi kwa wapiga kura wake na kupokewa kwa shangwe na hata kupewa baraka za Askofu wa kanisa lake. Kweli kwa Tanzania ya leo bila ufisadi labda maisha ya wengi yatasimama.

Wednesday, January 30, 2008

KIIZA BESIGYE NA MWAKA 2008

Kiiza Besyige anajulikana sana Uganda. Leo bado ni mwiba mkubwa kwa jeshi la uganda na anadai analijua wazi. Hivi tunajua ilimbidi amwache rafiki wake wa kike ili kujiunga na Museveni msituni na kuacha fani ya udaktari?
Kama unataka kujua madhara ya kupingana na Museveni, basi ona haya yaliyowakumba hawa waliojaribu.

MLIMA KILIMANJARO



Hii ndio Moshi, unauona mlima Kilimanjaro? Wanadai eti karibu theluji yake itakwisha. Ndivyo unavyoonekana leo hii.

Saturday, January 26, 2008

NIKIWA NGORONGORO NASHINO PAKI



Hapa nimesimama katika lango kuu la kuingilia Mbuga ya Ngorongoro.Mara nyingine hata mie natembea kidogo kama akina Majjid.Ilikuwa novemba mwaka jana.

NIKIWA SERENGETI

Hapa niko na wanafunzi wa BENDEL SECONDARY, huko mbuga za Serengeti november mwaka jana katika ziara ya mafunzo.

Friday, January 25, 2008

ODM INAWEZEKANA WAMEPOTEA NJIA KUANDAMANA

Raila Odinga na vigogo wenzake wa chama cha upinzani wamejaribu wiki iliyopita kuitisha maandamano mfulilizo katika juhudi za kutaka kumng’oa madarakani Raisi anayesemekana hakuchaguliwa kihalali—Mwai Emilio Stanley Kibaki. Muungano wa harakati za chama cha Chungwa (ODM) unajaribu kuiga yale maandamano ya wafuasi wa harakati za Chungwa kule Ukraine mwaka 2004 ambayo yalifanikiwa kuiondoa serikali batili madarakani baada ya kuiba kura.

Pamoja na juhudi hizi bado haionekani kama itawezekana kwani nadhani kuna sababu za msingi ambazo kwa wanaharakati hata wa hapa nchini hatuna budi tuzing’amue:

Kwanza kabisa, ODM inakosa kuungwa mkono katika maandamano na tabaka la juu pamoja na lile la kati. Hawa ni wale watu wanaojihusisha na biashara kubwa na za kati pamoja na wengine wengi ambao ni wafanyakazi katika serikali (Civil Servants) pamoja na sekta binafsi. Hawa ni watu wanaojiweza ambao kimtizamo wanaunga mkono ODM lakini kivitendo haiwezekani kabisa hata siku moja kujitokeza mitaani na kushiriki maandamano mitaani. Sana sana wanachofanya ni kuchanga fedha kuunga mkono waandamanaji kwa chakula, vinywaji na hata matibabu kwa wale wanaoumia. Wanafanya hivi kwani wanalinda mali na hata ajira zao nono zisipotee pale watakapogundulika wanaunga mkono upinzani.

Pili, ni raia masikini waishio kwenye mitaa ya mabanda (slums): Tofauti na tabaka la kati na matajiri, wakazi wa mitaa ya mabanda (slums) ambao ni masikini kila kukicha; hawana cha kupoteza ila wanabaki wakiamini labda ODM ikichukua madaraka wanaweza kubadili hali zao za maisha kitu ambacho ni vigumu kubashiri kama kitatokea. Tabaka hili la raia ndio wanaoandamana kila kukicha katika nchi nyingi za Afrika zilizojaa udikteta wa kila aina. Masikini ni vijana ambao wengi wao hawana elimu bora; wengine miongoni mwao wana elimu lakini kwasababu hawana ndugu (God fathers) ndani ya serikali ama hata ndani ya sekta binafsi basi ajira kwao ni ndoto.

