My Blog List

Thursday, July 31, 2008

CHACHA WANGWE ALIUAWA KWA RISASI?

MAZISHI YA CHACHA HAYAKUFANYIKA!

Huwezi amini lakini ndio hivyo, ndugu wa marehemu Chacha Wangwe walizuia mazishi yasifanyike kwa kile kilichoitwa kuwa hawaamini kama kuna ajali bali alipigwa risasi. Kwa mujibu wa redio free Afrika jana usiku, inasemekana familia ilimualika rafiki wa familia kutoka Kenya ambaye ni daktari na akawaambia kuwa jeraha lililopo kisogoni kwa marehemu ni la risasi.
Makubwa ndio haya inaonekana marehemu alipigwa risasi mdomoni na ikatokea kisogoni. Maoni yangu ni kuwa kama hii ni kweli basi marehemu alikuwa anafuatwa na maadui zake ambao naweza kuwaita (firing squad) ambao watakuwa walitumwa. Na inavyoelekea hawa jamaa watakuwa walilipita gari la marehemu na kumpiga risasi wakiwa mbele yake. Hii ndio itakayokuwa sababu ya ajali kwani kishindo ambacho Dennis Mallya alikisikia kabla gari halijabiringika ilikuwa ni risasi.
Kama hiyo sivyo, basi kwa vyovyote vile Dennis Mallya atakuwa ndie muuaji wa mbunge wetu mpendwa. Atakuwa ndie anahusika na mauaji haya na ashughulikiwe ikithibitika ni risasi imemuua Chacha.
Pia ni vyema gari lichunguzwe kama tairi zake zimepasuka kweli.
Nadhani baada ya mafisadi wa kisiasa Tanzania kuzidi kuwaua viongozi bora wa Tanzania sasa mwisho umefika. Alikufa Amina Chifupa alafu tukakaa kimya tu hatukuhoji lakini leo napenda niwapongeze ndugu wa Chacha Wangwe kwa walichokifanya kwani wameonesha kuwa wana akili na wanapenda nchi hii iwe na viongozi wenye weledi.
Mwisho nikumbushie kuwa kabla marehemu hajafariki, alikuwa ametoa maneno mazito dhidi ya hali ya “Ukabila ndani ya chama cha Chadema” na kuanzia hapo amepata misukosuko mingi hata kusimamishwa uongozi. Ni vyema wapenda amani wote Tanzania tujiulize hivi inawezekana maneno haya aliyoyasema ndio chanzo cha kifo chake? Wenye chama chao wamemuua? Je kwa kipindi hiki Chacha alikuwa ni tishio kwa CCM au Chadema? Iwe iwavyo, mojawapo ya hivi viwili ndio chanzo cha kifo hiki.

Tuesday, July 29, 2008

UGANDA VS MENGO - UNAIJUA KASHESHE?

Kwa sasa Uganda ina mgogoro mkubwa wa kisiasa na himaya ya Baganda, unajua chanzo chake?

Monday, July 28, 2008

MSIBA BUNGE LA TANZANIA TENA

TANZIA – SASA IMEKUWA ZAMU YA CHACHA WANGWE


Ni saa nne na dakika arobaini na saba, mara nikitizama taarifa ya habari ya ITV usiku nashanga mstari mweusi wa maneno unakatiza katika runinga na maneno: “mbunge wa Tarime, mheshimiwa Chacha Wangwe amefariki dunia usiku kwa ajali ya Gari” habari zaidi fuatilia redio one.

Na kweli ninazima runinga yangu na kuanza kusikiliza redio one. Ninakutana na mahojiano kati ya watangazaji: Asia Mohamed na Jerry Muro akiripoti kutoka Dodoma. Wanahojiwa waheshimiwa mbalimbali kwa masikitiko bado wanaonekana kutaharuki. Mtangazaji anadai eti nyakati za mchana mheshimiwa Chacha alionekana akiteta na mheshimiwa Mudhihir, hii inanikumbusha huyu ni mhanga mwingine wa ajali katika bunge hili. Hisia fulani zinanijia akilini lakini sisemi kitu najinyamazia.

