My Blog List

Wednesday, July 25, 2007

SHIRIKISHO LA AFRIKA MASHARIKI NI UTAPELI WA WATAWALA

Kamusi ya Kiingereza na Kiswahili inafafanua neno "MYTH" kama uwongo, jambo lililobuniwa na pia likimaanisha ngano. Mimi napenda nitumie neno 'ngano' kujenga mada yangu.

Kwa wale waumini wa dini mbalimbali neno 'Ngano" halitakuwa jipya kwani misaafu ya dini zote imejaa ngano za kila aina ambazo zinasaidia hasa wahubiri kufikisha ujumbe pale wanapohitajika kuhakikisha kuwa kondoo wa bwana hawapotei njia. Ninatizama Shirikisho la Afrika Mashariki ambalo hivi majuzi watanzania takriban 75% wameamua kulikataa hasa ule mpango wa wanasiasa wetu wa kuharakisha kufikia shirikisho itakapofika mwaka 2013. Binafsi siamini kuwa ni busara kuwa na shirikisho ila tu naunga mkono wazo la Jumuiya kama ilivyo sasa hivi ikiimarika kila kukicha kama taasisi itakayosaidia sekta ya uchumi kukua na urahisaji wa biashara miongoni mwa nchi zetu.

Shirikisho la Afrika Mashariki sio la lazima wala jibu toshelezi katika kupambana na umaskini. Kama lilivyokuwa tukio la uhuru katika miaka ya 1960 ambapo tunashuhudia nchi zetu zikiendelea kuwa katika kundi la nchi masikini zaidi ulimwenguni. Hali ya uchumi ni mbaya na nafikiri tutegemee pia ndivyo itakavyokuwa katika muungano wa kisiasa; kwani kwa mawazo ya uongozi tulionao hadi leo hii, kifikra si watu wa kutufikisha katika maendeleo. Bado mawazo yetu wengi tunafikiri kuwa kiongozi basi ni kujilimbikizia mali binafsi na familia pamoja na rafiki zetu.

Kwa kipindi chote cha ukusanyaji maoni ya wananchi juu ya kuharakishwa na pia kujua kama wazo la shirikisho ni muafaka, nimejaribu kutafakari maoni ya watu wengi na nikajiuliza swali: Hivi ni kwanini wanasiasa wetu wanatudanganya sana wanapotetea shirikisho au hata jumuiya kama ni jibu la umasikini,eti wigo wa soko utaongezeka na maisha bora yataibuka?Ndio hapa ngano ya Shirikisho inapoanzia; ni kweli, Shirikisho litakuwa na soko takriban la watu zaidi ya milioni mia moja. Hili ni soko la pili kwa ukubwa nadhani hapa Afrika ukiacha lile ya shirikisho la Nigeria lenye watu zaidi ya milioni mia moja arobaini na ushehe.

Pamoja ukubwa wa soko la Nigeria, bado watu wengi-wateja wa soko-ni masikini wa kutupwa sawa na hapa kwetu. Kimahesabu, "sifuri ukijumlisha sifuri ni sawasawa na sifuri". Unategemea masikini anunue nini kama tunatetea hoja ya wigo wa soko? Bila hatua madhubuti kwa kila nchi kuwezesha wananchi wake kuwa na nguvu za kushiriki kwenye soko ni bure kabisa. Hatuhitaji shirikisho manake hao wanaongoza nchi zao ambao wameshindwa kuwawezesha wananchi wengi kutoka kwenye umasikini, ndio haohao watakaotuongoza katika shirikisho. Je wana lipi jipya kukabiliana na dola kubwa la shirikisho ukiachilia mbali kushindwa kwao kwenye serikali zao ndogo?