Wamechanganyikiwa na kila ahadi kwao ni lazima waiamini hasa inapotolewa na wanasiasa mbadala kama Raila Amolo Odinga. Hili ni kundi kubwa katika miji ya Kenya kama Nairobi, Eldoret, Kisumu na Mombasa. Inakadiriwa ni nusu ya wakazi wa miji hii; lakini zaidi ya robo iliyobakia ni tabaka la kati na la juu na hawapo tayari kuhatarisha maisha yao kuingia mitaani kuunga mkono maandamano dhidi ya serikali batili. Wanachofanya hawa wanaojiweza ingawa hawaridhiki na serikali batili ni kukaa majumbani mwao wakiangalia runinga zao ni jinsi gani polisi wanavyopambana na waandamanaji; pia ni hawa wanaoandika sana barua kwa wahariri wa magazeti na hata kupiga simu redioni kushutumu serikali batili. Kamwe hawatashiriki maandamano au hatua yeyote ya harakati kivitendo ndani ya uwanja wa mapambano. Na ndio hapa Kibaki inawezekana kabisa akawa Raisi hadi miaka mingine mitano.

Kama tabaka la kati na la juu lingeshiriki maandamano haya basi ndani ya siku tatu polisi wa Kenya wasingeweza kuzuia waandamanaji kwani wangekuwa wengi sana hasa ukizingatia muundo wa miji ulivyo. Ila kwasababu maandamano yanatarajiwa yaanzishwe na masikini wa mitaa ya mabanda; na kwa mipango miji ilivyo, mitaa ya mabanda iko mbali na miji ama katikati ya miji (central business street) basi inakuwa ni rahisi kwa askari kwenda huko nje ya jiji na kuwazuia kuingia mijini. Wanafanya haya wakati wamewaacha matajiri na watu wa tabaka la kati wakiwa wamejifungia ndani ya nyumba zao zilizo mijini. Ni wazi kama watu wote wa tabaka zote wangejitokeza basi polisi watapata shida sana kuwazuia kwani itakuwa vigumu ukizingati kila kona ya jiji itabidi iwekewe ulinzi kitu ambacho si rahisi kwa askari kuhimili wingi wa watu kutoka kila upande.

Ingawa polisi wanaweza kuamua kuua kwa risasi za moto lakini kama watu wote niliotaja wataingia mitaani si rahisi kwa serikali ya Kibaki kuamrisha polisi kuua (shoot to kill) manake shinikizo la jumuiya ya kimataifa halitawaacha salama. Na ndio maana hadi sasa siku ya pili ya maandamano, silaha kuu ya polisi imekuwa ni maji yenye presha kali (water canon) katika kupambana na waandamanaji. Pia serikali haitakuwa na utashi na thubutu ya kuua wafanyakazi (Civil Servants) wake yenyewe ambao wengi wao ni kundi la tabaka la kati.

Kinachokwaza harakati ni kuwa tabaka la kati (middle class) hawana mwamko na uthubutu wa kushiriki maandamano wala harakati za mapinduzi moja kwa moja. Hawako tayari kupoteza kazi zao zenye malipo mazuri, mali zao kama nyumba zingine labda wamekopeshwa na serikali; pia la msingi kwao laweza kuwa ni wasiwasi kuwapoteza wapendwa wao: waume na wake zao wazuri pamoja na watoto wao wenye afya nzuri.

JE MAPINDUZI YATOKEE WAPI?