Nikiwa nimekwishaamini kuwa mheshimiwa huyu katutoka, navuta hisia kadhaa juu ya bwana huyu na mara moja nautambua Umachachari wake, ubishi wake hata pale pasipo na Mantiki lakini kwa yote , kauli ya John Cheyo inanikuna akihojiwa na Jerry Muro. Anasema: “Chacha alikuwa na msimamo ambao wengi wetu hatunao” . Nakubaliana na mheshimiwa Cheyo na ninaendelea kusikitika.

Mara ninaamua kumtumia mtu wangu wa karibu sms akiwa Dar es salaam nikimsihi afuatilie habari kuna tukio la kifo cha mbunge mashuhuri. Pia katika message yangu nampa hisia yangu kuwa sasa “ Chadema itachafuka hasa kwani kifo hiki kitatumiwa na wanazi kuonesha kukolimbana hakuko tu CCM”. Ninapoituma message ile mara napata message kutoka kwa rafiki mwingine akinihabarisha juu ya kifo cha Chacha. Ninamrudishia nikimsihi kuwa “Siasa za Afrika ni mchezo mchafu, nina hisia lazima kuna mkono wa mtu awe wa kambi ya marehemu ama kule tulikozoea kukolimba watu wabishi kama Wangwe”.

Hapo hapo napokea message nyingine ambayo inanijibu ile niliyotuma Dar es salaam: “Sio Chadema ni CCM walileta mgogoro alafu wamemuua ili tuone Chadema nao wana mchezo kama wao! Tunaelekea pazuri sana. Tutashuhudia mengi na ukweli utadhihirika mwisho”. Mie sijui kwanini watu wana maoni ya aina hiyo ila ndio jamii ya kitanzania ilipofikia sasa.

Inapofika saa sita na dakika kumi na sita usiku hisia zangu zinashangaa: Jerry Muro, mwandishi wa ITV anaongea na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, mheshimiwa Lukuvi ambaye anasema kuwa gari la Wangwe limepata ajali ya kuanguka baada ya kupasuka gurudumu. Lukuvi anamnukuu rafiki wa Wangwe ambaye alikuwa ndani ya gari la Wangwe na amepata michubuko tu. Anasema gari lenyewe lilibiringika mara nyingi sana na ndipo Israel akachukua roho ya mheshimiwa Chacha. Moja kwa moja hapa ninajenga kanuni za kihisia na chonganishi (conspiracy theories) kadhaa:

Moja, kwanini gari la mbunge kama tuyajuavyo ni magari imara , mazuri na nina hakika yanafanyiwa matengenezo bora, itakuwaje lipasuke tairi tena nyakati za usiku pasipo na joto sana la kupasha hiyo chubu? Inawezekana kirahisi namna hiyo? Au tuseme Chacha anatembelea ulimu?
Pili, hili Bunge letu lina matatizo gani? Ni balaa ama ni nini? Kwanini kila kikao kinapokutana hasa cha bajeti lazima Mbunge afe?
Tatu, kwanini katika bunge hili ukiacha mbunge mmoja tu, wote waliokufa kulikuwa na hali ya kuwa na maadui hasa juu ya misimamo ya marehemu hawa?
Nne, kwanini wabunge wa bunge hili wanapatwa na madhila kama ajali ama vifo mara baada ya kuwa ni watu wenye misimamo yenye kutetea maslahi ya umm a sana ama kudhoofisha maslahi ya umma?

SHUHUDA WA AJALI

Saa sita na dakika thelathini na sita, redio one inaripoti kuwa ndio mwili wa Chacha Unaingia hospitali ya Dodoma kutoka eneo la ajali huko Kongwa. Gari ni Land Cruiser namba: SM.4297 la Halmashauri ya Kongwa. Jerry Muro anaongea na Rafiki wa mheshimiwa Chacha ambaye alikuwa akisafiri na mheshimiwa Chacha, ndugu Deus Mallya, rafiki wa karibu wa Chacha, anaeleza walitoka Dodoma wakienda Dar, anasema alisikia kishindo kikubwa sana kabla ya ajali, ninapata hisia sio ajabu inawezekana gari hilo lilikuwa limetegwa bomu labda, na gari liliruka juu na kufuatiwa na mbiringiko mkubwa sana.