Nadhani tunahitaji tu jumuiya kama ilivyo sasa ili ichochee kuondoa umasikini na wala si shirikisho. Naamini kuwa si sahihi kuwa ukubwa wa eneo au wingi wa watu ni kigezo cha kuwa na nguvu za kiuchumi. Turejee vitaifa vidogo vidogo kama Uingereza, Ufaransa, Japan na tujiulize je wana ukubwa wa hata Tanzania? Au yapo mataifa yenye hadhi ya kuitwa bara kama vile: Antarctica na Australia pamoja na ukubwa wao bado si mataifa namba moja kwa utajiri au maisha bora ulimwenguni. Nasema hii ni ngano ya wanasiasa kutafuta ofisi za kuendeleza maisha yao labda.

Nikitizama upande wa faida ya uwekezaji kutoka nje (FDI) ambazo tayari zinajionesha katika kila nchi kwa sasa ni wazi kuna faida bila kutegemea shirikisho. Tuangalie mashirika mbalimbali ya kikanda kama vile ASEAN la bara Asia, COMESA na hata SADC utaona ongezeko la uwekezaji na ukuaji wa uchumi na biashara bila mfumo wa shirikiso katika nchi husika. Hivi Botswana au Mauritius chumi zao zinastawi sana kwa ajili ya Shirikisho au utawala bora? Ni wazi tuna tatizo la utawala na usimamizi wa rasilimali zetu na kama ni hivyo hata lije Shirikisho ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu. Inaonekana hatujui tatizo letu Afrika Mashariki sio kuongeza soko; tujitizame kwanza, la sivyo tutahamisha matatizo ya utawala mbovu kutoka vijinchi vyetu hadi kwenye Shirikisho.

Naamini hata kama Shirikisho litaundwa, bado serikali za ndani za nchi zetu zitabakia na hatamu ya kuvutia uwekezaji ili kutoharibu hali ya uchumi wa nchi zetu. Kwa mantiki hii tuturajie serikali hizi kuendelea kutoa misamaha ya kodi na hata ruzuku kuvutia wawekezaji ili kuzuia kuachwa nyuma. Sasa hapa Shirikisho ni kama mzigo tu wa kuongeza gharama za kiuendeshaji. Ninapowaza jinsi viongozi wetu wanavyopenda minjonjo ya ukubwa napata taabu sana kuelewa ni nini hasa lengo la kupigia mbiu Shirikisho. Naona kama vile ni kwa matakwa yao binafsi na wanatudanganya wananchi ndio maana naliona wazo la Shirikisho kama "ngano".

Jambo la msingi ni kuwa hata katika jumuiya nyamafu kama ya sasa ya EAC, haitawezekana kuleta maendeleo ya kiuchumi na kufuta umasikini katika jamii ambayo asilimia hamsini ya wananchi bado wanaathiriwa na malaria; nusu ya watoto wana kwashakoo na theluthi moja ya wanawake wanakufa kwa gonjwa la kuepukika kama ukimwi. Sioni ni kwa vipi shirikisho la kisiasa litaweza kuondoa madhila haya. Hatari iliyopo ni kutuongezea gharama za kuendesha shirikisho hasa za viongozi --mamwinyi--waliopania kujipandikiza ili kutawala eneo hili kama himaya yao na watoto na marafiki zao.

Kabla sijamaliza mada yangu, hebu tujiulize juu ya faida za Shirikisho la Afrika Mashariki kama zipo? Je Shirikisho hili linalotakiwa na watawala wetu litampa faida mwananchi wa kawaida? Na je katika "anga za kimataifa" tutakuwa na sauti kubwa ya kisiasa katika kada na duru za kisiasa za ulimwengu huu wa utandawazi? Je shirikisho litaweza kutukwamua dhidi ya "utegemezi wa wafadhili au wahisani?" Jibu naliona ni hapana: kwa taarifa tu ni kwamba yale mashirika makuu ya kiuchumi ulimwenguni kama Benki ya Dunia (World Bank), Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF), Shirika la Biashara Ulimwenguni (WTO) na hata Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) yanatoa mgawanyo wa nguvu za maamuzi kwa nchi au mataifa kupiga kura katika kufanya maamuzi mbalimbali kwa kuzingatia GDP.