Naamini kama kweli ODM itafanikiwa basi ni kutokana na jitihada za masikini wa kutupwa (makabwela) ambao hawana cha kupoteza kama vile vibanda vyao vilivyojengwa kwa maboksi pamoja na wake zao wasiotamanisha na hata watoto wao wengi wao wenye utapiamlo. Inawezekana hatimaye wakafanikiwa; ila kama Raila atafanikiwa kumlazimisha Kibaki ampishe basi mshangao mkubwa utawakumba walalahoi wanaoandamana leo hii:

Mosi, lile tabaka la kati pamoja na matajiri wachache ambao ni waoga na wamejichimbia ndani sasa hivi wakitizama televisheni zao jinsi makabwela wakipambana na polisi ndio watakuwa wa kwanza kujitokeza na kupangiwa nyadhifa kadhaa na serikali mpya ya Raila kama itatukia. Hii itakuwa ni katika kuthibitisha maneno ya biblia takatifu: “Aliyenacho ataongezewa na asiyenacho atanyang’wanywa kabisa”.

Pili, kama mapinduzi hayatafanikiwa, tabaka la kati (middle class) hawajali sana kwani maisha yao yasiyo na kero nyingi yataendelea kama kawaida tena watajiona kama vile hakuna kilichotokea kwani wataendelea na kazi zao; mishahara yao minono na yenye ongezeko la asilimia 3% hadi 5% kila mwaka. Ni hawa hawa kila jioni baada ya saa za kazi wanajumuika kupata kinywaji wakijadili juu ya mapinduzi ambayo yatakuwa yamefeli.

Tatu, kwa upande wa masikini ambao tunawashuhudia wakipambana na polisi; iwapo harakati zitafeli basi wanajirudia vibandani mwao; maisha ya msoto yataendelea yaani kuamka alfajiri na kurudi majumbani usiku baada ya kazi za kitumwa kama vile: kazi za utarishi, ulinzi, utunzaji bustani za maua na pia kazi za viwandani ambazo zinazalisha asilimia tisini 90% ya uchumi wa nchi ilihali wao wanapata vipato vidogo na vya aibu sana.

Nne, pia ikiwa harakati za ODM zitashindwa basi wakati masikini wanateseka, matajiri pamoja na tabaka la kati wataendelea na maisha bila kujali; kwa kujiweka karibu na wanasiasa batili ambao wamewashinda masikini. Zaidi kila jioni watakutana katika sehemu za starehe kupiga soga na hata kucheza gofu.

Napenda pia tukae chini: lazima tujiulize hadi sasa kwanini ODM haijaweza kufanya maandamano licha ya nia yao ya dhati? Ukichukulia nini kilitokea kule Ukraine kama nilivyotaja awali, basi ni wazi jumuiya ya kimataifa haijaamua kuwaunga mkono. Kule Ukraine, Marekani iliwaunga mkono wanaharakati wa chungwa (Orange Revolution) kifedha kitu ambacho inaonekana Marekani inasita kwani pia haiamini kama kweli ODM ina jipya. Pia kule Ukraine, polisi walitambua kuwa nao pia ni sehemu ya tabaka dhalili dhidi ya ufisadi wa wanasiasa. Ila kwa Kenya na hata nchi nyingi za Afrika si polisi wala askari jeshi ambao wametambua hili: kuwa maisha magumu kwa baadhi yao yanachangiwa na serikali batili wanayoilinda kimabavu.

Kule Ukraine, polisi hawakupambana na waandamanaji hata kidogo kwani walitaka pia mabadiliko. Hapa Afrika hatujafika hatua hiyo na ndio maana nadhani ODM kufanikiwa kuiondoa serikali batili ni vigumu sana ingawa naamini juhudi zao zapaswa kuungwa mkono zaidi.

Tayari kuna tetesi kuwa kama hali ya maandamano itaendelea hivi, basi iko siku wanajeshi watapindua serikali ya kibaki na ndipo itakuwa mwanzo na mwisho wa kadhia hii. Ndio njia pekee ya kuanzisha upya mchakato mzima wa kuiepusha Kenya kuwa Taifa lililofeli (failed state). La sivyo yaliyowahi kutokea Liberia ama Ivory Coast yatatokea hapa. Na ndipo hapo wanasiasa wetu fedhuli na fisadi huku wakilindwa na vyombo vya usalama kwa kodi ya wananchi watang’amua kuwa raia wa kawaida anayo nguvu kubwa kuliko majeshi na bunduki zao.

