My Blog List

Monday, January 30, 2006

JK ANATANIA TU.

Nakumbuka mzee kifimbo alipong’atuka mwaka 1985, nchi yetu ilikuwa hoi kiuchumi. Mzee Ruksa alikuja kama mkombozi. Wakati huo nasoma shule ya msingi, basi redio Tanzania ilizoea kucheza nyimo kuonesha mwelekeo mpya; nakumbuka kibao kimoja: ‘Usiopowajibika Ole Wako, Utakumbwa na Fagio la Chuma’. Pia kulikuwepo tangazo katika redio kila mara redioni eti: Mdudu rushwa ni hatari na anapiga na anaua’.

Hii yote ilikuwa kuonesha eti Mzee Ruksa kaja na ari mpya dhidi ya rushwa. Matokeo yake utawala wake uliikumbatia rushwa hadi mzee Kifimbo kumkemea kiana wakati Fulani pale Kilimanjaro Hoteli.Baadaye akaja Mkapa na kauli mbiu ilikuwa ‘Uwazi na Ukweli’. Kinyume chake huyu bwana hakupenda uwazi kabisa; ukweli ndio usiseme, waandishi wa habari watakuwa mashahidi hapa.

Sasa kaja Kikwete na kauli mbiu—Ari mpya, Kasi mpya na Nguvu mpya. Hisia zangu zinaniambia hivi: Kuna hatari haya majigambo tu. Katika uteuzi wake anaonekana kuja na sura mpya nyingi tu. Hii ni habari njema isipokuwa utendaji wao sidhani kama utafanikiwa.

Hii ni kwasababu raisi anapaswa, nafikiri analijua hili kwamba CCM imejaa wala rushwa wakuu nchi hii. Vyombo vya dola, mfano jeshi la polisi limejaa wala rushwa na huu ni utamaduni ndani ya chombo hiki inavyoonekana.

Nilipokuwa natizama hotuba ya JK ya ufunguzi wa bunge niligundua mambo mengi. Wapo wabunge kadhaa walionesha sura za woga na chuki dhidi ya maneno ya raisi. Wengi wa wabunge wazee pamoja na wabunge wanawake kadhaa walionekana kuogopeshwa na hotuba ile.

Kwa mtu yeyote aliyezoea kuishi kiujanjaujanja aliogopa sana. Nani asiyejua wabunge wengi wanalitumia bunge kama tanuri ya utajiri? Nani asiyejua wabunge wengi ni vihiyo ambao hata hawafahamu nchi yao kwa dhati. Mheshimiwa JK anaongea kama vile hajui wapo wazee, vigogo ambao hawashikiki nchini mwetu (untouchable) wamejazana bungeni ili kulinda maslahi yao. Hawa ni kikwazo kwa Ari mpya, Kasi mpya na Nguvu mpya.

Mwisho niseme tu ninamuunga mkono mheshimiwa JK, ila nina hakika itakuwa vigumu kwake kuleta mabadiliko tunayoyatarajia. Kutamba kwa majambazi ni kielelezo cha kwanza. Ila itabidi raisi awe mkweli tu kuwaridhisha watanzania. Kama waswahili walivyonena: “Bahari haiishi Zinge” nami ninene: JK anatania tu.

Monday, January 16, 2006

UCHAGUZI NA ODA KUTOKA JUU NANI ATANGAZWE MSHINDI

Hili nataka nilieleze kama nilivyolipata kupitia tetesi zilizozagaa mitaani pale Moshi mjini baada ya uchaguzi wa ubunge ambapo mgombea wa Chadema, Mzee Ndesamburo alimshinda yule wa CCM, Mama Elizabeth Minde. Nitaeleza mara baada ya kuweka wazi wasiwasi wangu juu ya hali ya usalama pale Moshi.

Kwa kipindi cha wiki tatu nikiwa Moshi mjini nilishuhudia hali ambayo kwangu ilinitia wasiwasi sana. Eti siku hizi ujambazi umeongezeka sana Tanzania hasa Moshi na utawala umeamua kwamba askari polisi lazima wapite mitaani wakiwa na silaha kuhakikisha usalama. Kwa kweli mitaa imejaa askari ila katika hali ya kunishangaza sikujiona salama kabisa. Niwachekeshe: katika matembezi yangu nilikutana na kijana, charafu, hajachana nywele, amevaa suruali ya jeanse chafu sana ambayo imechanwa sehemu mbalimbali na amebeba bunduki( short gun). Nusura nianguke manake nikajua huyu ni jambazi bahati nzuri watu wengine wakaniambia ni askari yuko kazini.

Nililoliona hapa ni kwamba tofauti ya jambazi na askari haionekani manake usalama unakuwa haupo, raia hawezi kumjua askari ni yupi.Nidhamu ya askari haipo kabisa hili nitalizungumzia siku nyingine kwani nina mifano mingi tu.

