My Blog List

Sunday, March 19, 2006

HABARI ZA LEO MAGAZETINI

Katika pitiapitia yangu ya habari leo nimekunwa na jinsi wanaume wa siku hizi wanavyochagua wanawake wanaowapenda wawe wenza wao. Mwandishi kaandika kwelikweli na akaonya sana juu ya makosa tufanyayo sisi wanaume. somahapa . Kuna hili la haki za ukombozi wa wanawake: inasemekana wengine wamejisahau na wakavuka mipaka. soma
Habari nyingine ni kuwa eti dunia ya leo mambo ya elimu sio tena msingi wa kufanikiwa kimaisha. Ukisoma mwandishi wa makala ile ameniacha nikipigwa butwaa ni kwanini ninasoma sasa? bonyezahapa
Alafu ningependa tumsome raisi wa hapa Yoweri Museveni katika mahojiano yake ya kwanza tangu achaguliwe kuwa raisi hivi majuzi. bonyeza

Saturday, March 18, 2006

HISTORIA KUJIRUDIA KOMBE LA MABINGWA ULAYA?

Arsenal ndio timu pekee kutoka ligi kuu ya Uingereza iliyobakia katika ligi ya mabingwa Ulaya. Sikutarajia hili kabisa ila napenda niwasifu wapiga bunduki wa London kwa hili. Waingereza huwa wanasema ‘due credit’.
Hii siyomara ya kwanza Arsenal kufikia hatua hii ya robo fainali ila emeweka rekodi ya ulaya kuiondoa Real Madrid. Hii, kwa kuzingatia misingi ya kihistoria katika soka la Ulaya, Arsenal itafika fainali kama kweli historia hujirudia. Nimechambua historia ya mashindano haya inaonesha kila timu iliyoweza kuondoa Real Madrid ilifika fainali. Hebu tujitahidi kukumbuka Bayern Munich, AC Milan, Juventus na Monaco katika miaka kadhaa michache iliyopita.
Ushindi wa Benfica dhidi ya Liverpool ni historia nyingine katika soka la Ulaya. Sio tu ni timu ya kwanza kuiondoa Liverpool katika vikombe vya Ulaya bali pia ni timu ya kwanza barani Ulaya kuifunga Liverpool ugenini na nyumbani tangu mwaka 2001/ 2002. Hii inanifanya niamini kuwa timu yeyote yenye uwezo wa kuiondoa Man United na Liverpool katika mashindano ni bora kufikia fainali. Labda hapa niwakumbushe kuwa Bayer Leverkusen iliiondoa Liverpool mwaka 2001/ 2002 na ikatinga fainali. Porto chini ya mtaalam Mourinho iliiondoa Man United mwaka 2003/ 2004 na wakafika fainali na kushinda.
Hadi sasa Arsenal wana rekodi bora kabisa ya kufungwa magoli mawili tu na ni timu pekee pamoja na Barcelona hazijapoteza mchezo wowote. Timu imebadilika ikicheza kwa umoja na nidhamu ya mchezo katika kulinda na kushambulia.
Kwa upande wa Chelsea, iliaminika na wengi kwamba ingeondolewa tu. Barcelona ni timu yenye vipaji asili (natural) pamoja na ufundi wa hali ya juu. Ukizingatia timu ya Mourinho inayotegemea ufundi wa kisayansi—yaani mtizamo wa kibinadamu (artificial) niwazi njia za asili zingeshinda tu. Kushinda ligi ya mabingwa unahitaji wachezaji wenye vipaji vya asili ambavyo vituvizidi vile vya kufundishwa na walimu wa timu pinzani. Mourinho alikosa jibu la Lionel Messi na Ronaldino katika timu yake.
Liverpool haina wafungaji magoli na ndio maana ikatolewa. Unapopata nafasi nyingi za kufunga alafu hufungi magoli ninachoweza kusema ni kuwa timu ni mbovu. Magoli ndio kiashirio cha ushindi na wala sio chati ya vielelezo vya umilikaji au majaribio mangapi timu imefanya golini mwa timu pinzani.
Mwisho, Liverpool kuondolewa katika ligi ya mabingwa ni sheria wala sio jambo la kustaajabisha. Hakuna bingwa mtetezi aliyewahi kutetea kombe hili. Arsenal wanalihitaji kombe hili na inaonekana matumaini yapo. Kwani nina hakika Juventus watapata shida sana kuenda na kasi na ari ya Arsenal. Hebu tusubiri robo fainali tuone.