Tukilitizama Shirikisho kama litaundwa ni kwamba litakuwa na GDP ya kama dola 30 bilioni sawa na asilimia 8% ya nchi ya Afrika Kusini. Kimsingi na kiutaratibu haitaweza hata kutimiza sharti la kutoa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia (WB). Tutaendelea kushikilia kiti kimoja katika Benki ya Dunia pamoja na nchi nyingine ishirini na mbili (22) za Afrika kwa kupokezana. Dunia ya leo bila kuwa na nguvu ya maamuzi ni kwa vipi tutajikwamua hali kandamizi kadhaa ambazo mataifa yenye nguvu yananyanyasa mataifa makubwa? Ni kutokana na muono wangu huu napatwa na hisia labda viongozi wetu hasa wanavyopigia debe hii ngano iharakishwe basi ni uzushi tu na usanii na si kwa maslahi ya uchumi bali ni maslahi binafsi labda.

Nawaona wanasiasa wetu katika mtizamo wa mnyama kondoo; hasa pale anapokuwa anapelekwa machinjioni na wala hajui kifo chake. Wanasiasa wetu hawatizami mbali katika utendaji wao mara nyingi. Nchi zetu tusipokuwa makini nahisi tumetekwa nyara na sera za kizamani za kiuchumi ambazo hazikidhi haja ya jamii kwa ujumla bali kwa matakwa binafsi zaidi. Wenye kuona mbali wamebaki tumechanganyikiwa ni kwa vipi bado barabara zetu ni mbovu, hakuna huduma bora hospitalini na bado kuna wanakijiji wanalala nyumba za majani na udongo miaka zaidi ya arobaini ya uhuru.

Je tiba ya haya ni shirikisho? Mimi siamini kabisa, ndio maana sitaki Shirikisho naona hii ni ngano ya wanasiasa katika kutudanganya kama watoto kwa maslahi yao zaidi; ni 'utapeli wa watawala' ila tu Jumuiya tuliyonayo hadi sasa ni hatua muafaka.

NANI ATAMRITHI MUSEVENI?

Kama kuna mtu pekee ambaye anaweza kumruthi rais Museveni siku za usoni ni mheshimiwa Amama Mbabazi. Museveni aliwahi kusema huyu ndie pekee 'presidential material' na sasa yeye mwenyewe kathibitisha. Lakini inasemekana Museveni kukaa madarakani muda mrefu kunamfanya sasa kununua umaarufu kwa kutumia pesa kuwarubuni wapinzani warejee NRM.Hata aliyekuwa katibu mkuu wa EAC, Amanya Mushega ambaye wametofautiana kwa muda mrefu sasa anatafuta njia za kurejeana japo inasemekana ni vigumu. Lakini pia rafiki na swahiba wa Museveni naye kaanza kumtenga bosi wake.

Kufuatia kuibuliwa kwa kashfa ya ngono ya yule askofu mkosoaji sana kule Zimbabwe, Pius
Ncube, inasemekana huu ni mtindo wa "Big Brother". Chama tawala Uganda kimependekeza kuanzishwa kwa mafunzo ya kijeshi kwa kila mwananchi kwa lazima; je ndio mwanzo wa vita Uganda?
Nchini Uganda kumetokea walokole ambao wanajitajirisha kwa jina la Yesu. Je umasikini ni kujitakia?

Mwisho kweli Uganda bado nchi ya kijeshi, makada wa chama tawala walikutana majuzi; ona mambo yaliyojiri na vituko vya waziri mmoja msomi.

Saturday, July 21, 2007

Kweli haya ni mambo makubwa, yaani Robert Mugabe anatumia mbinu chafu za akina Museveni kumchafua Askofu Ncube ambaye anampinga sana.