Basi nieleze juu ya uchaguzi pale jimbo la Moshi manispaa hasa kuhusu tetesi ambazo kama waswahili walisema: “lisemwalo lipo na kama halipo…….”.Mwaka jana mara baada ya CCM kuteua wagombea wake wa ubunge nilieleza uvumi uliokuwa umezagaa kule Moshi. Mgombea wa chama hicho, Mama Minde, ni wazi alikuwa ni chaguo bovu kwa wapiga kura.

Nilikuwa Moshi wakati ule na nikasema hatashinda huyu mama. Na kweli imekuwa hivyo; ila nilipokuwa huko hivi karibuni nilikusanya tetesi zingine ambazo nafikiri ni vizuri wanablogu mnisaidie kuchambua.

Ni hivi: uchaguzi wa Tanzania uliokwisha hivi karibuni umesifiwa sana na wanahabari na hata waangalizi mbalimbali. Kwa wapinzani umekuwa ni bumbuwazi kubwa sana. Ila kwangu naomba nijibiwe hili:

Kwa mfano, pale Moshi manispaa, inasemekana msimamizi wa uchaguzi, mkurugenzi wa manispaa, alichelewa sana kutangaza matokeo mara baada ya hesabu kukamilika. Eti ilimbidi afanye mawasiliano na wakubwa ili aruhusiwe kuyatangaza. Habari aisizothititishwa ni kwamba ilikuwa ni janja ya kumtangaza mgombea wa CCM kama mshindi. Ila hapa ilishindikana kabisa. Wigo wa kura ulikuwa mkubwa sana na inasemekana hata hizo alizopata mwanamama sizo zilizotangazwa kuondoa aibu. Je huu ndio uchaguzi ulio huru na haki?

Inasikitisha sana hizi sera za Mao hazifai kabisa.

KUTOKA TANZANIA HADI UGANDA

Mara ya mwisho niliaga kwamba sitakuwepo ulingoni mwaka jana. Nilikwenda mapumzikoni kule kwetu Moshi. Niliondoka hapa Uganda nikiacha hali ya kisiasa ikiwa ya vurugu, vitisho na udikteta ukiashiria kila hali ya zari kama sio dhahama ama kasheshe. Nimerudi hapa Uganda; ni wiki moja imekwisha sasa na hali imebadilika haswa kinume na nilivyokuwa nimetabiri kwamba hatima ya Besigye kisiasa. Nitaeleza baadaye.

Niwapashe wanaglobu wenzangu ni nini nilikikuta huko Moshi, uchagani katika wilaya ya Moshi Vijijini, jimbo la uchaguzi la Vunjo. Nilifika tu na Raisi mpya akatangazwa. Hii haikuwa tashwishwi kwangu kufuatilia kwani dhahiri nilijua JK angeshinda. Ila uchaguzi wa ubunge ulinikuna sana.

Baada ya miaka kumi ya utawala wa mbunge wa chama cha upinzani hatimaye jimbo langu la Vunjo likamchagua mbunge kutoka CCM kwa mara ya kwanza tangu siasa za vyama kurejeshwa. Hili lilinifurahisha kwani hawa jamaa wa upinzani wameirudisha Vunjo nyuma sana. Nasema hivi kwani katika eneo ninaloishi, kijiji cha Uparo, Kirua Vunjo, palw maeneo ya Kawawa Road ni dhihirisho tosha.

Nyumbani pale hakuna maji ya bomba tangu uhuru saa. Umeme ndio usiseme hakuna kabisa. Barabara ya kwenda Kirua Vunjo haifai kabisa; ikinyesha mvua inabidi magari yasubiri jua litoke ili pakauke ndio watu waweze kusafiri. Kuhusu mambo ya elimu ndio usiseme: eneo la Kawawa Road kwa mfano halina shule ya sekondari wala msingi na lina makaazi ya watu wasiopungua elfu tano. Watoto inawabidi kutembea kwa miguu zaidi ya kilomita saba kwenda shule kama za Pakula Sekondari, Mashingia na Uchira Sekondari. Hii ni hatari sana sasa tuone hawa CCM watafanya nini.

Niliposikia Kikwete na ari yake mpya, nguvu mpya na kasi mpya sikumwelewa sana ila nampa matarajio kama mkazi wa Kawawa Road kwani tumempa mbunge labda matatizo yetu yatapungua. Nafikiri mheshimiwa mbunge anajua hili.

Sasa niwarejeshe hapa Uganda: Mnakumbuka Museveni aliamua kumweka jela mpinzani wake mkuu Dr. Kiiza Besigye. Chama cha Besyigye kikaweka ukinzani wa hali ya juu. Nakwambea imesaidia sana , hali ya siasa ya Uganda kwa sasa ni shwari hata mimi nashangaa. Besigye yuko nje kwa dhamana ila kampeni in kama kawa. Vitisho dhidi ya fyombo vya habari na wapinzani vimekomeshwa; wale wanajeshi waliozoeleka kujazana mitaani hawapo tena.

Museveni kabadilika sana; uchaguzi utakuwa shwari kama hali itaendelea hivi. Nitaendelea kuwapasha zaidi ila tu Besigye anatuhumiwa kubaka na kesi inaendelea na imejaa vituko kwelikweli.