TANZANIA IMETEKWA NYARA NA CCM

Miezi kadhaa imepita sasa baada ya mwanasaikolojia na mshindi wa nishani ya Nobel kuja na wazo lake kuwa “Waafrika ni dhaifu katika kufikiri ukiwalinganisha na wazungu ama watu wasio weusi”. Si mwingine bali ni daktari James Watson, mtaalam maarufu wa Saikolojia na mgunduzi wa sayansi ya chembe hai ( DNA) nchini Marekani na duniani kwa ujumla. Mawazo yake yalipokewa kwa machungu sana na watu weusi wengi kila kona ya dunia; lakini kwangu nilijaribu kuona hili kama changamoto hasa nikizingati mambo kadha wa kadha yanayotukia hapa nchini mwetu Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Naye David Landes kaja na kitabu chake “The Wealth and Poverty of Nations: Why Some are so Rich and Some are So Poor”, akijaribu kutuonesha kwanini waafrika wako nyuma ya wazungu kiuchumi. Tatizo ni utamaduni anadai kwani anasema wazi utamaduni wa mwafrika ni dhaifu ama ni wa kiwango cha chini sana ukiulinganisha na ule wa wazungu. Kwa mfano anadai utamaduni wa mwafrika unakosa vikolezo kama kufanya kazi kwa bidii (hard working), uaminifu (honest), uwazi (open mindedness), na utashi wa dhati katika demokrasia (commitment to democracy)

Landes anasisitiza pia maendeleo ya kiuchumi yanategemea sana hisia (attitudes) za wananchi wake hasa uwezo wao katika kutumia au kutokutumia sayansi na teknolojia na hata fursa za kiuchumi pindi zinapojitokeza. Ni wazi utamaduni una nafasi kubwa sana katika kuendelea ama kutoendelea kwa jamii Fulani. Kwa mfano, Wajapan wanaamini kuwa utamaduni wao ndio chanzo cha mafanikio yao tunayoyaona leo hii. Yoshihara Kunio, kwa mfano ameandika kuwa: “Sababu moja kuendelea kwa Japan ni kuwa ina utamaduni wa maendeleo”. Wajapan wameweka msisitizo katika utafutaji mali (material pursuit), kufanya kazi kwa bidii, kuweka akiba ya siku zijazo( serving for future), kuwekeza katika elimu na kujali jamii (community value).

Tukirejea kwa Landes, anatuonya kuwa kuna tamaduni fulani ambazo ni sumu na mtu akiziamini na kuziishi basi ni umasikini. Kwa mfano, utamaduni wa wazungu/ magharibi ni wa ubinafsi (individualistic) zaidi wakati ule wa kiafrika ni wa kijamii zaidi ama tunaweza kusema kiasili ni utamaduni wa kijamaa unaojali wengi katika migawanyiko ya aina mbalimbali hasa kikabila. Ni katika msingi huu naweza kusema kuwa nadhani ni wazi utamaduni wetu hasa watanzania ni wa kijamii ambao leo hii umehama kutoka ukabila hadi kufikia kikundi cha watu ama jamii kisiasa: namaanisha vyama vya siasa vinavyowakutanisha makabila mbalimbali yenye maslahi yao ikiwa ni pamoja na kuing’ata nchi yetu bila huruma.

Kwa mfano, watanzania na waafrika kwa ujumla wao wamekuwa wakiamini ni lazima watumikie maslahi ya makabila yao. Hali si Kenya tu ila hata hapa kwetu mambo ni hayo tu. Katika kutumikia maslahi ya kikabila ndipo kwa mfano watanzania tunajikuta tukijirudisha nyuma sana kimaendeleo. Utamaduni huu mara nyingi hauruhusu kukosoana hasa pale viongozi ama wakuu wa kaya ama makabila mbalimbali wanapokiuka taratibu za kijamii. Kwa kawaida, wakuu wa familia ama jamii za kiafrika mara nyingi hawaadhibiwi; hakuna mfumo wa udhibiti kwao. Hawa ni sawa na miungu watu wanaotenda visivyo bila kuadhibiwa (impunity).