Kuhusu mwendo wa gari Deus Mallya anasema kuwa Mheshimiwa Wangwe hana hakika kama alifunga mkanda. Yeye alifunga mkanda, lakini kimazingira inaonekana marehemu alibanwa kwa hiyo napata hisia alikuwa amefunga mkanda la sivyo kwa mbiringiko huo lazima angerushwa nje.
Je mheshimiwa Wangwe alikuwa kwenye hali gani? Mwanzoni nilidhani ni Land Cruiser, kumbe sio, ila ni gari dogo. Alikuwa anaendesha gari aina ya Corola na anapoulizwa kama marehemu alikuwa mlevi anasema hadhani ila asubuhi alisema alikuwa na malaria.
Je hali ya gari ilikuwaje? Gari limekuwa kama kopo lililofinyangwa. Mheshimiwa Wangwe alikuwa katika hali gani baada ya ajali? Aliumia maeneo ya kichwani na kifuani.
Deus Mallya yeye anasema ameumia mguu wa kushoto kama ameteguka tu na ana maumivu kichwani. Haamini kama amepona, ndio maajabu ya Mungu.

Mwisho, Mkuu wa mkoa wa Dodoma anasema baada ya mwili kuingia Dodoma tusubiri maelezo ya Spika kesho asubuhi. Nami naamua kwenda kulala nitamsubiri Spika aseme zaidi asubuhi.

Binafsi niseme tu, kifo hiki kimenisikitisha na ndio maana nikaamua kuandika makala hii usiku huu wakati nikufuatilia habari zaidi za kifo hiki. Nimalizie kwa maneno ya rafiki yangu katika message yake ambayo yameingia sasa hivi wakati namaliza : “ Aise inasikitisha ubunge sio kazi nzuri kwa sasa afrika hakuna la maana wanalofanya bali kuadhibiana kiainaaina, ngoja tuone mengi yanaweza kufichuka”. Mie nabaki nikijiuliza sijui ni nani atafuata manake nina hakika kabisa kwa mtiririko huu basi kuna mbunge mwingine atakufa kikao kijacho cha bajeti. Kazi kwenu wabunge.

Nimalizie kwa kusema: “ Chacha tulimpenda sana lakini Mafisadi walimchukia sana”. Mungu amlaze mahali pema peponi, Amina.

Saturday, July 26, 2008

HABARI ZA JUMAPILI

Kutatokea kupatwa kwa jua wiki ijayo. Kupatwa kwa jua nusu hakutaonekana Afrika siku hiyo.

Kumbe udikteta na ubabe uongozini una faida? Je kuna faida gani kuweka maafisa wa Jeshi kama ndio mabosi wa jeshi la polisi?
Huko Kenya wanafunzi wa sekondari wanagoma, kumbe ni halali kugoma.
ICC imeamua kulia na dikteta wa Sudan, je kwanini ICC inadili na madikteta wa nchi masikini tu?

Monday, July 21, 2008

MAKAMU WA RAIS ANAPOINGILIA NDOA YA DEREVA

Profesa Bukenya ni makama wa rais Uganda. Ana vituko, hebu vione.

MUGABEISM – FALSAFA ILIYOZINDULIWA NA NYERERE

Robert Mugabe hatimaye jana alikutana na hasimu wake wa kisiasa na kusaini makubaliano ya kuanza kujadiliana ili kutanzua mgogoro mkubwa wa kisiasa wa Zimbabwe. Ni hatua ambayo imeendelea kunishangaza juu ya mwenendo mzima wa siasa za Kiafrika kama kweli zinafuata demokrasia ya Kimagharibi au ni demokrasia mpya ya Kiafrika. Morgan Tsavingarai yeye jana kasema ni siku ya kihistoria kukutana na Mugabe tangu miaka kumi.