Thursday, March 16, 2006

MKAPAISIM--LEGASI YA AWAMU YA TATU

Mimi ni mmoja wa watanzania wachache sana ambao wakati JK anaingia madarakani sikuwa namwamini kabisa. Unajua nimezaliwa nikakuwa nikiona wanasiasa wa CCM wakituongoza kwa migengwe ya kila aina. Ndio maana niliwahi kuandika JK Anatania tu. SOMA
Kama nilivyosema katika makala ile, kuwa JK anawafahamu walarushwa waliojikia mizizi ndani ya dola. Na nikahisi ataendeleza sera ya kulindana ya aliyemtanglia, mheshimiwa Mkapa. Nafurahi kusema kwa ninayoyaona sasa, JK kadhihirisha kuwa nilikosea. Kwa kiasi fulani ninaanza kuona Kasi Mpya. Na hii ni wazi kwangu ni juu ya suala la “Ujambazi”.
Ninasoma habari jinsi ambavyo serikali imewavalia njuga baadhi ya matajiri ambao wanalea majambazi nikafurahi sana. Imani yangu imeanza kumea kwani nataka niseme baadhi ya matajiri waliokamatwa ni watu ambao wamekuwa wakitawala tetesi kuwa ni majambazi tangu nikiwa mtoto nasoma shule ya msingi. Kwa hiyo mimi nimefurahishwa na hatua ya serikali.
Labda nimkumbushe kamanda Saidi Mwema kuwa tafadhali hakikisha dola inajua shughuli za wenye fedha wote. Kuna umuhimu wa serikali kujua baadhi ya wafanyabishara wanapata wapi mitaji mikubwa ya kuendeshea miradi yao feki. Utandawazi isiwe ndio mwanzo wa watu kuachiwa huru kujifanyia chochote watakacho. Nikumbushe pia hawa wafanyabiashara wanajihusisha na vigogo wa serikali; hivyo ni muhimu na vigogo kadhaa waanze kuhoiwa kama kweli tunataka kupambana na ujambazi kwa ari mpya na kasi mpya. Hii mambo ya kuhamisha baadhi ya maofisa polisi na kuwapeleka jijini makao makuu nataka niseme ni doa katika hii vita ya ujambazi. Yaani mtu anahamishwa eti kutoka mkoa unaosemekana ni kitovu cha ujambazi alafu anakwenda makao makuu? Kwa nini tusiwastaafishe watu kama hawa kwa manufaa ya umma? Hapa nimechanganyikiwa kabisa.
Katika gazeti la Nipashe toleo la tarehe 10/3 nilisoma eti kuna afisa wa polisi eti akaunti zake zimesimamishwa. Hakutajwa kwa jina na mimi naona nisimtaje ila walipoandika eti anatoka mikoa ya kaskazini hisia zangu zilinicheza. Unajua Tanzania watu wa kawaida wanaishi na kuzungumza tetesi nyingi sana. Ila tatizo ni kwamba hasa kipindi cha Mkapa alikuwa akipiga tetesi kabisa. Alikuwa anasisitiza eti wananchi walete ushahidi. Dhihirisho la jinsi ambavyo alivyokuwa anapenda kulea watendaji wake, wengi wao wakiwa wala rushwa na mafisadi wakubwa. Hii madhila ya jeshi la polisi ni dhihirisho la sera mbovu za uongozi mbovu wa awamu iliyopita.
Madhila ya ujambazi tunayoyaona leo ni matokeo ya sera: MKAPAISM—kuficha maovu, wala rushwa, mafisadi na kutochukua hatua dhidi ya maafisa wakubwa wa serikali pale walipokwenda mrama. Hii ilipelekea kwa mfano jeshi la polisi likafika mahali haliheshimu hata raia. Jeshi linaendeshwa kama mali ya mtu binafsi bwana. Nakumbuka kila mara ninapokuwa kule Moshi huwa nashangaa sana. Sina hakika kama ni watu wote wanashangaa kama mimi pale unapoona askari polisi wa usalama barabarani wanasimamisha vipanya navyo havisimami na unasikia kondakta akitumwa akawaone hawa mabwana. Huko nasikia huwa anapeleka noti ya shilingi 1500 au 2000. Huwa nabaki kujiuliza je hawa ni wafanyakazi wa umma au wakusanya ushuru? Kama unataka kuyaona haya nenda karibu na kituo cha mabasi Moshi Mjini sehemu inaitwa BORA, kuna nguzo ya umeme na utakuta askari kasimama pale mida ya asubuhi.
Hapa kamanda Saidi Mwema atajiju kwani jeshi letu la polisi lilikuwa likiendeshwa bila maadili, kizamani na kila aina ya michezo michafu. Mwisho, niulize: polisi imewatia kizuizini matajiri kadhaa lakini nikumbushe kitu kimoja: wataalam wa sosholojia wanasema wanawake pia wanajihusisha sana na uhalifu. Mbona hamjawatia lupango Wabejing? Wanalea majambazi sana pia.
Pamoja na kumkandia Mkapa na "Mkapaism yake" nafikiri ni bora pia tujue anaendeleaje na mapumziko yake. Hebu bonyeza hapa uone.