Maadam waafrika na watanzania tuna kasumba ya kutumikia jamii ama makabila yetu zaidi, basi leo hii tabia hii imejipenyeza hadi katika sehemu za kazi. Angalia hata siasa zetu sasa zimegeuka kuwa ni watu ndani ya vyama mbalimbali kama kikundi kwa maslahi yao na wala si maslahi ya pamoja (common interests) kama ilivyo Japan. Ni katika hili ambapo suala “uzalendo” limekufa na sasa ni maslahi ya kivikundi. Kwa mfano, unaposikia Taifa linakumbwa na upotevu wa fedha nyingi alafu serikali kuanzia Raisi hadi mawaziri wanashindwa kuweka mambo wazi juu ya wapi Gavana Ballali anakotibiwa, basi mtu unapata picha ni jinsi gani serikali ya CCM haiko tayari kuwa wazi kwa suala hili.

Hii yote ni kuonesha jinsi gani utamaduni wa kutoadhibu ama kutowajibisha wakuu wa kaya ama makabila ya kiafrika unavyoitafuna nchi yetu. Ni utamaduni wa karne kadhaa zilizopita ambao CCM inahakikisha utadumishwa ili watu fulani waitafune nchi yetu kwa maslahi yao na chama chao. Ukienda Bungeni na jinsi ambavyo hadi leo hii tangu kashfa ya BOT iibuliwe hakuna mbunge wa CCM aliyethubutu kusema jambo kuonesha kukerwa na hili. Nasubiri nione jinsi watakavyojiuma huko bungeni kuanzia wiki ijayo watakapokuwa wanachambua uchunguzi wa ripoti ya uchunguzi wa kashfa ya Richmond.

Tuna tatizo kubwa kitaifa: yaani mentalite (fikra) za viongozi wengi wa Tanzania ni mzigo mkubwa kwa Taifa. Kizazi cha uongozi cha sasa ni balaa kubwa sana kwa taifa hili kwani hawana tofauti sana na mababu zetu zamani enzi za ukoloni ambao hawakujua kufikiri kwa dhati. Naamini kama Rais Kikwete atatawala kwa miaka kumi basi utakuwa ndio mwisho wa mawazo mgando. Siku za kizazi cha mawazo mgando zinahesabika; kizazi kipya cha sasa chenye mawazo ya kisasa ya kuivusha nchi kutoka umasikini kinakuja taratibu. Ni kizazi ambacho kinawaza zaidi “utaifa” na si maslahi binafsi kama akina Balali na wenzake ambao wanajifanya wametengua uteuzi wake ilihali wengi wao ndio chanzo cha madudu aliyoyafanya.

Ninasema haya kwani hata yaliyotukia Kenya situ ni ukabila bali ni utamaduni huu wa watu katika vikundi vyao vya kikabila na kisiasa wanang’ang’ania madaraka ili kulinda maslahi yao. Chunguza kashfa kubwa kama Goldernberg alafu kama unalijua kundi la “ Mount Kenyan Mafians” ujiulize kwanini Kibaki anang’ang’ania madaraka? Ni hii tabia ya makundi fulani ya viongozi wetu ambao wataiibia nchi huku wakilindwa na wabunge wa chama chao dhidi ya ufisadi wao; kwani kwao bunge ni muhuri (rubber stump) wa kupitisha uchafu wao kwa maslahi yao. Ni tabia kama hii naiona ndani ya CCM ambapo ‘kupitia wingi wa wabunge wao ni wazi Tanzania imetekwa nyara na CCM’.