Kwangu nimeona tukio la hili la kukubali kuzungumza kwa watu hawa wawili kama mwelekeo tata wa siasa za Zimbabwe na pia kama hatua mpya kwa waafrika kujiuliza mambo kadhaa: Moja, nianze na Mugabe mwenyewe ni mtu wa aina yake. Kati ya maraisi wote wanaoitawala Afrika kwa sasa na hata wale waliowahi kutawala bara hili ndiye msomi sana kuliko wote. Mugabe ana shahada (degree) saba za chuo kikuu na wala sio zile zilizoeleka kwa vigogo wetu kutunikiwa za heshima. Huwa nafurahi kumsikiliza kila anapoongea kwa ufasaha lugha ya kiingereza huku akionekana hata kwa umri mkubwa bado ana uwezo mkubwa wa kufikiri.

Pili Mugabe pamoja na akili zote za darasani alizonazo amekosa busara za umri alionao. Nasema hivi kwani nadhani Mugabe ni mwanamapinduzi hasa wa harakati za kiafrika (Pan Africanist) ambaye kateleza sana kwa kile anachokitetea ama labda hajateleza basi ndio mwanzo wa Uwanamapinduzi mpya wa kiafrika. Namfananisha Mugabe na Mwalimu Nyerere ambaye naye alikuwa ni mwanamapinduzi halisi wa kiafrika ambaye hakuwa tayari kuwaruhusu mabepari waimeze nchi yetu chini ya utawala wake. Aliamua aanzishe mfumo wa kisiasa wa kiafrika hasa kwa kutumia mfumo wa kijamaa ambao asili yake ilikuwa ni mfumo mama wa sera za mwanafalsafa wa kijerumani Marx (Marxism).
Mfumo huu wa Ujamaa kwa kiasi fulani haukufanikiwa hadi pale Mwalimu Nyerere alipoamua ang’atuke (1985) kwani alijua wazi hawezi kushindana na mabepari kwa njia yeyote. Kwa kipindi kile nilikuwa nasoma shule ya msingi darasa la tatu nakumbuka jinsi maisha yalivyokuwa magumu kukikosekana hata bidhaa muhimu kama sukari ama sabuni za kuogea ama kufulia na biashara za magendo kushamiri hasa mpakani na Kenya. Nadhani Nyerere hakuwa tayari kuvumilia haya na akaamua akapumzike kwao Butiama.

Tatu, Mugabe pia alikuwa katika imani moja na Nyerere lakini yeye akaamua atofautiane kidogo na Nyerere kwa kuamua kupigana na maadui wakuu yaani mabepari. Ni vita ngumu sana na kuishinda hii mimi binafsi kama mwafrika na mzalendo siamini inawezekana hata kidogo kwa sasa. Nasema hivi kwani naona mfumo wa dunia kwa sasa ni wa unyonyaji kwa nchi kubwa kuzilazimisha nchi masikini kufuata matakwa yao na hata kwa kuruhusu rasilimali zetu kuchukuliwa kwa visingizio vya uwekezaji ama ukosefu wa teknolojia kwa nchi masikini.

Ni katika mtizamo wangu huu nadhani ndio maana Mwalimu Nyerere aliliona hili na ndio maana alikuwa kila akifanya hotuba anakumbushia eti siku zijazo kutakuwa na hali fulani na ambayo ndio tunaiona leo hii hapa Tanzania. Kwa Mugabe yeye ni tofauti na haoni sababu kuwaruhusu mabepari kuzikalia ardhi ya Zimbabwe na kufanya shughuli zao. Hivyo kwake aliona ni bora kuwanyang’anya ardhi na hapo ikawa ndio mwanzo wa dhahama lote hadi leo. Mwenzake Tsavingarai kwa kuona jinsi ambavyo unyang’anyi huo wa ardhi kutoka kwa walowezi ulivyoleta dhahama yeye akaamua kukubali kutumiwa na mabepari. Ni wazi Tsavingarai ni kibaraka (puppet) wa Waingereza; lakini pia naamini anatekeleza matakwa ya mfumo wa kidunia kwa sasa bila kujali ni kiasi gani Wazimbabwe wengi watakavyoumizwa na mfumo wa serikali itakayokuwa chini ya utawala wake kama angelishinda uchaguzi.