MU 7 HANA LENGO LA URAIS WA EAC

Rais Museveni ameamua kukanusha eti ana maslahi katika jumuiya ya Afrika Mashariki, yaani anataka kuwa Rais wa kwanza kama inavyosemkana licha ya hivi majuzi kufanya ziara kwa gari katika nchi zote tatu.
Pili kuhusu jumuiya ni vyema tukamfahamu spika wa sasa wa bunge la jumuiya.

Monday, July 16, 2007

HATUHITAJI SHIRIKISHO ILA JUMUIYA INATOSHA--EAC

Ripoti ya maoni ya wananhi wa Tanzania imetoka na ni wazi wananchi wengi wana woga mkubwa na hawataki shirikisho.Binafsi sitaki shirikisho ila tu napenda tuwe na jumuiya kwani nadhani Shirikisho ni maslahi ya wanasiasa tu na kwa mwananhi wa kawaida si tija.

Lakini pia, kama mtanzania, mimi ni mmojawapo wa wale wasioridhishwa bado kama kweli tunahitaji kuwa na shirikisho la Afrika Mashariki (EAC) .Ukiusoma mkataba wa kuanzishwa kwa EAC unaeleza kinagaubaga mtiririko mzima unaopaswa kufuatwa na nchi wanachama ili kufikia shirikisho.

Yanayotokea kwa kipindi hiki, kidogo yananishangaza hasa "uharakishwaji wa kupata shirikisho" fast traking.Kwenye mkataba wa jumuiya-mataifa shirika-Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi-yanawajibika hatua kwa hatua, taratibu; yaani kwanza, muungano wa mapato(custom union), pili, soko la pamoja(common market), tatu, sarafu moja(monetary union) na mwisho Shirikisho la Kisiasa(Federation).

Lengo la mchakato huo ni ili kupata ushirikiano makini wa kiuchumi ambapo watu wenngi masikini wataweza kuishi na kumudu maisha ya kiwango cha juu katika eneo hili. Inapowezekana kunyanyua kiwango cha maisha cha raia wengi masikini basi shirikisho linakuwa linawezekana. Shirikisho lingetakiwa lifikiriwe katika kipindi kifupi hadi 2013 kuweza kuzibadili taasisi mbalimbali za kitaifa katika mataifa shirika ziwe chini ya mtandao mmoja wa shirikisho.
Sioni itawezekanaje katika kipindi kifupi hadi 2013 kuweza kuzibadili taasisi mbalimbali za kitaifa katika mataifa shirika ziwe chini ya mtandao mmoja wa shirikisho. Hebu nitoe mifano michache:

Moja, Nchi ya Kenya iko tayari kwa shirikisho kwani ni njia mojawapo ya kuimarisha zaidi nguvu yake ya kiuchumi na kibiashara. Uchumi wa Kenya inasemekana ni karibu asilimia 50% ya uchumi wa Uganda na Tanzania kwa pamoja. Pili, ukienda Uganda na Tanzania hapa pia kuna kiini macho. Taarifa za kiuhumi zinaonesha kiwango kidogo cha biashara kati ya nchi hizi mbili. Kwa mfano, Uganda Bureau of Statistis-2004 zinaonesha mwaka 2003 Uganda iliuza bidhaa za thamani ya dola 78 millioni kwa Kenya, alafu ikauza dola 5.8 milioni kwa Tanzania.
La kushangaza kabisa ni kwamba mwaka huohuo Uganda iliuza bidhaa za thamani ya dola 13.7 milioni kwenda Sudan ambayo sio nchi mwanahama wa EAC.

Ninachokiona hapa kuna hatari inakuja hapo baadaye: Uganda inafanya biashara zaidi na Sudan kuliko Tanzania. Tukumbuke mwaka 2003, Sudan ya Kusini bado ilikuwa itani; sasa hii hali imebadilika kabisa hali ni shwari, na mpaka 2011 upo uwezekano wa Kusini mwa Sudan kuwa taifa huru.