Kama kweli CCM kingekuwa ni chama cha kuiendeleza nchi yetu basi leo hii hizi kashfa za BOT, Richmond, Buzwagi zisingechukua muda na kutumia muda mrefu bila wahusika kuchukuliwa hatua za kuwajibishwa namna tuonavyo leo. Chama chochote kinapokubali kutumika kama muhuri wa kupitisha wizi na utapeli wa baadhi ya watawala basi ujue ni kwa ajili ya utamaduni mbovu wa kiafrika umekimeza.

Na kwa maana nyingine ni kuwa uwezo wa kufikiri wa wengi walioshikilia hatamu za chama hicho ni mdogo kama alivyosema daktari Watson anavyomwona mwafrika. Jamii kama hii haishangazi hata kidogo sera za kishikaji zinawekwa mbele sana; na jamii hii kufikia maendeleo ya kweli ni vigumu sana ukiacha maendeleo ya wachache wenye mashiko ya kikabila, dini, rangi na kisiasa hasa ukada wa chama. Ni kwa msingi huu naiona Tanzania, nchi yangu kama Taifa lililotekwa nyara na kikundi cha watu Fulani wachache lakini wanaoungwa mkono na watu wenye wajibu wa kuwawajibisha lakini hawataki. Hawa ni wabunge fulani ambao ama kwa makusudi kabisa ama kwa ufinyu wa kufikiri kama ule aliouelezea Dr. Watson basi wanaamua kuhakikisha Mafioso wa Tanzania wanashamiri.

Ni wazi CCM ndio pekee kwa uwingi wa wabunge wao wakiamua wataisafisha nchi yetu na kupambana na mafisadi wa Taifa hili. Mafisadi wengi wa nchi hii ni wanachama wa chama hicho; na ndio hapa pagumu kutegua kitendawili. Mungu wangu: mara nyingine mtu unajuta kuzaliwa katika Taifa lisilopenda kufikirisha bongo ilihali likijiita eti ni Bongo land.

Tuesday, January 15, 2008

MKASA WA BALALI--WASOMI WANAPOCHEZA NGOMA YA WANASIASA

Balali kafukuzwa kazi na Raisi Jakaya Kikwete; ni habari ambayo ilinishangaza manake tayari nilikuwa najua alikuwa ameshaandika barua ya kujiuzulu lakini inasemekana rais akamkatalia. Mimi nilidhani alimkatalia kwa kuwa ni msafi sana; na, hata ile tu kutuhumiwa katika ile listi ya aibu (list of shame) ya mtanzania makini na mzalendo wa hali ya juu, daktari Wilbroad Slaa, kuwa yeye ni kati ya mafisadi wa Taifa letu naamini ilitosha kwa mtu mwenye akili timamu kukaa kando achunguzwe ili asafishwe.

Balali pamoja na vigogo wengine waliziba masikio na kutufanya tumwone Dr Slaa kama vile ni msanii tu. Nchi yetu sasa inadhihirisha kuwa imekumbwa na ugonjwa mbaya sana wa kimaadili. Nakumbuka baadhi ya watuhumiwa wa listi ile ya aibu walitishia kwenda mahakamani lakini hadi leo wamekaa kimya na hata hawajathubutu kujiuzulu angalau. Yaani angalau wangeandika barua angalau basi wakataliwe tujue raisi ana imani na mafisadi.

Leo nataka nizungumzie suala la uwajibikaji; yaani mtu akichafuliwa asiendelee kukalia madaraka bali ajiuzulu ili aruhusu kusafishwa au awapishe wengine ambao wataweza kuendeleza nchi yetu kwa uadilifu. Labda nikumbushie tu hali tete kama hii ambayo ilijitokeza kule Ghana mara tu raisi John Kuffour alipoingia madarakani. Waziri wake mmoja wa mawasiliano na uchukuzi, ndugu Richard Anane, alituhumiwa kufuja fedha chini ya wizara yake. Ilipoundwa tume ya uchunguzi iligundulika ni kweli zaidi ya dola laki moja ziliibwa na mara moja akafukuzwa kazi. Nchini Uganda mawaziri wawili wa afya, Waziri Jim Muhwezi na naibu waziri, Mike Mukula waliamua kung’ang’ania madarakani licha ya tuhuma nzito za ufujaji wa fedha za Global Fund. Ilipoundwa tume baada ya shinikizo la vyombo vya habari, tume ilipendekeza wafunguliwe mashtaka mahakamani. Kesi yao bado inaendelea hadi leo.