Sunday, March 12, 2006

USHOGA KUKUBALIKA KAMA DESTURI HIVI KARIBUNI

Nimekutana na makala moja ambayo imenikuna sana juu ya ushoga.
Ama kweli hivi majuzi katika nishani za Oskar kule kwa Joji Kichaka, walifikia mahali na kuitunza filamu ya ushoga.
Kwa kweli nina wasiwasi sasa si muda mrefu 'Ushoga utakuwa sio dhambi'. Jamani mimi nimechanganyikiwa manake sasa wazungu wanatuwekea viwango kwenye kila kitu. Na wakishapitisha kwamba kitu fulani ni bora ndio hivyo tena sisi makabwela tunaona ni fasheni. Bonyeza hapa uone yuko mzungu mmoja hapa Uganda ana maoni fulani.

NCHI INAPOMILIKISHWA KWA MTU BINAFSI

Ama kweli kuna viongozi wanaopenda kumiliki nchi kama mali yao. soma hapa

Tuesday, March 07, 2006

MAMBO YA LUGHA NA FRED MACHA

Makala ya Fred Macha imenikosha na nimeona niifadhi ili tuisome na tujikumbushe umuhimu wa kulea lugha yetu. soma

UGANDA BAADA YA UCHAGUZI

Kama kawaida hapa Uganda mambo ya siasa yanaendelea kuchacha. Museveni kashinda uchaguzi kwa mbinde. Leo mahakama kuu imetoa hukumu soma dhidi ya Dk Besyige kuwa hana hatia ya ubakaji. soma
Ni aibu kwa Museveni tena lakini yeye anaendelea kujitapa katika makala aliyoiandika mwenyewe leo magazetini hapa soma. Pia leo imeandikwa makala juu ya udhalimu wa serikali ya Museveni kutumia jeshi kwa manufaa yake binafsi na kuvunja katiba. Hebu soma uone udikteta ulivyokomaa.
Ni wazi majaji wa hapa wako makini kwani serikali inapoteza kila kesi si kawaida lakini ndio hali halisi bonyeza