Na kwa hali iliyo sasa biashara kati ya Uganda na Sudan itakuwa sana na wala Uganda haitahitaji nchi kama Tanzania kibiashara kabisa. Haya yote yameshaanza kutokea sasa. Kwa ushahidi tu, mtu aende kushuhudia ni malori mangapi yanapita usiku na mhana yakiwa na shehena ya bidhaa kutoka Uganda na Kenya katika barabara ya Yei hadi Juba.

Uchumi mzuri unapimwa na biashara, na kama ni hivyo je shirikisho la nini?Jumuiya inatosha kwani vikwazo vyote ya biashara vitaondolewa. Shirikisho ni mzigo kwa wanasiasa kutafuna kile kinachozalishwa na faida ya jumuiya kwa kuwakirimu wanasiasa na misafara yao ya kifahari.Nawaunga mkono wananchi kukataa shirikisho ila nasisitiza Jumuiya ni muafaka.

Saturday, July 14, 2007

LEO NI "BASTILE DAY"

Nchini Ufaransa leo ni siku ya kukumbukwa na kutafakari: "BASTILE DAY"

Wednesday, July 11, 2007

KAMPENI ZA MUSEVENI EAC ZAANZA?

Katika kile kinachoelezewa na baadhi kama kampeni ya Rais Museveni kuzunguka kwa gari nchi za Afrika Mashariki ni kampeni za kutawala eneo hili, basi jana Museveni alidhuru kaburi la Mwalimu Nyerere, nadhani kupata baraka za mzee.

Museveni kapita miji ya Busia, Kisii, Migori, Isbania, Mwanza hadi Butiama katika juhudi za kujitambulisha kama mfalme mpya wa kaya ajaye.Inasemekana hata mkewe aliwahi kusafiri kwa basi kutoka Kampala hadi Nairobi.Kuna hisia jamaa amepania uraisi wa Shirikisho la EAC na mkewe atamrithi kule Uganda. Ziara yake haikuweza kumalizika kwani kutoka Musoma ilimbidi apande ndege ya serikali ya Tanzania kurejea kwao kwani barabara hazifai.

Haya yakitokea, kwenye chama chake NRM, kuna makundi ya kisirisiri kama yale ya mitandao ya CCM.


Ama kweli duniani kuna mambo, kumbe bado usodoma na ugomora upo makanisani?

Mwisho nimalize na tahariri ya kuitetea NGO : HAKI ELIMU kwani waheshimiwa wetu na akili zao mgando hawaitaki kabisa. Napenda sana kazi yake.

Saturday, July 07, 2007

UJAMBAZI SASA UGANDA

Tanzania ni nchi ya usiri sana hasa juu ya masuala ya ujambazi lakini Uganda ni wazi kwani mtu unaweza kuwajua hata kwa sura majambazi gazetini.

Wednesday, July 04, 2007

UNITED STATES OF AFRICA-KIINI MACHO

Bara la Afrika kuwa nchi moja itabaki kuwa kiini macho milele.Mkutano uliomalizika karibuni viongozi wetu hawakuwa tayari kukubali wazo hili linalopigiwa chapuo na Ghadafi. Wengine wanatuambia kuwa ni wazi waafrika tumepotea njia hadi tutakapokubali kuwa na namna yetu ya kufanya mambo dhidi ya wazungu.

Hivi kuna sababu na haja ya kuharakisha jumuiya ya Afrika Mashariki?Pia ni vizuri tujue ile ripoti ya kiuchumi ya nchi za Mashariki ya Afrika inasemaje.
Habari ya kuvuti huko Uganda ni hii ya kubadilishwa kazi yule mlinzi au msaidizi wa Rais Museveni baada ya kumuumiza rais na sasa kuna mlinzi mpya.Hiyo ni burudani tosha ila kuna hii hadithi juu ya yale mapinduzi ya mwaka 1971 yaliyofanywa na Idd Amin.

Monday, July 02, 2007

MUSEVENI MTOTO MAFUNZO ZAID YA KIJESHI MAREKANI

Museveni anazidi kumuongezea ujuzi wa kijeshi mwanaye, je anamuandaa kumrithi?