Ni wazi kashfa inapoibuliwa kuna ukweli na ni vyema tujenge utaratibu wa kujiuzulu ili kuruhusu uchunguzi. Na kama hatufanyi hivyo ina maana kazi za umma zimegeuzwa kama za kifalme; yaani mtu hadi afe. Sasa yaliyomkuta Balali ndio kuanguka kwa mfalme.

Nimetoa mifano miwili kuonesha jinsi baadhi ya nchi za Afrika zinavyozingatia vita juu ya ufisadi. Hapa kwetu hata pale madai makubwa yanapotolewa bungeni,haindwi hata tume ya bunge na yanabezwa. Bado najiuliza ni kwanini tufanye uchunguzi kwa kutegemea kampuni za nje ilihali kamati ya bunge ama ya raisi ingeweza pia kuchunguza hili? Nina mashaka sana kama kweli jeshi la polisi, mwanasheria mkuu na hata Takukuru kama kweli wana utashi wa kimaadili (moral authority) kuweza kuchukua hatua kwa wahusika wa dhahama hili. Watanzania hatuna utamaduni wa kuwashughulikia watu wazito hasa wenye fedha na vigogo serikalini. Huu ni ugonjwa wa kitaifa na ndipo hapa nadhani Balali kaenda na maji kilichobaki baada ya miezi sita sidhani kama tutawajua zaidi waliohusika na sidhani kama kutakuwa na hatua kali zozote. Tanzania imejaa vigogo wasioshikika (untouchables) na sidhani kama tuna watu mashujaa kuwashughulikia mafisadi. Manake kama si utamaduni huu basi tangu wizi huu uanze ungekuta idara nilizozitaja zimeshughulikia lakini wapi.

Mara kwa mara nagusia sana juu ya “utawala bora”: serikali haieshimu sana taasisi zake (institutions) katika utendaji ila tunaamini zaidi katika watu (people). Unafikiri Balali angethubutu kuweka kapuni maadili ya utendaji ya gavana na aamue kuruhusu maamuzi ya watu binafsi yatawale utendaji wa Bot? Ni wazi gavana hawezi kufanya hasara kubwa hivyo kwa nchi kama kweli baadhi ya watu wa ngazi za juu hawashiriki katika maamuzi hayo. Ndio maana tumesikia eti baadhi ya fedha hizo zilitolewa kufanya “malipo nyeti”.

Serikali zetu za kiafrika zinaegemea zaidi katika utashi ama uswahiba unaozingatia mashiko ya kisiasa; yaani watendaji wetu pamoja na taaluma zao lakini wanacheza ngoma za wanasiasa. (pandering to the whims of politicians). Hii kwa kiasi kikubwa inasababishwa na mhimili mmoja wa serikali umekufa. Bunge letu, niliwahi kusema inawezekana kabisa ni Jumba la Sanaa la Taifa (National Theatre). Manake tukumbuke wakati madai haya yalitolewa bungeni yalibezwa sana kitu kilichowafanya wapinzani waamue kupeleka hasira zao kwa wananchi katika mikutano ya hadhara.