Nakubali kuwa Mugabe ndie mwanamapinduzi halisi anayetakiwa Afrika kwa wakati huu. Kwani yeye kaamua ajaribu kuendeleza pale akina Nyerere, Nkrumah, Sekou Toure na Thomas Sankara walipoachia baada ya tawala zao kushindwa kabisa kuhimili mitetemo ya mabepari. Mugabe aliamua avuruge uchaguzi unaoendeshwa kwa taratibu za kimagharibi zilizoanzia kule Athens Ugiriki karne nyingi zilizopita. Yeye kaja na demokrasia mpya kabisa ya kiafrika kwa kuhakikisha watu wanatishwa, kupigwa marungu, na hata kuuawa ili mradi tu wasivutwe na kutekwa na hisia za kupenda sera za mabepari. Hali hii ilifanya uchaguzi uharibike na mpinzani mkuu akaamua kujitoa nah ii ikamruhusu Mugabe kushinda kwa ulaini uchaguzi wa Zimbabwe.

Demokrasia ya Kiafrika haina vigezo vingi; yaani haina mambo ya taratibu za upigaji kura kama kujiandikisha, taratibu za kampeni, uhuru wa kutumia vyombo vya habari kwa wapinzani hauna nafasi kabisa. Ni uchaguzi ambao unazingatia tu ni nani tume ya uchaguzi itamtangaza kama ni mshindi. Hii ni mbinu ambayo hata hapa Tanzania imekuwa ikitumika hasa kule Zanzibar katika chaguzi kadhaa chini ya uasisi wa Mwalimu Nyerere tangu mwaka 1995.

Mugabe alifanikiwa kwa njia hii na hata pale jumuiya ya kimataifa ilipojaribu kuweka vikwazo iligonga mwamba pale Wachina na Warusi walipoamua kupiga kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Huu ukawa ushindi mkubwa kwa Mugabe na sasa ameamua kuanza mazungumzo na Tsavingirai, kwa kiasi fulani ni hatua moja mbele zaidi ya watangulizi waliowahi kupingana na mabepari lakini wakashindwa. Ninasema hivi kwani naamini kwa hotuba aliyoitoa baada ya kusaini na hasimu wake Tsvangira, kuwa sasa “Tuanze kuwaza na kutenda kizimbabwe” ilionesha kuwa hataki mawazo ya kibepari na hii ndio imekuwa shida yake kubwa. Anataka mambo yafanyike Kiafrika kwa kuzingatia mashiko ya kiafrika.

Kufikia hapa ndipo napata maswali ambayo siku zijazo nitayajengea hoja zaidi: Kwanza, Je Mugabe kama atakubali kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na Tsvangira, je ataweza kuwafanya hawa jamaa wa MDC kuwaza na kutenda “Kizimbabwe” ? Hapa nina mashaka sana, sijui itakuwaje.
Pili, je kwa hatua iliyofikiwa hadi leo ya chuki dhidi ya Waingereza na Wamarekani, itawezekana Zimbabwe chini ya Mugabe iwe na ushirikiano wowote wenye manufaa na nchi hizo? Na je nchi zingine zitachukuliaje hatua hii ya maelewano kati ya mafahali hawa wawili, wataweza kuanzisha mashirikiano mapya?