Bunge letu limedumaa na ndio maana watu kama akina Balali wanajifanyia watakavyo wakishurutishwa na wanasiasa kwani wanajua Bungeni hakuna mtu hajali kuhoji. Kama Bunge letu lingekuwa la nguvu na la viwango kama tulivyodanganywa wakati linazinduliwa Balali na mafisadi wenzake ungekuta wameshashughulikiwa siku nyingi sana. Ila jamii yenye bunge dhaifu (feeble parliament) wabunge walio wengi (majority) wataitetea serikali hata kwenye maovu. Mfumo mbovu wa bunge unamfanya mbunge wa chama tawala kuogopa kutengwa pindi atakapokwenda kinyume na maslahi ya chama chake pale yanapokinzana na utashi wake (conscience). Bunge halina sheria za kumlinda katika kuihoji serikali na kwa maana hiyo wabunge wengi wa chama tawala wanalazimika kuziasi akili zao na kunyamaza ama kuongea pumba pale hoja nzito kama ya Bot ilipoletwa bungeni.

Kucheza ngoma ya wanasiasa unakwenda mbali zaidi ya bungeni hadi katika taasisi mbalimbali za serikali. Naamini kabisa wakubwa wengi wa ngazi mbalimbali za serikali hawana uwezo wa kuzuia wimbi la kutumiwa (manipulation), kufanya maamuzi chini ya vitisho (threats) pamoja na mashinikizo au mibinyo (pressure) mbalimbali. Ni katika mtizamo huu ndio maana nakuwa na mashaka kama kweli polisi ama ofisi ya mwanasheria mkuu ina ubavu wa kuwashughulikia mafisadi.

Tunahitaji kuimarisha taasisi ya Bunge (legislature) ili kashfa kubwa kama hizi za ufisadi zisipigwe danadana kama ilivyokuwa kwa skandali hili la Bot. Ninaamini kabisa kama Bunge lingekuwa la viwango wala tusingefika leo; siku nyingi wahusika wangeadabishwa. Namaliza kwa kumsikitikia gavana Balali kwani sasa imethibitika kumbe yeye ni fisadi haswa; lakini nataka nihoji wasomaji: kuna tetesi kuwa jamaa haumwi, eti kazamia ughaibuni kama mkakati maalum wa mafisadi kupambana na skandali hili. Je kama ni kweli tutawashinda mafisadi?

Mwisho, ni wazi huu ndio mwanzo wa ukweli wa aliyokuwa akiyasema mheshimiwa Dr. Slaa. Hili la Bot limedhihiri; lakini maswali bila majibu vipi mafisadi wengine waliobakia katika ile listi ya aibu? Nasikitika hata mkuu wa nchi alitajwa. Kweli maneno ya meseji ya simu ya rafiki yangu juu ya kunijulisha Balali katimuliwa yana kila sababu ya kuaminiwa; aliandika hivi: “Jk amecharuka!Hapo kuna wengi wataguswa, ila sijui kama sheria itafanya kazi yake maana hilo ndio muhimu. Kwa jamii yenye taasisi zisizo huru (independent) sina mategemeo sana kama sheria itafuata mkondo kwa skandali hili.

Nabakia nikiamini inawezekana lakini tusipoona “mapapa” wakishughulikiwa kwa hili bali “kambale” sitashangaa kabisa. Demokrasia yetu bado hairuhusu kufika huko labda tuamue kwa dhati kabisa kubadilika. Na si kizazi hiki cha akina JK na wenzake. Nina wasiwasi sana kama kuna utashi wa kutosha kukabili hili. Eti kumbe Balali na wenzake ndani ya serikali wametuibia kiasi cha fedha kinachotosha kujenga shule za sekondari 1000? Jamani kumbe Tanzania inang’atwa haswa na mafisadi.

Monday, January 07, 2008

UTATA WA KENYA

Chanzo cha machafuko Kenya ni hiki;machafuko haya yanafananishwa na hali ya Pakistan. Pia Yesu kristu kagusiwa juu ya utata wa Kenya. Kutokuwa na machafuko haina maana eti kuna amani kama tunavodhani. Unajua madaraka yanapendwa sana na vigogo ila pia hata masikini imedhihirika Kenya.

Lakini Kibaki alisahau amani bila haki haiwezekani. Lazima tukubali demokrasia ni gharama.