Tatu, Je inawezekana nchi za Kiafrika zikaendelea na utengamano ikiwa hazifuati matakwa ya kiutandawazi ambayo kwayo lengo lake ni “utandawizi” ambao Mugabe na akina Nyerere hawautaki? Na je kama kweli Zimbabwe itatulia je mapinduzi haya mapya ya Mugabe (Mugabeism) yataenea barani Afrika ili kumkomboa mwafrika dhidi ya Utandawizi?
Labda niseme tu ni maoni yangu kuwa sina imani kama kweli hii “Mugabeism” ina tija sana kwa bara letu. Ni falsafa ambayo ni tamu sana kimatamshi lakini kiutekelezaji nadhani ni chanzo cha migogoro hasa ikizingatiwa bado bara letu hatujawekeza ipasavyo katika sekta ya elimu kuweza kuwa na wanataaluma hasa wahandisi ambao wangewezesha nchi zetu kuweza kujitengenezea na kufaidi rasilimali zake kwa asilimia mia moja bila kuibiwa kwa kutumia utandawizi. Ni wazi Zimbabwe na hii “Mugabeism” haitakuwa na tija yeyote ingawa ni tamu masikioni miongoni mwa wazalendo wa kiafrika lakini mtu ukifikiri sana ni bure tu. Ni falsafa inayojaribu kugeuza mwenendo wa dunia pale pasipowezekana.

Naiona Zimbabwe kama ilivyokuwa Kenya kwani mara baada ya Kibaki kukubaliana na Raila, imekuwa kama kuahirisha mwelekeo mpya wa siasa za Kenya na kuendelea mawazo ya kale ( status quo). Mugabe alipaswa atumie busara kwa kuiga wenzake akina Nyerere ama Moi walipoamua kujing’atua pale upepo ulipoonesha wazi kuwa wimbi la dunia lilikuwa dhidi ya falsafa zao na kama wangelijaribu kushinikiza falsafa zao basi wananchi wengi wangeumia sana. Kwa akina Mugabe na Kibaki wao si tija watu kufa ama kuumia ilimradi falsafa zao zinabaki madarakani.

Huku haya yote yakitokea nitabaki najiuliza bila jibu inakuwaje mtu msomi wa shahada saba ang’ang’ane na falsafa potofu (Mugabeism) yake huku uchumi mzima wa nchi ukiangamia? Ni wazi Mugabe atabakia kama mwanamapinduzi halisi ila ameshindwa kuelewa kuwa katika dunia ya utandawizi kamwe mtu huwezi kuwashinda mabepari. Huu ndio ukweli mchungu kwetu wote tunaoipenda Afrika. Na si Wachina wala Warusi ambao watairejesha Zimbabwe katika mafanikio ya kiuchumi kama zamani bali ni hao Waingereza ama Wamarekani ndio tu wanaoweza kurekebisha mambo ya Zimbabwe.
Mwisho, hapa nataka wote tujiulize hivi Ali Hasan Mwinyi kama angeliamua kufuata sera za Nyerere alipopewa jukumu la kuliongoza Taifa la Tanzania je nchi yetu ingelifika hapa ilipo leo? Umefika wakati kwa watawala wetu kujua mipaka ya sera wanazozitetea la sivyo wataharibu kabisa nchi wanazopigania na kujitoa mhanga kuzipigania. Nina mashaka sana bila kufuata kile Watandawizi wanataka basi ni kiama kwa nchi zetu. Kama nimekosea basi naomba nipewe wazo mbadala.

Saturday, July 19, 2008

Bashiri Kukamatwa?

Wiki hii ilikuwa siku ya Kupanga Uzazi je unajua kupanga uzazi ni vizuri sana? Pia jambo lililosemwa sana ni hii hatua ya Mahakama ya ICC kutaka kumkamata Rais Bashir.

Friday, July 04, 2008

MUSEVENI KAMA MUGABE?

Saa nyingine serikali za Kiafrika zinajiabisha sana pale zinapowatumia wahuni tu wa mtaani katika shughuli zake. Ona hili la Uganda jinsi lilivyo. Uganda ya Museveni sasa imeanza kumchoka; kuna kila dalili kuwa wapo watu tena wengine wa karibu na Museveni wameanza kupanga jinsi ya kuondokana naye. Hii inachangiwa na kukuwa kwa rushwa na pia jeuri ya baadhi ya maswahiba wa Rais Museveni ambao kwao hata mkaguzi mkuu wa serikali si kitu.
Si hayo tu, kuna hili la Mugabe kufananishwa na Mobutu.